Saturday 30 November 2013

MENEJA NMB ABULUZWA KORTINI AKIDAIWA KUIBA SH48 MIL

Filled under:



Meneja wa Benki ya NMB  Ilala,  Gasper Urassa (49) amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la wizi wa Sh48 milioni.

Urasa alifikishwa katika mahakama hiyo kujibu shtaka linalomkabili la wizi wa Dola   30,000 za Marekani, mali ya Kampuni ya Epoch Mining Tanzania.

Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 11, mwaka huu katika benki ya NMB iliyopo Ilala.

Martin alidai siku ya tukio  kwenye benki  hiyo,  mshtakiwa aliiba Dola 30,000 za Marekani (Sh48 milioni) mali ya Kampuni ya  Epoch Mining Tanzania.

Mshtakiwa alikana shtaka na Hakimu Janeth Kinyage aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 10, mwaka huu itakapotajwa.
Mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, watakao saini hati ya Sh22.5 milioni.

Posted By Unknown09:12

IMEBAINIKA VIDONGE VYA UZAZI WA MPANGO VINASABABISHA UPOFU

Filled under:







Pamoja na kuwa ni njia nzuri ya kuzuia ujauzito, vidonge vya Uzazi wa Mpango vinatajwa kusababisha  ugonjwa wa macho ujulikanao kama Glaucoma, unaoelezwa kuwa ni chanzo kikuu cha upofu.

Ugonjwa huu unaelezwa kuwa sababu kubwa ya kusababisha upofu kwa wanawake wanaotumia vidonge hivi kwa muda mrefu.

Hayo yamebainishwa kwenye Utafiti wa  Afya na Lishe  uliofanywa na Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa cha Marekani(CDCP).

Utafiti huo unasema kuwa, seli zilizoko katika neva za macho zina homoni za estrogen  ambazo hufanya kazi ya kulinda macho, vidonge hivyo huingilia mchakato  huo wa ulinzi kwa kupunguza kiwango cha homoni hizo.

Unasema kuwa wanawake wanaofunga hedhi mapema au wanaotumia vidonge ambavyo huzuia kuzalishwa kwa vichocheo vya estrogen, na dawa za saratani ya matiti, huweza kupata upofu.
Wanawake zaidi  ya 3,400  wenye umri wa zaidi ya miaka 40 walifuatiliwa kwa zaidi ya miaka mitano ikiwa ni sehemu ya utafiti huo.

Profesa Shan Lin wa Chuo Kikuu cha Carlifonia, San Francisco anasema wanawake wanaotumia vidonge hivyo kwa zaidi ya miaka mitatu, wanatakiwa kupima maradhi ya macho aina ya Glaucoma na afya zao zifuatiliwe kwa uangalifu na wataalamu wa macho.

Utafiti huo umebaini kuwa wanawake waliotumia vidonge hivyo kwa miaka zaidi ya mitatu walikuwa na hatari kwa asilimia tano ya kupata upofu usababishwao na glaucoma ukilinganisha na wasiotumia vidonge  hivyo.

 Kiongozi wa utafiti huo, Dk Louis Pasquale  wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Havard anasema vichocheo vya Estrogen  vina umuhimu katika  seli za retina ambazo zinajulikana kwa kupokea homoni hizo.
“Kuwepo kwa homoni za estrogen kunazisaidia seli hizo kuwa hai kwa hiyo wanawake wanapotumia vidonge vya uzazi, homoni hizo huharibiwa na kurahisisha uharibifu wa macho,” anasema Dk Pasquale.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk Cyriel Masawe wa Chuo  Kikuu cha Tiba cha Muhimbili (MNH) anasema  ni hatari kwa wasichana wadogo ambao hawajaolewa kutumia dawa hizo ovyo.
“Kwa mfano mikoa ya Lindi na Mtwara, tumegundua wasichana wadogo ambao hawajaolewa wanatumia zaidi sindano za uzazi wa mpango na vidonge,” anasema

Posted By Unknown08:56

JK AMUWEKA KITANZINI PROFESA KAPUYA

Filled under:









Rais Jakaya Kikwete ameviagiza vyombo vya dola kuhakikisha vinamkamata mtu yeyote bila kujali cheo, atakayebainika kumbaka au kumuoa mwanafunzi wa shule.

Ametoa kauli hiyo huku aliyekuwa waziri wa wizara tofauti katika awamu mbalimbali za uongozi, Profesa Juma Kapuya, akiandamwa na tuhuma za kumbaka na kutishia kumuua binti, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16.

Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina, lakini ni dhahiri kuwa kauli hiyo inamgusa pia Profesa Kapuya, Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM).
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara kwenye wilaya za Itilima, Meatu na Maswa mkoani Simiyu, Rais Kikwete alisema mtu anayefanya mapenzi na wanafunzi lazima akamatwe, ahojiwe na kufunguliwa mashitaka ya ubakaji na si vinginevyo.

