Friday 18 April 2014

DIAMOND AFUNGIWA ASHINDWA KUMZIKA MZEE GURUMO

Filled under:

Kuna madai kwamba Nasibu Abdul ‘Diamond’ alishindwa kushiriki zoezi la kuuaga mwili wa mwanamuziki mkongwe Tanzania, marehemu Muhidin Mwalimu Mohamed Gurumo ‘Maalim Gurumo’ kwa sababu alifungiwa asitoke ndani na mwandani wake madam Wema Sepetu,
 
Wema Sepetu na Diamond wakiwa faragha.
Imedaiwa kuwa, Wema alimfanyia ‘umafia’ mpenzi wake huyo, Aprili 15, mwaka huu ambapo ilikuwa ndiyo siku ya mwili wa marehemu huyo kuagwa nyumbani kwake Mabibo jijini Dar na kwenda kuzikwa kijijini Masaki, Kisarawe, Pwani.
Itakumbukwa kuwa, Diamond ndiye msanii aliyewahi kumpa zawadi ya gari marehemu Gurumo kutokana na kuguswa na mchango wake katika tasnia ya muziki nchini.
Diamond akimsaidia mzee Gurumo kupanda  stejini kabla ya kumkabidhi gari Agosti 29, 2013.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kitendo cha Diamond kutoonekana katika mazishi hayo ni kama amejishushia heshima kubwa aliyojijengea pale alipomthamini marehemu huyo kwa kumpa gari aina ya Toyota FunCargo.

“Tulitegemea tungemuona msibani lakini kwa kutokuwepo kwake ni kama mchango wake wa kumpa gari Gurumo hauna maana,” alisema shuhuda mmoja aliyekuwepo msibani hapo.
Mapaparazi wetu walidamka asubuhi hadi nyumbani kwa marehemu Gurumo na kujumuika na waombolezaji.
Mwili wa mwanamuziki mkongwe Tanzania, marehemu Muhidin Mwalimu Mohamed Gurumo ukiingizwa kaburini.
Baada ya mapaparazi wetu kufanya upekuzi yakinifu msibani hapo, walibaini kuwa, Diamond hakutia ‘maguu’ hivyo shughuli ya kumsaka ikaanza.

Breki ya kwanza kwa mapaparazi wetu ilikuwa nyumbani kwa Diamond Sinza-Mori jijini Dar ambako hawakumkuta.
Mapaparazi hawakuchoka, wakahamishia ‘majeshi’ nyumbani kwa mwanandani wake Wema, Makumbusho, Dar ambako mlinzi alibainisha kuwa, Diamond yupo na ‘bebi’ wake Wema.
Mzee Maalim Gurumo enzi za uhai wake.
Mapaparazi waliondoka na kurudi tena saa 8:37 mchana ambapo pia waliambiwa wapendanao hao bado wamejifungia ndani, wakaondoka hadi muda wa jioni baada ya shughuli za mazishi, walirejea na kuambiwa 

Diamond alitoka muda si mrefu pasipo kujulikana alikoelekea.
Waandishi wetu walimvutia waya Diamond lakini simu yake iliita kwa muda  mrefu bila kupokelewa.

Kusaka data zaidi, mapaparazi wetu walimtafuta meneja wa msanii huyo, Babu Tale ambaye alidai kuwa eti Diamond alikuwepo msibani Mabibo lakini hakwenda Kisarawe ambako mazishi yalifanyika.
Mzee Gurumo akionyesha ufunguo wa gari alilozawadiwa na Diamond.
“Tulikuwepo nyumbani kwa marehemu. Nilikuwa mimi na Diamond tena tumefika muda huohuo ndiyo mwili ukawa unapelekwa kwenye gari. Huwezi amini tulijumuika kuupandisha mwili kwenye gari na sisi tukarudi nyumbani kuendelea na shughuli zetu,” alisema Babu Tale.
Mapaparazi wetu baada ya kutoshibishwa na maelezo hayo, juzi Jumatano walimtwangia simu Diamond ambaye alizungumza kwa ‘kujikanyagakanyaga’.
Diamond na mpenzi wake Wema katika pozi.
“Mh! Nilikuwepo msibani ila sikwenda kuzika tu maana nilikuwa na Babu Tale pale na tulikuwa karibu kabisa na gari la Global Publishers, mara tu baada ya kumaliza kuupandisha mwili wa marehemu kwenye gari tuliondoka na kurejea kwenye majukumu yetu,” alisema Diamond.
Mapaparazi wa Global walikuwa jirani na gari alilotaja Diamond lakini hawakumuona staa huyo achilia mbali waombolezaji wengine ambao waliuliza kwa nini msanii huyo hakufika kwenye msiba wa rafiki yake mkubwa!

Source:Global publisher

Posted By Unknown00:30

Thursday 17 April 2014

UKAWA.HATURUDI BUNGE LA KATIBA

Filled under:

WAJUMBE  wa Bunge Maalumu, wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamesema hawatarudi bungeni na badala yake kuanzia kesho wataanza mikutano ya hadhara nchi nzima kuwaeleza wananchi juu ya hila za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na washirika wake kutaka kuhodhi mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya.

UKAWA wamesema katika mikutano hiyo watazisambaza ‘CD’ zinazomuonesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akiwa katika Kanisa la Methodist, mkoani Dodoma akiwaeleza waumini wakatae muundo wa serikali tatu.

Walisema kwenye CD hizo, Lukuvi, anaonekana akiwaambia wananchi iwapo wataridhia muundo wa serikali tatu, jeshi litachukua nchi na Zanzibar itaingia katika utawala wa Kiislamu.

Juzi wajumbe wa UKAWA walisusia kikao cha Bunge Maalumu kwa madai ya kuchoshwa kusikiliza matusi, ubaguzi na kauli za chuki zinazotolewa na wajumbe kutoka CCM bila viongozi wakubwa kukemea.

Jana wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi wa UKAWA walisema hawatarejea bungeni mpaka watakapoketi kwenye vikao vya maridhiano ambavyo pia watakwenda na masharti yao mojawapo ni rasimu ya Tume ya Warioba ndiyo iwe msingi wa majadiliano.

Masharti mengine ni kukaa kwenye meza ya maridhiano na viongozi wa serikali na CCM, kusiwepo matusi, ubaguzi na kauli za chuki.

Mmoja wa viongozi wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa watazunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni na namna CCM wanavyopenyeza rasimu yao kwa mlango wa nyuma.

“Sisi tupo tayari kwa mazungumzo kama tulivyoombwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, lakini hatutakubali kubeba matakwa ya CCM, tunataka tujadili rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ambayo ilikwenda kuwahoji wananchi,” alisema.

Profesa Lipumba, alisema wameamua kususa vikao vya Bunge kwa sababu hawako tayari kushiriki kupitisha masuala yenye masilahi ya CCM yaliyopelekwa bungeni kwa mlango wa nyuma.

Alisema walitegemea wajumbe wangejikita kujadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa hoja lakini badala yake wameshuhudia matusi, ubaguzi, kauli za chuki ambazo zinachangia zaidi kuligawa taifa.

Lipumba alisema rasimu iliyopo mezani inataja serikali tatu hivyo kama wajumbe wa CCM wanataka kujadili serikali mbili, lazima Bunge livunjwe na iundwe tume nyingine itakayotoa rasimu ya serikali mbili.

“Wenzetu wanatushangaza sana yaani walivyokuwa wakijadili rasimu ile kama imetolewa na wapinzani, hii ni rasimu iliyotolewa na tume iliyoundwa na rais, sasa kama wenzetu hawaamini sisi tunakwenda kuwaeleza wananchi CCM isivyotaka kuandika Katiba yenye masilahi ya wananchi,” alisema.
Lipumba pia alisema Chama cha Wananchi (CUF) kitaangalia hatua za kisheria za kumchukulia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alivyokihusisha chama hicho na taasisi ya kidini ya UAMSHO.

Alisema si kweli kwamba CUF imekuwa ikishirikiana na taasisi hiyo ambayo mara kadhaa imekuwa ikihusishwa na mihadhara ya kidini yenye vurugu visiwani Zanzibar.

Naye James Mbatia, alisema maridhiano ndiyo yatakayosaidia mchakato wa Katiba kusonga mbele lakini kwa hali inavyoonekana CCM hawana dhamira ya kuandika Katiba yenye kujali masilahi ya wananchi.
Alisema wiki iliyopita TCD iliitisha mkutano wenye lengo la kutafuta maridhiano lakini CCM walituma wawakilishi wasio na nyadhifa za juu kama zilivyofanya pande nyingine.

Naye Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, alisema wameamua kususa vikao vya Bunge kwakuwa wajumbe wengi kutoka CCM wameacha kujadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Warioba ambayo ndiyo msingi wa majadiliano yao.

Alisema Tume ya Warioba iliwekwa kisheria na ilifanya kazi ya kuwahoji watu pamoja na kutumia nyaraka mbalimbali hadi kufikia kutoa rasimu isiyotakiwa na wajumbe wa CCM walioanza kujadili rasimu waliyopewa na chama chao.

“Kususia vikao vya Bunge ni miongoni mwa hatua za kutafuta haki, kuendelea kushiriki vikao hivi ni kuhalalisha na kubariki udhalimu wa CCM ambayo imeamua kukwamisha Katiba mpya.
“Matusi, ubaguzi, chuki haviwezi kutusaidia kupata Katiba mpya, UKAWA hatuko tayari kuendelea kushiriki majadiliano yenye mambo hayo….tunakwenda kwa wananchi kuwaeleza kile kinachofanywa na wajumbe humu bungeni,” alisema.

Mbowe alisema si lazima Rais Jakaya Kikwete aondoke madarakani wakati Katiba mpya imepatikana bali mchakato huo unaweza kuendelezwa na rais mwingine lakini katika mazingira yanayokubalika na watu wote.

Posho
Hata hivyo wajumbe wa Katiba, walikuwa wakipigana vijembe kuwa UKAWA wameamua kususa vikao vya Bunge baada ya kulipwa posho ya vikao mpaka Aprili 22 mwaka huu.

