Thursday 22 May 2014

TAARIFA YA BAVICHA ILIYOTOLEWA KUHUSU UKAWA

Filled under:

TAARIFA KWA UMMA

UPOTOSHWAJI NA PROPAGANDA CHAFU DHIDI YA CHADEMA/UKAWA NA KIKUNDI KILICHOJIVIKA VYEO HEWA


Zimetolewa taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mtu anayejitambulisha kwa jina la Fikiri Migiyo na ambaye amejitambulisha pia kama Mwenyekiti wa Mabaraza ya kanda ya Ziwa Magaharibiinayojumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Kagera na Geita akipinga kuundwa kwa umoja wakutetea katiba ya wananchi (UKAWA)

Aidha mtu huyo anayejitambulisha na BAVICHA ameenda mbali kwa kutoasiku 14 kwa CHADEMA kujiondoa kwenye UKAWA na pia kulaani kitendo cha UKAWA kususia Bunge la Katiba.

Barazala Vijana wa Chama cha Demokrasisa na Maendeleo (CHADEMA) linapenda kuufahamisha umma wa Tanzania na wapenda mabadiliko mambo yafuatayo:-

1. BAVICHA haina kiongozi wa jina hilo la Fikiri Mayingi kwa Mkoa wa Geita 

2. Katika muundo wa chama na Mabaraza yake hakuna cheo kinachoitwa Mwenyekiti wa makatibu wa Mabaraza kwa Kanda. Hivyo mtu huyo aliyetoa tamko hilo amejipachika cheo hicho ili kukidhi hajana matakwa yake binafsi kwa nia ovu ya kuichafua CHADEMA 

3. Pia ni muhimu umma ukaelewa kuwa Muundo wa uongozi wa BAVICHA na hata mabaraza mengine ya chama unakomea kwenye ngazi ya mkoa na kisha Taifa mpaka hapo muundo wa kanda utakapohuishwa kwenye mfumo wa baraza kuanzia kwenye chaguzi zijazo. Hivyo kilichotolewa kwa umma ni cha kuupuuza.

4. BAVICHA haijawahi kufanya uchaguzi kwa mikoa yote mipya ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi hivyo kusema kwamba yeye ni mwenyekiti wa makatibu wa mabaraza ya chama kwa mikoa tajwa ni hila za kisiasa zinazoendeshwa na kundi la vijana waasi wanaoendeshwa na kivuli cha mtu badala ya itikikati, falasafa na sera za CHADEMA.

5. Aidha, mkoa wa Simiyu uliotajwa kwenye taarifa ya mpotoshaji huyo kuwa ipo kanda ya Ziwa Magaharibi si sahihi licha ya kwamba tu haina uongozi wa BAVICHA zaidi ya Kamati ya Msukomo kwa masuala yote ya kichama ikiwemo mabaraza. Mkoa wa Simiyu uko kanda ya Ziwa Mashariki na si ziwa Magharibi kama alivyosema mpotoshaji.

6. Ieleweke kuwa, Hakuna Mwanachadema mwenye akili timamu anayeweza kupinga uwepo na shughuli za UKAWA kwenye mchakato huu wa katiba mpya, umoja unaobeba maslahi mapana ya taifa letu, umoja unaotete maoni ya wanachi dhidi ya wapinga maoni ya wananchi anaye jitambullisha kama mwanachadema, wanaopinga maoni ya wananchi na rasimu ya katiba mpya wanajulikani.

7. Aidha, hakuna mwanachadema/ BAVICHA mwenye akili timamu anayeweza kuunga mkono vitendo vya kibaguzi, kidini na kikabila, achilia mbali matusi na vitisho vilivyofanywa na Serikali na Wabunge wa CCM kwenye bunge la katiba kwa kupinga kitendo cha UKAWA kutoka nje ya bunge hilo. Mwanachadema anayeweza kutetea vitendo hivyo anajinasibisha kwa utambulisho wa CHADEMA lakini si mwanachadema.

8. Baraza la vijana la chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) linawaomba wanachama na Watanzania kuwapuuza vijana hao wanao tumika kwa kujipachika vyeo visivyokuwepo hata kwenye Katiba ya Chama na Mabaraza yake ili kukidhi adhima na nia ovu ya kuchafua taswira nzima ya CHADEMA.

9. BAVICHA daima itaendelea kuunga mkono juhudi za UKAWA za kupigania upatikanaji wa Katiba bora ya Wanatanzania inayotokana na maoni yao wenyewe.

Imetolewa leo Jijini Dar es salaam na:
Deogratias Munishi
Katibu Mkuu - BAVICHA

Posted By Unknown21:50

BIBI AKAMATWA UWANJA WA NDEGE AKIWA AMEMEZA KETE 82

Filled under:


Dar es Salaam. Bibi mmoja raia wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) amevunja rekodi ya umri wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Cole alikamatwa Jumatatu akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si rahisi kuonekana katika mitambo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa zimesema pamoja na mbinu zake na kujiamini, mwanamke huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa vitengo mbalimbali vya uwanja wa ndege.
Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema mwanamke huyo alikamatwa Mei 19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Selemani alisema raia huyo aliwasili nchini Mei 15, mwaka huu na alikaa muda wote bila ya kuwa na shughuli yoyote, jambo ambalo lilitiliwa shaka na kumkamata.
“Huyu mwanamke achana naye, akisimama mbele yako huwezi ukaamini kwa jinsi anavyojiamini. Alikuwa na mbinu mpya ya kufunga hizo kete. Kila moja ilifungwa kwa karatasi inayofanana na ganda la sigara,” alisema Selemani.
Alisema mwanamke huyo alitumia mbinu hiyo ili asigundulike wakati akikaguliwa kwa mitambo maalumu inayogundua dawa za kulevya.
Taarifa zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake ya ufungaji wa kete, mwanamke huyo alikuwa tayari amevuka hatua ya kwanza ya ukaguzi.
Nzowa alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
“Wakati tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha Kuthibiti Dawa za Kulevya kilibaini na kugundua kuwa alikuwa amemeza dawa za kulevya.
“Huyu ni mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana nguvu za kutosha na tulishangaa baada ya kutoa kete 20 kwa mara moja katika awamu ya kwanza, jambo hili si rahisi kutokana na umri wake,” alisema Nzowa.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Nzowa alisema kikosi chake kimejipanga kukabiliana na mbinu zote zinazobuniwa na wanaosafirisha dawa za kulevya.
Takwimu za kitengo cha dawa za kulevya cha polisi zinaonyesha kuwa kati ya Januari na Aprili mwaka huu, Cole ni mtu wa 26 kukamatwa katika uwanja huo na raia wa tano wa kigeni kukamatwa na dawa hizo.
Raia wa kigeni wengine waliokamatwa kutoka nje ya nchi ni kutoka Marekani, Ugiriki, Kenya na Liberia na kesi zao zinaendelea.

Posted By Unknown21:29

BOKO HARAM WAFANANISHWA NA MAGAIDI WA KIMATAIFA

Filled under:


Baraza la Usalama la UN

Baraza la usalama la umoja wa mataifa hatimaye limeidhinisha kuwekewa vikwazo kundi la Boko Haram baada ya utekaji nyara wa takriban wasichana 300 wa shule katika eneo la Chibok Nigeria.
Kundi hilo limeshutumiwa kuwaua maelfu ya watu nchini Nigeria katika miaka michache iliyopita.
Nigeria ni mwanachama wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwa kipindi cha miaka miwili. Kwa nafasi hii imeweza kushinikiza baraza hilo kuimulikia tochi.

Vikwazo na adhabu

Hatua ya baraza hilo kuiorodhesha Boko Haram miongoni mwa magaidi wa kimataifa, wakipishana au hata kuhusishwa moja kwa moja na AL Qaeda, huenda isionekane kama hatua kubwa. Lakini hii ina maana kuwa sasa jamii ya kimataifa italichukulia kwa uzito mkubwa zaidi kundi hilo.
Baraza hilo limeidhinisha pia vikwazo kuwekewa kundi hilo, viongozi wake na yeyote anayehusishwa nalo. Hii ina maana kuwa hata mali zao zitazuiliwa na akaunti zao zote zinazojulikana kufungwa.

Jamii ya kimataifa

Mjumbe wa Marekani katika Umoja wa mataifa Samantha Power amepongeza hatua hiyo akisema kuwa itaimarisha vita vya serikali ya Nigeria dhidi ya Kundi hilo, ambalo limetikisa jamii ya kimataifa mwezi uliopita kwa kuwateka zaidi ya wasichana mia mbili wa shule.
Kwa upande wake mjumbe wa Australia katika baraza hilo balozi Gary Quinlan amesema kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa Boko Haram wamepewa mafunzo na kundi la Al Qaeda hasa namna ya kujitengenezea mabomu, mtindo ambao umekuwa mbinu mpya zaidi ya ugaidi.

Abubakar Shekau wa Boko Haram
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau amenukuliwa katika mtandao akitoa matamshi ya kuunga mkono AL Qaeda nchiuni Afghanistan, Yemen na Somalia.

Magaidi wanaojulikana

Kabla ya kujumuishwa Boko Haram katika orodha ya Al Qaeda, kulikuweko makundi 62 kote duniani waliowekewa vikwazo kuhusika na Ugaidi, na watu binafsi 162, ambao wamewekewa vikwazo vya usafiri na mali zao kutwaliwa.

Wamesababisha maafa

Shughuli za Boko Haram katika miaka 5 iliyopita zimesababisha vifo vya maelfu ya waislamu na wakristu wakiwemo watu 1500 waliouawa mwaka huu pekee.
Jina la Boko Haram lina maanisha masomo ya magharibi ni Haram na kundi hilo limetumia nembo hiyo kuendeleza mashambulio yao na chuki dhidi ya chochote kinachhusishwa na nchi za magharibi.

Posted By Unknown21:15

TAHADHARI YA PSPF KUHUSU UJUMBE WA KITAPELI

Filled under:

                                                



                                                 MFUKO WA PENSHENI WA PSPF

TAARIFA KWA UMMA

Mfuko wa Pensheni wa PSPF unapenda kuwataarifu wananchi wote kuwa, hivi karibuni kumekuwa na watu au kikundi cha watu wanaosambaza taarifa potofu kwa wanachama wa PSPF kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kwa nia ya kuwatapeli.

Taarifa hizo zinazotolewa siyo sahihi na PSPF inawaomba wanachama wake kuchukua tahadhari dhidi ya
ujumbe huo wa kupotosha unaosambazwa kwa njia ya simu na watu au kikundi cha watu wakidai kuwa ujumbe huo unatoka PSPF.

PSPF inatoa huduma mbalimbali kwa wanachama wake bila sharti lolote wala malipo ya namna yoyote. Ujumbe wowote unaomtaka mwanachama kutuma fedha kwa ajili ya kulipia huduma yoyote inayotolewa na Mfuko siyo sahihi na ujumbe wa namna hiyo hautolewi na PSPF. Hivyo, ninawaomba wanachama wa PSPF kuwa makini na ujumbe huo unaosambazwa na watu wachache ambao wanataka kuuchafua Mfuko na kujinufaisha kwa njia zisizo halali.

Iwapo itatokea mwanachama amepata ujumbe wenye utata, tafadhali piga simu katika Kituo cha Huduma kwa Wateja wa PSPF kwa kutumia namba 022 5510400 au fika katika ofisi ya PSPF iliyopo karibu nawe au toa taarifa kituo chochote cha polisi kilicho karibu nawe kwa hatua stahiki.

Taarifa hii imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mfuko wa Pensheni wa PSPF,
Makao Makuu, Golden Jubilee Towers, S. L. P. 4843, Dar-es-Salaam.

Simu: +255222120912/52 au +255222127375 /6
Nukushi: +255222120930
Barua pepe: pspf@pspf-tz.org
Tovuti: www.pspf-tz.org
www.facebook.com/PSPFTanzania
@Pspf_Tanzania

Posted By Unknown04:25

WAZIRI AJIUWA BAADA YA KUSHINDWA UCHAGUZI MALAWI

Filled under:

Naibu waziri wa serikali za mitaa wa Malawi amejipiga risasi na kujiua nyumbani kwake mjini Lilongwe.

Godfrey Kamanya alikuwa anayegombea kutetea kiti chake cha ubunge katika jimbo la Nzonzi Kusini amejiua alfajiri ya leo katika mojawapo ya vyumba vya nyumba yake iliyopo Area Ten mjini Lilongwe.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali kuu ya Kamuzu mjini humo, na jeshi la polisi litatoa taarifa rasmi ya kifo hicho baada kukamilisha uchunguzi.

Haijajulikana sababu za Kamanya kujiua japokuwa ameacha barua ya maelezo ambayo polisi wataitoa baadae.

Matokeo ya kura bado hayajatangazwa rasmi katika kile kinachosemekana kuwa uchaguzi wenye ushindani mkali sana.

Afisa mkuu wa uchaguzi, amesema kuwa mfumo wa elektroniki umeharibika na maafisa wanatumia matokeo kwa njia ya barua pepe.

Posted By Unknown04:11

Tuesday 20 May 2014

UNDP JOBS OPPORTUNITIES FOR TANZANIANS

Filled under:



A program is about to start in Tanzania, funded by Bill Merinda Gate Foundation, for transformation of the agricultural industry.
Someone says they have failed to find qualified Tanzanians to fill the positions indicated below so they have to recruit from a neighboring country. Please prove them otherwise.
Though it may seem closed, UNDP will still welcome good candidates. Please write to Ernest Salla at ernest.salla@undp.org when applying to any of the following job openings:
  1. Director of Agricultural Productivity: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45669
  2. Director of Performance Analytics and Evaluation: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45659
  3. Manager of Market Efficiencies: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45670
  4. Manager of Planning and Budget: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45673
  5. Manager of Production Monitoring: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45672
  6. Senior Analyst: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45674
  7. Communications Analyst: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=41731
  8. Analyst: http://jobs.undp.org/cj_view_job.cfm?cur_job_id=45675

Posted By Unknown10:08

UTATA WABAINISHWA KUHUSU KIFO CHA MENEJA WA EWURA

Filled under:

Wakati kukiwa na utata wa kifo cha Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imebainika kuwa tofauti ya takwimu kati ya mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyotolewa kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ni Sh25 bilioni.

Meneja huyo, Julius Gashaza alikuwa akihudhuria kikao kilichokuwa kikijadili tofauti hiyo bungeni Dodoma na baadaye aliporudi Dar es Salaam akakutwa amejinyonga hotelini huku ikielezwa kuwa alirudi akiwa amejawa hofu na kukosa amani.

Vyanzo vyetu ndani ya kamati hiyo vimeeleza kuwa tofauti iliyobainika katika hesabu za taasisi hizo za Serikali ni lita 11,755,161, ambazo zingeuzwa kwa bei ya sasa ya petroli mkoani Dar es Salaam ya Sh2,200 zingepatikana Sh25.86 bilioni.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, takwimu za TRA zinaonyesha kuwa kati ya Julai 2013 hadi Machi mwaka huu, kiasi cha mafuta kilichoingizwa nchini kilikuwa lita 2,189,240,000 wakati Ewura ilionyesha ni lita 2,177,484,839.

Hata hivyo, baada ya utata huo na Kamati ya Bajeti chini ya Andrew Chenge kuitaka Serikali itoe ufafanuzi wa tofauti hizo, Serikali iliwasilisha taarifa yake Jumapili ikisema takwimu zote ni sawa.

Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema uhakiki wa takwimu hizo ulibaini kuwa zote zilikuwa ‘sahihi’ na kwamba tofauti iliyopo inatokana na upimaji wa mafuta.

Nchemba alikaririwa akisema TRA hupima mafuta kwenye meli mara inapoingia na kukadiria kodi wakati Ewura hupima mafuta yanapopokewa kwenye matanki.

