Tuesday 29 July 2014

WABUNGE WA TANZANIA WAZITWANGA NGUMI KISA WIVU WA MAPENZI NCHINI MALAYSIA

Filled under:

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanadaiwa kupigana huko Malaysia baada ya kukutana hotelini, wakati wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), walipokuwa katika ziara ya kikazi nchini humo.
Tukio hilo lilitokea siku nne zilizopita baada ya mbunge wa kamati hiyo kutoka CCM kuvamiwa alipokuwa akipata kifungua kinywa kwenye hoteli aliyofikia na wenzake wawili mmoja wa CCM na mwingine wa CHADEMA. Majina ya wabunge hao watatu tunayahifadhi kwa sasa kwa sababu hatukuwapata kujibu tuhuma hizo.

Hata hivyo, mbunge wa CHADEMA ambaye siyo mjumbe wa PAC haikufahamika ilikuwaje akawamo katika ziara hiyo.

Habari zilizolifikia gazeti hili (Mwananchi) jana zinadai kuwa chanzo cha ugomvi huo masuala ya
uhusiano na kwamba mbunge aliyevamiwa alipigwa vibaya.
Chanzo cha mbunge huyo kupigwa kinaelezwa kuwa ni hatua yake ya kuweka ujumbe kwenye mtandao wa WhatsApp unaowaunganisha baadhi ya wabunge, akiwasuta wenzake hao wawili kwamba wamekuwa wakichochea kuvunjika kwa uhusiano wake na mbunge mwenzake.

Ujumbe huo unadaiwa kuambatana na uliotumwa na wabunge hao wawili kwa binti mmoja anayefanya kazi katika benki moja mjini Dodoma ambaye pia anatajwa kuwa na uhusiano na mbunge huyo mwanamume, wakimtaka asiachane naye kwa maelezo kwamba mwenzao huyo atatamba.

Binti huyo alikuwa ametuma ujumbe kwenye mtandao wa pamoja na wabunge hao wawili akieleza kwamba ameamua kuvunja uhusiano wake na mbunge (mwanamume) kwa maelezo kwamba asingependa kuingia kwenye mvutano wa kimapenzi.

Baada ya kutuma ujumbe huo wabunge hao wawili (wanaotuhumiwa kumshambulia mwenzao), wanadaiwa kumjibu wakimsisitiza kuendelea na uhusiano huo mawasiliano ambayo yalikuja kunaswa na mbunge aliyeshambuliwa.

Inaelezwa kwamba baada ya kunasa mawasiliano hayo, mbunge huyo alichukua ujumbe wa wabunge hao kama ulivyo na kuuweka kwenye mtandao unaowaunganisha wabunge wengi akiwasuta kwamba ni wanafiki na kwamba wamekuwa wakihaha usiku na mchana kuhakikisha ‘ndoa’ yake inavunjika.

Kutokana na kuumbuliwa huko, wabunge hao walimvamia mwenzao hotelini na kumpiga mbele ya wenzake. Gazeti hili lilimpigia simu mbunge anayedaiwa kumpiga mwenzake kwa kiasi kikubwa na baada ya kuelezwa tukio zima na kabla ya ufafanuzi, alikata simu bila kujibu chochote.

Kiongozi wa msafara huo Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alipopigiwa simu na mwandishi wetu hata kabla ya kuulizwa kuhusu ugomvi huo alisema: “Hakuna kilichotokea. Mimi ni mwandishi wa habari kama wewe, hakuna kilichotokea na hakukuwa na ugomvi wowote.”

Alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka mtindo wa wabunge kusingiziwa kuwa wamefanya jambo fulani, huku akisisitiza kuwa kama kulizuka ugomvi asingeweza kuficha chochote.

via gazeti Mwananchi

Posted By Unknown01:06

SERIKALI YA TANZANIA YAZUIA AJIRA ZA IDARA YA UHAMIAJI

Filled under:


Serikali ya Tanzania  yazuia ajira za Idara  za Uhamiaji kwa madai ya upendeleo wa kindugu na kujuana.

Posted By Unknown00:42

WATUHUMIWA 10 WA UJAMBAZI WAKAMATWA NA SILAHA NZITO

Filled under:

 
MAJAMBAZI 10 wanaounda mtandao hatari wa uhalifu nchini, wametiwa mbaroni wakati wa msako mkali uliofanikisha pia kukamatwa kwa silaha mbalimbali.
Silaha hizo ni bunduki tisa zikiwemo SMG tatu, bastola mbili, short gun nne na risasi 15 zilikamatwa.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliyasema hayo ofisini kwake kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Majambazi hao wamekamatwa katika msako mkali unaoendelea jijini Dar es Salaam katika harakati za kuhakikisha kwamba maisha na mali za wakazi wa Dar es Salaam vinalindwa kikamilifu.