Said Nkumba, alisema UKAWA ni wanafiki kwakuwa wamesusia vikao hivyo baada ya kulipwa fedha hizo na kama wasingelipwa wasingethubu kulikimbia Bunge.

Livingstone Lusinde, alisema UKAWA, hawana ujasiri wa kutetea masilahi ya umma bali wapo kwa ajili ya kuangalia masilahi binafsi ndiyo maana waliondoka bungeni baada ya kusikia wamelipwa fedha mpaka Aprili 22.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu, Nchemba, alisema jana waliwasiliana na benki kuona kama zilikuwa zimefanya malipo kwa wajumbe hao wazuie fedha hizo ili kuwadhibiti wajumbe wa UKAWA ambao wanachukua fedha bila kufanya kazi

Hata hivyo kauli hiyo ilionekana kupinga na Katibu wa Bunge, Yahya Khamis, aliyesema fedha hizo tayari zimeshaingizwa kwenye akaunti za wajumbe.

Khamis, alisema kuanzia Aprili 22, ndiyo watajua kama wajumbe wa UKAWA, hawatahudhuria vikao vya Bunge  hawataingiziwa fedha za kujikimu na ile ya vikao.
Kwa siku moja wajumbe hao wanalilipwa sh 300,000 ambapo sh 230,000 ni posho za kujikimu, sh 70,000 posho ya vikao.

Makatibu Wakuu UKAWA watoa kauli
Makatibu wakuu wa UKAWA wamesema wabunge wao hawatarejea bungeni badala yake watazunguka nchi nzima kuelezea namna serikali ya CCM isivyotaka wananachi wapate katiba wanayoitaka.
Mbali ya msimamo huo, pia wameeleza mbele ya waandishi wa habari kuwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alipopata fursa ya kulihutubia Taifa wakati wa kulizindua bunge, alianzisha vita ya kisiasa na kuigawa nchi vipande kutokana na vitisho alivyovitoa kama mkuu wa nchi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, alisema wao kama makatibu wakuu wanaunga mkono wabunge wao kutoka nje na kukiita kitendo hicho kuwa ni  cha kishujaa na uzalendo wa kukataa kuburuzwa.

Alisema hakuna chama kinachotaka Katiba Mpya kwa dhamira ya kuvunja muungano kama wanavyodai CCM, badala yake wanataka katiba ya maridhiano yanayoongozwa na uamuzi wa wananachi.

“Haya ni mapambano  na vita inayohitaji kuunganisha nguvu zote kwa kuwa hili ni jambo kubwa kwa mustakabali wa taifa na tunapoona watu wanafanya masikhara kwa ajili ya masilahi na misimamo ya vyama vyao, hatuwezi kukubali,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa kuna hatari ya mfumo uliozaa katiba inayotumika sasa kurejeshwa katika mfumo mzima wa upatikanaji wa katiba mpya na kwamba kama vyama vya siasa walionya hali hiyo mapema kwa ajili ya kulinda umoja wa kitaifa.

“Tulikuwa tayari kuridhiana kuanzia mwanzo lakini wenzetu hawataki maridhiano zaidi ya misimamo yao inayolindwa na wingi wao ndani ya bunge, sasa sisi tuna watu nje ya bunge na kama wanasema kuwepo kwa serikali tatu jeshi litapindua nchi huo ni uongo, kama mapinduzi yangefanyika sasa kwa kuwa wamewadhulumu hao wanajeshi hata hela zao za Operesheni Tokomeza,” aliongeza Dk. Slaa.

Dhana ya Vitisho
Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mketo, alisema ni jambo la kusikitisha kuona serikali inatumia vitisho kwa wananchi wakati walibariki mchakato mzima wa kukusanya na kuandika maoni ya wananchi ya kupatikana katiba mpya

Mketo alisema kitendo cha wabunge wao kutoka nje kilitosha kulivunja bunge kwani rasimu haisemi mjadala wa serikali mbili.

UKAWA haitarudia makosa
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema kulikuwa na makosa mengi wakati vyama vya siasa viliporidhia kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 bila kupata katiba mpya.
Alisema hoja zinazotolewa kuwa wapinzani hawataki katiba mpya zinapotoshwa makusudi, kwa kuwa madai ya vyama vya upinzani kuhusu katiba ya wananachi yalianza miaka ya 1960.

Posted By Unknown23:44

LUKUVI ALIKOROGA KWA CUF

Filled under:

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, amekiri kutoa maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi kanisani kwa madai ya kuingiwa hofu na harakati za asasi ya kidini ya Uamsho, kufanana na za Chama cha Wananchi (CUF) za kudai Serikali ya mkataba.

Waziri Lukuvi alitoa kauli hiyo jana bungeni, akitoa ufafanuzi wa kauli aliyopata kuitoa katika Kanisa la Methodist wakati wa kumsimika Askofu Mteule, Joseph Bundara.

Katika misa hiyo, Lukuvi aliwaambia waumini wa kanisa hilo kwamba muundo wa serikali tatu utavunja Muungano na ikipitishwa, jeshi litaingilia kati kuongoza nchi, kauli ambayo juzi ilisababisha UKAWA wasusie Bunge.

Katika ufafanuzi wake jana bungeni Lukuvi alikiri kutoa kauli hiyo kanisani kwa madai ya kuingiwa hofu ya kutokea ubaguzi wa kidini.

Alisisitiza kuwa hofu yake inatokana na harakati zinazofanywa na kikundi cha  Uamsho visiwani Zanzibar, kufanana na za CUF ambazo ni kudai Serikali ya Mkataba.

Alisema uamsho imekuwa ikihusishwa na vurugu zinazotokea mara kwa mara visiwani humo, zinazohusishwa na vuguvugu la kudai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Akitolea mfano, Lukuvi alisema Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta,  alipotumwa Zanzibar kupeleka Rasimu ya Katiba, rasimu hiyo ilichukuliwa na wanauamsho na kuichanachana, kisha kuisigina mbele yake.
“Sasa niwaulize humu ndani…Uamusho ni nani…?”  Wajumbe kwa wingi wao na vigelegele wakajibu  “Ni CUF”. Akauliza mara ya pili: “Uamusho ni nani…?” akajibiwa: “ CUFUUUUU”.

“Lakini kuna swali liliulizwa hapa bungeni, CUF wakaja juu wakasema ni Taasisi ya Kidini…sasa unaniambiaje mimi nisiwe na hofu ya kidini wakati kuna chama cha siasa kinahusiana na Uamsho lakini ina ladha ya kidini.

“Na kwa kuwadhihirishia hivyo,  kila mara CUF na Uamsho utakapomtaja  Mwalimu Nyerere na kumtaja Karume wanakwambia alaaniwe.. lakini hizi ndiyo sera za hao mnaowasema, sasa tunakuwaje na chama cha siasa ambacho tayari kinajipanga kutawala Zanzibar, lakini kinaendeshwa na Sera za Uamsho…uamsho wenyewe wanasema ni Taasisi ya Kidini, kwa nini usiwe na wasiwasi na mihemko yote ile ya Uamsho mpaka na Bara tukatikishika, kwa nini tusiwe na wasiwasi kwamba CUF ikichukua nchi basi Uamsho ndiyo 
utatawala, kwa nini tusiwe na hofu, yametokea na sisi tumeyaona, kwa nini wanajificha kwenye kivuli cha dini ili kufanya siasa…na kwa nini dini imetumika vizuri sana kueneza sera za CUF za serikali tatu, na kila wachosema CUF ndicho wanachosema uamsho?,”  alihoji Lukuvi.

“Na ukishaona chama kinajitayarisha kuchukua madaraka kama ilivyo kwa CUF, kinatumia taasisi hii yenye msimamo mkalii kueneza sera zake ni hatari kwa mustakabali wetu, ni hatari kubwa,” alisema.
Alisema kama kweli Uamsho ni taasisi ya kidini na inatekeleza sera ambazo zinatekelezwa na vyama vya siasa, lazima Watanzania wajiulize kuna nini.

Alisema kuna tishio la baadhi ya watu ambao wameanza kufikiria kwamba Wazanzibar wanafaidi sana wakiwa Tanzania Bara na kufikiria kuwafukuza na kunyang’anya mali zao na iwapo watafanikiwa kuwanyang’anya watawafukuza.

“Sasa baada ya Wazanzibari kuondoka, tutaanza kuangalia hawa Wachina, hawa Wahindi na vinginevyo tutakuja hata kwenye dini, Wakristo wana mali zaidi kuliko Waislamu.Lakini kwa Zanzibar ambayo ina dini kubwa moja na tunajua hizi dini, kwa mfano katika dini ya Ukristo kuna dini ndogo ndogo nyingi na ndani ya ukristo kuna watu wenye siasa kali lakini na ndani ya Uislamu kuna watu wenye siasa kali kwa hiyo mimi nina hofu nyingine ya ubaguzi .
 
“Nasema kunaweza kukatokea ubaguzi wa kidini, inaweza ikatokea ubaguzi wa kieneo kwani inaweza kutokea hata Unguja akaenda mtu akasema Waunguja wote ondokeni hapa pamejaa, sasa hizi ni hofu zangu, mfumo huu wa serikali mbili umetuondolea hofu hizi hatuna hofu kabisa ya maisha haya, leo hatumfikirii Mpemba atoke au Muunguja atoke, Msukuma atoke, hatufikirii,” alisema.

Awali kabla ya Lukuvi kutoa ufafanuzi huo, Sitta aliwaambia wabunge kuwa amemlazimisha Lukuvi kukatiza safari yake nchini India ili atoe ufafanuzi wa kauli alizozitoa katika Kanisa la Methodist.

Alisema amelazimika kumwita Lukuvi ambaye alikuwa akijiandaa kuondoka nchini jana kwenda India kwa matibabu ili atoe ufafanuzi wa kauli yake ambayo juzi ilisababisha UKAWA, wanaounga mkono serikali tatu, kususia Bunge hilo.

Moto wa wajumbe wa UKAWA, kutoka bungeni juzi uliwashwa na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alisema serikali na mawaziri wake wameanza kampeni ya kupinga muundo wa serikali tatu unaopendekezwa na rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema hoja ya Lukuvi inafanana na ile ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati wa kufungua Bunge, Machi 21, mwaka huu.