“Kwa kuwa wakati mwingine meli hutumia muda mrefu tangu zinapoingia hadi zinapoteremsha mafuta, sehemu ya mafuta ambayo TRA huhesabu kama yameingizwa katika mwezi mmoja wakati Ewura hupata takwimu za kiasi cha baadhi ya mafuta hayo katika mwezi unaofuata na hiyo ndiyo iliyosababisha kuwapo kwa tofauti hiyo ambayo hata hivyo ni ndogo.”

Kulingana na takwimu hizo, kiasi cha mafuta kilichoonyeshwa na TRA kilikuwa juu kuliko kile kilichoonyeshwa na Ewura na haijajulikana iwapo kutofautiana huko kwa takwimu kuliifanya Serikali kumweka kitimoto Gashaza.

Alikuwa na hofu
Sintofahamu imeendelea kugubika kifo cha Gashaza na sasa imeelezwa kuwa alirudi kutoka Dodoma akiwa amejawa hofu na kukosa amani.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema jana kuwa ingawa hakuzungumza na Gashaza baada ya kurudi kutoka Dodoma, taarifa za polisi na kutoka kwa mkewe zinaeleza kuwa alirudi akiwa na hofu na ndiyo sababu ya kuondoka nyumbani kwake na kwenda kulala hotelini.

“Tumepata mshtuko mkubwa kuhusu msiba huu. Ndiyo maana tunataka kujua alikuwa na hofu ya nini na kwa nini. Kama alitishiwa maisha ni watu gani walimtishia maisha. Ndiyo majibu tunayoyataka kutoka kwa wanausalama,” alisema Ngamlagosi.

Mkurugenzi huyo alisema si kweli kuwa marehemu Gashaza alikwenda bungeni kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti, bali alikwenda kuhudhuria mkutano wa kawaida ambao haukuwa ukihusisha Ewura na tuhuma zozote.

“Gashaza alikwenda kuniwakilisha, hakwenda kwa minajili ya kuhojiwa, Ewura iliitwa kushiriki mkutano wa kawaida, ambao ni miongoni mwa taratibu za kawaida za kazi,” alisema.

Ngamlagosi alisema kifo cha Gashaza bado ni kitendawili kikubwa ambacho kinaweza kufumbuliwa na watu wa usalama pekee, kwa kuwa meneja huyo alikuwa mwadilifu na tegemeo kubwa kwa mamlaka hiyo.

“Tunamfahamu kama mtu ambaye si mwepesi kurubuniwa kwa lolote lile, hakuwahi kukumbwa na kashfa yoyote ile tangu aanze kazi hapa mwaka 2007,” alisema na kuongeza:

“Ameleta mabadiliko makubwa kwenye mamlaka. Mpaka sasa hatujui nini au nani amemkwaza.”

Alisema Gashaza alikuwa mwadilifu kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa alikuwa akifanya kazi kwenye kitengo nyeti cha ukaguzi wa mafuta ambako majukumu yake makuu yalikuwa ni kuangalia ubora, miundombinu, biashara, bei na ununuzi wa mafuta, kusimamia uingizwaji wa mafuta nchini, utoaji wa leseni na kuangalia jinsi wafanyabiashara wanavyofanya kazi.

Mhudumu wa gesti
Mhudumu wa gesti ya Mwanga Lodge ambayo Gashanza alipanga kabla ya mauti kumkuta, Ngina Riwa alisema mteja wake huyo alifika Jumamosi saa 3:00 usiku na kupanga chumba namba 113.

Alisema baada ya muda mfupi walifika watu watatu, wanawake wawili na mwanamume mmoja na kuonana na mteja wao na baada ya kushauriana kidogo wakaingia naye chumbani.

“Huko chumbani hawakukaa sana na haikuzidi hata nusu saa na baadaye yule mteja akatoka nao kuwasindikiza. Hakufika mbali, akarudi tena na kuingia chumbani.

Riwa alisema wakati mteja wake anaingia chumbani kulala ilikuwa takribani saa nne usiku na hakutoka tena.

Alibainisha kuwa asubuhi kati ya saa 12:30 na 1:00 asubuhi alikuja tena yule rafiki yake mwanamume kumulizia mteja wake kama alikuwa ameamka.

“Alikwenda kumgongea lakini hakufungua, akarudi kwangu tukaenda naye tukagonga hakufungua, ndipo tukashirikiana na mlinzi kufungua dirisha kwa nje na kumwona akiwa amelala chini.

“Tukawapigia simu polisi kutoka Kituo cha Ali Mboa ambao hawakuchukua muda wakaja. Baadaye wakaja polisi wenye vyeo vya juu wakapimapima wakaondoka na mlinzi na bosi wetu kama saa tatu asubuhi hivi,” alisema mhudumu huyo.

Uchunguzi wa polisi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engbert Kiondo alisema uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho unaendelea kwa kuangalia maeneo matatu.

Alisema utajielekeza kubaini kama kulikuwa na mgogoro wowote wa kifamilia au iwapo alikuwa na tatizo lolote kazini kwake kabla ya kifo chake na mazingira kilipotokea kifo hicho na baada ya kujiridhisha watatoa taarifa kamili kwa vyombo vya habari.

“Kuna maswali mengi ya kujiuliza kwa nini hakutaka kulala nyumbani kwake usiku ule badala yake akaamua kulala hotelini, tunafanya upelelezi kubaini nini hasa kilimsukuma kujinyonga,” alisema.

Alisema pia wanasubiri ripoti ya uchunguzi ya daktari ambayo wataitumia katika upelelezi wao kubaini chanzo.

Alisema polisi watachunguza kama Gashaza alijinyonga kweli au aliuawa na kutengenezewa mazingira ya kujinyonga.

Ampigia simu rafiki yake
Kiondo alisema Gashaza alipofika katika nyumba ya kulala wageni, alimpigia simu rafiki yake wa karibu anayeitwa Sibitwango na kumweleza kuwa mambo yamekuwa magumu na hakujisikia vizuri.

Usiku huo, Kiondo alisema Sibitwango pamoja na mke wa marehemu Judith walimfuata katika hoteli aliyofikia na kumsihi arudi nyumbani akapumzike lakini yeye (Gashaza) alisisitiza kulala hapo kwa sababu tayari alikuwa ameshalipia chumba hicho.

Kiondo alieleza kuwa siku iliyofuata Sibitwango mwenyewe ndiye aliyetoa taarifa polisi na kueleza mazungumzo yao kabla ya kifo.

Utata bungeni
Wakati inaelezwa kuwa kulikuwa na tofauti ya takwimu kati ya zile za TRA na Ewura kuhusu kiwango cha mafuta kilichoingia kwenye soko, taarifa zaidi zimeeleza kuwa katika kikao cha Kamati ya Bajeti, Gashaza hakuulizwa swali hata moja.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema marehemu hakuhojiwa labda kilichomfanya ajiue ni hofu iliyotokana na mahojiano baina ya kamati hiyo na watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Alisema kamati hiyo iliwaita viongozi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini ili kuwahoji kwa nini Sh50 zilizoongezwa katika mafuta ya petroli na dizeli hazikwenda Rea?

Mjumbe huyo alisema kati ya zaidi ya Sh100 bilioni zilizotakiwa kwenda Rea ni Sh17 bilioni tu zilizopelekwa na fedha nyingine zilielekezwa kwenye matumizi mengine ambayo hayakuidhinishwa na Bunge.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Sharon Sauwa na Fidelis Butahe, Florence Majani, Nuzulack Dausen na Peter Elias via gazeti la MWANANCHI

Posted By Unknown09:50

MILIPUKO MIWILI YATOKEA KATIKA SOKO

Filled under:

Milipuko hiyo imetokea katika soko ambalo lina shughuli nyingi na ambalo lilikuwa na msongamano wa watu eneo la Kati mwa Nigeria.

Mwandishi wa BBC Ishaq Khalid aliye mjini humo anasema kuwa kuna hofu ya watu wengi kujeruhiwa hasa kwa kuwa soko hilo lilikuwa na idadi kubwa ya watu.

Haijulikani kilichosababisha milipuko hiyo mjini Jos, mji ambao umeshuhudia mashambulizi makali kati ya wakristo na waisilamu.

Kundi la Boko Haram, pia limekuwa likifanya mashambulizi katika mji huo.

Posted By Unknown09:33

Tuesday 6 May 2014

KAMPUNI YA COCA-COLA YAAMUA KUONDOA KIUNGO TATANISHI KATIKA VINYWAJI VYAKE

Filled under:

Bidhaa ya BVO tayari imeondolewa katika Kinywaji cha Powerade chenye ladha tofauto tofauti

Kampuni kubwa zaidi ya vinywaji duniani Coca-Cola, inapanga kuondoa kiungo tatanishi katika baadhi ya vinywaji vyake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Hii ni kufuatia shinikizo kutoka kwa wateja wa vinywaji hivyo nchini Marekani waliotia saini ujumbe wa kusihinikiza kampuni hio kuondoa kiungo hicho kupitia kwenye matandao. 

Kiungo hicho ni kemikali yenye mafuta ya kupikia iitwayo (Brominated vegetable oil au BVO) inayopatikana katika vinywaji kama Fanta na Powerade kinywaji cha kuongeza mwili nguvu.
Kampuni hasimu ya vinywaji Pepsi iliondoa viungo hivyo vya kemikali kutoka katika kinywaji chake kijulikanacho kama Gatorade mwaka jana.

Nchini Japan na katika muungano wa Ulaya kiungo cha BVO hakiruhusiwi kuongezwa katika vyakula au vinywaji.
Je nini umuhimu wa kiungo cha BVO?

Kampuni ya Coke hukitumia ili kuzuia viungo vingine vilivyo katika vinywaji hivyo kuachana.
Lakini watafiti wanasema kuwa kiungo hicho kinaweza kusababisha mtu kuwa msahaulifu ,kupata maradhi ya ngozi na matatizo ya Neva za mwili.

Hata hivyo msemaji wa kampuni ya Coke Josh Gold amesema kuwa hatua ya kuondoa kiung hicho sio kutokana na tisho la kiafya kwani vinywaji vyake vyenye kiungo cha BVO viko salama na daima vimekuwa salama.

Kampuni hiyo imesema kuwa kiungo cha BVO hakitumiki sana katika nchi nyingi lakini kitaondolewa katika bidhaa zake zinazouzwa nchini Canada na Marekani ya Kusini.
Hatua ya Coke imetokana na shinikizo za watu na wadadisi wanasema kuwa ni funzo kwa kampuni nyingine kuanza kuhakikisha usalama wa bidhaa za o kiafya.

Kampeini hiyo ilianzishwa na kijana mmoja anayeishi katika jimbo la Mississippi, aliyehoji kwa nini Coke inatyumia kiungo hicho katika vinywaji vinavyotumiwa na wanariadha.


Posted By Unknown11:04

HOTUBA YA WAZIRI MKUU MZENGO PINDA YA MAKADIRIO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA BUNGE 2014/15

Filled under:

HOTUBA  YA  WAZIRI  MKUU,  MHESHIMIWA 
MIZENGO  PETER  PINDA (MB),  KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2014/2015


UTANGULIZI

1.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kutokana na Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa Mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.

2.            Mheshimiwa Spika, awali ya yote na kwa masikitiko makubwa
 naomba  nichukue  fursa  hii kutoa salamu za pole  kwako  na kwa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01 Januari, 2014 na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze, ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape pole Wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa Wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa kifo cha Mheshimiwa Anna Magowa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe 24 Septemba 2013. Vilevile, natoa pole kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa kifo cha Mheshimiwa Moshi Mussa Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, aliyefariki tarehe 21 Aprili 2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa Wabunge na  Wananchi  wote  waliofiwa  na ndugu na jamaa zao kutokana na majanga na matukio mbalimbali tangu  nilipowasilisha  Bajeti  yangu  ya  mwaka  2013/2014.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina! Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga mbalimbali yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati wote waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.

3.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014, Bunge lako Tukufu limepata Wabunge wapya watatu ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha Wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaomba watumie fursa waliyoipata kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

MAANDALIZI YA BAJETI

4.            Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili tangu tuanze utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti ambao unatuwezesha kukamilisha Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka.  Taarifa za awali zinabaini kwamba utaratibu huu umeanza kuonesha mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa kazizilizopangwa. Bajeti hii imeendelea kutayarishwa kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi   ya   Chama   Cha   Mapinduzi  ya  mwaka  2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN). Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kipaumbele  iliyoainishwa  kwenye  mipango  hiyo  ya  Kitaifa ili kuleta maendeleo endelevu na ya haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa Tanzania.

5.            Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi waliyoifanya ni kubwa na ambayo imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha leo. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.

HALI YA SIASA

6.            Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya siasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu  yao. Nchi  yetu inapitia kwenye kipindi cha mpito ambapo tunaandika Katiba Mpya itakayoweka mustakabali wa  mwelekeo wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo ambayo baadaye wananchi wote wataipigia kura ya maoni.  Nawaomba tushindane kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu katika kuandaa Katiba hii ambayo itatuongoza sasa na vizazi vijavyo.

7.            Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi Nchini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa Nchini. Hadi Aprili 2014, idadi ya Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa kudumu imefikia 21 baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013. Aidha, Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-TANZANIA), Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) vimepata usajili wa muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi na Wanachama wa vyama vyote vya siasa kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kutohamasisha siasa za chuki na vurugu ambazo zinaweza kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa Taifa letu tulioujenga kwa miaka mingi.

ULINZI NA USALAMA


8.            Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kudumisha amani na utulivu kama tunu ya Taifa iliyojengwa na kuimarishwa tangu tulipopata uhuru. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza Uhalifu ambavyo vimeongeza ushirikiano na wananchi. Jeshi hilo limeongeza Vikundi 1,778 vya Ulinzi Shirikishi na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa Nchi nzima. Vikundi hivyo vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini kutoka Asilimia 4.3 mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo kuchangia kupungua kwa makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa 566,702 mwaka 2012 hadi makosa 560,451 mwaka 2013.

Mauaji ya Wanawake

9.            Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, hivi karibuni kumetokea wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane (8) wameuawa kikatili katika Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na Nyegina Wilayani Butiama. Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji hayo yamefanyika mchana na kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga au kamba na miili yao kufukiwa kwenye mashimo mafupi au kufichwa vichakani. Mara zote walengwa ni wanawake wanapokuwa kwenye shughuli zao za kilimo.

10.         Mheshimiwa Spika, Serikali inalaani vitendo hivyo visivyokubalika katika jamii na itawachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote. Serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya mauaji ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13 wamefikishwa mahakamani.  Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi kazi kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii kuhusu kuanzisha na kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe wito kwa wananchi wema, wenye upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye vyombo vya usalama ili Sheria ichukue mkondo wake.

Ajali za Barabarani

11.         Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani zimeendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu na mali zao. Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa katika mwaka 2013, kulitokea ajali za barabarani 24,480 zilizosababisha vifo vya watu 4,091 na majeruhi 21,536 ikilinganishwa na  ajali 23,604 zilizosababisha vifo vya watu 4,062 na majeruhi 20,037 mwaka 2012.  Kwa upande wa pikipiki pekee, mwaka 2012 zilitokea jumla ya ajali 5,763 na kusababisha vifo 930 na majeruhi 5,532.  Mwaka 2013, zilitokea ajali 6,831 na kusababisha vifo 1,098 na majeruhi 6,578. Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2014 zimetokea ajali 1,449 na kusababisha vifo 218 na majeruhi 1,304. Ajali hizi ni nyingi na zinasababisha vifo vingi na majeruhi ambao wengi wao ni nguvukazi ya Taifa. Ni vyema ikumbukwe kwamba, Serikali iliruhusu matumizi ya pikipiki kwa nia njema ya kupunguza matatizo ya usafiri hususan maeneo ya Vijijini. Hata hivyo, fursa hiyo imeambatana na changamoto ya ajali nyingi barabarani. Hivyo ni wajibu wa madereva wote kuzingatia sheria za barabarani na kukidhi vigezo vyote vya kuwa na vibali halali vya kufanya biashara hizo pamoja na leseni za udereva. SUMATRA, Jeshi la Polisi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Mamlaka nyingine zinazohusika zinatakiwa kukaa pamoja ili kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Kanuni za Leseni za Usafirishaji wa Pikipiki na Bajaji za mwaka 2010zinatekelezwa ipasavyo.