Katika msako huo watuhumiwa walisachiwa katika miili, makazi, na maficho yao na wakakamatwa na jumla ya silaha 9 kama ifuatavyo:-
  1. SMG NO. 13975 ikiwa na risasi 11 na magazine 2
  2. SMG 1 haikuwa na magazine na namba hazisomeki.
  3. BASTOLA 1 aina ya LUGER yenye namba 5533K
  4. BASTOLA 1 aina ya BROWNING yenye namba TZACR83494 S/No.7670 Na risasi 6 ndani ya magazine.
  5. S/GUN PUMP ACTION na risasi 55
  6. MARCK IV iliyokatwa mtutu na kitako yenye magazine 1 na risasi 4
  7. BASTOLA 1 yenye namba A963858 browning ambayo ina risasi 1
  8. SMG 1 ambayo iko kwa mtaalam wa uchunguzi wa silaha (Balistic)
  9. SHOT GUN TZ CAR 86192 ilitelekezwa baada ya msako

Majina ya watuhumiwa ni ifuatavyo:-

1. MAULIDI S/O SEIF MBWATE miaka 23, mfanyabishara, mkazi wa Mbagala Charambe.

2. FOIBE D/O YOHANES VICENT miaka 30, hana kazi, mkazi wa Mbagara Kibondemaji.

3. VICENT S/O OGOLA KADOGOO miaka 30, mkazi wa Mbagara Kibondemaji

4. SAID S/O FADHIL MLISI – miaka 29, dereva wa Bodaboda, Mkazi wa Gongolamboto

5. HEMEDI S/O AWADHI ZAGA miaka 22, dereva wa Bodaboda, mkazi wa Gongolamboto

6. MOHAMED S/O IBRAHIM SAID miaka 31, Fundi welder mkazi wa Kigogo.

7. LUCY MWAFONGO. Miaka 41, mama lishe mkazi wa Vingunguti Ukonga

8. RAJABU S/O BAHATI RAMADHANI, miaka 22, Mkazi wa Kariakoo

9. DEUS JOSIA CHILALA miaka 30, Mgonga Kokoto Kunduchi , mkazi wa Yombo Kilakala.

10. MARIETHA D/O MUSA miaka 18, mkazi wa Yombo Kilakala

Mwanamke pekee katika kundi hilo anayejulikana kwa jina la FOIBE D/O YOHANES VICENT ameshiriki katika matukio ya uporaji wa kutumia silaha, mauaji, n.k. na yeye mwenyewe alikuwa akitumia bunduki aina ya SMG.

Katika baadhi ya matukio wananchi walioshuhudia matukio haya wamekuwa wakitoa taarifa kwamba alikuwepo mwanamke aliyekuwa akifyatua risasi na hatimaye polisi walifanikiwa kumkamata akiwa na wenzake katika kundi hilo.

Licha ya kukamatwa kwa mtandao huu hatari Jeshi la Polisi linaendelea na misako ya mitandao mingine ya ujambazi kwa madhumuni yaliyotajwa hapo juu.

Hivyo tunawashukuru wananchi kwa namna walivyoendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu.

Majambazi hao watafikishwa mahakamani baada ya Mwanasheria wa Serikali kutafuta majalada yao ya kesi mbali mbali.

S.H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

Posted By Unknown00:29

Monday 28 July 2014

SIRI NZITO YAZIDI KUVUJA KUHUSU VIUNGO VYA BINADAMU

Filled under:



SIKU moja baada ya serikali kufunga Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), kwa madai ya kuendeshwa kwa kukiuka taratibu za tiba, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa hatua hiyo imefikiwa ili kukinusuru chuo hicho na adhabu ya utupaji viungo vya binadamu.

Kwamba uamuzi huo umefikiwa kutuliza hasira za makundi mbalimbali, kikiwamo Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), waliolaani utupaji huo.

Wakati hatua hiyo ikionekana kutaka kunusuru kufungwa kwa chuo, viongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo wamesema kikifungwa watakuwa wanaonewa kwakuwa wanaostahili adhabu ni utawala.

Chanzo hicho kimesema kama chuo hicho kingefungwa, ingeathiri wanafunzi wengi ambao wengine wanasubiri kufanya mitihani yao ya mwisho kumaliza elimu yao ya tiba.

Tanzania Daima Jumapili, lilidokezwa kuwa kitendo cha Manispaa ya Kinondoni kufanya ukaguzi huku timu za uchunguzi wa suala hilo zikiwa kazini, kinalenga kutoa ahueni kwa chuo kuendelea na shughuli zake.

Itakumbukwa kuwa  serikali iliunda tume ya watu 15 kuchunguza jambo hilo, huku nalo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam likiteua timu ya kufuatilia watuhumiwa waliohusika na utupaji viungo hivyo.

Tanzania Daima Jumapili, limebaini kuwa ufungaji hospitali hiyo unaonekana uliratibiwa mapema kwakuwa wakati timu ya wakaguzi hao ikifika hospitalini hapo, hakukuwa na mgonjwa aliyelazwa tofauti na ilivyo kawaida.

Gazeti hili lilikuwapo eneo la tukio na kushuhudia maeneo mbalimbali yakiwa yamesafishwa kuashiria kutegemea ugeni.

Baadhi ya wafanyakazi walidokeza kuwa adhabu ya kufungwa kwa hospitali hiyo inaweza kukinusuru chuo kwakuwa ripoti itakayotolewa na tume ya watu 15 iliyoundwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inaweza kutoa pendekezo la aina hiyo.

“Adhabu hii ya kufunga hospitali ni kama kinga ya kuunusuru uongozi wa chuo hicho ambao kimsingi na kisheria ndio wanaostahili kufanya kazi za utafutaji, usafirishaji, utunzaji, uhifadhi na kuzika au kuchoma miili hiyo kwa kufuata miiko ya kazi hiyo inavyotaka,” kilisema chanzo hicho.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kufungwa kwa chuo hicho kungekuwa na hasara zaidi kuliko ilivyofungwa hospitali.

Juzi timu ya Menejimenti ya Afya ya Manispaa ya Kinondoni, iliyokuwa imeongozana na Mganga Mkuu wa Manispaa, Dk. Gunini Kamba, wameifunga hospitali hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa upungufu sehemu mbalimbali.