Tanzania Kwanza wamruka Lukuvi
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaojiita Tanzania Kwanza, wamemruka Mjumbe wa Bunge hilo, William Lukuvi, kuwa kauli aliyoitoa kanisani na kusababisha mtafaruku ndani ya bunge ni maoni yake binafsi na si maoni ya serikali ya CCM.

Akitoa ufafanuzi jana, Kiongozi wa kundi hilo, Adam Malima, alisema Lukuvi kama mjumbe ana uhuru wa kutoa maoni yake na kwamba aliyoyasema ni yake na wala si ya chama wala serikali.
Kuhusu kauli za matusi, Malima alisema haoni kama kuna matusi na kuongeza kuwa tusi kubwa ni lile alilolitoa Profesa Lipumba kwamba  wote wanaodai serikali mbili ni Interahamwe.


Posted By Unknown23:25

UCHUNGUZI UMEBAINI NAHODHA MKUU WA FERI YA SOWEL HAKUWEPO KWENYE USUKANI

Filled under:

Waokoaji wamefaulu kuingia ndani ya feri iliyozama
Naibu wa tatu wa nahodha wa ferri iliyozama ''Sewol'' ndiye aliyekuwa usukani wakati feri hiyo ilipozama.
Uchunguzi wa kimsingi umebaini.

Nahodha mkuu haijabainika alikuwa wapi wakati wa tukio ila inadhaniwa feri hiyo iligonga mwamba na kupinduka kwa haraka baada ya shehena yake kuegemea upande mmoja.

Wachungizi sasa wanaelekeza juhudi zao kubaini kwanini Nahodha wa Sewol hakuwa kwenye usukani na pia kwanini baada ya tukio la kwanza abiria walikanywa wasiruke baharini ilikuokoa nafsi zao kama ilivyodesturi chombo
kikigonga mwamba ?
Waokoaji wamefaulu kuingia ndani ya feri iliyozama

Kiongozi wa Mashtaka ya umma nchini Korea bwana Park Jae-Eok amesema kuwa nahodha mkuu Lee Joon-seok,atakuwa na swali la kujibu .

Kufikia sasa abiria 270 waliokuwa ndani ya feri hiyo hawajulikani walipo asilimia kubwa kati yao wakiwa ni wanafunzi waliokuwa wakieleka katika kisiwa cha Jeju kwa safari ya masomo.
Watu 26 pekee ndio wamedhibitishwa kufariki kufikia sasa, huku 179 wakiokolewa.
Muundo wa feri iliyozama
Makundi ya waokoaji wamefanikiwa kuingia ndani ya feri hiyo kwa mara ya kwanza leo asubuhi baaha ya kutoboa shimo upande wa juu wa chombo hicho kilichozama.

Waokoaji walikuwa wameshindwa kuingia ndani ya feri hiyo baada ya bahari kuchafuka.

Mamia ya jamaa na marafiki ya wahasiriwa wamelalamikia ukosefu wa habari za uokaji .
Wengi wamekuwa wakivumilia hali mbaya ya hewa wakiomba kuruhusiwa kusubiri wapendwa wao ufukweni.

Posted By Unknown23:05

Wednesday 16 April 2014

BUNGE LA KATIBA:UPINZANI WASUSIA KIKAO

Filled under:

Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameondoka kwa hasira katika kikao cha bunge hilo kinachoendelea mjini Dodoma. 


Hasira yao inatokana na madai kwamba maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya yamekuwa yakipuuzwa.

Wajumbe wa bunge hilo ambao ni kutoka upande wa upinzani chini ya umoja unaojulikana kama UKAWA, yaani Umoja wa Katiba ya Wananchi, wameamua kutoka nje kupinga kile wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka muungano wa muundo wa serikali tatu kama yalivyopendekezwa katika rasimu ya katiba hiyo.

Kilio cha mwananchi


Akichangia katika kikao cha bunge hilo Jumatano jioni, mmoja wa wajumbe Profesa Ibrahim Lipumba amelalamikia kauli za ubaguzi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe, hususan wanaotaka muundo wa muungano wa serikali mbili, alieleza sababu za kutaka serikali tatu kuwa zitasaidia kutatua matatizo yaliyopo katika muundo wa sasa.

Hata hivyo hakusita kupinga kile anachokiita kauli za ubaguzi kutoka kwa wajumbe wanaopinga mawazo ya wachache bungeni humoi.

"Hatuwezi kuwa kama kundi la wapiganaji linalohamamisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatulikubali, hatulikubali, hatulikubali, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia muendelee na kikao chao.Ahsanteni sana".

Mara baada ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.

Hata hivyo, kikao cha bunge hilo kiliendelea baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo kusema idadi ya wajumbe waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.

Muundo wa serikali


Wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa kutatua masuala yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za muungano, hivyo kudhoofisha muungano huo.


Hata hivyo wajumbe wanaounga mkono serikali mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu ni kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha serikali ya tatu.


Bunge hilo lenye zaidi ya wajumbe mia sita linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa na rais wa Tanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.


Wajumbe 191 kutoka upinzani walitoka nje ya bunge kupinga mwenendo wa bunge hilo katika kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Posted By Unknown10:10

KOREA KUSINI:WATU ZAIDI YA 300 BADO HAWAJAPATIKANA

Filled under:



Zaidi ya watu miatatu bado hawajapatikana baada ya meli iliyokuwa imewabeba wanafunzi kuzama nchini Korea Kusini.

Awali maafisa walikuwa wamesema kuwa wengi wa abiria waliokuwa katika meli hiyo waliokolewa.
Baadhi ya walionusurika wamekuwa wakielezea hali ilivyokuwa ya kutisha ndani ya meli ilipoanza kusimama kwa kuyumba, ikiegemea upande mmoja na haraka kuanza kuzama.

"Kwa kweli kulikuwa na sauti kubwa na meli ghafla ikaanza kuegemea upande mmoja," amesema abiria aliyeokolewa, Kim Song-Muk.

"watu walikuwa wakihangaika kukimbilia maeneo ya juu ya meli, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na meli kupinduka."

Bado haijafahamika kilichosababisha kuzama kwa meli hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa iliwabeba wanafunzi wa shule, lakini watu walionusurika katika ajali hiyo wanatoa maelezo sawa kuhusu tukio hilo la kutisha.

Kikosi cha Walinzi wa Pwani ya Korea Kusini kimesema abiria wapatao mia tatu hawajulikani walipo baada ya meli kupinduka na kuzama.

Watu wawili wamefahamika kupoteza maisha na watu mia moja na sitini na wanne wameokolewa.

Wengi wa abiria wa meli hiyo walikuwa wanafunzi wa sekondari wakiwa katika safari ya masomo kuelekea kisiwa cha Jeju, nchini Korea Kusini.

Meli hiyo ilikuwa na watu 460. Zaidi ya miatatu hawajapatikana , wengine 164 wameokolewa na wengine wawili wamethibitishwa kufariki.

Posted By Unknown10:04

Monday 14 April 2014

KITUO CHA MABASI CHALIPULIWA

Filled under:



Watu kadha wameripotiwa kuuawa nchini Nigeria kutokana na milipuko miwili iliyotokea katika kituo cha mabasi katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Mwandishi wa BBC mjini Abuja, Haruna Tangaza anasema milipuko hiyo ilitokea wakati abiria wakiwa katika harakati za kupanda mabasi na teksi wakienda maofisini katikati ya mji wa Abuja.

Watu walioshuhudia tukio hilo wanasema miili ya watu imetapakaa katika eneo la tukio.
Waandishi wa habari wanasema huenda tukio hili ni shambulio la kikundi cha wapiganaji wa Kiislam kijulikanacho kama Boko Haram.

Mmoja wa walioshuhudia mlipuko huo, Badamsi Nyanya ameiambia BBC kuwa ameona miili 40 ikiondolewa. Watu wengine walioshuhudia tukio hilo wanasema wamewaona wafanyakazi wa uokoaji na polisi wakiokota sehemu za miili zilizotawanywa na milipuko hiyo.

Mlipuko huo ulichimba chini mita 1.2 katika viwanja vya Nyanya Motor Park, kiasi cha kilomita 16 kutoka katikati ya jiji, na kuharibu zaidi ya magari 30, na kusababisha mlipuko zaidi kutokana na matangi ya mafuta ya magari hayo kushika moto na kuwaka.
Magari ya wagonjwa yamekuwa yakibeba miili ya watu waliokufa na wale waliojeruhiwa katika hospitali za karibu.

Shuhuda mwingine Bi Mimi Daniels, ambaye anafanya kazi mjini Abuja, anasema: "nilikuwa nasubiri basi niliposikia mlipuko mkubwa halafu nikaona moshi," ameiambia Reuters.
"Watu walikuwa wakikimbia ovyo kutokana na taharuki."

Posted By Unknown07:26

BUNGE LA KATIBA: MAONI YA WAJUMBE WALIO WACHACHE WA KAMATI NAMBA SITA YA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUHUSIANA NA SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA ZA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Filled under:

MAONI YA WAJUMBE WALIO WACHACHE WA KAMATI NAMBA SITA YA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUHUSIANA NA SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA ZA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


(Kwa mujibu wa Kanuni 32 (4) ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014)

UTANGULIZI

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita za Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Hii ni kwa sababu Sura hizi mbili zinazungumzia mfumo na muundo wa Muungano. Katika Sura ya Kwanza, mfumo na muundo wa Muungano unatajwa kwenye Ibara ya 1 na Ibara ya 2 na kwa upande wa Sura ya Sita, sura nzima inahusu Muundo wa Jamhuri ya Muungano.

Katika kufikia maamuzi ya Kamati Namba Sita, wajumbe waligawanyika, na katika Ibara ya 1 na ya 3 ya Sura ya Kwanza na Ibara zote za Sura ya Sita, sharti la kupata theluthi mbili za wajumbe wote wa kamati kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili za wajumbe wote wa Kamati kutoka Zanzibar lilishindwa kufikiwa.
Maoni haya ya wajumbe walio wachache yametokana na maoni ya wajumbe sita (6) kutoka Zanzibar na wajumbe sita (6) kutoka Tanganyika.