“Kuna watu wanafanya mapenzi hadi na wanafunzi wakati sote tunajua ukimwi upo na hauna dawa na unaua. Kwa hiyo kila mmoja wetu awe makini kujikinga nao na tuepuke kuwaambukiza wengine,” alisisitiza Rais Kikwete.

Wakati Rais Kikwete akisisitiza wahalifu wa makosa ya kubaka na kuoa wanafunzi wachukuliwe hatua, polisi jijini Dar es Salaam wamekuwa wakisuasua kumchukulia hatua Profesa Kapuya licha ya binti anayedaiwa kumbaka, kufungua jalada namba OB/RB/21124/13 katika kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam, akidai kutishiwa kuuawa na mbunge huyo.

Kauli ya Rais Kikwete imeonyesha dhahiri kukerwa na moja ya ujumbe mfupi wa maneno wa simu ya mkononi kutoka kwenye simu inayodaiwa kumilikiwa na Profesa Kapuya kwenda kwa binti aliyebakwa, ambapo mbunge huyo alijigamba kwamba serikali haiwezi kumfanya chochote.
Ujumbe huo unasomeka hivi: “Mkiuawa itakuwa vizuri…itawapunguzia gharama za kuishi, usitake kugombana na serikali mtoto mdogo kama wewe, sisi ndiyo wenye nchi yetu, mwenye hilo gazeti ni Mbowe, sasa mwambieni nyumba ya kuishi si mmemuingizia hela leo? Mnatumika tu bure watu wanaingiza hela nyingi, ila mmenitibua lazima niwaue, wiki hii haitaisha, nitapiga kambi kote, jana si wamekuficha, tuone utalindwa milele, maana washatengeneza hela, lazima mvae sanda tu, hilo sio ombi ni wajibu wenu, mnajitia na nyie mafia watoto siyo, watoto wetu wanauza unga nani anawakamata? Nani atapingana  nasi.”

Habari kutoka Ikulu ya Rais Kikwete zinaeleza kuwa kiongozi huyo wa nchi amekerwa na kauli ya mbunge huyo wa Urambo Magharibi kwamba serikali haiwezi kumfanya jambo lolote.
Ni kutokana na kauli hiyo, mtoa taarifa wetu alisema rais aliagiza vyombo vya dola kufuatilia kwa karibu sakata hilo na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.

Pamoja na msimamo wa Rais Kikwete na binti anayedaiwa kubakwa kuripoti polisi, Profesa Kapuya alifanikiwa kusafiri nje ya nchi huku polisi wakimshuhudia bila kumtia mbaroni.
Akiwa nje ya nchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikaririwa mara kadhaa akijigamba kuwa polisi inamsaka mbunge huyo na itamtia mbaroni mahala popote alipo.

Hata hivyo, Profesa Kapuya alirejea nchini juzi huku polisi wakimshuhudia bila kuchukua hatua zozote.
Mwanafunzi huyo anadai kubakwa na Profesa Kapuya kwenye moja ya hoteli ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho ndani ya ofisi yake katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipomuita kwenda kuchukua ada.

Posted By Unknown07:36

MTUHUMIWA WA WIZI M-PESA ATOROKA NA KUWAACHIA KASHFA POLISI

Filled under:



Jeshi la Polisi limeingia kwenye kashfa ya kumuachia mtuhumiwa wa wizi wa fedha zaidi ya sh milioni 1.2 kwa kutumia njia ya utapeli kwenye huduma ya kutoa na kuweka fedha kwa njia ya simu ya Kampuni ya Vodacom (M-pesa).

Tukio la utatanishi la kuachiwa kwa kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Ahmed Ahmad, limethibitishwa na askari aliyekuwa ameshikilia faili lake, Venance Ngeze ambaye alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitoroka jana asubuhi alipokuwa kwenye chumba cha mahojiano.

Ilielezwa kuwa kabla ya kutoroka, mtuhumiwa huyo alilala selo siku moja baada ya walalamikaji ambao ni mawakala wa M-pesa, Melina Marki, Rose Marki na Teresia Wilhad kukataa kushawishiwa kufuta kesi hiyo kwa makubaliano ya kurudishiwa fedha zao wanazodai kuibiwa na Ahmad.

Katika tukio hilo, Melina alidai aliibiwa sh 300,000, Rose sh 684,000 na Teresia sh 229,000. Wote wameibiwa katika ofisi zao zilizopo maeneo tofauti katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Melina alieleza kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akifika katika shughuli zao akiwa na kadi za Vodacom zaidi ya 150 alizokuwa akihitaji kusajiliwa ambapo baadaye iligundulika kuwa huzitumia kwa utapeli.

“Alifika kwangu akiwa na kadi za simu 150 na kuhitaji huduma ya kuzisajili, lakini alikuja hana vielelezo ndipo akasema kuwa anaomba tuendelee kumsajilia yeye anaenda kutoa photocopy ya kitambulisho, huku akiwa ameacha simu yake ya mkononi na kiasi kidogo cha fedha, kuonyesha kwamba anarudi, lakini aliporudi aliniambia amekosa photocopy, ila anahitaji kutoa fedha kwenye simu yake.