Alisema upungufu walioubaini ni kutokuwa na wauguzi, vifaa vya kutosha, sehemu ya kuteketeza taka ngumu, wamekuwa wakichanganya dawa zilizokwisha muda na ambazo zinatumika katika kabati moja.
Dk. Gunini alisema: “Upungufu wa madaktari umesababisha tumkute mfanyakazi mmoja wa msalaba mwekundu akifanya kazi za madaktari.”

Alisema kuwa kama viongozi wa IMTU watataka kuendelea na huduma ya hospitali, wanatakiwa kurekebisha matatizo hayo waliyoambiwa ikiwamo kutuma maombi upya kwa kuanzia manispaa.

Serikali ya wanafunzi yanena
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa IMTU, Meekson Mambo, alisema tangu sakata hilo lianze, limesababisha wanafunzi kushindwa kusoma kwa uhuru na muda mwingi kuutumia katika kutafakari hatima yao.

Mambo, alisema wanapinga vikali kauli ya Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Primus Saidia ya kutaka serikali ikifute chuo hicho.

Rais huyo alisema kuwa kiongozi wa MAT, alitoa kauli hiyo bila kutafakari kwa kina mustakabali wa uamuzi anaotaka uchukuliwe, kwani hatua hiyo ni sawa na kutaka kuwahukumu wanafunzi wasiohusika na tukio hilo.
Alifafanua kuwa alitarajia Dk. Saidia, angesikiliza maoni ya wanafunzi juu ya tukio hilo na kuwaona viongozi na mmiliki wa chuo kupata ukweli.

Aliongeza kuwa uamuzi wowote utakaofanywa kukifuta chuo hicho utakuwa na athari kubwa kwa wanafunzi, na hawatakubali hatua hiyo.

“Tumeshawaambia watu wanaofanya uchunguzi kuwa hatutakubali wazo la kufutwa kwa chuo au kufungwa… sisi tuna kosa gani, kina nani walitupa viungo?” alihoji.

Waziri Mkuu wa Serikali hiyo, Edward Mhina, alisema jumuiya yao inalaani kitendo cha utupaji wa miili hiyo kwa kuwa inakiuka maadili na sheria za mafunzo ya udaktari.

“Tanzania ina uhaba wa madaktari, MAT inashinikiza chuo hiki kifutwe, tunaelekea wapi? Tuache vyombo vya dola vifanye kazi yake,” alisema.

Mabaki ya miili ya binadamu yaliyokuwa kwenye mifuko 85 ya plastiki, yalikutwa wiki iliyopita yakiwa yametelekezwa maeneo ya Mto Mpiji, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na haikujulikana mara moja imetoka wapi, kabla ya polisi kufanya uchunguzi.

Miili mingi inatoka nje
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kwamba mabaki ya miili mingi inayotumika kwenye hospitali kwa ajili ya mazoezi ya vitendo inatoka nje ya nchi, hasa zile zenye vita.

Kwa mujibu wa madaktari mbalimbali, mara nyingi maiti zinazokaa muda wa kuanzia miezi sita hadi mwaka bila kutambuliwa na ndugu zao ndizo hutumika katika mazoezi ya tiba kwa wanafunzi.

Hata hivyo, Tanzania Daima Jumapili, limeelezwa kuwa Tanzania haina uwezo wa kuzalisha maiti nyingi za kufanyia mazoezi ya tiba, bali hutegemea kutoka nje ya nchi kwa msaada wa taasisi mbalimbali za kimataifa.
Imebainishwa kuwa lengo la kufanya hivyo pia ni kuepusha madakatari wanafunzi kukutana na viungo vya watu wanaowafahamu au nduzu zao.

Katika sakata hilo lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani, katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo madaktari wa IMTU, walikamatwa na polisi kwa mahojiano, wakituhumiwa kuhusika katika utupaji viungo vya binadamu jalalani.

Posted By Unknown02:27

KATIBA MPYA:WASSIRA,LIPUMBA NA LISSU WACHUANA VIKALI

Filled under:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira akiwakilisha CCM, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jana walitoana jasho katika mdahalo wa Katiba ulioandaliwa na East African Business and Media Institute.

Mdahalo huo uliohudhuriwa na watazamaji wapatao 500, ulikuwa na mada inayosema: ‘Nani anakwamisha Upatikanaji wa Katiba Mpya.’ Kila upande ulitumia fursa hiyo kutupa shutuma kwa mwingine huku jazba na kelele vikitawala miongoni mwa waliohudhuria.
Hata hivyo, suala la muundano wa serikali ndiyo uliochukua nafasi kubwa katika mdahalo huo huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukiishutumu Serikali ya CCM kuwa ndiyo kikwazo cha upatikanaji wa Katiba Mpya nayo ikitupa mpira huo kwa Ukawa kwa kitendo chake cha kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba.
Profesa Lipumba alisema wahafidhina wa CCM ndiyo waliomshauri Rais Jakaya Kikwete abadilike kimsimamo kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya.
“Rais Kikwete alikuwa na nia njema kabisa kuhusu Katiba Mpya lakini wahafidhina wa CCM wanaopenda madaraka walipoona muundo wa serikali tatu wakambana naye akabadilisha msimamo, tunamwomba abadilike, nchi hii ni yetu sote ili tupate katiba ya wananchi,” alisema.
Lissu aliongeza kwa kusema kuwa anayekwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni CCM ambao wanaweka maoni yao badala ya kujadili rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo maoni ya wananchi.
“Hatuwezi kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwenda kujadili rasimu ya CCM kwa sababu wanaonyesha hawana nia ya Katiba Mpya, bali wanataka kuwadanganya Watanzania, watawadanganya wananchi kwa kuleta Katiba ileile ila ikiwa na rangi tofauti,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema Ukawa hawawezi kushiriki katika udanganyifu wa aina hiyo na kwamba wameamua kuwaachia CCM ili wananchi waweze kuwahukumu kwa uovu watakaoufanya.
Alisema kati ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika Kundi la 201, wajumbe 166 ni wana CCM walioteuliwa ili kuongeza idadi ya watu.
“Humo kuna viongozi wa dini mashehe na maaskofu na waganga wa kienyeji ambao ni wana CCM ili wapitishe Katiba yenye masilahi yao binafsi,” alisema.
Hata hivyo, Wassira alisema hoja za Ukawa hazina mashiko na kumtaka Lissu kuwaomba radhi masheikh na maaskofu kwa kuwa hawakuteuliwa na Rais kutokana na kuwa wanachama wa CCM, bali ni mapendekezo ya taasisi wanazozitumikia.
“Namwomba Tundu Lissu akawaombe radhi masheikh na maaskofu kwa sababu kundi hili liliteuliwa kutokana na mapendekezo ya wahusika wenyewe pasipo shinikizo la Rais. Hapakuwa na uwezekano wa Rais kuwatambua wana CCM ili awateue wanaofaa. Kama ana ugomvi na Kingunge Ngombale Mwilu aseme.”

