Tuesday 25 March 2014

KINGWANGALLA AKAMATWA NA POLISI KISA!!

Filled under:



JESHI la Polisi wilayani Nzega, mkoani Tabora limemkamata na kumuachia kwa masharti Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangallah, kwa madai ya kuongoza maandamano ya wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao wanapinga kufungwa kwa machimbo ya Mwashina, yaliyo jirani na mgodi wa Resolute Tanzania Limited.

Mbunge huyo alikamatwa majira ya saa 10:00 jioni juzi baada ya kufanya maandamano yasiyo na kibali yaliyoanza saa saba mchana.
Kabla ya hapo mbunge huyo alifanya mkutano wa hadhara na wachimbaji hao katika Kijiji cha Nzega Ndogo wilayani humo ambapo alielezwa matatizo ya kufungwa kwa machimbo hayo na Kamishna wa Madini nchini, Paulo Masanja, bila kujali gharama walizoingia wachimbaji hao.

Katika mkutano huo wachimbaji hao walidai ni vema serikali iangalie haki zao zilizotumika kwenye uendeshaji na uchimbaji wa mashimo hayo kuliko kuwafungia bila kujali ingawa eneo hilo liko ndani ya leseni ya mgodi wa Resolute.

Hata hivyo katika hoja hiyo mbunge huyo aliwataka wachimbaji hao kudai haki yao kwa kufuata taratibu bila kujali tofauti zao kisiasa, kikabila na kidini na badala yake wawe kitu kimoja.

Dk. Kigwangallah aliwaambia wachimbaji hao haki zao ziko mikononi mwao hivyo ni uamuzi wao kudai haki na yeye kama mwakilishi wao yuko nyuma yao mpaka pale haki yao itakapopatikana.

Aidha, wachimbaji hao walimwomba mbunge huyo kuambatana nao kwenye maandamano ya amani kutoka Kijiji cha Nzega Ndogo kwenda Mwashina yalipo machimbo yaliyofukiwa umbali wa zaidi ya kilomita tatu kujionea hali halisi.

Kufuata hali hiyo, wachimbaji hao walianza maandamano ambayo yaliungwa mkono na mbunge huyo hadi Kijiji cha Mkwajuni kabla ya kufika Mwashina, ambapo polisi waliibuka na kuyasambaratisha kwa mabomu ya machozi.

Katika  purukushani hizo polisi walimkamata Dk.  Kigwanhallah   na kumjeruhi mtu mmoja kwa risasi ya moto kwenye paji la uso, ambapo waliondoka naye kwenye gari pamoja na mbunge huyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda, alisema Dk. Kigwangallah alikamatwa na kuachiwa huru ili akamalizie kazi zake kama mjumbe wa Bunge la Katiba.

0 comments:

Post a Comment