Hali ya Mipaka ya Nchi

12.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutimiza majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi yetu na raia wake. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewezesha Wanajeshi wetu kupata mafunzo mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya Nchi pamoja na kushiriki katika mazoezi ya ushirikiano kikanda. Aidha, Jeshi limeshiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa huko Darfur (Sudan), Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini. Nafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi limefanya kazi kubwa, nzuri na kwa weledi mkubwa, nidhamu na kujituma hivyo kuendelea kuipatia heshima kubwa Nchi yetu. Katika jitihada za kuwapatia Askari mazingira mazuri ya kuishi, Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za Askari ambapo ujenzi wa majengo 191 kati ya 6,064 unaendelea katika vikosi mbalimbali vya Jeshi Nchini.

Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa

13.         Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 ni wa tatu tangu Serikali iliporejesha utaratibu wa kuwachukua Vijana wanaohitimu kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria. Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, jumla ya Vijana 15,167 wamehitimu mafunzo ya JKT wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili Tukufu. Mafunzo hayo yamewapatia vijana hao fursa ya kujifunza juu ya Ulinzi, Usalama na Ukakamavu, Uzalishaji mali, Uzalendo na Umoja wa Kitaifa. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itachukua vijana zaidi kujiunga na JKT kwa Mujibu wa Sheria. 

SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi

14.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na kuendesha chaguzi ndogo za Wabunge katika Majimbo matatu na Udiwani katika Kata 53 nchini. Chaguzi hizo zimefanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vifo na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani kukosa sifa za kuendelea na nyadhifa hizo. Katika Uchaguzi wa Ubunge uliofanyika katika Jimbo la Chambani - Zanzibar, CUF ilishinda kwa kupata Asilimia 84 ya kura zote. CCM ilipata kura Asilimia 12.4, ADC ilipata kura Asilimia 3.5 na CHADEMA ilipata Asilimia 0.4 ya kura zote. Katika Jimbo la Kalenga – Iringa, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 79.3 ya kura, CHADEMA ilipata kura Asilimia 20.2 na CHAUSTA ilipata kura Asilimia 0.5. Katika Jimbo la Chalinze – Pwani, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 86.61, CHADEMA ilipata kura Asilimia 10.58, CUF ilipata kura Asilimia 1.98, AFP ilipata kura Asilimia 0.59 na NRA ilipata Asilimia 0.25 ya kura zote. Aidha, katika Chaguzi za Madiwani zilizofanyika katika Kata 53, CCM ilishinda viti 40, CHADEMA viti 12 na NCCR – Mageuzi kiti kimoja (1).

15.         Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Katika awamu hii ya uboreshaji wa Daftari, Mfumo wa Biometric Voter Registration utatumika tofauti na Mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji. Mfumo huu wa kisasa unawezesha uandikishaji na uchukuaji wa alama za vidole kwa haraka zaidi na hatimaye mwananchi kupatiwa kitambulisho cha kupiga kura kwa muda mfupi. Hii itasaidia sana kuokoa muda na kupata takwimu sahihi za wapiga kura watakaoshiriki kwenye chaguzi.

16.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa kuhamasisha Wanachama na Watanzania wote wenye sifa kujiandikisha kwenye Daftari hilo na kupata kitambulisho halali cha mpiga kura pale zoezi hilo litakapoanza rasmi.  Aidha, ninatoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa kujitokeza kujiandikisha. Ni imani yangu kwamba tukitumia fursa hii kikamilifu tutaondoa malalamiko ya majina ya baadhi ya wapiga kura kutokuwepo kwenye orodha wakati wa chaguzi.  Ni muhimu tukumbuke kwamba ni wananchi wenye sifa tu ndiyo watakaoandikishwa. Katika mwaka 2014/2015, Tume itakamilisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kusimamia Kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Mpya, na kuendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa Wananchi.

Bunge

17.         Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai, 2013 hadi Aprili 2014, Ofisi ya Bunge imeendesha Mikutano Mitatu ya Bunge na Mikutano mitatu ya Kamati za Bunge. Maswali ya Msingi 410 pamoja na maswali 73 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa.  Aidha, Miswada minane (8) ya Sheria ilipitishwa na Bunge. Pia, Bunge limekamilisha ukarabati wa Ukumbi wa Bunge na Miundombinu yake kuwezesha Mkutano wa Bunge la Katiba kufanyika na ujenzi wa Ofisi za Wabunge Majimboni umeendelea kufanyika. Vilevile, Ofisi ya Bunge imewajengea uwezo Wabunge na Watumishi wake kupitia semina mbalimbali katika masuala ya Utawala Bora. Katika mwaka 2014/2015, Ofisi ya Bunge itaendelea kuratibu Mikutano ya Bunge, Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kuimarisha miundombinu na majengo ya Bunge.

Muungano

18.         Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili 2014, tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi.  Tumeweza kufika hapa tulipo kutokana na misingi imara ya Muungano iliyowekwa na Waasisi wetu na kuendelezwa na Viongozi walioongoza Taifa letu katika awamu zilizofuatia. Tunajivunia kwamba Muungano wa Tanzania umejengeka kwenye historia ya muda mrefu ya ushirikiano wa watu wa pande hizi mbili. Jamii hizi zina uhusiano wa damu, kifikra na mapambano ya pamoja dhidi ya wakoloni waliotawala kwa vipindi tofauti. Walichofanya waasisi wetu mwaka 1964 ni kurasimisha ushirikiano wetu wa muda mrefu. Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano. Aidha, ninawashukuru kwa dhati Viongozi wote walioongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar tangu kuasisiwa kwa Muungano. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Uongozi wao ambao umezifanya pande mbili za Muungano kuwa karibu zaidi.

19.         Mheshimiwa Spika, tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano tukiwa na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.  Takwimu hizo zinaweka jambo moja wazi kwa Muungano wetu; kwamba zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania  wote wamezaliwa baada ya Muungano.  Hivyo, tuliozaliwa kabla ya Muungano ni chini ya asilimia kumi.  Kwa mujibu wa takwimu hizo, Tanzania nzima ina watu 44,926,923.  Kati yao, watu 40,640,425, sawa na Asilimia 90.6 ni wa umri wa siku moja hadi miaka 50.  Kwa upande wa  Tanzania  Bara, idadi  ya  watu  ilikuwa  43,625,354,  kati ya hao, watu 39,456,065 sawa na asilimia 90.5 wamezaliwa baada ya Muungano.  Kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na watu 1,303,569, ambapo watu 1,184,360 sawa na asilimia 90.9 wamezaliwa baada ya Muungano.  Takwimu hizo zina maana kwamba, asilimia 90.6 ya watu wote wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.

20.         Mheshimiwa Spika, tuna kila sababu ya kuadhimisha Miaka hii 50 ya Muungano kwa furaha.  Katika maadhimisho ya mwaka huu, tuliandaa maonesho maalum, makongamano na shughuli nyingine ambazo zilisaidia wananchi kuelimishwa kuhusu masuala ya Muungano. Aidha, kimeandaliwa kitabu maalum kinachoelezea historia, utekelezaji wa mambo ya Muungano, mafanikio, changamoto, fursa na matarajio ya Muungano kwa miaka ijayo.  Kitabu hicho kitatumika kama rejea kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.

21.         Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwa nguvu zote tukiwa na uelewa kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita Watanzania wameishi kwa amani na kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo wakiwa upande wowote wa Muungano. Tunatambua changamoto zilizopo na tumeweka utaratibu mzuri wa vikao ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo. Vikao hivyo vitaendelea kufanyika katika ngazi ya wataalam, Watendaji Wakuu na Viongozi wa Kitaifa. Ni imani yangu kwamba, Muungano huu utaendelea kudumu na watu watapata maendeleo makubwa kwani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina fursa nyingi zinazoweza kutumika kwa manufaa ya wote.  Sote tukumbuke kuwa, UTANZANIA WETU NI MUUNGANO WETU, TUULINDE, TUUIMARISHE NA KUUDUMISHA!

Mabadiliko ya Katiba

22.         Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba 2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikamilisha Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuikabidhi kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Napenda kuishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu hiyo imeliwezesha Bunge Maalum la Katiba kuanza mjadala. Nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania wote kwa kutoa maoni yaliyowezesha Tume kuandaa Rasimu hiyo ya Katiba.


23.         Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la Katiba linaundwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201 walioteuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa kupata fursa hii ya kuwawakilisha Watanzania katika kuandaa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Ni dhahiri kuwa dhamana hii ni kubwa sana!

24.         Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la Katiba lilianza kazi rasmi tarehe 18 Februari, 2014 kwa kumchagua Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kulisimamia Bunge Maalum hadi kuwezesha kupatikana kwa Kanuni za kuliongoza Bunge hilo. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa Samwel John Sitta kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba. Nampongeza Katibu wa Bunge la Katiba Bwana Yahaya Hamadi Khamis na Naibu wake Dkt. Thomas Kashililah pamoja na Wajumbe wote waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati 12 za Bunge Maalum. Baada ya kukutana kwa muda wa siku 67, Bunge Maalum limeahirisha Mkutano wake tarehe 25 Aprili, 2014 ili kupisha majadiliano ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015. Ni matumaini yangu kwamba, Bunge Maalum la Katiba litakaporejea litakamilisha kazi hiyo kwa umakini na kupata Rasimu ambayo hatimaye itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.

Vitambulisho vya Taifa

25.         Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2013/2014 nilielezea dhamira ya Serikali ya kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa Wananchi wake. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imekamilisha usajili na utambuzi wa watu kwa upande wa Zanzibar, Watumishi wa Umma na vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa vituo vya kuingiza na kuhakiki taarifa, kituo cha kutengeneza Vitambulisho na kuhifadhi kumbukumbu pamoja na kituo cha uokozi na majanga ya taarifa na takwimu. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea  na zoezi la Utambuzi na Usajili wa Watanzania katika Mikoa mingine ili kwa pamoja tuweze kunufaika na Vitambulisho vya Taifa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kiusalama.

Sensa ya Watu na Makazi

26.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea kutoa machapisho mbalimbali ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Machapisho hayo yanajumuisha Taarifa ya Mgawanyo wa Watu kwa Maeneo ya Utawala; Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia na Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi. Taarifa hizo zimebaini kuwa, katika miaka kumi iliyopita kumetokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika kimeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi asilimia 78 mwaka 2012. Aidha, uandikishaji halisi katika shule za msingi umeongezeka kutoka  asilimia 69 mwaka 2002 hadi 77 mwaka 2012. Idadi ya watu wanaoishi kwenye nyumba zenye kuta imara ni asilimia 74 na asilimia 65.4 wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa bati. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo,


hali ya utegemezi nchini ni kubwa kutokana na ukweli kuwa kati ya Watanzania Milioni 44.9, Asilimia 50.1 ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Aidha, takwimu zimebainisha kuwa Asilimia 7.7 ya Watanzania ni watoto yatima. Kutokana na hali hiyo, ni jukumu letu kama Taifa kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo katika sekta za huduma za jamii ili hatimaye kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie ipasavyo katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu.

MASUALA YA UCHUMI

Hali ya Uchumi

27.         Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa katika mwaka 2013 lilikua kwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 mwaka 2012. Ongezeko hilo limetokana na ukuaji mzuri wa shughuli za huduma za mawasiliano, viwanda, ujenzi na huduma za fedha. Kutokana na ongezeko hilo, wastani wa Pato la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi 1,025,038 mwaka 2012 hadi Shilingi 1,186,424 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 15.7. Mfumuko wa Bei umepungua kutoka Asilimia 9.8 Machi 2013 hadi Asilimia 6.1 Machi 2014. Kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya kupanda bei za bidhaa na vyakula hasa mahindi, mchele na aina nyingine ya nafaka.

28.          Mheshimiwa Spika, pamoja na uchumi wetu kukua kwa kasi ya asilimia 7.0 kwa mwaka 2013 na Pato la Mtanzania kuongezeka, kiwango hicho siyo kikubwa sana kuwezesha umaskini wa wananchi kupungua kwa kasi.  Utafiti wa kitaalam unaonesha kwamba, ili umaskini upungue kwa kasi kubwa, uchumi unatakiwa kukua kwa zaidi ya Asilimia 8 kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.  Ukuaji huo pia unatakiwa kulenga Sekta ambazo zinagusa maisha ya watu wengi, hususan kilimo, mifugo na uvuvi. Mwelekeo wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua kwa kushirikisha Sekta Binafsi.

Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano

29.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016 ambao unatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitekeleza Mpango huo kupitia Kauli mbiu ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Msingi wa kauli mbiu hii ni kuainisha maeneo  machache  ya  kimkakati  na  kuyatengea  rasilimali za kutosha, kusimamia na kufuatilia utekelezaji kwa karibu zaidi. Chombo maalum cha Ufuatiliaji wa Utekelezaji  wa  Miradi  ya  kimkakati   chini  ya  Ofisi ya Rais kinachojulikana kama President’s Delivery Bureau – (PDB) kimeanzishwa na Watendaji Wakuu wameteuliwa. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, matunda ya utekelezaji wa Mfumo huo yameanza kuonekana katika maeneo makuu sita ya kipaumbele kitaifa ambayo ni Nishati ya Umeme, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato.  Utekelezaji wa miradi hiyo na mafanikio yaliyoanza kupatikana yatatolewa maelezo na Mawaziri katika Sekta husika.

Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji

30.         Mheshimiwa Spika, njia ya uhakika ya kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi imara na wa kisasa utakaohimili ushindani katika masoko ya Kikanda na Kimataifa ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Katika kufikia azma hiyo, tarehe 31 Januari, 2014 nilizindua rasmi Taarifa ya Tathmini ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji Tanzania. Mapendekezo ya Taarifa hiyo yatatumika kuihuisha Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997. Aidha, ili kuwawezesha Wawekezaji na Wafanyabiashara kupata huduma  na taarifa zote muhimu kama vile Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali kuhusu biashara na uwekezaji kwa njia ya mtandao, Serikali imezindua upya Tovuti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania.  Kupitia Tovuti hii, Wawekezaji popote  duniani  wanaweza  kupata  taarifa kuhusu usajili wa  Kampuni  na  viwango  vya  kodi  kwa  njia  ya mtandao.

Dhamira ya Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza gharama za kufanya biashara nchini ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka nchi nyingine zilizotekeleza maboresho ya mifumo yao ya udhibiti wa biashara.

31.          Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi inaendelea kupewa nafasi kubwa katika kukuza uchumi Nchini. Takwimu zinaonesha kwamba, Miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania imeongezeka kutoka 869 yenye thamani  ya Shilingi Bilioni 31.5 mwaka 2012 hadi miradi 885  yenye  thamani  ya  Shilingi  Bilioni 141.2 mwaka 2013.
Napenda pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Nchi nyingi duniani zinaendelea kuiamini Tanzania kama Kituo maarufu cha uwekezaji Duniani. Mwezi Novemba, 2011 nilizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza unaojulikana kama Partnership in Prosperity. Mpango huo umelenga kuongeza uwekezaji kutoka Sekta Binafsi ya Uingereza kwenye mafuta na gesi, kilimo na Nishati jadidifu. Lengo ni kuongeza uwekezaji kutoka Nchi hiyo kwa zaidi ya maradufu ya kiwango cha sasa. Aidha, tumekubaliana kushirikiana kuimarisha mazingira ya biashara ili kurahisisha uwekezaji katika sekta hizo.