Alisema wanaokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni Ukawa... “Katiba Mpya haiwezi kupatikana mitaani, bali kwa majadiliano na maridhiano kwenye Bunge Maalumu la Katiba, nawashauri warudi bungeni ili tuweze kupata Katiba Mpya.”
Alisema Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka ya kubadilisha vifungu kwenye rasimu ya Katiba na kwamba halipo kwa ajili ya kupitisha tu vifungu vilivyowekwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ya Wassira ilifanya kila aliposimama kuzomewa na wananchi waliohudhuria mdahalo huo huku wafuasi wa Chadema na CCM wakitishiana kupigana hali iliyosababisha mabaunsa kuwatoa nje ya ukumbi baadhi yao walioshindwa kustahimiliana.
Wajumbe wawili waliokuwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole na Awadh Said, katika michango yao walitaka kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi ili kupata katiba itakayowafaa kwa muda uliokusudiwa.
Polepole alisema tatizo la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni masilahi binafsi na ya makundi katika utafutaji wa Katiba Mpya.
“Wananchi wasimamie masilahi ya taifa na wasiwaachie mchakato mzima wanasiasa ambao wana masilahi binafsi pamoja na yale ya kikundi yenye shinikizo la masilahi binafsi,” alisema Polepole.
Awadh alisema maoni yalikusanywa kutoka katika mabaraza ya katiba 170 na 600 ya taasisi na vyama vya siasa kutoka katika wilaya zote 43 za Zanzibar.
“Kwa nini juhudi zote hii zibadilishwe na wajumbe 629 peke yao kwenye Bunge Maalumu la Katiba?  Tufuate maoni ya wananchi kupitia tume ndipo tutakuwa tunawatendea haki Watanzania,” alisema.
Alielezea kusikitishwa na kitendo cha Serikali kufunga tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba akisema kimewanyima wananchi haki ya kupata taarifa mbalimbali za tume hiyo.

Posted By Unknown01:54

TAARIFA ZILIZOTOLEWA HIVI KARIBUNI KUHUSU UGONJWA WA DENGUA

Filled under:

Gazeti la Mwananchi limechapisha habari kuwa kasi ya kuenea kwa homa ya dengue hapa nchini imepungua baada ya taarifa kuonyesha kuwa hakuna mgonjwa mpya kuanzia Julai 15.
Dk Vida Mmbaga, mtaalamu wa Kitengo cha Epidemiolojia cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alisema kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo ambao umeathiri watu 1384, inaendelea kupungua.

Alisema hadi sasa hakuna mgonjwa aliyelazwa wala kubainika kuwa virusi vya ugonjwa huo.

Alisema hii ni mara ya tatu kwa homa ya dengue kuibuka nchini. Mara ya kwanza ilikuwa Julai 2010, Juni 2013 na mwaka huu ambao umesababisha madhara zaidi.

Dk Vida alisema tangu kutokea kwa ugonjwa huo ni watu wanne tu kutoka Dar es Salaam waliopoteza maisha.

Posted By Unknown01:37

Thursday 24 July 2014

MNADA WA HADHARA WA VIFAA VYA UBALOZI WA SWITZERLAND,FINILAND AND SWEDEN

Filled under:

UBALOZI WA SWITZERLAND, FINLAND
& SWEDEN


MNADA WA HADHARA:

UNIVERSAL AUCTION CENTRE Kwa idhini waliyopewa na Ubalozi wa Switzerland, Finland & Sweden  watauza kwa mnada wa hadhara  Magari, Generators & Fanicha za Ofisi na nyumbani tarehe 26 July, 2014 Jumamosi saa 4.00 asubuhi. Mnada utafanyika Golden Resort Sinza,  Lion Street.

MALI ZITAKAZOUZWA:

Sofa sets, Dining Table & chairs, Coffee table, Book Shelves, Meza za ofisi/viti, File
cabinets, Fridges, Cookers, TV set, Washer, Dryer, Camping Tents, Computer set, Photocopy m/c,  A/c split units Etc.

MAGARI YATAKAYOUZWA:


Mali zote zinaweza kukaguliwa Golden Resort Sinza,Lion Street tarehe 24 na 25 July,  2014 kuanzia saa 4.00. asubuhi mpaka saa 10.00 jioni.

MASHARTI YA MNADA:

Mnunuzi  wa fanicha atatakiwa kulipa malipo yote pale pale. Na mnunuzi wa Generator/gari atatakiwa kulipa 25% pale pale na salio lilipwe ndani ya siku 7 ukishindwa kulipa kwa muda huu gari litauzwa tena na dhamana haitarudishwa.