MAONI, SABABU NA HOJA KUHUSU IBARA YA 1 YA SURA YA KWANZA

Mjadala mkubwa kuhusu Ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza ulihusu mfumo na muundo wa Muungano iwapo ni wa Shirikisho, kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu, au ni Muungano uliounda Nchi Moja (Unitary State), kama ilivyodaiwa na wajumbe walio wengi kwenye Kamati.

Maoni na msimamo wa wajumbe walio wachache ni kukubaliana na maoni ya Watanzania walio wengi waliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni SHIRIKISHO na wala si MUUNGANO ULIOUNDA NCHI MOJA (UNITARY STATE).

Tunasema hivyo kwa sababu ya hoja za kitaaalamu zilizofanyiwa utafiti na wataalamu mabingwa wa sheria wa ndani na nje ya Tanzania, tafsiri za vifungu vya Mkataba wa Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar pamoja na hali halisi ya uendeshaji wa Muungano ilivyo.

MAONI YA WATAALAMU WA SHERIA:

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliundwa kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa nchi hizo mbili, Rais Julius Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Abeid Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambayo yamo kwenye Mkataba wa Muungano. Wataalamu mbali mbali ambao ni mabingwa wa sheria wa ndani na nje ya Tanzania wamefanya uchambuzi wa Mkataba huo na pia Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na wamekuja na hitimisho kwamba Muungano huu ni Shirikisho. Tunawanukuu wachache hapa chini:
  1. Profesa Issa Shivji katika kitabu chake, Tanzania: The Legal Foundations of the Union, kilichochapishwa mwaka 1990 na kurejewa tena mwaka 2009 anasema baada ya kuufanyia uchambuzi wa kina Mkataba wa Muungano ameridhika kwamba Mkataba huo umeanzisha Shirikisho. Kwa maneno yake mwenyewe Profesa Shivji anasema kwamba ukiyaangalia Makubaliano ya Muungano kutoka upande wa Zanzibar na upande wa Tanganyika na kwa ujumla wao, “… msingi wa Shirikisho ndiyo wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano yanaweza kutafsiriwa kwa usahihi kama Katiba ya Shirikisho. Kwengineko kwenye kitabu hicho hicho, Profesa Shivji anasema kwamba: “Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba Makubaliano ya Muungano siyo Katiba ya Muungano wa Nchi Moja (Unitary Constitution).”
  1. Waandishi Earl E. Seaton na S.T. Maliti katika kitabu chao, Tanzania Treaty Practice kilichochapishwa mwaka 1973 walikubali kwamba Makubaliano ya Muungano yaliunda Katiba ya Shirikisho na siyo Katiba ya Muungano wa Nchi Moja (Unitary State).
  1. Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Muungano unaundwa, Wolfango Dourado, katika Waraka wake aliouita, The Consolidation of the Union: A Basic Re-Appraisal, ambao aliutoa mwaka 1983 wakati wa mjadala wa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, alibainisha kwamba Makubaliano ya Muungano hayakuunda Muungano wa Nchi Moja bali yaliunda “Shirikisho la Kweli” (A True Federation).
  1. Profesa B. P. Srivastava katika waraka wake wa mwaka 1984, The Constitution of the United Republic of Tanzania 1977: Some Salient Features, Some Riddles ameandika kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una sura ya Shirikisho.
  1. Profesa Palamagamba Kabudi katika utafiti wake uliopelekea kutunukiwa Shahada ya Uzamili (Masters Theses) ambao unaitwa, International Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar: A Federal or Unitary State? naye amefikia hitimisho kwamba Makubaliano ya Muungano yameunda Shirikisho na siyo Muungano wa Nchi Moja.
  1. Profesa Yash Ghai, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Kenya na ambaye ni bingwa wa sheria anayeheshimika duniani, katika utangulizi wa toleo jipya la kitabu cha Profesa Issa Shivji kilichochapishwa upya mwaka 2009, ameandika kwamba, “Tanzania inakidhi vigezo vingi rasmi vya Shirikisho.”
Hayo ni maoni ya wataalamu waliobobea katika fani ya Sheria ambayo hayawezi kupuuzwa kwa sababu tu ya misimamo ya kisiasa ya kikundi fulani cha watu ndani ya Tanzania ambao wanataka kulazimisha ionekane kwamba Makubaliano ya Muungano yaliunda Nchi Moja.

MITAZAMO YA VIONGOZI WAKUU WA KISIASA:

Hoja na mtazamo kwamba Makubaliano ya Muungano yameanzisha Shirikisho na siyo Muungano wa Nchi Moja yametolewa pia na baadhi ya viongozi wa juu wa kisiasa wa hapa nchini. Tuchukue mifano miwili tu hapa:
  1. Tume ya Mabadliko ya Katiba katika Randama ya Rasimu ya Katiba inamnukuu Mwalimu Julius Nyerere akiuambia mkutano maalum wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM uliofanyika Dodoma kati ya tarehe 24 – 30 Januari, 1984 kuwa, “… Muungano wa Tanzania ukiuangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa Shirikisho lakini ukiuangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni Serikali Moja.”
Pamoja na kutetea muundo wa Serikali mbili, Mwalimu Julius Nyerere anaonekana wazi kuelewa kwamba mantiki ya nchi mbili zinapoungana ni kuwa na Shirikisho la Serikali Tatu. Katika kitabu chake alichokichapisha mwaka 1994, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, anasema:

“Nchi zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili, kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka za nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani… Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa na nchi moja yenye serikali tatu, serikali ya shirikisho na serikali mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”

Lakini Mwalimu Julius Nyerere hakuishia hapo tu. Ana hoja nzuri sana kuwajibu wale wanaohoji kwamba ukiwa na Serikali Tatu, mbili za nchi washirika na moja ya Shirikisho, hiyo Serikali ya Shirikisho itakuwa na eneo gani la kutawala na nchi yake itatoka wapi. Mwalimu Nyerere anapozungumzia muundo wa Shirikisho la Afrika Mashariki pale litakapofikiwa anasema:

“Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa Shirikisho; ama shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne, au Shirikisho la Nchi Nne lenye Serikali Tano. Kwa kweli hata kesho nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili – ya Zanzibar na Tanganyika – kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar.”

Suala la kujiuliza iwapo wale wanaohoji kama ukiwa na Serikali Tatu ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hiyo ya tatu eneo lake litakuwa lipi, nadhani kwa mantiki hiyo hiyo wangemuuliza Mwalimu Nyerere kama kungekuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki linaloshirikisha Nchi Nne (kwa maana ya Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar) zenye Serikali Tano, hiyo Serikali ya Tano ambayo itakuwa na Shirikisho eneo lake litakuwa lipi? Bila shaka, eneo lake ni eneo lote la nchi nne kwa pamoja lakini mamlaka yake yatakuwa yanahusu yale mambo ya Shirikisho tu. Huyo ni Mwalimu Nyerere. Sasa tumgeukie kiongozi mwengine aliyewahi kushika madaraka ya juu kabisa Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano.
  1. Aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, katika kitabu chake, The Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – Miaka 30 ya Dhoruba alichokichapisha mwaka 1994 amesema wazi kwamba:
“Ibara za Mkataba wa Muungano ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu na serikali shiriki katika Muungano kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani mfumo wa Shirikisho ambao kuna mgawiko wa mahakama, baraza la kutunga sheria na urais baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na kila Serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”

IBARA YA 1 (1) NA 1(3) KUHUSIANA NA HATI YA MAKUBALIANO YA MUUNGANO KUWA NDIYO MSINGI MKUU WA MUUNGANO

Ibara ya 1(1) na (1(3) za Rasimu zinafanya rejea kwenye Hati ya Makubaliano ya Muungano na kutamka kwamba Hati hiyo ndiyo “msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Kama tunakiri kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano ndiyo msingi mkuu wa Muungano, hatuna budi kurudi katika historia yake, jinsi ulivyofikiwa, kujua maudhui yake, na kuona utekelezaji wake umekwenda vipi.

Kama tulivyokwisha kuona kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliundwa kupitia Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union). Mkataba huu, kwa kutumia ushahidi wa picha, ulitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, kwa niaba ya nchi zao mbili katika Ikulu ya Zanzibar, tarehe 22 Aprili, 1964.

Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union between the Republic of Tanganyika and the People’s Republic of Zanzibar) ni Mkataba wa Kimataifa (an international treaty) na ndiyo maana kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kiingereza (English Common Law System) zilizokuwa zikifuatwa na Zanzibar na Tanganyika wakati huo na hadi leo uliweka sharti katika kifungu cha (viii) kwamba unapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likishirikiana na Baraza lake la Mawaziri ili kuupa nguvu za kisheria ndani ya nchi mbili hizo.

Hoja ya kwanza inayojitokeza hapa na ambayo imeshindwa kupatiwa majibu hadi leo ni kushindwa kupatikana kwa nakala halisi (original copy) ya Mkataba huo ikiwa na saini za Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hoja hii imeibuliwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia katika Mahkama Kuu ya Zanzibar ambako Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeshindwa kutoa nakala hiyo licha ya kuahidi kufanya hivyo.
Yalikuwepo maelezo kwamba nakala halisi ya Mkataba wa Muungano ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumbukumbu za Umoja huo kujiridhisha kwamba nchi mbili hizi zimeungana. Hata hivyo, kumbukumbu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba maelezo hayo si ya kweli.