32.          Mheshimiwa Spika, baadhi ya Kampuni za Uingereza tayari zimeanza kutekeleza makubaliano hayo kwenye Sekta ya kilimo.  Kampuni ya Unilever kwa mfano, itawekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 275 kwenye kilimo cha chai kwa kushirikiana na wakulima wadogo. Tayari Kampuni hiyo imeanza kupanua Kiwanda cha Chai Kibwele, Mufindi na kufungua zaidi ya Hekta 300 za mashamba ya chai katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, Kampuni hiyo imeingiza nchini vipando 250,000 vya miche bora ya chai. Pia, Kampuni inaandaa zaidi ya miche milioni 2 kwa ajili ya kuwagawia wakulima wadogo Wilayani Njombe ili waongeze uzalishaji wa chai Nchini.

33.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Kituo cha Uwekezaji kimeshirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali Nchini kuratibu maandalizi ya Makongamano ya Uwekezaji yenye lengo la kuhamasisha, kukuza na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo. Jumla ya Mikoa 11 imeshiriki kikamilifu kuandaa na  kufanikisha  Makongamano  ya Uwekezaji katika maeneo yao. Mikoa hiyo  ni  Mwanza,  Mara, Kagera, Geita, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Makongamano hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo, pamoja na kuihamasisha Mikoa na Halmashauri za Wilaya ndani ya Mikoa hiyo kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Aidha, Wawekezaji wengi walioshiriki kwenye Makongamano hayo wameonesha nia na utayari wa kuwekeza kwenye Mikoa husika. Jitihada hizi zitaendelezwa katika kipindi kijacho.

Majadiliano na Sekta Binafsi

34. Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yangu ya Bajeti mwaka 2013/2014, nilieleza kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote. Mkutano huo ulifanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 1 Julai 2013, Jijini Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo ulitoa fursa ya kipekee kwa Viongozi wa Serikali kujadiliana na kupata maoni ya makundi mbalimbali ya Wananchi kuhusu mbinu za kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Serikali imedhamiria kufanya Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote kila mwaka kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa kwa kuzingatia fursa kubwa za maendeleo shirikishi zilizopo kwenye maeneo husika.

35. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Biashara lilifanya Mkutano wake wa Saba tarehe 16 Desemba 2013 chini ya Kauli Mbiu ya “Ukuaji Shirikishi wa Uchumi”. Maazimio ya Mkutano huo ni pamoja na kuunda Kamati Tatu ambazo zitashughulikia Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mazingira Wezeshi ya Biashara na Matumizi Endelevu ya Maliasili za nchi. Kamati ya Mazingira Wezeshi ya Biashara imeanza kuishauri Serikali kuhusu mikakati ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na kuongeza ushindani  wa bidhaa za Tanzania. Kazi hiyo imefanyika kwa utaratibu wa Maabara chini ya Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Utaratibu huo ulianzisha maeneo sita muhimu ambayo yakishughulikiwa yataboresha mazingira ya biashara nchini. Maeneo hayo ni kuboresha Kanuni na Taasisi zinazosimamia biashara; upatikanaji wa ardhi na haki za umiliki wake na kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupunguza wingi wa kodi  na tozo mbalimbali. Maeneo mengine ni kuzuia na kupambana na rushwa; kuboresha Sheria za Kazi na kuimarisha mafunzo na stadi za kazi pamoja na kusimamia utekelezaji wa mikataba na utawala wa sheria.  Katika mwaka 2014/2015, Baraza la Taifa la Biashara litaendelea kuratibu utekelezaji wa maazimio hayo ya Mkutano wa Saba sanjari na kusimamia mikutano ya Mabaraza ya Wilaya na Mikoa.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

36.         Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya kubuni na kutekeleza Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ni kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na rasilimali  za nchi yao badala ya kubaki kuwa watazamaji. Kwa  kutambua  umuhimu wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, katika Mwaka 2013/2014 Serikali imeanzisha Taasisi  ya  Ujasiriamali na Ushindani wa Kibiashara (Tanzania  Entrepreneurship Competitiveness Centre). Taasisi hiyo itatekeleza jukumu la kutoa miongozo ya uandaaji wa mitaala ya ujasiriamali katika ngazi tofauti na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa bora zitakazohimili ushindani. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kuongeza ufanisi wake. Hadi kufikia mwezi Februari 2013, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi ulikuwa umepokea Shilingi Bilioni 2.1 zilizotumika kudhamini mikopo ya wajasiriamali kupitia Benki ya CRDB kwa makubaliano ya kukopesha mara tatu ya dhamana ya Serikali. Kutokana na makubaliano hayo, hadi kufikia mwezi Desemba 2013, mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shillingi Bilioni 9.5 ilikuwa imetolewa kwa Wajasiriamali 9,790 waliojiunga kwenye Vikundi 283 na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 51 katika Mikoa 12 na Wilaya 27.

37.         Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Mfuko wa Kuendeleza  Wajasiriamali  Wadogo  na wa Kati, hadi kufikia Desemba 2013,  ulikuwa  umetoa  mikopo  yenye thamani ya  Shilingi  Bilioni  36.39  kwa  Wajasiriamali  62,720. Aidha, Mfuko wa  Maendeleo ya Vijana ulikuwa umetoa mikopo kwa  Vijana  yenye  thamani  ya  Shilingi  Bilioni  1.22 kupitia SACCOS 244; na Mfuko  wa  Maendeleo ya  Wanawake  ulikuwa  umetoa  mikopo  yenye  thamani  ya  Shilingi   Bilioni   5.44  kwa  Wanawake  500,000  Nchini. Vilevile, Mradi wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF) ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 57.1 kupitia Asasi 375 za Kifedha ambapo Wajasiriamali 95,034 walinufaika.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF

38. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zilizo katika Mazingira Hatarishi Tanzania Bara na Zanzibar.  Katika kutekeleza Mpango huo, utaratibu wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini ulifanyika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 22 ambapo kaya 138,032 katika Vijiji na Shehia 1,179 zilitambuliwa na kuandikishwa katika Mfumo wa Masijala wenye walengwa 464,552. Hadi sasa, Shilingi Bilioni 5.5 zimehawilishwa katika kaya hizo. Lengo ni kuziwezesha kaya hizo kupata chakula na kujiongezea fursa ya kipato.

39.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia imejenga uwezo kwa Viongozi na Wataalam kutoka maeneo ya utekelezaji wa Mpango huo. Uwezo umejengwa kwa kutoa mafunzo katika masuala ya utambuzi, uandikishaji na ukusanyaji taarifa za kaya maskini. Aidha, mafunzo ya usanifu wa miradi ya ujenzi yalitolewa kwa wataalam kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia, Wajumbe 17 wa Baraza la Wawakilishi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka Zanzibar walitembelea Vijiji vya Pongwe-Kiona na Malivundo (Bagamoyo) na Gwata (Kibaha) ili kujifunza kuhusu utekelezaji bora wa Mpango huo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kufanya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini kufikia maeneo yote 161 ya utekelezaji wa Mpango Tanzania Bara na Zanzibar. Lengo ni kutambua na kuandikisha Kaya 920,000 kutoka Vijiji, Mitaa na Shehia 9,000.

UZALISHAJI MALI

Uzalishaji wa Mazao

40.         Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa chakula ni ya kuridhisha katika maeneo mengi nchini kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa 2012/2013. Uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu huo ulikuwa Tani Milioni 14.38 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya Tani 12.15 kwa mwaka 2013/2014 ikiwa ni ziada ya Tani Milioni 2.3 za chakula. Ongezeko hilo limefanya Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 118 na hivyo, kufanya wastani wa bei za mazao ya chakula katika masoko Nchini kuwa za chini katika kipindi chote cha mwaka 2013/2014.

Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo

41.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na juhudi za kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kulingana na Mipango inayotekelezwa chini ya Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, na Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imesambaza jumla ya vocha za ruzuku 2,796,300 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 83 kwa ajili ya mbolea na mbegu bora za mpunga na mahindi kwa Kaya 932,100. Pia, Serikali ilitoa ruzuku ya dawa za korosho kiasi cha lita 158,845 na Tani 620 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5. Vilevile, ruzuku ilitolewa kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za pamba Tani 4,000 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.8, miche ya kahawa 350,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 100 na miche ya chai 1,850,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 300.

42.         Mheshimiwa Spika, ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao unategemea sana huduma bora za ugani kwa wakulima. Serikali katika mwaka 2013/2014, ilitoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani 1,452 ili kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya kuwa na Afisa Ugani wa Kilimo mmoja kwa kila kijiji. VilevileSerikali imeongezaMashamba Darasa kutoka 16,330 yenye wakulima 344,986 mwaka 2012/13 hadi 16,543 yenye wakulima 345,106 mwaka 2013/2014  ili kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima.

43.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikisha Washirika wa Maendeleo kuchangia Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Miongoni mwa malengo ya Programu hiyo ni kuwaunganisha wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa kibiashara wa Makampuni makubwa ya ndani na nje ya nchi. Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeanzisha Mfuko Chochezi wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT Catalytic Trust Fund). Mfuko huo utatoa mitaji itakayogharamia hatua za awali za miradi inayotoa tija ya haraka ambayo imebainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Uwekezaji. Vilevile, Mfuko huo utahamasisha biashara inayolenga kumuinua Mkulima mdogo kwa kumuunganisha na mnyororo wa thamani na kampuni kubwa kupitia madirisha makuu mawili. Dirisha la kwanza ni Matching Grant Fund  linalolenga kuwezesha kampuni kubwa zilizoanzisha biashara ya Kilimo Nchini, kuimarisha minyororo ya thamani inayowahusisha wakulima wadogo zaidi au kuanzisha kilimo cha Mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wadogo. Dirisha la pili ni Social Venture Capital Fund, linalolenga kuziwezesha biashara changa na za kati kwenye Sekta ya Kilimo au kuwezesha Kilimo cha mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wadogo. Tayari Bodi ya Mfuko imeteuliwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko ameajiriwa.

44.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, inategemea kuvutia uwekezaji na kuanzisha Kilimo cha mashamba makubwa 25 ya Kilimo cha kibiashara kwa mazao ya mpunga na miwa kwa utaratibu wa kuwaunganisha wakulima wakubwa na wadogo wanaozunguka mashamba hayo. Aidha, itaanzisha, itaboresha na kuendesha kitaalamu maghala 275 ya kuhifadhi mahindi kwa kuwaunganisha wakulima katika umoja wa kibiashara kwa ajili ya kupata masoko ya pamoja.


Umwagiliaji

45.         Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji Nchini, Sheria ya Umwagiliaji Namba 5 ya mwaka 2013 imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itaiwezesha Serikali kuanzisha Tume ya Umwagiliaji ambayo ni chombo cha kitaifa chenye dhamana ya kusimamia, kuendeleza na kudhibiti shughuli za Umwagiliaji Nchini. Sheria hiyo pia itaanzisha Mfuko wa Taifa wa Umwagiliaji utakaosaidia kutekeleza mipango ya umwagiliaji kwa kulipia gharama za umwagiliaji zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja na wawekezaji kupitia mikopo na dhamana. Serikali pia iliendelea na ujenzi na ukabarati wa skimu 24 za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 15 Nchini. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendeleza Skimu za Umwagiliaji 39 kwa ajili ya Kilimo cha mpunga.

Miundombinu ya Masoko ya Mazao

46.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kupitia Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini imekarabati kilometa 352 za barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe katika Halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Singida Vijijini, Mbarali, Lushoto, Same, Mbulu, Msalala na Mpanda. Halmashauri nyingine ni Maswa, Songea Vijijini, Rufiji, Karatu na Kwimba. Vilevile, imejenga maghala matano yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000 za mazao kila moja katika halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Same, Songea na Mbarali na kukarabati maghala matatu katika Halmashauri za Sumbawanga, Mbulu na Kahama. Aidha, Programu hiyo imezijengea uwezo benki tisa za wananchi/ushirika ili kuimarisha mfumo wa kifedha Vijijini.

47.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Programu hiyo imepanga kukarabati kilometa 434 za barabara kwa kiwango cha changarawe, kujenga maghala 14 na masoko saba katika Halmashauri 64 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar. Aidha, wazalishaji wadogo  kutoka Mikoa 24 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar watajengewa uwezo wa kuhifadhi mazao na mbinu za kufikia masoko ambapo zaidi ya wananchi 100,000 watanufaika na mafunzo hayo.

Maendeleo ya Ushirika

48.         Mheshimiwa SpikaSheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013 imetungwa na imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itawezesha kuanzishwakwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo itakuwa na majukumu ya kusimamia moja kwa moja Vyama vyote vya Ushirika. Aidha,  kupitia Sheria hiyo, Serikali imetoa Waraka Namba 1 wa mwaka 2014 unaotoa ufafanuzi kuhusu Chaguzi katika Vyama vya Ushirika. Ili kuondoa migogoro ya kimaslahi, Waraka huo umewaondoaViongozi wa Siasa na Serikali katika uongozi wa  Vyama vya Ushirika katika ngazi zote. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaimarisha uratibu wa Vyama vya Ushirika kulingana na mahitaji ya Wananchi na kuunganisha Vyama vya Ushirika na Taasisi za fedha ili kuboresha utoaji wa huduma za kifedha kwa Vyama vya Ushirika.


Maendeleo ya Sekta ya Mifugo

49.         Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Ruzuku ya dawa ya kuogeshea mifugo, Serikali ilitoa jumla ya lita 11,020 zenye thamani ya Shilingi Milioni 181.8 na kusambazwa nchini. Vilevile, ilitoa chanjo kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo ambapo dozi 150,000 za chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa zenye thamani ya Shilingi milioni 119 ilitolewa katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Dodoma. Vilevile, Serikali imeimarisha Kituo cha Uhamilishaji kilichopo katika eneo la Usa River, Arusha pamoja na Vituo vingine vitano vya Kanda kwa kusimika mitambo ya kuzalisha kimiminika cha naitrojeni na kujenga Vituo vitano vya madume bora. Vilevile, ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka 132,246 mwaka 2011/2012 hadi kufikia 175,000 mwaka 2013/2014. Ili kuboresha upatikanaji wa maziwa Nchini, Serikali imeongeza uzalishaji mitamba katika mashamba yake kutoka mitamba 943 kwa mwaka 2012/2013 hadi mitamba 1,046 mwaka 2013/2014 na kusambaza Mbuzi wa maziwa 9,530 kupitia Mpango wa Kopa Mbuzi lipa Mbuzi. Jitihada hizi, zimesaidia wafugaji kuongeza tija na hivyo kuchangia ongezeko la uzalishaji wa maziwa kutoka lita Bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita Bilioni 2 mwaka 2013/2014.

50.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa ruzuku ya dawa za kuogesha mifugo na kununua dozi milioni moja kwa ajili ya chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa kwa Mikoa ya Arusha, Tanga, Tabora na baadhi ya mikoa katika Kanda ya Ziwa. Vilevile, Serikali itaimarisha Vituo vya uhamilishaji, mashamba ya kuzalisha mifugo bora na yale yanayozalisha mbegu bora za mifugo pamoja na kununua mifugo wazazi.

Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi

51.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilihuisha Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia. Katika kuimarisha ufugaji wa samaki, wakulima 2,604 walipewa mafunzo ya ufugaji bora wa samaki na mabwawa 64 yalichimbwa. Hatua hiyo imeongeza idadi ya mabwawa ya Samaki kufikia 20,198 yenye uwezo wa kuzalisha Tani 3,029.7 za samaki ikilinganishwa na mabwawa 20,134 yaliyokuwepo mwaka 2012/2013.  Vituo vya kuzalisha vifaranga wa samaki kwa wingi kwa kutumia teknolojia ya ndani viliongezeka kutoka kituo kimoja mwaka 2012/2013 hadi kufikia vituo vitano mwaka 2013/2014 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga bora vya samaki Milioni 10 kwa mwaka. Serikali pia, ilijenga matanki sita yenye lita za ujazo 8,000 kila kimoja kwa ajili ya kuzalisha vifaranga vya samaki.

52.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanzisha Vituo vya kuzalishia vifaranga vya samaki katika maeneo ya Bacho Dareda - Manyara, Hombolo – Dodoma, na Kigoma. Vilevile, itajenga bwawa la kufuga samaki katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro – KATC; na kutoa ruzuku kwa ajili ya kuchimba mabwawa na kuzalisha vifaranga wa samaki.