Mali zote zitauzwa kama zilivyo.

Mnunuzi atawajibika kulipa ushuru.

Mali yote iliyouzwa itatakiwa kuondolewa siku hiyo hiyo  baada ya kulipia malipo yote pamoja na ushuru

Kwa maelezo zaidi waone:

UNIVERSAL AUCTION CENTRE
NKRUMAH STREET MKABALA NA CO-CABS
SIMU NA:  0754-284 926, 0757 284 926               Email : universalauction@hotamail.com

DAR ES SALAAM.

Posted By Unknown10:58

NDEGE YA AIR ALGERIE IMEPOTEA IKIWA NA ABIRIA 116

Filled under:

Ndege ya Air Algerie imetoweka ikiwa na abiria 116

Shirika la ndege la Algeria , Air Algerie, limesema kuwa limepoteza mawasiliano na moja ya ndege zake ilipokuwa ikitoka mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou.

Afisa huyo anasema kuwa ndege hiyo ya Air Algerie ilikuwa imepaa dakika 50 katika anga ya Sahara mara ya mwisho mawasiliano yao.

Ndege hiyo iliokuwa inaeelekea mji mkuu wa Algiers, ilikuwa na watu mia na kumi na wahudumu sita .
Oparesheni ya dharura ya kuitafuta ndege hiyo imeanzishwa,

Ndege hiyo nambari AH 5017 inamilikiwa na shirika la ndege la kihispania la Swiftair.

Mwandishi wa BBC Alex Duval Smith aliyeko katika mji mkuu wa Mali Bamako anasema kuwa kuna habari kuwa ndege hiyo huenda ilianguka katika eneo la janga la sahara kati ya
mji wa Gao and Tessalit .

Mwandishi huyo wa BBC ananukuu ripoti kutoka kwa wanajeshi wa kulinda amani walioko huko Mali na duru za shirika la habari la AFP.

Brigadia mkuu wa majeshi ya kulinda amani nchini Mali Koko Essien, amesema kuwa maeneo hayo ya jangwani yana idadi ndogo sana ya wakaazi kwa hivyo ni vigumu kupata habari kutoka huko na inawabidi kutafuta ilikoanguka ndege hiyo.
                     
Ndege ya Air Algerie imetoweka ikiwa na abiria 116
Aidha Brig Essien anasema kuwa eneo hilo linamilikiwa na wapiganaji waasi .

Wamiliki wa ndege hiyo Swiftair wamesema kuwa ndege hiyo aina ya MD83 ilikuwa imeomba kubadili uelekeo wake kutokana na hali mbaya ya anga na ukungu mkubwa karibu na mpaka wa Algiers.

Ndege namba AH 5017 husafiri kupitia njia ya Ouagadougou-Algiers mara nne kwa wiki,AFP imeripoti.

Raia wa Algeria ni miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya Ndege hiyo,Gazeti moja la Algeria limeripoti.

Mwezi Februari ndege ya kijeshi ya Algeria ilianguka na kuuwa watu 77 waliokuwemo.

Tukio hili la hivi punde Linaloongeza wasiwasi kuwa njia inayotumiwa na misafara ya ndege ziendazo sehemu hiyo inapitia eneo lenye utata la anga ya Mali.

Posted By Unknown10:29

Wednesday 23 July 2014

TIBA,KINGA YA UKIMWI YAGUNDULIKA

Filled under:

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple, Marekani wamegundua dawa ya kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambayo ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na zilizowahi kupatikana katika tafiti za awali duniani.
 
Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari juzi mjini Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao wamegundua namna ya kukiondoa kirusi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua.
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa kupenya ndani ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake, ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).”
ARV huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi mwathirika anapoacha kutumia dawa.
Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU.
“Kama imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo likawa gumu.
“Inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.

 Lazima dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na utendaji wa mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi zinaposhindwa… Tusubiri tuone hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” alisema Majani.

Mkutano wa Ukimwi
Ugunduzi huo umekuja wakati wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli za kukata tamaa kwenye mkutano wa Ukimwi unaomalizika kesho huko Melbourne, Australia.
Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za utafiti za VVU wameweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio kwa sababu dawa zake zinapotumika, vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya.
“Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili ili visiathirike na kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty ya Australia, Profesa Sharon Lewin.

Dawa mpya inavyofanya kazi
Dk Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa protini maalumu ambayo inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta nje.
Baada ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga mwilini mwa binadamu bila tatizo.
VVU kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha kuzalishia virusi vingine.
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk Khalili.
Alisema tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama.

Katika maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Dk Khalili anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache... “Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu.”
Alisema wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya tiba ya binadamu.
Kwa namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema wanaweza kuitumia kwa ajili ya kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa na hata kuwakinga wale ambao siyo waathirika.
Uzuri wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo kuingiliana kiutendaji.
Ugunduzi wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa la Elimu ya Sayansi la National Academy of Science la Marekani na kuonekana kuvuta hisia za wengi.

Hali ya Ukimwi duniani
Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa Lewin alisema tafiti za sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 14 duniani wanaishi na VVU.
Alisema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Alisema ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha matumaini waliotarajia ya kupata kinga na chanjo, bado juhudi zinaendelea ili kuhakikisha wanafikia mahali HIV inakuwa haina nafasi katika mwili wa mwanadamu.
Alisema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, bado anaamini kwamba ipo siku chanjo na tiba vitapatikana.
Wanasayansi waliohudhuria mkutano huo waliitaka dunia isiogope kutokana na kushindwa kwa baadhi ya tafiti kama ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la Mississippi, nchini Marekani ambaye alitangazwa amepona na baadaye virusi vikaibuka upya.