Kumbukumbu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba siku moja baada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutangazwa, yaani tarehe 27 Aprili 1964, Mwanasheria Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. C.A. Stavropoulos alimwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. U Thant, waraka wa kiofisi uliohusu ‘Uanachama Katika Umoja wa Mataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’ Kwa mujibu wa Bw. Stavropoulos, waraka wake ulitokana na taarifa za vyombo vya habari zilizoonyesha kwamba Tanganyika na Zanzibar, ‘ambazo kabla zilikuwa wanachama tofauti wa Umoja wa Mataifa’, zilikuwa zimeungana na kuunda dola moja yenye uwakilishi wa pamoja nchi za nje. Kwa vile Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikuwa hazijapeleka taarifa rasmi Umoja wa Mataifa juu ya Muungano wa nchi zao, Bw. Stavropoulos alipendekeza kwamba “mwakilishi wa Tanganyika ataarifiwe juu ya haja ya kupata tamko rasmi kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano … kuhusu kuanzishwa kwa Jamhuri hiyo … na hati mpya za utambulisho wa mwakilishi mmoja kutoka Jamhuri (ya Muungano). (Itakuwa vizuri vile vile kwa mwakilishi husika kutupatia nakala ya makubaliano yaliyopelekea Muungano huo.)”

Ijapokuwa tarehe 6 Mei, 1964, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilipeleka taarifa ya maandishi iliyodai kuambatanisha nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano, kuna mashaka ya msingi kama kweli Hati hiyo ilipelekwa Umoja wa Mataifa. Hii ni kwa sababu, tarehe 14 Mei, 1964, yaani wiki moja tu baadaye na takriban wiki tatu baada ya Muungano, Bw. Stavropoulos alimwandikia Deputy Chief de Cabinet wa Umoja wa Mataifa Bw. Jose Rolz-Bennett kumwelekeza apeleke ujumbe wa simu ya maandishi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuhusu masharti ya kusajili Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kama inavyotakiwa na Ibara ya 102 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (United Nations Charter). “… Serikali inayosajili inatakiwa kuwasilisha kwa Sekretarieti nakala moja ya Makubaliano iliyothibitishwa kwamba ni nakala ya kweli na kamili … nakala mbili za ziada na taarifa inayohusu tarehe na namna ya kutiliwa nguvu Makubaliano hayo.”

Baada ya sarakasi yote hiyo, sasa kuna uthibitisho kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano haijawahi kusajili Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Andrei Kolomoets, ambaye ni Afisa Habari za Kisheria katika Kitengo cha Mikataba ya Kimataifa ndani ya Ofisi inayoshughulika na Mambo ya Sheria kwenye Umoja wa Mataifa, alipoulizwa na mtafiti mmoja, alijibu kwa maandishi tarehe 25 Machi, 2009  kwamba:

“Hakuna ushahidi wowote kwamba Mkataba wa Muungano ulisajiliwa kwenye Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Kama ungesajiliwa, kungelikuwa na kumbukumbu kwenye kitengo cha hifadhi ya kumbukumbu na kungekuwa na shahada ya kusajiliwa ikiwa imeambatanishwa. Nimeangalia, hakuna kitu hicho.”

Kuonekanwa kwa nakala halisi ya Mkataba huo ni muhimu sana katika kujiridhisha uhalisia wa kile kilichokubaliwa baina ya nchi hizi mbili. Hilo ni suala la msingi ili kumaliza mabishano ya kisheria na kisiasa juu ya nini hasa Rais Nyerere na Rais Karume walikubaliana kwa niaba ya nchi zao.
Hata tukichukulia kwamba kile tulichoaminishwa kwamba ndiyo Hati ya Makubaliano ya Muungano kuwa ni sahihi, hoja ya pili inazuka kuhusu utekelezwaji wa matakwa ya uthibitishaji (the want of ratification) wa Mkataba huo kwa upande wa Zanzibar. Upo ushahidi wa kutosha kwamba Bunge la Tanganyika lilikutana na kuuridhia Mkataba huo tarehe 25 Aprili, 1964. Kwa upande mwengine, hakuna ushahidi wowote kwamba Baraza la Mapinduzi likishirikiana na Baraza la Mawaziri la Zanzibar lilikaa kuuridhia Mkataba huo kwa kupitisha Sheria ya Kuthibitisha (Ratification Decree) kama ilivyotakiwa na Mkataba wenyewe. Kwa hakika ushahidi ulioibuliwa na Prof. Issa Shivji katika kitabu chake, Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Unionkilichochapishwa mwaka 2008 umeweka wazi pasina chembe ya wasiwasi kwamba Mkataba huo haujaridhiwa na upande wa Zanzibar hadi hii leo. Profesa Shivji anaeleza kwamba:

“Uhalisi wa mambo ni kwamba ushahidi wote unaelekeza kwenye ukweli kwamba kile kinachodaiwa kuwa ni Sheria ya Zanzibar ya kuridhia Hati ya Makubaliano ya Muungano iliandaliwa na kuandikwa na maofisa wa sheria wa Tanganyika wakiwa ndani ya Tanganyika. Maofisa hao wa sheria walikuwa wakijua mahitaji na matakwa yote ya utungaji wa sheria kama yalivyokuwa katika Sheria za Kikatiba za Zanzibar za wakati ule kwa sababu wamezitaja kwenye kifungu kidogo cha 2 cha kifungu cha 7 cha Sheria hiyo. Uhalisi wa mambo kwamba masharti hayo hayakutekelezwa ulitokana na ukweli wa kisiasa uliokuwepo wakati huo, mkubwa na muhimu kuliko yote ukiwa ni kwamba Baraza la Mapinduzi kwa ujumla halikuukubali Muungano. Hapana shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa’. Kwa hivyo, maofisa wa sheria wa kigeni wa Serikali ya Tanganyika (ambao katika kadhia hii walisadifia pia kuwa ni marafiki wa Nyerere) walitumia mbinu na hila ya kisheria ya kuchapisha Sheria ya Kuridhia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, waliyoitengeneza wao, kwenye Gazeti Rasmi la Jamhuri ya Muungano kama Taarifa ikiwa na saini ya [Kaimu Mshauri Mkuu wa Sheria wa Tanganyika] Fifoot. Taarifa kwamba Sheria ile ilitungwa na ‘Baraza la Mapinduzi la Zanzibar likishirikiana na Baraza la Mawaziri’ ilikuwa ni ya uongo. Kwa hivyo, mamlaka husika za Zanzibar hazikuridhia, kisheria na kiuhalisia, Hati ya Mapatano ya Muungano.”

Ukiachilia mbali hoja hizo, na kwa msingi wa hoja tukichukulia kwamba Mkataba huo ni halali, bado ukitazama kwa jicho la sheria, utaona kiini cha matatizo ya Muungano kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964. Suala kubwa lililoumiza na linaloendelea kuumiza vichwa vya wengi na hivyo kuendelea kuulizwa ni mfumo gani wa Muungano ulikusudiwa kuwekwa na Mkataba huu? Ni muungano wa moja kwa moja (unitary) au wa shirikisho (federal)?

Mfumo uliopo sasa ambao ulianza kutekelezwa 1964 ni ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar. Tanganyika haikuwekewa serikali yake tofauti; madaraka yake kwa yale mambo yasiyo ya Muungano yalielezwa kwamba yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu umeendelea kuhojiwa na hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio yaliyomo katika Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.

Mkataba wa Muungano wenyewe hauelezi bayana aina au mfumo wa muungano inaouanzisha lakini uko wazi kuhusiana na mgawanyo wa madaraka (distribution of power) inaouweka na idadi ya mamlaka (number of jurisdictions) zitakazokuwepo. Ibara ya (iii) (a) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Baraza la Kutunga Sheria na Mamlaka ya Utendaji’ (Legislature and Executive) ndani ya na kwa ajili ya Zanzibar ikiwa na mamlaka kamili (exclusive authority) kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa Zanzibar. Kwa upande mwengine, Ibara ya (iv) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Bunge na Mamlaka ya Utendaji’ (Parliament and Executive)ya Jamhuri ya Muungano ikiwa na mamlaka kamili katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano kuhusiana na mambo ya Muungano na, pia, ikiwa na mamlaka kamili ndani ya, na kwa ajili ya Tanganyika kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa Tanganyika. Kwa hivyo, katika sehemu ya pili, mamlaka mbili tofauti zimechanganywa pamoja.

Mjadala mkubwa na mkali umekuja kuhusiana na tafsiri ya Ibara hiyo ya (iv) na kule kuchanganya kwake mamlaka mbili hizo.

Haya si masuala ya kisheria tu kama ambavyo baadhi yetu wanataka tuamini (ingawa nayo ni muhimu mno kama ilivyodhihirika hivi karibuni), bali pia ni masuala ya kisiasa kwa vile yanahusisha uwezo wa maamuzi, madaraka na mamlaka, na zaidi mchango wa gharama za uendeshaji na mgawanyo wa rasilimali na mapato kati ya wahusika wakuu. Mambo haya, katika uzoefu wa nchi za wenzetu, ndiyo yaliyopelekea kuvunjika kwa miungano yao kwani huzaa kutiliana shaka na kutokuaminiana. Kwa vile yanachukua sura ya kisiasa (kutokana na sababu nilizozitaja), haya hayana chama wala itikadi. Kama alivyowahi kusema Prof. Issa Shivji mwaka 1994 kwenye makala yake ‘The Union: Hopes and Fears’ iliyochapishwa katika gazeti la The Family Mirror (Dar es Salaam), First Issue, January 1994, uk. 5:

“Ultimately, the question of the Union is primarily a political question and no amount of rhetoric about blood and cultural ties will matter when it comes to realpolitik.”

Yaani, “Mwisho wa yote, suala la Muungano linabakia kimsingi kuwa ni suala la kisiasa, na inapofikia kwenye siasa hasa, hotuba na kauli kali za jazba kuhusiana na mahusiano ya damu na ya kidugu, zote hazitafaa kitu.”
Kwa hakika, kinyume na inavyojaribiwa kuoneshwa na wengi kwamba Tanganyika imepoteza kila kitu katika muundo huu wakati Zanzibar imekabidhi sehemu tu ya madaraka yake, muundo wa Serikali mbili umepelekea wengi kuamini kwamba kilichofanyika ni kiini macho tu kwani ni Zanzibar iliyokabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Na haya si maoni ya ngumbaru (kwa kutumia lugha ya Mwalimu Julius Nyerere) bali ni maoni ya watu wazito wakiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge na baadaye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Pius Msekwa ambaye alisema kwa jinsi mambo yalivyofanyika, Zanzibar inaonekana kama vile ni ‘invited guest’ (mgeni aliyealikwa) katika Muungano (Rejea Pius Msekwa (1994) ‘The State of the Union’ –Paper presented to a Seminar on the State of the Union, Mkonge Hotel, Tanga 25 – 27 February, 1994). Naye msomi mashuhuri ulimwenguni, Prof. Ali Mazrui katika makala yake ‘Imperialism after the Empire: Lessons from Uganda and Tanzania’ iliyochapishwa katika gazeti la The Sunday Nation (Nairobi), May 22, 1994 alisema baada ya Muungano, Zanzibar imepoteza kila kitu muhimu wakati Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania huku ikiwa na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo yake ya Taifa, wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa Mataifa.