Ufugaji Nyuki

53.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya ufugaji nyuki imeendelea kuimarika na kuchangia kuongeza ajira na kupunguza umaskini. Mwaka 2013, thamani ya mauzo ya asali nje yalifikia Shilingi Milioni 287.3 ikilinganishwa na mauzo ya Shilingi Milioni  262  mwaka 2012. Katika kipindi hicho, jumla ya Tani 384 za nta zenye thamani ya Shilingi Milioni 4,660 ziliuzwa nje ikilinganishwa na Tani 277 zenye thamani ya Shilingi Milioni 2,583 zilizouzwa mwaka 2012. Nchi zilizoongoza katika ununuzi wa Asali na Nta ya Tanzania ni Ujerumani, Oman, China, Japan, Yemen, India, Ubelgiji, Botswana, Kenya na Marekani. Kutokana na maendeleo haya mazuri katika mwaka 2013/2014, Serikali imetenga maeneo 20 yenye ukubwa wa Hekta 58,445 sehemu mbalimbali Nchini kwa ajili ya hifadhi za nyuki. Aidha, imetoa mafunzo kwawafugaji nyuki 924 na vikundi 49 kutoka Wilaya 12 pamoja na kutoa elimu ya miongozo na sheria za ubora wa mazao ya nyuki kwa wafanyabiashara wa mazao ya nyuki. 

54.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tanzania ilishiriki kwenye Kongamano la Ufugaji nyuki lililofanyika Kiev, Ukraine. Katika Kongamano hilo, mazao ya nyuki kutoka Tanzania yalikuwa kivutio kikubwa na yaliwezesha kupata medali ya Banda Bora la Asali kutokana na asali yake kuwa na viwango vya  ubora na  usalama vinavyokubalika Kimataifa. Aidha, kampuni  mbalimbali  zilionesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya ufugaji nyuki Nchini. Kama ambavyo nimesisitiza mara kwa mara, sekta ya nyuki ina fursa kubwa ya kibiashara hapa nchini na nje ya nchi.  Ni sekta inayoweza kuleta mapinduzi makubwa katika maeneo mengi kwani yanahitajika mafunzo kidogo na vifaa vichache ambavyo vinaweza  kutumika  kikamilifu  kupata  asali  na  mazao yake.  Niendelee kusisitiza kwamba, tuwahimize wananchi katika Majimbo yetu watumie fursa za ufugaji nyuki zinazopatikana katika maeneo yao ili kujiongezea kipato.

Maendeleo ya Viwanda

55.          Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imeendelea kutoa mchango muhimu katika upatikanaji wa ajira, ongezeko la kipato na ukuaji wa uchumi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imefungua Vituo vya Teknolojia Mikoani kwa ajili kuhudumia Wajasiriamali wanaotengeneza mashine za kusindika mazao na kutengeneza bidhaa mbalimbali za uzalishaji mali. Vituo hivyo vimewezesha kuanzishwa kwa miradi mipya 4,127 ya uzalishaji mali kwenye mikoa ya Lindi, Mbeya, Iringa, Arusha, Kigoma na Kilimanjaro. Aidha, Wajasiriamali 23,546 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi maalum wa ufundi na utumiaji wa mashine za uzalishaji mali. Vilevile, huduma za ushauri na ugani zilitolewa kwa Wajasiriamali 20,769 kwenye Vikundi na Vyama vyao vya Biashara kwa kuviimarisha na kuviwezesha kujenga misingi ya kujitegemea.

56.          Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mkakati wa “Wilaya Moja, Bidhaa Moja” kwa kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa kutokana na malighafi zilizopo kwenye Wilaya husika. Kupitia Mkakati huo, Serikali imejenga uwezo wa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali, kuzalisha mitambo na vipuri pamoja na zana za kilimo ambapo viwanda vidogo 198 vilianzishwa na kuwezesha upatikaji wa ajira 1,809. Aidha, Serikali inatekeleza Mradi wa Kuendeleza Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa kutumia dhana ya kuimarisha mlolongo wa thamani kimikoa kwa mazao mbalimbali. Mradi umewezesha uanzishwaji wa miradi midogo 15,580 Vijijini; urasimishaji wa Vikundi 65,308 vya uzalishaji na upatikanaji wa ajira 39,574.

57.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na juhudi za kuhamasisha uwekezaji kwenye miradi mipya katika Maeneo Maalum ya Uzalishaji (Export Processing Zones) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Special Economic Zones). Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, kampuni 32 zilikuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya EPZ kwa ajili ya kuanzisha viwanda vipya kwenye maeneo hayo. Aidha, Serikali imekamilisha utafiti kwenye Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na kuthibitisha uwepo wa tani Milioni 370 za makaa ya mawe katika eneo la kilomita za mraba 30 kati ya kilomita za mraba 140 zilizotengwa kwa ajili ya Mradi huo. Aidha, utafiti huo ulithibitisha uwepo wa tani Milioni 219 za madini ya  chuma katika eneo la kilomita za mraba 10 kati ya kilomita za mraba 166 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo. Ujenzi wa mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na madini  ya  chuma  Liganga unatarajiwa kuanza mwaka 2014 na kukamilika mwaka 2018. Katika mwaka 2014/2015,

Serikali itajielekeza katika kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo. Aidha, itaendelea kujenga Mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Ngaka na Mradi wa Chuma Liganga.

Sekta ya Utalii

58.          Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile vipeperushi, majarida, matangazo ya Televisheni na kutumia Balozi za Tanzania zilizoko nje ya nchi. Mbinu nyingine zilizotumika ni kutumia maonesho ya Kimataifa na kuweka matangazo kwenye viwanja sita vya Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Uingereza. Pamoja na matangazo hayo, huduma za kitalii hususan hoteli, miundombinu ya barabara na mawasiliano zimeimarishwa na hivyo kuwashawishi watalii wengi kutembelea nchini Kutokana na hatua hizo, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka Watalii 1,077,058 mwaka 2012 hadi 1,135,884 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 5.46. Watalii hao wameliingizia Taifa Dola za Marekani Bilioni 1.8 ikilinganishwa na Dola za Marekani Bilioni 1.7 zilizopatikana mwaka 2012. Vilevile, Serikali imeanzisha utalii wa usiku katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara; utalii wa kuangalia wadudu katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo na Hifadhi ya Amani; utalii wa makasia katika Hifadhi ya Arusha – Ziwa Momela na Utalii wa kutembea katika Hifadhi za Mahale na Gombe.

59.          Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara, imeandaa mkakati maalum wa kukuza sekta ya utalii hasa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha kasi ya ukuaji wa sekta hii. Aidha, katika kukuza utalii wa ndani, Serikali inatumia fursa za maonesho na matamasha mbalimbali ya ndani kuelezea vivutio vya utalii na imeandaa kijitabu cha utalii wa Utamaduni kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatafsiri tovuti ya Bodi ya Utalii pamoja na vielelezo mbalimbali kwa lugha za Kifaransa, Kijerumani, Kichina na Kihispaniola ili zitumike kutangaza utalii kwa nchi zinazotumia lugha hizo.  Hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa utalii katika masoko hayo yenye fursa kubwa.

Wanyamapori

60.          Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kuhifadhi   wanyamapori katika Hifadhi na Mapori ya Akiba Nchini kwa nia ya kuwalinda na kuendeleza utalii. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendesha doria mbalimbali ndani na nje ya hifadhi zilizowezesha kukamatwa watuhumiwa 391 pamoja na silaha 73 zikiwemo bunduki 22 za kivita. Jumla ya kesi 277 zilifunguliwa ambapo kesi 123 zimemalizika na kesi 154 zinaendelea. Vilevile, katika kuhamasisha wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi hizo kuzilinda, Halmashauri 38 zenye vitalu vya uwindaji zilipatiwa Shilingi Bilioni 8.7 kama mgawo wa Asilimia 25 ya fedha zinazotokana na uwindaji wa kitalii kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi.

61.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili. Mkakati huo umeainisha uwezo tulionao, upungufu uliopo na mahitaji muhimu ambayo yataimarisha uhifadhi Nchini na kupunguza migongano iliyopo ya matumizi ya ardhi. Vilevile, itaanzisha Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania itakayosimamia shughuli zote zinazohusu uhifadhi wa wanyamapori ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato, kuendeleza hifadhi na kuimarisha ulinzi wa wanyamapori.

Sekta ya Madini

62.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeimarisha ukaguzi kwenye uzalishaji na biashara ya madini. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka Wakaguzi katika migodi yote mikubwa na baadhi ya mitambo ya uchenjuaji madini. Aidha, imeanzisha dawati maalum la kukagua madini yanayosafirishwa nje ya Nchi kupitia viwanja vya ndege ili kudhibiti utoroshaji wa madini. Kutokana na jitihada hizo, madini ya dhahabu na vito yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.9 yalikamatwa na kuwasilishwa kwenye vyombo husika kwa hatua za kisheria.

63.         Mheshimiwa Spika, Serikali inathamini mchango wa Wachimbaji Wadogo wa Madini katika kukuza uchumi wa Nchi yetu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewajengea uwezo wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mafunzo na mikopo ili kuongeza uzalishaji. Kutokana na juhudi hizo, jumla ya kilo 237 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 14.5 zilizalishwa na kuingiza mrabaha wa Shilingi Milioni 519. Aidha, Serikali imetenga maeneo mapya ya uchimbaji ya Isamilo na lwenge (Geita); Rwabasi (Butiama) na Saza na Itumbi “B” (Chunya). Jitihada hizo zimefanya shughuli za wachimbaji wadogo hasa katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu kukua.

64.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha Mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009, Sheria ya Uongezaji Thamani Madini na Sheria ya Baruti pamoja na Kanuni zake. Serikali pia itahamasisha uwekezaji kwenye sekta ya Madini na kuziwezesha taasisi zake kama vile Tanzania Extractive Industrials Transporency Initiatives (TEITI) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi. Vilevile, itatenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuwawezesha kupata mitaji na teknolojia. Pia, itaboresha Mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini kwa kuanzisha huduma za kuomba leseni kwa njia ya mtandao.



65.          Mheshimiwa Spika, ardhi ni msingi na kichocheo muhimu cha maendeleo ikiwa itapangiwa matumizi bora, itapimwa na kusimamiwa ipasavyo. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali  inachukua  hatua madhubuti kuhakikisha kuwa  kila  kipande  cha  ardhi Nchini kinapangwa, kupimwa,  kumilikishwa  na kutumiwa kwa mujibu wa Sheria. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha sehemu ya kwanza ya ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management Information System) na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji na matumizi mengine. Sambamba na hatua hiyo, Serikali inaboresha utunzaji wa kumbukumbu za upimaji Ardhi kwa kuzibadili zilizopo kuwa katika mfumo wa Kanzidata za Kielektroniki ili ziweze kuunganishwa na Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi. Hatua hiyo inalenga kurahisisha  upatikanaji wa taarifa za upimaji ardhi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hadi mwezi Februari 2014, kumbukumbu za ramani 5,000 za Jiji la Dar es Salaam zimebadilishwa na kuwekwa katika ramani unganishi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaandaa Kanzidata ya viwanja 300,000 katika Miji mbalimbali Nchini.

66.         Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Sekta ya Ardhi imekumbwa na tatizo la migogoro ya mara kwa mara inayotokana na matumizi mbalimbali ya ardhi hususan baina ya wakulima na wafugaji. Aidha, migogoro hiyo imekuwa ikihusisha wananchi na maeneo ya hifadhi, Vijiji kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi, wananchi dhidi ya wawekezaji na  baina  ya  wananchi wenyewe kwa wenyewe. Migogoro hii imekuwa ikiongezeka zaidi katika siku za hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, mifugo na shughuli za kiuchumi zinazotegemea ardhi kama vile madini, utalii, viwanda, kilimo na makazi. Migogoro ya ardhi ina athari  kubwa  kwa wananchi ikiwemo uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali na hata vifo. Serikali imekuwa ikichukua hatua kudhibiti migogoro hiyo kila inapotokea.      Ili kupata suluhisho la kudumu la kushughulikia migogoro ya ardhi, Serikali imeanza kusimika mifumo ya kisasa kwa ajili ya upimaji, umilikishaji na usimamizi wa sekta ya ardhi. Hii ni kwa sababu uzoefu umeonesha kwamba ukosefu wa ramani, mipaka rasmi na miliki kamilifu ndicho chanzo kikuu cha migogoro inayojitokeza mara kwa mara.  Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa kipaumbele katika Sekta ya Ardhi hasa kushughulikia maeneo yanayolenga kutatua migogoro ya ardhi kama vile upimaji wa mipaka ya vijiji, kutoa hati miliki na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya Vijiji. Aidha, Serikali itajenga Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi, kukamilisha usimikaji wa alama za msingi za upimaji, kurasimisha hati milki na kupima mipaka ya Kimataifa.

Nishati

67.          Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za upatikanaji wa umeme Nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme. Mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha kwa Asilimia 90 Awamu ya Kwanza ya Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme unaotekelezwa katika Mikoa 16 Nchini. Pia, Mradi huo unajumuisha usambazaji wa umeme Vijijini ambapo wateja 15,305 kati ya wateja 22,000 waliolengwa wameunganishiwa umeme. Vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini imesaini Mikataba 35 na Wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme Vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme Vijijini. Aidha, tarehe 8 Septemba 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mtambo wa kufua umeme wa Megawati 60 unaotumia mafuta mazito katika eneo la Nyakato, Mwanza. Mtambo huo umeongeza uwezo wa kufua umeme kwenye gridi ya Taifa na kufikia Megawati 1,583. Mtambo huo umeimarisha upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara. Kutokana na juhudi za kusambaza umeme Mijini na Vijijini hadi mwezi Machi 2014, zaidi ya Asilimia 30 ya Watanzania wamepatiwa huduma hiyo, na hivyo kuvuka lengo la Asilimia 30 lililotarajiwa kufikiwa mwaka 2015.

68.         Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa kasi kwa Sekta ya gesi, Serikali katika mwaka 2013/2014, imeandaa Sera ya Gesi Asilia ambayo inatoa miongozo ya kusimamia rasilimali hiyo. Serikali pia inatekeleza miradi mbalimbali chini ya sekta ndogo ya gesi ikiwa ni pamoja na kuendelea na Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam. Hadi sasa, mabomba yote kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wenye urefu wa Kilomita 542 yamewasili na kazi ya kuunganisha inaendelea. Ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Gesi pamoja na mitambo miwili ya kuchakata gesi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014. Aidha, Awamu ya Kwanza  ya  Mradi wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 150 kwa kutumia  Gesi  Asilia  umeanza kutekelezwa. Katika hatua nyingine, Serikali imepitia upya miundo ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania na Shirika la Umeme Tanzania kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa utendaji wa Mashirika hayo.

69.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mchakato wa Maboresho ya sera mbalimbali za Nishati ikiwemo Sera ya Nishati ya Mwaka 2003; Sera Mpya ya Mafuta na Sera Mpya ya Uwezeshaji Wazawa. Kukamilika kwa sera hizo kutaimarisha usimamizi wa Sekta ya Nishati kwa maendeleo ya Nchi yetu. 

Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano

70.         Mheshimiwa Spika,  Serikali imekamilisha Awamu ya Kwanza na ya Pili  ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 7,560 ambao pia unatoa maunganisho ya mawasiliano kwa Nchi jirani. Awamu ya Tatu ya ujenzi itakayoziunganisha Unguja na Pemba na Mkongo wa Taifa imeanza mwezi Desemba, 2013 na inatarajiwa kukamilika katika miezi 18. Mkongo umesaidia watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano kwa Wananchi  kwa uharaka zaidi, uhakika na kwa gharama nafuu. Hatua hiyo inaharakisha  maendeleo  ya  Taifa  kwa Wananchi kupata fursa ya kutumia TEHAMA katika kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo kwa kasi zaidi.  Pia, Serikali kwa kutumia ruzuku imeendelea kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara kwa kushirikiana na Sekta binafsi. Katika mwaka 2013/2014 jumla ya Kata 52 zenye Vijiji 316 vimefikishiwa huduma za mawasiliano kupitia Mpango huo. Aidha, Serikali imetia saini makubaliano na watoa huduma za mawasiliano kufikisha huduma hizo katika Kata  nyingine163 zenye Vijiji 922. Watu 1,211,841  watanufaika na juhudi hizo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mkongo maeneo ya mijini katika Miji ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma na kuendelea kuunganisha Unguja na Pemba na Mkongo huo.