Posted By Unknown23:13

TAARIFA RASMI ILIYOTOLEWA NA POLISI KUHUSU KUTUPWA VIUNGO VYA BINADAMU MAENEO YA BONDE LA BWENI

Filled under:

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE

22/07/2014

WATU WANANE WAKIWEMO MADAKTARI WASHIKILIWA NA KUHOJIWA NA JESHI LA POLISI KUTOKANA NA KUTUPWA VIUNGO VYA BINADAMU MAENEO YA BONDE LA MBWENI MPIJI ENEO LA BUNJU 


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu wanane na kuwahoji kuhusu tukio la kupatina kwa viungo vya binadamu vilivyogundulika katika maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji ambapo mifuko ya plastiki ipatayo 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu yaligundulika. Polisi walipata taarifa 21/07/2014 jioni kutoka kwa wasamaria wema na ndipo jopo la wapelelezi likiongozwa na Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ACP. Camilius Wambura walifika hapo majira ya saa 1.00 usiku.

Walipofika katika tukio waligundua mifuko ipatayo 85 mieusi yenye viungo vya aina mbali mbali vya binadamu kama vile Vichwa, Miguu, Mikono, Mioyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbali mbali ya binadamu. Viungo hivyo havikuwa na uvundo au harufu ya aina yoyote na vilionekana kwamba vimekaushwa na kukakamaa. Katika eneo hilo pia vilikutwa vifaa vinavyotumika hospitali kama vile mipira ya kuvaa mikononi (gloves) mifuko miwili iliyotumika ,nguo maalum (apron) zipatazo 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.

Wananchi wasiopungua 1,000 walifika katika eneo hilo la tukio lakini hakuna aliyekuwa na taarifa sahihi. Viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Aidha jopo la Wapelelezi chini ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ACP. Japhari Mohamed walianza uchunguzi mara moja kwa kusaidiana na Daktari wa Jeshi la Polisi anayehusika na uchunguzi wa miili ya binadamu (Forensic Doctor) ambaye kwa pamoja walishirikiana na madaktari wengine kutoka hospitali wa Taifa Muhimbili.

Hatimaye uchunguzi wa kina ulibaini kwamba viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika Maabara ya Chuo Kikuu Madaktari IMTU jijini D’Salaam. Baada ya kugundulika hivyo Polisi wamewakamata na sasa wanaendelea kuwahoji watu wanane ambao wanasadikiwa kuhusika na miili hiyo ikiwa ni pamoja na baadhi ya madaktari wa IMTU. IMTU (International Medical and Technolegical University) ni chuo Kikuu cha Madaktari ambacho pia hufanya mafunzo ya udakitari kwa vitendo (practical). Jeshi la Polisi Kanda Maalum litamuhusisha Mkemia Mkuu wa Serikali na hatimaye mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi jalada litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zake ili sheria ichukue mkondo wake.

S. H. KOVA

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

Posted By Unknown22:29

MTIKILA AENDA KORTINI KUOMBA AINGIZWE KWENYE KESI YA IPTL VS KAFULILA

Filled under:

MWENYEKITI wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, ameomba kuunganishwa katika kesi ya madai inayomkabili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.

Awali, Kafulila akizungumza kwenye mjadala katika eneo la Urusi Mwanga mjini Kigoma jana, alisema Mchungaji Mtikila ameomba kuwa mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo huku Chama chake cha DP kikiwa mshitakiwa wa tatu.

Pia alisisitiza kuwa kamwe hakukurupuka kuibua kashfa hiyo ya ufisadi katika akaunti ya Escrow na
kwamba, yuko tayari kwa lolote.
“Nimefarijika kuona wenzangu wananiunga mkono katika mapambano dhidi ya ufisadi na Mchungaji Mtikila ameomba kuwa mshitakiwa wa pili,” 
alisema Kafulila.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mchungaji Mtikila, alikiri kuwa amekubali kuunganishwa kwenye kesi hiyo inayomkabili Kafulila.
“Nimekubali kuunganishwa katika kesi hiyo ili kutetea haki ya wananchi wa nchi yetu kama Katiba inavyosema,” 
alisema.

Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL), imefungua kesi ya madai dhidi ya Kafulila katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, ikiomba aamriwe kuilipa fidia ya sh. bilioni 310 kutokana na kutangaza taarifa za kashfa dhidi yao na hasara ya taswira ya biashara na hadhi yao.

Fadhili Abdallah, Kigoma

Posted By Unknown22:18

TAMKO LA CHADEMA KUHUSU KUONDOKA KWA WALIOKUWA VIONGOZI

Filled under:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kigoma Kaskazini tunapenda kutoa taarifa kwa umma kutokana na sintofahamu inayotaka kulazimishwa mbele ya jamii kuhusu uimara wa chama chetu mkoani Kigoma.

Tangu jana na leo kumeenea taarifa zinazowahusu watu watatu, Jaffari Kasisiko, Msafiri Wamarwa na Mama Malunga Masoud, ambao vyombo mbalimbali vya habari vimeandika kuwa wamehama chama chetu cha CHADEMA na kukimbilia wanakojua wao (maana CCM inafanya kazi zake katika sura mbalimbali).
Katika hatua ya awali, sisi CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini tungependa kusema machache juu suala hilo la watu hao kuhama;

1. Kwanza watu hao mbali ya kwamba walikuwa ni viongozi wa chama ngazi ya mkoa, kwa uhakika kabisa walikuwa ni kikwazo kama si kizuizi cha muda mrefu sana kwa chama chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika mkoa mzima wa Kigoma ili kiweze kukimbizana na wenzetu wa maeneo mengine nchi nzima. Badala yake walikikumbatia na kukiatamia chama. Wakati maeneo mengine wenzetu wakiongeza wabunge majimboni, Kigoma chini ya uongozi wao ikauza majimbo.