MAPENDEKEZO:
Ibara ya 1:
Jina la Muungano

Muungano huu umetokana na Jamhuri mbili kuungana kwa hiyari. Jamhuri hizo ni Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Jina la awali lililotajwa katika Mkataba wa Muungano la muungano wa jamhuri hizi mbili lilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jina hili baadaye tarehe 28 Oktoba, 1964 lilibadilishwa na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 2 Novemba, 1964, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Umoja wa Mataifa ukapeleka taarifa ya kubadilisha jina hilo lakini taarifa hiyo haikuwa na saini na badala yake ikagongwa mhuri wa Jamhuri ya Tanganyika, ambayo tumefanywa tuamini kwamba ilishafutika tokea tarehe 26 Aprili, 1964. Tunachojiuliza ni upi uhalali wa taarifa hiyo iliyopelekwa Umoja wa Mataifa na Jamhuri ya Tanganyika, nchi ambayo tunaambiwa haikuwepo tena tarehe 2 Novemba, 1964?

Tunaelewa kwamba tarehe 3 Desemba, 1964 ikiwa ni takriban wiki sita tokea jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilipoanza kutumika, ulipelekwa Mswada wa Sheria katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kubadilisha jina hilo. Suala linalokuja hapa ni kwamba: Je, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipata wapi mamlaka ya kubadilisha jina rasmi la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ ambalo ndilo jina lililotajwa katika Sheria ya Kuridhia Hati ya Makubaliano ya Muungano (Sheria Nam. 22 ya 1964) wakati Hati yenyewe ya Makubaliano haikutoa mamlaka kwa chombo chochote kubadilisha masharti yaliyomo kwenye Hati hiyo?

Wakati umefika sasa wa kurudisha jina linaloakisi msingi wa Muungano wenyewe ambao umetokana na nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na pia kuutambua na kuukiri ukweli huo.

Hata ukiangalia mifano ya nchi nyingine zilizoungana, jina la miungano huweka bayana kwamba zilizoungana ni zaidi ya nchi moja. Kwa mfano, Muungano wa Nchi (states) za Marekani unaitwa kwa kiingereza United States of America (USA), ule uliokuwa Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti ukiitwa Union of Soviet Socialist Republics (USSR) na ule Muungano wa Falme za Kiarabu unaitwa United Arab Emirates (UAE).

Ili kuondosha dhana iliyojengeka kwamba muungano wa jamhuri zetu mbili umeunda nchi moja na kuzifuta nchi zetu, Katiba Mpya inapaswa kuweka jina linalotambua msingi huo na historia hiyo. Hivyo basi, jina jipya liwe ni Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar na kwa kiingereza The Federal Republics of Tanganyika and Zanzibar.

Ibara ya 1, maneno ya mwisho yanayosomeka “ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru” yaondoke. Muungano haukukusudia kufuta uhuru wa nchi zilizoungana na hatuamini kwamba kwa kukubali kuingia katika muungano, nchi washirika zilisalimisha uhuru wao. Kinachozungumzwa katika utangulizi wa Mkataba wa Muungano wa 1964 ni mahusiano au maingiliano ya watu (furthering that association and strengthening of these ties) na siyo kusalimisha mamlaka au kufuta uhuru wa nchi washirika (associating states).

Kwa vyovyote vile, Uhuru wa Tanganyika uliopatikana tarehe 9 Desemba, 1961 na ambao unasherehekewa hadi leo na Uhuru wa Zanzibar uliopatikana kwa njia ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ambayo yanaadhimishwa hadi leo, uko pale pale na nchi zetu mbili hazikuwa na maana ya kusalimisha uhuru huo kwa kuingia kwenye Muungano baina yao.

Isitoshe, maelezo yaliyomo kwenye Ibara ya 1 yanayosomeka kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili” siyo sahihi. Kilichoundwa kupitia Muungano huu ni SHIRIKISHO na siyo NCHI. Hakuna kifungu chochote katika Mkataba wa Muungano ambacho kinazifuta nchi za Tanganyika na Zanzibar. Kwa hakika, maneno “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” yaliyomo kwenye Ibara ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, ni maneno mapya yaliyoingizwa mwaka 1984 wakati wa marekebisho ya Katiba hiyo. Hayakuwemo kwenye Katiba ya Muda ya 1964; hayakuwemo kwenye Katiba ya Muda ya 1965; na wala hayakuwemo kwenye Katiba ya mwaka 1977 (kabla ya kufanyiwa marekebisho makubwa mwaka 1984).

Katiba ya Muda ya 1964, Ibara ya 1 ilisema: “Tanganyika and Zanzibar is one United Sovereign Republic” ambayo tafsiri yake ni: “Tanganyika na Zanzibar ni Jamhuri huru moja iliyoungana”. Katiba ya Muda ya 1965, Ibara ya 1  ilisema: “Tanzania is a United Sovereign Republic” ambayo tafsiri yake ni: “Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano”. Na Katiba ya 1977 (kabla ya marekebisho ya mwaka 1984) , Ibara ya 1  ilisema: “Tanzania ni Jamhuri ya Muungano”.

Kwa hivyo, Ibara ya 1 inapaswa isomeke kama ifuatavyo:

“1.-(1) Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ulioundwa kupitia Hati ya Makubaliano ya Muungano baina ya nchi hizo mbili tarehe 26 Aprili, 1964.

(2) Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu, na lisilofungamana na dini ijapokuwa raia wake wana imani zao za dini.

(3) Hati ya Makubaliano ya Muungano baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyorejewa katika ibara ndogo ya (1), ndiyo msingi mkuu wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar na Katiba hii, kwa kadiri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.”

Pendekezo la kuongeza Ibara ndogo mpya ya 1(4):

Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964 umeweka wazi katika Utangulizi wake kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hatua ya mwanzo kuelekea Umoja wa Afrika ambapo inaelezwa:

WHEREAS the Governments of the Republic of Tanganyika and of the Peoples’ Republic of Zanzibar being mindful of the long association of the peoples of these lands and of their ties of kinship and amity, and being desirous of furthering that association and strengthening of these ties and of furthering the unity of African peoples have met and considered the union of the Republic of Tanganyika with the Peoples Republic of Zanzibar;”

Hata sasa tunapojadili Katiba Mpya, hoja kubwa inajengwa kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mwanzo tu wa kufikia muungano mkubwa zaidi wa nchi za Afrika Mashariki na hatimaye wa nchi zote za Afrika.

Iwapo malengo hayo ni ya dhati na si propaganda tu za kisiasa ni muhimu basi msingi huu ukazingatiwa katika Katiba Mpya ili kufuta ile dhana kwamba muungano huu ulikuwa na dhamira moja tu ya kuimeza Zanzibar na kuifanya sehemu ya Tanganyika mpya iliyopewa jina la Tanzania.
Rasimu ya Katiba kama ilivyo sasa haitoi fursa wala haioneshi kama kuna uwezekano wa nchi nyengine kujiunga na Muungano huu.  Je, ile dhana ya kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hatua ya mwanzo tu ya muungano mkubwa zaidi wa nchi za Afrika na ambayo inatajwa pia kama ni mojawapo ya sababu za kuunda muungano huu katika maelezo ya utangulizi wa Mkataba wa Muungano wa 1964 kwa maneno “and being desirous of… furthering the unity of African peoples”, sasa haipo tena?

Kuna haja ya kuzingatia utaratibu kama ule uliomo katika kifungu cha 3(1) cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unatoa uhuru na fursa kwa nchi nyengine yoyote kujiunga iwapo itakubaliana na masharti yaliyowekwa.
Tunapendekeza kuwepo kwa Ibara Ndogo mpya ya 1(4) itakayoruhusu nchi nyengine ikitaka kujiunga na Shirikisho hili iweze kufanya hivyo, alimradi tu wanakubaliana na masharti ya Katiba hii; na kifungu hicho kisomeke kama ifuatavyo:

“1(4).- Nchi yoyote inaweza kuomba kujiunga katika Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ikiwa nchi hiyo itatimiza masharti yaliyowekwa katika Katiba hii, na kwa ridhaa ya Serikali na Bunge la Tanganyika na Serikali na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na ridhaa ya Serikali na Bunge la Shirikisho.”

Ibara ya 2:
Eneo la Shirikisho na Mipaka ya Zanzibar na Tanganyika

Katika eneo hili, Kamati Namba Sita ilikubaliana jinsi ya kuiandika upya Ibara ya 2 kwa msingi wa kutambua  kwamba eneo la Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni eneo lote la Tanganyika ikijumuisha na sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha na sehemu yake ya bahari na maeneo yao yatakayoongezwa.

Mbali na kutaja eneo la Shirikisho, Katiba Mpya ni lazima itamke bayana na kwa uwazi kabisa na kutambua na kuheshimu mipaka ya nchi washirika (Zanzibar na Tanganyika) kama ilivyokuwa kabla ya siku ya Muungano tarehe 26 Aprili, 1964. Hili ni muhimu katika kuheshimu mamlaka ya nchi washirika katika kusimamia mambo yasiyo ya Muungano katika maeneo yao.

Baada ya hapo, Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Tanganyika (itakayotungwa baada ya kupata Katiba mpya ya Muungano) kila moja iweke wazi mipaka yake.

Jambo zuri ni kwamba wakati zinaungana, Zanzibar na Tanganyika zilikuwa tayari ni nchi zenye mamlaka kamili zikiwa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na hivyo kila moja ilikuwa na mipaka yake inayoeleweka ambayo ilitajwa katika Katiba za Uhuru za Tanganyika na Zanzibar.

Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1961 inafafanua eneo la Tanganyika kupitia Ibara ya 89(1) yenye tafsiri kama ifuatavyo:

“Tanganyika” means the territory that, immediately before the ninth day of December, 1961, was comprised in the Trust Territory of Tanganyika under United Kingdom administration;

Yaani “Tanganyika” maana yake ni eneo ambalo, mara kabla ya tarehe 9 Desemba, 1961, lilijumuishwa kwenye Eneo la Amana la Tanganyika lililokuwa chini ya utawala wa Uingereza;

Na kwa upande wa Zanzibar, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1963 inafafanua eneo la Zanzibar kupitia Ibara ya 136 yenye tafsiri kama ifuatavyo:

“The State of Zanzibar” means the Islands of Zanzibar, Pemba and Latham including the territorial waters thereof, and any islets within those waters;
Yaani “Dola ya Zanzibar” maana yake ni visiwa vya Unguja, Pemba na Latham pamoja na eneo lake la bahari, na visiwa vyovyote vidogo vilivyomo kwenye eneo hilo la bahari;

SEHEMU YA PILI:
Ibara ya 8:
Mamlaka na Utii wa Katiba

Ibara hii inapaswa itamke wazi kwamba Ukuu wa Katiba hii utahusika na mambo ya Muungano tu kama yalivyo kwenye Nyongeza ya Katiba. Hivyo basi, Ibara Ndogo ya 8(1) mwishoni iongezewe maneno, “kwa kadiri yatakavyohusika na utekelezaji wa mambo ya Muungano”.

Kwa msingi huo huo, Ibara Ndogo ya 8(4) inapaswa iongezewe maneno kwamba sheria, mila, desturi au uamuzi ambao hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili “kwa kadiri utakavyokuwa unahusu utekelezaji wa mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa kwenye Nyongeza ya Katiba hii.

Hili ni muhimu kwa sababu katika Rasimu ya Katiba Mpya kuna suala la Haki za Binadamu (ambalo tutalitolea maoni makhsusi tutakapofikia kujadili Sura ya Nne ya Rasimu ya Katiba). Ibara ya 8(3) isipobainisha wazi kwamba sheria, mila, desturi au uamuzi unaokusudiwa ni kuhusiana na mambo ya Muungano tu, utekelezaji wake unaweza ukaja ukaleta mtafaruku hasa ikizingatiwa sehemu ya mfumo wa sheria wa nchi mshirika mmoja (Zanzibar) inatambua sheria za kiislamu katika mambo ya kifamilia na mfumo huo umewekewa Mahkama ya Qadhi ambayo uwezo wake unatambuliwa ndani ya Katiba ya Zanzibar.

Mahkama mara nyingi hutafsiri mfumo wa ulinzi wa haki za binadamu katika kila nchi kulingana na mazingira ya nchi husika. Mfumo huu usipowekwa wazi unaweza kuja kusababisha migongano au mitafaruku isiyo na sababu baina ya mamlaka ya Shirikisho na mamlaka ya nchi washirika na kwa madhumuni ya maelezo haya inakusudiwa zaidi Zanzibar.

SURA YA SITA YA RASIMU – MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO

Sura ya Sita yenye ibara tisa kuanzia Ibara ya 60 hadi 69 inahusu muundo wa Muungano. Ni maoni yetu kwamba ili kufahamu maoni ya wajumbe walio wachache kuhusiana na muundo wa Muungano, ni vizuri kwanza kujikumbusha hali halisi ya Muungano ilivyo katika miaka hamsini iliyopita ili kujua ni muundo upi unaweza kutuondoa katika hali iliyopo sasa.

MISUKOSUKO KATIKA MUUNGANO

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umepita katika masaiba kadhaa tokea kuasisiwa kwake miaka 50 iliyopita lakini mtikisiko ulioukumba katika siku za karibuni ni mkubwa sana. Ni mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu ambapo suala linaloulizwa ni iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika baadhi ya mambo, je, Zanzibar na Tanganyika zimejifuta na hivyo kupoteza hadhi zake kama nchi? Hilo limekuwa ndiyo suala kubwa linaloulizwa na wananchi wa Tanganyika na Zanzibar hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutamka Bungeni kwamba Zanzibar si nchi.

Hakuna awezaye kubisha kwamba tokea kuasisiwa kwake, Muungano huu umejengeka kutokana na misingi ya khofu, kutiliana shaka na kutokuaminiana baina ya pande mbili zinazouunda, ambako wakati mwengine kumepelekea hata kutishia uhai wa Muungano wenyewe.

Muungano umekuwa gumzo kuu katika takriban kila mjadala wa katiba na siasa katika nchi yetu. Umejitokeza na kujionyesha hivyo katika mwaka wa mwanzo wa Muungano kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar, kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mwaka 1964 – 1966, wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe, wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi Maalim Seif Sharif Hamad na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake 6 mwaka 1988, katika harakati za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na Muungano huo mwaka 1989/90, wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi mwaka 1991, katika sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993, wakati wa mjadala wa G-55 kudai kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, katika mjadala wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano mwaka 1994/95, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na karibuni kabisa kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar, harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki na pia baada ya kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyofanywa mwaka 2010.

Ukiondoa kuibuka kwake katika mijadala mikubwa ya kikatiba na kisiasa nchini, kwa upande mwengine katika uendeshaji wa shughuli za Serikali za kila siku, “matatizo na vikwazo kadhaa ya kiutawala na kiutendaji” vimekuwa vikiripotiwa kila mara kwamba vinakwamisha uimarishaji wa Muungano.

Tume na Kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda Tume na Kamati zifuatazo, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala haya:
  1. Kamati ya Mtei
  2. Tume ya Jaji Francis Nyalali (1991)
  3. Kamati ya Shellukindo (1994)
  4. Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
  5. Kamati ya Jaji Mark Bomani (1995)
  6. Kamati ya Jaji Robert Kisanga (1998)
  7. Kamati ya ‘Harmonization’
  8. Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
  1. Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
  2. Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna)  ya 1997
  3. Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman)
  4. Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
  5. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje
  6. Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001
  7. Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
  8. Kamati ya Mafuta
  9. Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
  10. Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
  11. Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu
  12. Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
  13. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa (2004)
Ukiacha Tume, Kamati na Ripoti hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao ulitarajiwa uwe ndiyo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa Muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa. Utaratibu huu uliachwa kwa muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali yake huko Ngurdoto, Arusha mwezi Februari, 2006. Mikutano hiyo sasa imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mikutano, Makongamano, Semina na Warsha vimefanywa kujadili masuala haya na kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Wasomi na wanafunzi wamefanya tafiti kadhaa na kujipatia shahada na stashahada hadi ngazi ya Ph.D juu ya Muungano lakini bado matatizo yako pale pale na yanaongezeka kila kukicha.
Yanayoonekana na kuelezwa kama matatizo, mapungufu, dosari, kasoro na, kwa msamiati wa sasa, kero yamekuwa ndiyo yale kwa yale. Kwa mtazamo wetu, sababu kuu mojawapo iliyotufikisha hapa ni muundo wa Muungano wa Serikali Mbili uliopo sasa na kitendo cha Tanganyika kuvaa koti la Muungano.

MKATABA WA MUUNGANO HAUJAFUTA SERIKALI YA TANGANYIKA

Katika makubaliano ya kimataifa yaliyounda Muungano, ambayo kama tulivyoonesha hapo juu uhalisia wake umezua mashaka makubwa kutokana na kutoonekana kwa Hati ya Makubaliano ya Muungano, lakini hata tukichukulia kuwa hicho kinachodaiwa kuwa Makubaliano ya Muungano kuwa ndicho, basi hakuna kifungu hata kimoja ndani yake kilichotoa au kuagiza kwamba Serikali ya Tanganyika ifutwe. Serikali ya Tanganyika, kama ilivyo ile ya Zanzibar, imelindwa na kifungu cha (v) kinachosomeka kwamba: “The existing laws of Tanganyika and of Zanzibar shall remain in force in their respective territories…”. Kinachosemwa hapa ni kwamba “Sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kufanya kazi na kuwa na nguvu katika maeneo yao.”
Wataalamu wa katiba na sheria wanafahamu kwamba katiba ndio sheria mama ya sheria zote za nchi. Hivyo Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na Serikali yake iwepo, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano. Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye Muungano kama ambavyo Katiba (au kabla ya hapo Dikrii za Kikatiba –Constitutional Decrees) na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa yale mambo ambayo si ya Muungano. Hiyo ndio tafsiri ya ‘maeneo yao’.

Wazanzibari wanafahamu kwamba Katiba na Serikali ya Tanganyika vimefutwa kwa makusudi na Mwalimu Julius Nyerere na Bunge la Tanganyika ili kujipa nafasi kuitumia Serikali ya Muungano, kama kwamba ndio Serikali ya Tanganyika. Lengo ni hatimaye kuiuwa Serikali ya Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa na jina jipya la Tanzania lenye mipaka mipya, yaani kuwa nchi moja yenye Serikali Moja.

Hiyo ndio ghilba iliyofanywa na viongozi wa Tanganyika mara baada ya kutiwa saini makubaliano. Kwa kusaidia kufichuwa ukweli wa hadaa hii, ni vyema ikaangaliwa Sheria Na. 22 ya mwaka 1964 inayoitwa “Union of Tanganyika and Zanzibar Act, 1964.” Sheria hii ilipitishwa na Bunge la Tanganyika Aprili 25, 1964, siku moja kabla Muungano kuanza kufanya kazi. Ilikusudiwa kuthibitisha kukubalika Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar upande wa Tanganyika(ratification). Kifungu cha (viii) cha Makubaliano ya Muunganokinaagiza ifanyike hivyo kwa pande zote mbili za Muungano.
Inasikitisha kusoma katika kifungu Na. 2 cha sheria hiyo kwamba:

“existing law” means the written and unwritten law as it exists immediately before the Union Day … but does not include the Constitution of Tanganyika insofar as it provides for the government of the Republic of Tanganyika or any declaration or law, or any provision thereof, which expires with effect from commencement of the interim Constitution;”

(“Sheria iliyopo maana yake ni sheria iliyoandikwa na isiyoandikwa kama ilivyo kabla tu ya siku ya Muungano… lakini haijumuishi Katiba ya Tanganyika kwa mintaraf ya kuiweka kwake Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika au tamko au sheria, au kifungu chochote ambacho kinafutika kwa kuanza kufanya kazi Katiba ya Muda).”