“Nikamtajia namba yangu ya uwakala, akatoa na ujumbe ukaja ukionyesha anatoa kiasi cha sh 300,000 baada ya kuondoka nilishangaa kadi yangu ya simu ilikuwa imefungwa, nilipokwenda Vodacom kujua sababu ya kufungiwa, nilielezwa kwamba hawatanifungulia kwa sababu bado wanamtafuta mtu anayefanya mchezo huo,” alisema Melina.

Naye Teresia akielezea tukio hilo, alisema mtuhumiwa huyo ambaye hutumia kadi za simu ambazo zimekuwa zikisajiliwa bila ya kuwa na picha za kitambulisho kwa nia ya kuondoa ushahidi pindi linapotokea tatizo la kufungiwa, alifika na kumtaka atoe kiasi cha sh 229,000 huku akiomba asajiliwe kadi zaidi ya 150, lakini baada ya kumshughulikia naye alijikuta simu kadi yake ikifungwa pasipo kujua sababu hadi pale alipokwenda Vodacom.

“Baada ya kufika Vodacom, waliniambia kwamba hawataweza kuifungua kwa sababu wanamtafuta mtuhumiwa anayefanya mchezo huo wa kuiba fedha, kwani kumekuwa na malalamiko mengi yaliyoripotiwa katika ofisi hizo,” alisema Teresia.
Akielezea kushangazwa kwake na kutoroka kwa mtuhumiwa huyo, 
 Melina anayefanya shughuli zake Mtaa wa Samora, alisema kuwa 
baada ya kufika katika kituo hicho jana, walielezwa na askari Venance aliyemkamata mtuhumiwa huyo juzi kuwa ametoroka katika mazingira ya kutatanisha huku akiwa ameacha  sh 300,000 na vifaa vyake vingine.

Anasema kuwa Venance aliwaeleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kutoroka, alichukua uamuzi wa kuwakamata ndugu zake wawili waliokuwa wamefika kwa ajili ya kumdhamini ili aweze kumpata kirahisi mtuhumiwa huyo, huku akiwaomba walalamikaji kukubali kulimaliza suala hilo kinyemela.
Taarifa ilizozipata Tanzania Daima zinasema kuwa mtuhumiwa huyo hakutoroka kama ilivyoelezwa, ila aliachiwa na kuwaacha ndugu zake na vifaa vyake ikiwa kama dhamana ili akatafute fedha za kuwalipa walalamikaji wa tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kipolisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema kutokana na mazingira ya kutoroka kwa mtuhumiwa huyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na endapo litabaini kuwa askari huyo alimuachia kwa uzembe litamchukulia hatua kwa kosa la kinidhamu.
Kamanda Minangi alisema jukumu la kumtafuta mtuhumiwa huyo amekabidhiwa polisi aliyedaiwa kumuachia mtuhumiwa, na walalamikaji wakatakiwa kurudi leo saa nne asubuhi.

Posted By Unknown06:44

SIRI YA KUPOROMOKA KWA GHOROFA ILALA YATOLEWA

Filled under:








Kuporomoka kwa jengo la ghorofa  Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam Machi 29 mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 36, kunadaiwa kutokana na  uzembe wa serikali.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyotolewa Novemba 24 mwaka huu na taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza, asilimia 87 ya watu waliohojiwa, iliitupia lawama serikali kwamba inahusika kwa kiasi kikubwa.

Asilimia  47 ya  watu waliotoa maoni yao juu ya kuanguka kwa jengo hilo, ilisema kuwa uzembe wa wakaguzi wa majengo wa serikali pia ni miongoni mwa chanzo kingine.
Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 32 ya waliohojiwa walisema kuporomoka kwa jengo hilo kulisababishwa na kampuni ya ujenzi iliyokuwa ikishikilia dhamana ya ujenzi wake.

Aidha, ripoti hiyo ambayo imejikita katika mahojiano ya watu 333 katika wilaya zote tatu za Dar es Salaam, inaonyesha kuwa asilimia 18 ya maoni yaliyotolewa kuhusu sababu za kuporomoka kwa jengo hilo ni uzembe wa manispaa husika.
Mbali ya hayo, ripoti hiyo inaeleza kuwa  asilimia 57 hawafahamu chochote kama kuna fidia zilizokuwa zimelipwa kwa waathirika ama familia zao.

Ripoti hiyo ya utafiti ilikwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa maoni juu ya suala la mgawanyo wa wajibu ni sehemu kubwa ya jukumu, ambapo asilimia 46 ilisema wahusika  hawafanyi  kazi kwa kuhakikisha kuwa sheria za ujenzi zinafuatwa badala yake imekuwa ni kinyume.

Asilima 32 ya waliohojiwa pia waliitupia lawama kampuni ya ujenzi kwa ajali mbaya wakati ni suala la wajibu binafsi, lakini pia asilimia 78 walikubaliana kwamba rushwa ni chanzo cha majanga kama hayo.


Posted By Unknown06:37