2. Tunaweza kusema kuwa viongozi hawa pamoja na wengine wachache ambao tunajua wako mbioni kuondoka kati ya leo na kesho, walikuwa ni sawa na KOTI LILILOTUBANA. Kwa muda wao wote wa uongozi hawakuwahi kufanya kazi yoyote ya kioganazesheni na kukieneza chama mkoa mzima. Wao walikuwa watu wa mikutano ya hapa na pale Kigoma mjini pekee au pale ambapo kunakuwa na uongozi wa kitaifa au wabunge.

3. Kwa muda mrefu saa wamekuwa viongozi ‘waliotubana’ kwa sababu walifanya kazi kwa kuangalia zaidi maslahi yao. Sasa kuondoka kwao, ni nafuu kwa chama. Pia ni fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka kwa wanachama makamanda waaminifu na watiifu waliofungiwa milango kwa muda mrefu, kusonga mbele kukijenga chama chetu kwa imani kubwa ya kuendelea kubeba matumaini ya Watanzania wanyonge.

4. Upo ushahidi wa wazi katika hili. Kwa muda mrefu sasa viongozi hao na wengine wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine, wamekuwa wakilalamikiwa kufanya kazi ya chama kingine cha siasa kwa maslahi na maelekezo ya CCM.

5. Katika madai yao ya kuhama chama watu hao wamesema wamefikia hatua hiyo eti kutokana na chama chetu kuwa cha kibabe eti kwa sababu tu Zitto Kabwe alivuliwa nafasi Naibu Katibu Mkuu ndani ya chama!

6. Madai hayo yanashangaza kwa sababu mbali ya chama kuwa na sababu nzito za kumvua Zitto (na wenzake akina Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) cheo hicho kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu, pia tunaamini hakuna mwanaCHADEMA amejiunga na chama hiki kwa ajili ya cheo. Ndani ya chama chetu tunaamini katika kugawana majukumu si vyeo.

7. Katika hali ya kushangaza zaidi wanasema eti Zitto amezuiwa kugombea uenyekiti. Sasa tunajiuliza hiyo nia ya kugombea ambayo hatujawahi kuisikia ikitangazwa kwa kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na itifaki za chama, waliambizana wao wenyewe na mtu wao? Lakini kwa wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma tunaelewa Jafari Kasisiko analipa fadhila za misaada binafsi ikiwemo kupelekwa nje ya nchi.

8. Ninaomba kutoa wito kwa viongozi wenzangu wa wilaya na majimbo ya Kasulu Mashariki, Muhambwe, Buyungu, Kasulu Magharibi, Manyovu, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini na Kigoma Mjini, tukutane kwa ajili ya kikao cha Baraza la Mashauriano la Mkoa ili sasa tuchukue hatua zingine za muhimu na haraka za kuhakikisha tunasafisha chama chetu kwa kuwaondoa vibaraka na wasaliti wote waliosalia.

9. Pia tunaomba katika hali ya dharura Chama Makao Makuu pia kiingilie kwa kutumia kifungu cha Katiba 6.1.3, ili kupata chombo cha kuendelea kuwaunganisha wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua hatua hiyo kupitia Baraza la Mashauriano.

10. Sisi wa CHADEMA Kigoma Kaskazini tunawataka wale wengine waliosalia katika mkakati huo wa kuhamisha watu wachache lakini kwa makundi ili eti kujenga taswira ya CHADEMA kubomoka, wakiwemo viongozi kadhaa wa Kanda wasisubiri. Chama chetu kitajengwa na watu wenye imani watakaoweka maslahi na matakwa ya wananchi mbele kwa kuzingatia misingi yetu kama inavyoelezwa katika Katiba ya Chama, kanuni, maadili na miongozo.

Kwa niaba ya Wanachadema imara na makamanda watiifu na waaminifu kwa mabadiliko yanayobeba matumaini na haki za Watanzania wanyonge, naomba kutoa taarifa hii.

Ally Kisala

Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini
Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma

Posted By Unknown02:31

WATUMISHI WA NMB MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUUIBIA BENKI BILIONI 1

Filled under:

WATU watatu, akiwemo mtumishi wa Benki ya NMB, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka 13, yakiwemo ya kuiibia benki hiyo zaidi ya sh. bilioni moja na kutakatisha fedha haramu.

Mtumishi wa benki hiyo, Mtoro Suleiman, Daudi Kindamba na John Kikopa, walisomewa mashitaka hayo jana na Wakili wa Serikali Pius Hilla, mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.


Hilla aliwasomea washitakiwa hao mashitaka ya kula njama, kuiibia benki hiyo sh. 1,029,454,383, kufanya udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababishia benki hiyo hasara ya kiasi hicho.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, 2007 na Julai 30, 2009 katika makao makuu ya benki hiyo, mkoani Dar es Salaam.
Alidai katika kipindi hicho, mkoani Dar es Salaam, washitakiwa kwa udanganyifu na bila haki, waliiba kiasi hicho cha fedha.
Mtoro anadaiwa katika kipindi hicho, makao makuu ya NMB, yaliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa mtumishi wa benki hiyo, aliingiza maingizo yasiyo sahihi katika akaunti maalumu na kuhamisha sh. milioni 579.8 kwenda akaunti binafsi ya Kindamba.