Simu za Mkononi na Intaneti

71.         Mheshimiwa Spika, mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali kwenye Sekta ya Mawasiliano yameonesha matokeo chanya na ya kuridhisha sana. Idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Nchini imeongezeka  kutoka laini za simu za mkononi Milioni 2.96 mwaka 2005 hadi Milioni 27.45 mwaka 2013. Watumaji wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka Milioni 3.56 mwaka 2008 hadi Milioni 9.3 mwaka 2013. Pia, kuna ongezeko kubwa la huduma  kupitia  mawasiliano ya simu za mkononi. Huduma hizo ni pamoja na miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma  na  bidhaa  kwa  kutumia  miamala  ya  kibenki. Hivi sasa wananchi wanaweza kufanya malipo ya huduma mbalimbali wanazozitumia kupitia simu za kiganjani. Hatua hiyo imesaidia kuokoa muda na kupunguza msongamano sehemu za kulipia na kupata huduma hizo.

Mfumo wa Kuhakiki na Kusimamia Huduma za Mawasiliano

72. Mheshimiwa Spika,  Serikali ililiahidi Bunge lako Tukufu kwamba ingesimika Mfumo wa Kusimamia Mawasiliano  ya  Simu  Nchini.  Lengo la kujenga Mfumo huo ni kubaini takwimu zinazopita katika mitandao ya mawasiliano. Mfumo huo unaweza kutoa takwimu za mawasiliano  yanayofanyika  ndani na nje ya Nchi; kutambua mapato na miamala ya fedha; kufuatilia na kugundua mawasiliano ya ulaghai; na kutambua taarifa za laini ya  simu na za kifaa cha mawasiliano. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, tayari Mtambo wa kuwezesha Mfumo wa Kusimamia Mawasiliano Tanzania umejengwa kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 25 kwa kutumia utaratibu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (Build, Operate and Transfer). Ili kuweza kutumia Mfumo huo ipasavyo, Serikali imekamilisha Kanuni za Uhakiki na Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na simu zinazoingia  Nchini kutoka nje ya Nchi. Mfumo huo umeanza rasmi kutumika mwezi Oktoba, 2013 na kwa  kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba, 2013 umeingizia Serikali  Shilingi  Bilioni 5. Katika  mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuboresha taarifa za kiutendaji zitakazowezesha kupunguza kasi ya udanganyifu wa simu zinazoingia nchini kwa lengo la kuongeza mapato. Vilevile, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itasimamia miamala ya malipo ya fedha kupitia simu za mkononi yanayofanywa na kampuni za simu.

Mfumo wa Utangazaji wa Digiti

73.         Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, Serikali ilianza kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi la kuhama kutoka mfumo wa utangazaji wa Analojia kwenda Digiti tarehe 31 Desemba, 2012.  Awamu hiyo ilihusisha Miji Saba ya Dar es Salaam, Mbeya, Tanga, Mwanza, Arusha, Dodoma na Moshi. Uhamaji huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa na tathmini ilifanywa ili kuweka mazingira bora zaidi ya kuendelea na zoezi hilo. Kufuatia tathmini hiyo, Awamu ya Pili ilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 31 Machi, 2014 na inatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2014. Miji kumi itakayohusika na zoezi hilo ni Singida na Tabora, ikifuatiwa na Miji ya Musoma, Bukoba, Kigoma, Kahama, Iringa, Songea, Morogoro na Lindi. Uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya Analojia unahusisha maeneo yote yanayopata huduma za matangazo kupitia mitambo ya kusimikwa ardhini tu, ambayo ni Asilimia 24  ya eneo lote la Nchi yetu. Maeneo  yanayopata huduma za matangazo kupitia mitambo  ya  Satellite  na  Cable   hayahusiki  na  zoezi hilo.
Serikali imelenga ifikapo mwezi Oktoba, 2014 mitambo yote ya Analojia iwe imezimwa Nchini. Napenda kurudia wito wangu kwamba, zoezi hili ni la muhimu na lina lengo la kuifanya Nchi yetu iendane na mabadiliko yanayotokea duniani ambayo hayakwepeki.  Wadau wote watoe ushirikiano kwa vyombo vinavyohusika.

Barabara na Madaraja

74.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 505.7 za Barabara Kuu na kukarabati kilometa 146.6. Aidha, imejenga kwa kiwango cha lami kilometa 22.3 za Barabara za Mikoa na kukarabati kilometa 145.1 kwa kiwango cha changarawe. Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Kigamboni – Dar es Salaam na Mto Malagarasi - Kigoma. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga Barabara mpya zenye urefu wa kilometa 633 za Barabara kuu na Barabara za Mikoa kwa kiwango cha lami. Vilevile, itakarabati kilometa 165 za barabara za lami na kilometa 1,150 za barabara za changarawe katika Barabara Kuu na Barabara za Mikoa. Aidha, itaendelea na ujenzi wa madaraja 57 ya barabara hizo.

Msongamano wa Magari Jijini Dar es Salaam

75.         Mheshimiwa Spika,  msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam umekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za kiuchumi na kijamii.            Katika kukabiliana na tatizo hilo, mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za lami za Ubungo Bus Terminal - Kigogo - Kawawa yenye urefu wa kilometa 6.4; barabara ya Jet Corner –Vituka - Davis Corner yenye urefu wa kilometa 10.3 na barabara ya Ubungo Maziwa - Mabibo External yenye urefu wa kilometa 2.25 pamoja na daraja la External.  Ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Kigogo - Jangwani yenye kilometa 2.72 na zile zitakazotumika kwa Mabasi yaendayo haraka unaendelea.

76.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga barabara sita Jijini Dar es Salaam kwa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Tabata Dampo - Kigogo (km 1.6); Kifuru - Kinyerezi (km 4); Goba - Mbezi Mwisho (km 7); Tangi bovu (Samaki) - Goba (km 9); Kimara Baruti - Msewe (km 2.6) na Kimara - daraja la Maji Chumvi External (km 3). Tayari Serikali imesaini mikataba na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo ambazo zinatarajiwa kukamilika kati ya miezi 8 hadi 18.

HALI YA UCHUKUZI

Reli ya Kati na TAZARA

77.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli ya Arusha – Musoma yenye urefu wa Kilomita 600. Lengo ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kwa Mikoa ya Kaskazini na Nchi jirani ya Uganda kupitia Bandari ya Tanga. Vilevile, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa yenye urefu wa Kilometa 1,464 kutoka Dar es Salaam - Isaka - Keza - Kigali na Kilometa 197 kutoka  Keza hadi Msongati.

78.         Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Maelewano kati ya Tanzania na Burundi kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Uvinza hadi Msongati umesainiwa.  Kuhusu Reli ya TAZARA, Serikali inatekeleza Makubaliano ya Itifaki ya 15 iliyosainiwa mwezi Machi, 2012 kati ya Serikali ya Watu wa China na Serikali za Tanzania na Zambia ambapo ununuzi wa vichwa vinne vya treni, vichwa vinne vya Sogeza umefanyika pamoja na ununuzi wa mabehewa 18 ya abiria ya Reli ya TAZARA. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaboresha Kilometa 308 za miundombinu ya Reli ya Kati na vituo vya Bandari kavu vya kuhifadhi Makasha vya Ilala na Isaka. Aidha, Kampuni ya Reli (TRL) itakarabati vichwa nane vya treni na kununua  vichwa vipya 12 na mabehewa 204 ya mizigo na kukarabati majengo ya Stesheni.  


79.         Mheshimiwa Spika, kijiografia nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo kubwa la maziwa na bahari ambalo limetuwezesha kuwa na bandari zinazohudumia pia Nchi jirani zisizopakana na bahari. Ili kutumia fursa hii kikamilifu, Serikali katika mwaka 2013/2014, imekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuboresha Gati namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es SalaamVilevile, inatekeleza miradi ya ujenzi wa magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Aidha, kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Mamlaka ya Bandari imevuka malengo kwa kuhudumia zaidi ya tani Milioni 13 za mizigo hadi Desemba 2013, ikilinganishwa na tani Milioni 12 kwa mwaka 2012. VilevileSerikali imeanza kutekeleza utaratibu wa kufanya kazi bandarini kwa saa 24 kwa siku zote za juma ili kuongeza kasi ya uondoshaji wa mizigo inayotoka. Hatua  hiyo imesaidia  kupunguza  msongamano  wa  mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza malalamiko  kutoka kwa  watumiaji  wa  bandari  hiyo. Aidha, kumekuwa na ongezeko la ufanisi katika kuhudumia wasafirishaji wa mizigo katika maeneo ya mipakani, hususan Rusumo, Tunduma, Namanga, Kasumulo na Mtukula. Wasafirishaji wanatumia muda mfupi hivi sasa ikilinganishwa na hapo awali. Kwa mfano, muda wa huduma katika mpaka wa Rusumo, umepungua kutoka siku tatu hadi nusu saa.

80.         Mheshimiwa Spika,  katika  mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kuboresha Gati namba 1 hadi 7 ili kuwezesha Bandari  ya  Dar es Salaam kuhudumia mizigo tani Milioni 18 kutoka tani Milioni 13.5 za sasa. Aidha, itakamilisha ujenzi wa magati katika Bandari ya Mtwara, kukamilisha majadiliano na kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na kuendelea na miradi ya ujenzi wa magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Vilevile, itakarabati meli za MV Umoja, MV Victoria, MV Butiama, MV Serengeti, MV Liemba, MT Sangara, MT Ukerewe na meli ya MV Songea ili kuboresha usafiri na usafirishaji katika maziwa.


81.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha miundombinu ya viwanja vya ndege Nchini na kuviwezesha kutoa huduma kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za uendeshaji za kimataifa. Katika mwaka 2013/2014, jumla ya viwanja vya ndege 13 ikiwemo Viwanja vya Mwanza, Musoma, Bukoba, Kigoma, Tabora, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa, Songea, Nachingwea na Kilwa Masoko vilifanyiwa ukaguzi na kupata leseni ya uendeshaji. Aidha, Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa jengo jipya la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere utakaogharimu Shilingi Bilioni 518. Mradi huo ambao umewekwa jiwe la msingi na Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Aprili, 2014 unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2015. Jengo hilo litakuwa na ukubwa wa  meta za mraba 70,000 ambao ni zaidi ya mara nne ya ukubwa wa jengo lililopo sasa lenye ukubwa wa meta za mraba 15,000. Baada ya kukamilika kwa jengo hilo na miundombinu yake, Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa za abiria. Aidha, utahudumia abiria milioni sita kwa mwaka ikilinganishwa na abiria milioni 2.5 kwa sasa. Vilevile, Uwanja huo utatoafursa mbalimbali za kiuchumi, kibiashara na kukuza utalii nchini. Aidha, utazalisha ajira mpya zaidi ya 7,000 kwa Watanzania.

82.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuimarisha huduma za usafiri nchini pamoja na kuvutia uwekezaji na utalii. Kwa kuzingatia azma hiyo, mwezi Oktoba 2013, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua rasmi Uwanja wa Ndege wa Mafia  baada ya ujenzi wake kukamilika kwa kiwango cha  lami. Kuzinduliwa  kwa  uwanja  huo  kumefungua  fursa za kibiashara, hususan ya utalii katika kisiwa hicho. Vilevile, mwezi Julai 2013, Mheshimiwa Rais, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kukamilisha ujenzi wa Uwanja mpya wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe, Mbeya. Serikali pia itakamilisha ukarabati wa Viwanja vya ndege vya Mwanza, Bukoba, Kigoma na Tabora na kuanza kukarabati viwanja vya ndege vya Shinyanga, Mtwara na Sumbawanga.



83.         Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu unafuata Sera, Miongozo na Mitaala, Serikali imeendelea kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995. Aidha, kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa katika elimu ya msingi, utaratibu wa kupima stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (K3) kwa wanafunzi wa darasa la Kwanza na la Pili umeanzishwa kwa lengo la kupima na kuweka msingi wa kuboresha stadi husika kabla ya kuingia darasa linalofuata.  Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,928 wa shule za msingi na kupangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.  Kuajiriwa kwa walimu hao kutapunguza pengo la walimu lililopo.

84.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, itaimarisha elimu ya msingi kwa kuongeza uwazi wa kiutendaji, kuwajengea  walimu uwezo wa kutoa msaada wa kimasomo kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum, kuinua ubora wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuongeza uwajibikaji wa watendaji katika utoaji wa elimu.

Elimu ya Sekondari

85.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeweka juhudi kubwa katika kuimarisha Elimu ya Sekondari hasa ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara, ununuzi wa madawati na vitabu pamoja na kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Aidha, Serikali imeajiri Walimu wapya wa Sekondari 18,410 na kutoa mafunzo kazini kwa Walimu 12,476. Kati ya hao, Walimu 8,400 ni wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Hatua hizo zimechangia kuongeza ufaulu wa Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013 kufikia Asilimia 58.25 ikilinganishwa na Asilimia 43.08 mwaka 2012. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa kipaumbele cha uwekezaji kwenye miundombinu ya Shule za Sekondari, Walimu, Ukaguzi na Vitendea kazi.


86.          Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018. Mpango huo unalenga kuongeza udahili katika ngazi mbalimbali za Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kujenga uwiano wa nguvukazi katika ngazi mbalimbali kwa kila fani. Vilevile, unalenga kujenga nguvukazi yenye kuhimili ushindani wa soko la ajira kwa kuinua ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi  ili  kukidhi  mahitaji ya soko la ndani na nje ya Nchi. Ili kutekeleza mpango huo, katika mwaka 2013/2014, Serikali ilianza kutumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 25 kutoa mafunzo ya masomo ya ufundi stadi ili kuongeza udahili wa wanafunzi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika Mikoa ya Rukwa, Geita, Simiyu na Njombe.

Elimu ya Juu

87.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia masomo ya sayansi na teknolojia kwenye Vyuo Vikuu nchini. Katika mwaka 2013/2014, kupitia Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Serikali imekamilisha ujenzi wa vyumba 48 vya Mihadhara, Maabara 93 za sayansi  na Ofisi 302 za wafanyakazi katika Vyuo Vikuu mbalimbali vya Umma nchini. Aidha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vya TEHAMA vilinunuliwa katika Vyuo hivyo na kuziunganisha Taasisi 28 za elimu ya juu katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

88.         Mheshimiwa Spikakutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu Vyuo Vikuu nchini kutoza ada tofauti kwa mafunzo ya aina moja, Serikaliimekamilisha Mwongozo wa Gharama Halisi ya Kumsomesha Mwanafunzi wa Elimu ya Juu. Mwongozo huo unatoa ukomo wa ada inayotakiwa kutozwa na chuo kwa kila programu au kozi kwa mwanafunzi. Lengo ni kuondoa upangaji na upandishaji wa ada kiholela kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu pasipo kuzingatia gharama halisi ya kumsomesha mwanafunzi husika kulingana na kozi anayosomaKatika mwaka 2014/2015, Serikali itasimamia utekelezaji wa  Mwongozo huo.

MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA

Huduma ya mama na mtoto

89.          Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha huduma ya afya ya Mama na Mtoto kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo vitokanavyo na Matatizo ya Uzazi na Vifo vya Watoto wa mwaka 2008 hadi 2015. Katika kutekeleza Mkakati huo, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Uzazi wa Mpango Uliothaminiwa. Mpango Kazi huo unalenga kununua na kusambaza dawa na vifaa vya uzazi wa mpango nchini. Aidha, Serikali imeimarisha mfumo wa rufaa kwa mama wajawazito kwa kununua vyombo vya usafiri kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuvisambaza katika mikoa yenye kiwango cha juu cha vifo vya mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi. Vilevile, Serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Kutokomeza Maambukizi Mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambao ulizinduliwa tarehe Mosi, Desemba, 2012 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu ya kwanza ya Mpango huo ilianza mwezi Oktoba, 2013 na kuhusisha Mikoa tisa yenye uambukizo mkubwa wa VVU kwa wajawazito. Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita  na Kagera. Awamu ya pili imeanza mwezi Januari, 2014 kwa Mikoa 16 iliyobakia.

90.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mapitio ya Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo vya Mama vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto na kutekeleza afua nyingine za kipaumbele. Aidha, kupitia Mpango wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango dawa na vifaa vyote vya uzazi wa mpango vitanunuliwa na kusambazwa ili viweze kuwafikia wananchi wanaovihitaji. Lengo ni kufikia Asilimia 60 ya kiwango cha utumiaji huduma za uzazi wa mpango kama ilivyoanishwa kwenye Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria

91.         Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa malaria, Serikali imeendelea kugawa vyandarua shuleni na kuhimiza matumizi endelevu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali iligawa vyandarua 510,000 katika shule 2,302 za msingi na Sekondari za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kupitia Programu ya Wanafunzi Shuleni. Aidha, kupitia mikakati na afua nyingine Serikali ilisambaza vyandarua 879,856 vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo kwa wajawazito na watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja.

92.         Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba, inatekeleza Mpango wa kuangamiza Viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia katika Jiji la Dar es Salaam. Mpango huo pia, utatekelezwa katika Mikoa mingine mitano. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau iliendelea na zoezi la kupulizia dawa ya ukoko katika kaya 838,000 zilizopo kwenye Mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza ambapo zaidi ya Wananchi 4,505,752 wamekingwa dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria. Pia, Serikali imekamilisha kusambaza  kipimo  cha  malaria  kinachotoa majibu ya haraka    katika   vituo   vyote   vya   kutolea   huduma   Nchini.  Vilevile, jumla ya dozi 14,655,000 za Dawa Mseto na Vitendanishi 9,853,710 vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya huduma na hivyo kuimarisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi Nchini.

 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kugawa vyandarua Milioni 7.2 vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo, na kuendeleza kampeni maalum ya kugawa vyandarua kwa jamii katika ngazi ya kaya. Aidha, zoezi la kugawa vyandarua kwa wanafunzi shuleni litaendelezwa kwa Mikoa ya Kusini. Sambamba na hatua hizo, mradi wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia utapelekwa katika Mikoa mingine mitano kwa kutumia viuatilifu (Biolarvicides) vitakazozalishwa katika kiwanda kinachojengwa Kibaha, Mkoa wa Pwani ambacho kinatarajiwa kuanza kazi mwaka huu wa 2014.

Huduma kwa Wazee na Watu Wenye Ulemavu

93.         Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 na Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 zinasisitiza kuwa makundi hayo yana haki ya kupata matunzo katika jamii. Katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitoa huduma za msingi kwa wazee na watu wenye ulemavu wasiojiweza wanaotunzwa na kulelewa katika Makazi 17 ya Serikali. Jumla ya wahudumiwa 1,235 walipatiwa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi, mavazi pamoja na kuwapatia vifaa yakiwemo magodoro, mashuka, vitanda na nyenzo za kujimudu.  Vilevile, Serikali iliratibu huduma za matunzo katika Makazi 24 yanayoendeshwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kupunguza malalamiko kuhusu upungufu wa huduma zinazotolewa.

94. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kusisitiza kuwa, wazee na watu wenye ulemavu na wasiojiweza wanahitaji kupatiwa matunzo katika jamii zao.  Huduma zinazotolewa kwenye vituo na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ni hatua ya mwisho pale ambapo itathibitika kuwa mzee au mlemavu huyo hana mtu kabisa wa kumtunza katika familia na jamii. Natoa rai kwa wananchi kuendeleza utamaduni wa kuwatunza wazee wetu na watu wenye ulemavu.  Huu ni utamaduni mzuri sana. Aidha, nazikumbusha Halmashauri kutenga fedha za kuyahudumia makundi hayo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itazindua Baraza na Mfuko wa Taifa wa Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ili kuwajengea na kuongeza uwezo wao katika kuzifikia fursa za maendeleo na kuimarisha utawala bora.

Lishe

95.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea kusimamia Kanuni za Uongezaji wa Virutubishi katika vyakula ambapo viwanda vikubwa sita vya kusindika unga wa ngano na viwanda vitatu vya kusindika mafuta ya kula vinaweka virutubishi katika vyakula vinavyotengenezwa. Takwimu zinaonesha kuwa, takribani watu milioni 10 wanatumia unga wa ngano uliorutubishwa na Milioni 4 wanatumia mafuta ya kupikia yaliyorutubishwa na vitamin A. Vilevile, Serikali imeandaa Mpango wa Uongezaji wa Virutubishi kwenye vyakula Ngazi ya jamii ambapo utekelezaji wake ulishaanza katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Arusha na Dar es Salaam. Mpango huo unalenga uwekaji virutubishi kwenye unga wa mahindi unaozalishwa na wajasiriamali wadogo na kusagwa kwenye viwanda vya kati na vidogo.

96.         Mheshimiwa Spika, Sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya utapiamlo nchini. Mwezi Mei 2013, Serikali ilikabidhi tani nane za Madini joto kwa Muungano wa Wasindikaji wa Chumvi katika maeneo mbalimbali Nchini kama sehemu ya mchango wa Serikali wa kuimarisha Sekta Binafsi katika mapambano dhidi ya utapiamlo. Serikali pia imeimarisha Maabara za uwekaji madini joto katika chumvi kwa kununua na kugawa vitendanishi katika Maabara 13 za Mikoa. Lengo ni kupanua wigo wa Wananchi wanaopata vyakula vyenye virutubishi. Natoa wito kwa Viongozi katika ngazi zote. Kusimamia juhudi hizo za Serikali na kuhakikisha zinaendelezwa katika maeneo yao. Aidha, ninawasihi Wafanyabiashara wote wenye viwanda vya chakula kutekeleza jukumu hilo kikamilifu. Kwa wale ambao hawajakamilisha taratibu za ufungaji wa mashine za kuongeza virutubishi wafanye hivyo mapema iwezekanavyo.
HALI YA UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI

Huduma ya Maji Vijijini
97.  Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga kuboresha huduma ya maji Mijini na Vijijini kwa kushirikisha Wananchi na Sekta Binafsi.  Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali iliweka lengo la kutoa huduma za maji kwa Asilimia 65 Vijijini katika umbali usiozidi mita 400. Ili kuongeza kasi ya kufikia lengo hilo, katika mwaka 2013/2014, Serikali iliongeza bajeti ya maji kwa Shilingi Bilioni 184 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maji.

98.         Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Maji kwa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji 248 katika Vijiji 270 umekamilika.  Pia, jumla ya vituo 10,393 vya kuchotea maji vinavyohudumia Watu 2,598,250 vimejengwa. Ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye Vijiji 613 upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na miradi katika Vijiji 374 inafanyiwa tathmini ya zabuni. Aidha, katika kipindi hicho, vyombo vya watumia maji 373 vimeundwa. Vilevile, katika kipindi cha miezi sita ya utekelezaji wa miradi ya maji chini ya BRN! kinachoishia Desemba 2013, Wanavijiji 2,390,000 wamefikishiwa huduma za maji safi na salama, ikilinganishwa na Wanavijiji 300,000 hadi 500,000 waliokuwa wakipatiwa huduma za maji safi Vijijini kabla ya mpango huo kuanza.

99.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia inatekeleza Awamu ya Pili ya mradi wa maji wa Chalinze ambao utatoa huduma ya maji kwa Vijiji 47 vyenye Watu 197,684 katika Wilaya za Bagamoyo, Pwani. Hadi kufikia Desemba 2013, utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia Asilimia 88. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa mabwawa katika maeneo mbalimbali hususan maeneo kame kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo. Ujenzi wa mabwawa ya Iguluba (Iringa Vijijini) na Wegero (Butiama, Mara) na ukarabati wa Bwawa la Ingodini –Longido Arusha umekamilika. Ujenzi wa mabwawa ya Kawa (Nkasi, Rukwa), Sasajila (Chamwino, Dodoma), Mwanjoro (Meatu, Shinyanga) na Kidete (Kilosa, Morogoro) umekamilika kwa zaidi Asilimia 75. Mabwawa yaliyokamilika kwa wastani wa Asilimia 50 ni Habiya (Itilima, Simiyu), Sekeididi (Kishapu, Shinyanga) na Matwiga (Chunya, Mbeya). Natoa wito kwa Wananchi kulinda vyanzo na miundombinu ya maji. Vilevile, natoa wito kwa Viongozi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia vyema Vyombo vya watumia maji ili miradi hii iwe endelevu.

Huduma ya Maji Mijini

100.       Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika miji mikuu ya mikoa zinatoa huduma ya maji kwa wakazi wake kwa wastani wa Asilimia 80. Katika Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa huduma ya maji utaongezeka zaidi mara baada ya upanuzi na ujenzi wa bomba kuu la maji kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini kukamilika. Kazi ya kulaza bomba la maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini hadi Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 55.5 umekamilika kwa Asilimia 60.5 na kazi ya kupanua mtambo wa Ruvu Juu na kulaza bomba hadi Dar es Salaam imeanza mwezi Februari, 2014. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Mpango Maalum wa Kuhifadhi na Kutunza Vyanzo vya Maji wa Miaka Mitano (2014/2015 – 2018/2019) ili kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa rasilimali za maji. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Maji kwa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri.

UTAMADUNI NA MICHEZO

Utamaduni

101.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea na urasimishaji wa tasnia za filamu na bidhaa zake  kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika ili kuiongezea Serikali mapato na kulinda kazi za wasanii. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni  kufanyika kwa operesheni ya kufuatilia matumizi ya stempu za kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo zaidi ya  stempu milioni moja za bidhaa za filamu zimetolewa. Jumla ya operesheni nane za kufuatilia filamu zilizoingia sokoni kinyume na taratibu zimefanyika na jumla ya filamu 301 zilibainika kuingia sokoni kinyume na taratibu na wahusika kuchukuliwa hatua. Natoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika Nchi nzima na linakuwa endelevu. Vilevile, natoa rai kwa wananchi kununua bidhaa za filamu zenye viwango zinazothibitishwa na uwepo wa stika maalumu.

Michezo

102.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo ya michezo imetekeleza Mradi wa Kimataifa wa Kukuza Ari ya Michezo wenye  lengo la kuimarisha ushiriki wa vijana na watoto katika michezo bila kujali jinsia ama uwezo. Kutokana na juhudi hizo, katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani yaliyofanyika Nchini Brazil mwezi Aprili 2014, Timu yetu ya Watoto wa Mitaani ya Mkoani Mwanza imetwaa Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani. Napenda kuwapongeza Vijana hao kwa kuiletea Nchi yetu heshima kubwa. Vijana hao wanapaswa kuendelezwa ili waweze kutuwakilisha vyema katika mashindano mengine ya Kimataifa. Aidha, mafanikio hayo yawe chachu ya  kuendeleza michezo mingine Nchini. Ni muhimu tukakumbuka kwamba vipaji vya michezo viko vingi na vimejificha. Kinachotakiwa ni kufanyika jitihada za dhati kuviibua na kuvitumia. Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ishirikiane kwa karibu na Maafisa Utamaduni wa Halmashauri zote nchini kubuni mkakati maalum wa kuibua vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya kitongoji.

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA KIKANDA

103.      Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kufanya vyema katika medani za Kimataifa kufuatia kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutunukiwa Tuzo tarehe 9 Aprili, 2014 kwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo Barani Afrika kwa mwaka 2013, huko Jijini Washington, Marekani. Tuzo hiyo ya heshima kubwa inayotolewa kwa Viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao, hutolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group. Tuzo hiyo imetolewa kutokana na mwelekeo wake thabiti na wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya utawala bora. Vilevile, napenda kumpongeza Dkt. Stergomena Lawrence Tax kwa kushinda kinyang’anyiro cha nafasi ya Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi Agosti, 2013. Namtakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yake na kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Nchi yetu.

104.      Mheshimiwa Spikatarehe 1 hadi 2 Julai, 2013 Watanzania walipokea ugeni mkubwa wa Kiongozi wa Taifa la Marekani, Rais Barack Obama aliyeambatana na mamia ya Wafanyabiashara. Kupitia ziara hiyo, Marekani ilizindua Mpango wa Umeme Afrika (Power Africa), ambao utaongeza kwa mara mbili upatikanaji wa umeme katika Bara la Afrika. Tanzania ni miongoni mwa Nchi zitakazonufaika na Mpango huo unaolenga kuzalisha zaidi ya Megawati 8,000 za umeme katika Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Serikali ya Marekani imeahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 7.  Kampuni za Marekani, Ulaya, Asia na Afrika ziliahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 9 kwa ajili ya Mradi huo kwa miaka mitano ijayo. Nchi yetu pia kupitia ziara hiyo ilipata fursa ya kujitangaza na kujiweka katika nafasi nzuri ya kukuza Uchumi, Biashara, Utalii na Uwekezaji.

105.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji mzuri wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yatafikia ukomo wake mwaka  2015 umeifanya Nchi yetu izidi kung’ara Kimataifa na hivyo kuwa kati ya Nchi 30 zitakazounda kikundi kazi kitakachoandaa Malengo ya Maendeleo Endelevu yatakayotekelezwa  baada  ya  mwaka  2015.  Aidha,   katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi (WEF) uliofanyika mjini Davos, Uswisi mwezi Februari 2014, Mpango wa WEF wa kuvutia uwekezaji katika miundombinu muhimu ulijadiliwa ambapo Bandari ya Dar es Salaam ilichaguliwa kuwa miongoni mwa Bandari zitakazonufaika na Mpango huo. Tayari Timu ya Wataalam imefika Nchini kufanya tathmini ya awali ya mradi huo. Aidha, Kongamano maalum lililohusisha Nchi kadhaa zinazohusika na Mpango wa Uchukuzi wa Ukanda wa Kati lilifanyika tarehe 15 Aprili, 2014. Kongamano hilo lilizinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Vita Dhidi ya Rushwa

106.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea na mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa elimu kuhusu rushwa, athari zake na wajibu wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia semina, midahalo, maonesho ya kitaifa, vipindi vya Radio na Televisheni pamoja na machapisho. Aidha, tuhuma 3,872 zikiwemo tuhuma mpya 679 zilichunguzwa, ambapo hadi sasa uchunguzi wa tuhuma 589 umekamilika. Majalada 4 ya tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa  hatua za kisheria. Katika mwaka 2014/15, TAKUKURU itaendelea kuchunguza tuhuma 3,193 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kuendesha kesi 635 zilizopo Mahakamani hivi sasa na zitakazoendelea kufunguliwa. Vilevile, itaendelea  na uchunguzi wa tuhuma zitokanazo na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za mwaka 2011/2012.


107.      Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi. Lengo ni kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi, kusikiliza Wananchi, kupambana na rushwa na kujenga dhana ya kuaminika kwa Wananchi. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imechapisha, Bajeti yake kwa lugha rahisi za Kiswahili na Kingereza na kuiweka katika Tovuti ya Wizara ya Fedha ili iweze kusomwa na Wananchi wote. Aidha, imeanzisha Tovuti ya Serikali (Government Portal) yenye anuani ya http://www.egov.go.tz/ na Kituo Maalum cha Mawasiliano kwa masuala ya OGP Nchini pamoja na kuimarisha Tovuti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango huo kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Uhuru wa Habari; kukamilisha na kuimarisha Mfumo wa Kuweka Wazi Taarifa na Takwimu kwenye Tovuti.

Maafa

108.       Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kukumbwa na Maafa ambayo yameleta athari kwa Wananchi na mali zao. Katika mwaka 2013/2014, ukame umesababisha upungufu wa Chakula kwa Watu 828,063 katika Wilaya 54 za Mikoa 14 Nchini. Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani ya Shilingi Bilioni 15.2 pamoja na Shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya kukisafirisha hadi kwa walengwa. Mafuriko makubwa pia yametokea katika maeneo mengi hususan, Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Iringa, Kagera na Mara na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu. Katika kukabiliana na athari zilizojitokeza, Serikali na wadau mbalimbali  imetoa misaada ya dharura ya kibinadamu kwa waathirika na imechukua hatua za kurejesha miundombinu ya maji, elimu, afya, barabara na madaraja na umeme. Nitumie fursa hii kulipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania, TANROADS, Wakandarasi,  Wadau mbalimbali pamoja na Wananchi wote kwa kazi kubwa waliyoifanya na misaada waliyoitoa kwa Waathirika  wa  Maafa  yaliyojitokeza.  Napenda kurudia  wito  wangu  kwa  Wananchi  wote  wanaoishi katika maeneo hatarishi hasa mabondeni, kutii maagizo ya Serikali  kuondoka katika maeneo  hayo na kuhamia maeneo yaliyoainishwa ambayo ni salama kwa maisha  yao.      
Aidha, ninatoa wito kwa Wananchi wote kufuata Sheria ili kuepuka uvunjifu wa amani na kusababisha maafa kutokana na mapigano, hasa ya kugombea ardhi na malisho.


109.      Mheshimiwa Spika, mafunzo ya kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana na maafa ikiwemo kupokea na kugawa misaada wakati wa maafa yametolewa katika ngazi za Mkoa na Wilaya kwa Mikoa ya Mara, Geita, Singida, Simiyu, Shinyanga, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora na Arusha. Pia, Mipango ya Kujiandaa Kukabili  Maafa katika Halmashauri za Wilaya za Maswa, Bariadi, Meatu, Mwanga na Same imeandaliwa. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itafanya Tathmini ya Maafa yanayoweza kutokea na uwezo wa kuyakabili pamoja na mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika Halmashauri za Wilaya za Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini, Masasi, Mvomero na Kilosa. Vilevile, itaanza Ujenzi wa Kituo cha Dharura cha Utendaji na Mawasiliano (Emergency Operation and Communication Centre) katika  eneo la Mabwepande Wilayani Kinondoni.

Udhibiti wa Dawa za Kulevya

110.        Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi kubwa  zinazofanywa na Serikali dhidi ya uingizaji na utumiaji wa Dawa za Kulevya, tatizo hili limeendelea kuwa kubwa kutokana na wanaojihusisha na Dawa hizo kubuni mbinu mpya za kukwepa mkono wa Sheria. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendeleza mapambano dhidi ya dawa hizo kwa kuelimisha Umma  kuhusu madhara ya dawa hizo. Serikali pia imepanua  huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia dawa ya Methadone. Huduma za tiba hiyo zinapatikana katika kliniki zilizopo katika Hospitali ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke. Vilevile, imeendesha operesheni zilizowezesha kilo 12,820 za mirungi kukamatwa, ekari 127 za mashamba ya bangi, na kilo 3,445 za mbegu za bangi na magunia 1,107 ya bangi kavu kuteketezwa. Pia, kilo 236.5 za Heroin na kilo tatu za Cocaine zilikamatwa.

111.      Mheshimiwa Spika, katika  mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma na huduma za matibabu kwa watumiaji wa Dawa za Kulevya. Serikali pia itaendelea kuwachukulia hatua kali wahalifu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya Dawa za Kulevya. Vilevile, ili kuondoa mianya inayojitokeza katika kupambana na uhalifu utokanao na biashara ya Dawa za Kulevya, Serikali itakamilisha kutunga Sheria mpya ya Kuzuia   na  Kupambana  na   Dawa za Kulevya itakayowezeshakuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Mazingira

112.      Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2013/14, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2013 hadi 2018, utakaoziwezesha sekta zote kujumuisha masuala ya mazingira kwenye majukumu yao na mipango yao ya maendeleo. Sambamba na hatua hiyo, Serikali iliratibu utekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Moja ya miradi hiyo ni Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (African Adaptation Programme) wenye thamani ya Dola za Marekani  Milioni  2.5  unaofadhiliwa  na  Serikali  ya  Japan. 

Fedha hizo zimetumika kuanzisha miradi ya majaribio ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika Wilaya za Misenyi (Kagera), Mbinga (Ruvuma), Igunga (Tabora) na Zanzibar. Mradi mwingine ni Mradi wa Vijiji vya Mfano vya Mazingira (Eco-Village) wenye thamani ya Euro Milioni 2.2 unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya chini ya utaratibu ujulikanao kama Climate Change Alliance Initiative. Hadi sasa mradi umeainisha Vijiji vya mfano na kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika Mikoa ya Morogoro, Kigoma, Dodoma na Pemba. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa umma kuhusu Sera, Sheria na Mikataba ya Kimataifa ya kuhusu Mazingira pamoja na kuendelea  kuhamasisha kampeni ya upandaji miti Nchi nzima.

Udhibiti wa UKIMWI

113.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014,  Serikali  imeanza kutekeleza  Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI  wa mwaka 2013 hadi 2018. Mkakati huo una shabaha ya kufikia Malengo ya Kimataifa ya  Sifuri Tatu, ikimaanisha Kutokuwa na Maambukizi Mapya,  Kutokuwa na Vifo Vitokanavyo na UKIMWI  na Kuondokana kabisa na Unyanyapaa na Ubaguzi. Hadi Desemba 2013, kati ya watu  1,261,931 walioandikishwa kuwa wanaishi na VVU, watu 669,730 walianzishiwa dawa. Aidha, ili kurahisisha upimaji wa VVU, Serikali imeipatia Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Katavi na Rukwa mashine kubwa za kupima kiwango cha kinga (CD4). Serikali pia imeidhinisha kuanzishwa kwa Mfuko wa UKIMWI, utakaojulikana kama AIDS Trust Fund. Kuanzishwa kwa Mfuko huo kutawezesha kupunguza utegemezi wa Wahisani kwenye shughuli za UKIMWI kwa wastani wa Asilimia 40. 

114.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuimarisha kampeni za uraghibishaji zinazolenga mabadiliko ya tabia ili kuachana na mila na desturi hatarishi. Vilevile,  Serikali  imepanga  kuimarisha  kampeni za  kinga  kwa  vijana  wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 dhidi ya maambukizi ya VVU kwa kutoa elimu.  Juhudi zaidi zitaelekezwa kwenye mikoa 10 yenye maambukizo  zaidi  ya  wastani  wa  Kitaifa  wa  Asilimia 5.1. Mikoa hiyo ni Njombe (14.8), Iringa (9.1), Mbeya (9.0), Shinyanga (7.4),  Ruvuma (7.0), Dar es Salaam (6.9). Rukwa (6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9) na Tabora (5.1). Aidha, Serikali itakamilisha maandalizi ya Sheria ya Mfuko wa UKIMWI.

Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu

115.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendeleza miundombinu muhimu katika Manispaa ya Dodoma. Ujenzi wa Barabara zenye urefu wa kilomita 47.55  kwa kiwango cha lami  katika maeneo ya  Kisasa, Chang’ombe, Kikuyu, Area A pamoja na eneo la Uwekezaji la Njedengwa umekamilika.  Aidha, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 6.4 katika eneo la Nkuhungu na Mwangaza umekamilika. Serikali pia imefungua barabara zenye urefu wa kilomita 105 kwenye maeneo yaliyopimwa ya Miganga, Iyumbu na Ndachi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga mitaro ya maji ya mvua katika maeneo ya Ilazo, Kisasa na Ipagala na kupima viwanja vipya 1,850. Pia ,Serikali itaandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika maeneo ya Mkonze Mashariki, C-centre, Nkuhungu na maeneo yanayozunguka Chuo Kikuu cha Dodoma.

HITIMISHO

116.      Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari nimeelezea baadhi ya shughuli ambazo zimetekelezwa na Serikali katika mwaka 2013/2014. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazotekelezwa katika mwaka 2014/2015. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo yafuatayo:

a.            Uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri, kwa mfano katika mwaka 2011 ulikua kwa asilimia 6.4, mwaka 2012 ulikua kwa asilimia 6.9 na mwaka 2013 kwa asilimia 7.0. Ukuaji huu ni mkubwa ikilinganishwa na Nchi nyingine za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo Wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo ulikuwa asilimia 4.6 mwaka 2011, asilimia 3.5 mwaka 2012 na asilimia 4.5 mwaka 2013. Takwimu zinaonesha pia kwamba kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni cha juu ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa uchumi kwa Nchi za Afrika Mashariki. Kwa mfano, uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia 4.4 mwaka 2011, asilimia 4.6 mwaka 2012 na asilimia 5.0 mwaka 2013. Uchumi wa Uganda ulikua kwa asilimia 6.6 mwaka 2011, asilimia 4.6 mwaka 2012 na asilimia 6.3 mwaka 2013. Takwimu hizo zinadhihirisha kwamba uchumi wetu unaendelea kuimarika ikilinganishwa na nchi nyingine, jambo tunalopaswa kujivunia. Mabadiliko makubwa yanayoonekana Nchini katika sekta za mawasiliano, ujenzi, viwanda na biashara ni matokeo ya ukuaji huu wa uchumi. Tunahitaji kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuhakikisha kwamba ukuaji huu unakuwa endelevu na kuelekeza juhudi zaidi katika sekta nyingine hususan kilimo, ufugaji na uvuvi kwani ndizo zinazotegemewa na Watanzania wengi.

b.            Tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa amani na utulivu. Muungano huu ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni kielelezo kamili cha  umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi jambo lililowezesha kuwepo kwa amani na usalama Nchini. Muungano umetuletea maendeleo makubwa katika miaka 50 ya uhai wake. Ni wajibu wetu kuendelea kuenzi, kulinda na kudumisha Muungano huu kwa nguvu zetu zote.

c.            Tumeingia katika kipindi muhimu katika historia ya Nchi yetu ambapo Bunge Maalum la Katiba limeanza mjadala wa kutunga Katiba Mpya. Ni matumaini yangu kuwa Bunge Maalum litakamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Tatu itakayopelekwa kwa Wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni. Ninawasihi Wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki maalum na kufuatilia kwa makini mjadala wa Katiba kwa kupima mawazo yanayotolewa wakati wa mjadala ili hatimaye kupiga kura ya maoni vyema. Ni matarajio yangu kuwa Katiba Mpya itakayopatikana itatusaidia kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kupata muafaka wa kitaifa wa uendeshaji wa Nchi yetu katika miaka mingi ijayo.

d.            Sote tumeshuhudia juhudi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa nishati Nchini. Mradi wa Ujenzi wa Mitambo ya Kusafisha Gesi Asilia na Bomba la kusafirishia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam unaoendele kujengwa utasaidia sana kuongeza umeme wa gharama nafuu kwenye Gridi ya Taifa. Natoa wito kwa wananchi wote kushirikiana na Serikali kufanikisha miradi hiyo kwa kulinda miundombinu yake pamoja na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa miradi hiyo.

117.      Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika mwaka 2013/2014 na Mwelekeo  wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2014/2015.

SHUKRANI

118.      Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi  Ombeni Yohana Sefue kwa kusimamia Shughuli za Serikali vizuri. Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo kwa michango yao ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.

119.      Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Mheshimiwa  Dkt.  Mary  Michael  Nagu, Mbunge wa Hanang na Waziri wa Nchi (Uwekezaji na Uwezeshaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Ismani na Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa  Aggrey Joshua Mwanri, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi  ya  Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu)  kwa  ushirikiano  walionipa katika  utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri  Mkuu. Nawashukuru  pia  Wakuu  wa  Mikoa na Wilaya  kwa kusimamia shughuli za Serikali vyema katika Mikoa na Wilaya.

120.       Mheshimiwa Spika, ninawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Florens M. Turuka na Bwana Jumanne A. Sagini, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ninawashukuru Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Regina L. Kikuli, Bwana Kagyabukama E. Kiliba,  Bwana Zuberi M. Samataba, Naibu Katibu Mkuu  (Elimu), Dkt. Deo M. Mtasiwa, Naibu Katibu Mkuu (Afya) kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Ninawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/2014.

121.      Mheshimiwa Spika, ninapenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Ninawashukuru sana Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wanaonipa katika kuleta maendeleo ya Jimbo letu.

122.        Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kumshukuru sana Mama Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kuniombea, kunitia moyo na kunivumilia kwa kila hali katika utekelezaji wa majukumu yangu ya Kitaifa. Ninawashukuru sana!!



MAKADIRIO YA  MATUMIZI  YA  FEDHA  YA OFISI  YA  WAZIRI MKUU, OFISI  YA  WAZIRI MKUU - TAWALA  ZA  MIKOA  NA  SERIKALI  ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE  YA MWAKA 2014/2015

123.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/2015, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja na Tano, Milioni Mia Tano Ishirini na Saba na Ishirini na Nne Elfu (105,527,024,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Themanini, Milioni Mia Saba Sitini na Tano na Ishirini na Tisa Elfu (80,765,029,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Ishirini na Nne, Milioni Mia Saba Sitini na Moja, Mia Tisa Tisini na Tano Elfu (24,761,995,000) ni za Miradi ya Maendeleo.

124.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Taasisi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Nne Sabini na Tisa, Milioni Mia Mbili Ishirini na Nne na Sitini na Mbili Elfu (479,224,062,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili Sabini na Tatu, Milioni Sitini na Tano, Mia Nane Tisini na Tano Elfu (273,065,895,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Mbili na Sita, Milioni Mia Moja Hamsini na Nane, Mia Moja Sitini na Saba Elfu (206,158,167,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
125.       Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili Sitini na Saba, Milioni Mia Tisa na Tisa, Mia Tatu Tisini Elfu (267,909,390,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili na Mbili, Milioni Mia Tatu na Kumi, Mia Mbili Themanini na Sita Elfu (202,310,286,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Sitini na Tano, Milioni Mia Tano na Tisa, Mia Moja na Nne Elfu (65,509,104,000) ni za Miradi ya Maendeleo. Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Mbili Thelathini na Moja, Milioni Mia Nne Arobaini na Mbili, Mia Tisa Sabini na Nne Elfu (4,231,442,974,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni Tatu na Bilioni Tisini, Milioni Mia Tatu Sabini, Mia Tatu na Nane Elfu (3,090,370,308,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Sita Themanini na Mbili, Milioni Mia Sita na Mbili na Arobaini na Nne Elfu (682,602,044,000) ni za Miradi ya Maendeleo. Aidha, jumla ya Shilingi Bilioni Mia Nne Hamsini na Nane, Milioni Mia Nne Sabini, Mia Sita Ishirini na Mbili Elfu (458,470,622,000) ni mapato ya ndani ya Halmashauri zote.

126.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Thelathini na Mbili, Milioni Mia Sita Tisini na Sita, Mia Nane Tisini na Nne Elfu (132,696,894,000) kwa ajili ya Mfuko  wa  Bunge  ambapo  Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Tisa Arobaini na Moja, Mia Nne Hamsini na Tano Elfu (123,941,455,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Saba Hamsini na Tano, Mia Nne Thelathini na Tisa Elfu (8,755,439,000) ni za Miradi ya Maendeleo.



MUHTASARI

127.        Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2014/2015 ya jumla ya Shilingi Trilioni Tano, Bilioni Themanini na Nne, Milioni Mia Moja na Tatu, Mia Nne Hamsini Elfu (5,084,103,450,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Thelathini na Mbili, Milioni Mia Sita Tisini na Sita, Mia Nane Tisini na Nne Elfu (132,696,894,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.

128.       Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.

129.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.

Posted By Unknown10:41