Pia, Mtoro anadaiwa kuhamisha sh. milioni 389 kutoka akaunti ya NMB kweda akaunti ya Cariton Trading Co. Industrial na alihamisha tena sh. milioni 60.5 kwenda akaunti ya Jacques Investment.

Mtoro anadaiwa katika kipindi hicho, alitakatisha fedha kwa kuhamisha sh. 1,029,454,383, kutoka akaunti maalumu ya NMB kwenda akaunti za Kindamba, Cariton na Jacques huku akijua ni kosa.
Katika shitaka lingine, Mtoro anadaiwa kutakatisha fedha haramu kwa kubadilisha fedha kwa kununua nyumba maeneo ya Mbezi.

 
Mshitakiwa Kindamba anadaiwa kutakatisha fedha sh. milioni 579,887,395, ambazo zilikuwa zimehamishwa kutoka akaunti ya NMB kwa udanganyifu na Mtoro, na kwamba sehemu ya fedha hizo alinunulia nyumba maeneo ya Mabibo.


Kikopa anadaiwa kutakatisha sh. milioni 389 zilizohamishwa kutoka akaunti ya NMB na Mtoro kwenda akaunti ya Cariton, ambayo yeye alikuwa mtiaji saini pekee na alitakatisha tena sh. milioni 60 na sehemu ya fedha hizo ambazo ni sh. 449,566,988 alinunulia nyumba maeneo ya Mbezi Mshikamano.


Washitakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho waliisababishia NMB hasara ya sh. 1,029,454,383.
Washitakiwa walikana mashitaka ambapo Hilla alidai upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya usikilizwaji wa awali. 


Hakimu Hellen aliahirisha shauri hilo hadi Agosti Mosi mwaka huu kwa usikilizwaji wa awali na washitakiwa walirudishwa rumande.

Posted By Unknown01:48

TAARIFA YA MKURUGENZI WA UPELELEZI YA KUKAMATWA KWA WASHUKIWA 25

Filled under:

Kufuatia tukio la mlipuko wa bomu siku ya tarehe 7/7/2014 majira ya saa 22.15 usiku katika mgahawa wa VAMA, eneo la Uzunguni Jijini Arusha, ambapo watu wanane walijeruhiwa, Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa 25 kwa uchunguzi.

Kufuatia uchunguzi huo kati yao watu sita watafikishwa mahakamani mapema iwezakanavyo.
Watuhumiwa watakaofikishwa Mahakamani kwa tukio hilo ni: SHAABAN MUSSA MMASA @ JAMAL, Umri miaka 26 Kabila, Msambaa. Mlinzi aliyekuwa zamu siku hiyo kwenye mgahawa huo. 

Wengine ni ATHUMAN HUSSEIN MMASA, Umri miaka 38 kabila Msambaa, Mlinzi katika Mgahawa wa Chinese uliopo eneo la GYMKHANA jirani na eneo la tukio na MOHAMED NURU @ MUHAKA, Umri miaka 30 Kabila Msambaa, Mlinzi katika mgahawa wa Chinese jirani na eneo la tukio. 

Mwingine ni JAFFAR HASHIM LEMA, Umri miaka 38 Mchaga Mwalimu wa Shule ya Msingi Olturmet Wilaya ya Arumeru. Pia alikuwa Imam wa Msikiti wa QUBA mjini Arusha. 

Huyu ametambuliwa kama mmoja wa viongozi walioratibu matukio ya milipuko ya mabomu maeneo mbalimbali nchini. 

Wengine ni ABDUL MOHAMED HUMUD SALIM,@Wagoba;umri wa miaka 31, Mmanyema wa Ujiji Kigoma, wakala wa Mabasi Stendi Arusha, SAIDI MICHAEL TEMBA;umri wa miaka 42, Mchaga, mfanyabiashara wa Arusha. Aidha tarehe 21/07/2014 majira ya saa 20.00 usiku maeneo ya Sombetini walikamatwa YUSUFU HUSSEIN ALLY @ HUTA, kabila Mrangi, umri wa miaka 30 na mkewe SUMAIYA JUMA , kabila mwasi umri wa miaka 19 wakiwa nyumbani kwao baada ya kupekuliwa walikutwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono saba, risasi sita za shortgun, mapanga mawili, unga wa baruti unaokadiriwa kufika nusu kilo na bisibisi moja. #

Mtuhumiwa YUSUFU HUSSEIN ni miongini mwa watuhumiwa waliokuwa wanatafutwa kwa ulipuaji wa mabomu maeneo yote jijini Arusha. Mahojiano yanaendelea dhidi yake. 

Uchunguzi wa shauri hili pamoja na matukio mengine ya milipuko unaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwahoji watuhumiwa walioko mikononi mwa Polisi na kuwakamata watakao bainika kuhusika na matukio hayo, mtajulishwa matokeo ya uchunguzi huo mara utakapokamilika. 

Hata hivyo Jeshi la Polisi linatangaza kumtafuta YAHAYA HASSAN HELLA, kabila mrangi, umri wa miaka 33, mkazi wa Mianzini Arusha, mwenye asili ya eneo la Chemchemu Kondoa Dodoma kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya ulipuaji mabomu nchini. 

Zawadi nono itatolewa kwa yeyote atakaye toa taarifa zitakazowezesha ukamatwaji wa mhalifu huyu. Jeshi la Polisi linawashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa.

IMETOLEWA NA ISAYA MNGULU-CP
MKURUGENZI WA UPELELEZI WA MAKOSA YA JINAI TANZANIA

Posted By Unknown01:41