Kwa hivyo, wakati Bunge la Tanganyika linapitisha sheria ya kuridhia (ratify) kuwepo kwa Muungano kwa upande wa Tanganyika, sheria hiyo ilianza kuvunja masharti ya vifungu vya makubaliano hayo. Mfano mwengine ni kifungu Na. 7 cha sheria hiyo kinachosema:

“7. On the commencement of the interim Constitution of the United Republic, the Constitution of Tanganyika shall cease to have effect for the government of Tanganyika as a separate part of the United Republic”.

(“Itapoanza kufanya kazi Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Tanganyika itasita kuwa na nguvu kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika kama sehemu nyengine ya Jamhuri ya Muungano.”)

Kwa maneno mengine, sheria ambazo zilitakiwa zitumike Tanganyika kwa mambo ambayo si ya Muungano zilipewa maana mpya kwamba eti zisijumuishe Katiba ya Tanganyika.

Jambo moja lililo wazi, pamoja na hatua hii ya kuifuta Katiba ya Tanganyika, ni kwamba kule kuendelea kutambua kuwepo kwa sheria nyengine za Tanganyika bado kunamaanisha kuwepo kwa mamlaka ya Tanganyika ambako sheria hizo kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano ziliendelea na zinaendelea kutumika hadi leo.

Zaidi, inapaswa ifahamike kwamba kufuta Katiba ya Tanganyika kulikofanywa na vifungu vya sheria hii hakukubadilisha makubaliano yaliyokwishatiwa saini kati ya Serikali mbili zilizounda Muungano, yaliyosema kwamba sheria za nchi mbili hizi zitaendelea kutumika katika maeneo yao. Bunge la Tanganyika, na hata Bunge la sasa la Muungano, halikuwa na mamlaka kutafsiri vifungu vya Mkataba wa Muungano ambao ni mkataba wa kimataifa.

Utaratibu wa kisheria ni kwamba kama Mkataba ulitakiwa kutafsiriwa basi mkataba huo ulipaswa kutoa tafsiri ya vifungu vyake, tafsiri ambayo ingepaswa iwe sehemu ya Mkataba huo. Na wala makubaliano yale hayakufuta wadhifa wa Rais wa Tanganyika. Si hivyo tu, bali pia Katiba ya Muungano ambayo ilitakiwa iwe ya muda tu kwa mwaka mmoja (interim) ilikuwa ni ile ya Tanganyika iliyofanyiwa marekebisho kwa ajili ya kutumika kwa Serikali ya Muungano.
Haikuruhusiwa kutumika kuiongoza Tanganyika kwa sababu Tanganyika ilikuwa na Katiba yake na Rais wake. Mwalimu Nyerere alikuwa na vyeo viwili, Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano na Katiba ya Muungano na Rais wa Tanganyika kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika, kama alivyokuwa Mzee Karume ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano na Katiba ya Muungano na akaendelea kubaki kuwa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Dikirii za Katiba ya Zanzibar (Constitutional Decrees).

Hivyo ndivyo makubaliano yalivyokuwa na ndivyo yalivyopaswa yawe hadi hii leo. Waliobadilika ni watu tu. Kufanya vyenginevyo ni kinyume na makubaliano yale na ndio sababu ya migogoro ya Muungano.

Hatua zote za kuepusha Serikali ya Tanganyika kuwepo zilifanywa kwa makusudi kabisa, ili itumike Serikali ya Muungano kama ndio Tanganyika. Katika Sheria ile Na. 22 ya 1964, Rais wa Tanganyika amejipa madaraka ya kutunga na kutoa maagizo yanayohusu Muungano kwa kutumia amri (Decrees) za Sheria ya Tanganyika.

Siku moja tu baada ya kupitishwa Sheria Na. 22 ya 1964, Rais Julius Nyerere alitoa Amri za Rais (Decrees) mbili zilizotokana na kifungu cha 5(2), cha 7(2) na (3), na cha 10 vya Sheria hiyo Na. 22 ya 1964, yaani The Provisional Transitional Decree 1964, na ile ya Interim Constitution Decree 1964 ambazo zilifanya mabadiliko makubwa ya Muungano nje ya yale makubaliano yaliyokuwemo katika Mkataba wa Muungano.

Miongoni mwa mambo yaliyodhihirisha kuwa hakukuwa na nia njema katika Muungano huu tokea awali ni pale watumishi wa Serikali ya Tanganyika wote, bila kujali kama wanashughulikia mambo ya Muungano au mambo yasiyo ya Muungano, walipopandishwa vyeo kwa pamoja na kufanywa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kama kifungu cha 3(1) cha Provisional Transitional Decree kinavyosema:

“Every person who holds office in the service of the Republic of Tanganyika immediately before the Union Day, shall on the Union Day be deemed to have been elected, appointed or otherwise selected to the corresponding office in the service of the United Republic.”

Yaani kila mtumishi wa Serikali ya Tanganyika mara kabla ya siku ya Muungano kufumba na kufumbuwa (au tuseme kwa mtindo wa abra cadabra) anakuwa mara moja mtumishi wa Serikali ya Muungano kuanzia siku ya Muungano.
Vivyo hivyo, kifungu cha 6(1) cha Provisional Transitional Decree kinasema mara tu baada ya kuanza Muungano, Mahkama ya Tanganyika na Majaji wake wote nao watakuwa ndio Mahkama na Majaji wa Jamhuri ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano. Hati ya Makubaliano ya Muungano na hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano mpaka leo hazitambuwi Mahkama kama ni suala la Muungano (ukiondoa Mahkama ya Rufaa, ambayo nayo kuongezwa kwake kama jambo la Muungano kumejaa utatanishi). Nembo ya Tanganyika inatumika kama nembo ya Jamhuri ya Muungano, Wimbo wa Taifa wa Tanganyika unatumika kama Wimbo wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano na Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika inachukuliwa kama Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Haya yote hayamo na ni kinyume na Makubaliano ya Muungano ya 1964. Yote haya na kile kifungu cha 7 cha Sheria Na. 22 ya 1964 kinachofuta kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika hayakubadilisha na wala hayana mahusiano na Makubaliano ya Muungano ya 1964. Yote haya yalifanywa na Rais Julius Nyerere kwa maslahi ya Tanganyika nje ya Mkataba wa Muungano.
Aliyekuwa Spika wa Bunge na baadaye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Pius Msekwa, analifahamu vyema suala hili. Katika waraka wake alioutoa kwenye Semina kuhusu Muungano hapo Hoteli ya Mkonge, Tanga tarehe 25—27 Februari 1994 anasema:

“The Transitional Decree, 1964 published on 01/05/64, transferred persons who were holding office in the public service of the Republic of Tanganyika to the corresponding office in the public service of the United Republic of Tanzania. By the same decree the High Court of Tanganyika also became the High Court of United Republic of Tanzania and the public seal of Tanganyika became public seal of the United Republic.”

Athari za hatua hizi kwa Zanzibar ziko wazi. Tanganyika imejigeuza Tanzania na imechukua mamlaka ya mambo muhimu ya Zanzibar huku ikijipa hadhi ya kuwa juu ya Serikali ya Zanzibar kinyume na Mkataba wa Muungano.
Hii ndiyo siri ya viongozi wa Tanganyika wanaoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano kung’ang’ania mfumo wa Serikali mbili na kukataa kata kata mabadiliko yoyote ya mfumo huo kwani Tanganyika inanufaika nao kwa kuwa yenyewe ndiyo imekuwa ‘Muungano’. Hili limethibitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, katika hotuba yake ya uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum. Kukubali muundo wa Serikali tatu ni kuzifanya Tanganyika na Zanzibar ziwe na hadhi na fursa sawa katika Muungano, jambo ambalo Tanganyika hailitaki maana kulikubali ni kukubali kupoteza fursa zote inazozipata hivi sasa kwa kujikweza kwake na kujifanya kuwa ndiyo ‘Muungano’.

Ushahidi wa wazi wa hoja hii ni kwamba mtu anapoangalia taasisi zote za Muungano zilizoundwa chini ya Katiba au sheria za Muungano ambazo zinazikutanisha Serikali mbili zilizopo sasa, ataona kuwa wajumbe wanaowakilisha upande wa Serikali ya Muungano wote ni kutoka Tanganyika. Hoja inayojitokeza ni kwamba Serikali ya Muungano ni ya shirika ambapo Zanzibar ni sehemu ya ushirika huo, kwa nini basi wajumbe wanaowakilisha Serikali hiyo ya Muungano watoke upande wa Tanganyika peke yake? Jawabu ni rahisi. Serikali ya Muungano kwa hakika ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika koti la Muungano.

Katiba ya Muda ya 1965 na ya 1977 zaitambua Tanganyika

Kuthibitisha zaidi kwamba Tanganyika haikufutwa na wala haikufutika kupitia Makubaliano ya Muungano ya 1964,  mtu ataona kwamba bado inatambuliwa hata katika Katiba ya Muda ya 1965 na hata kuwekewa Mkuu wake wa kushughulikia mambo yanayoihusu kama ambavyo Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Zanzibar anayeshughulikia mambo yanayoihusu.

Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Muda ya 1965 inaeleza kwamba:

“13.-(1) There shall be two Vice-Presidents of the United Republic (who shall be styled the First Vice-President and the Second Vice-President respectively), one of whom shall be the principal assistant of the President in the discharge of his executive functions in relation to Zanzibar and, under the style of President of Zanzibar, the head of the Executive for Zanzibar, and the other shall be the principal assistant of the President in the discharge of his executive functions in relation to Tanganyika and the leader of Government business in the National Assembly.”

Tafsiri yake kwa Kiswahili ni kwamba:

“13.-(1) Kutakuwa na Makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano (ambao wataitwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais), ambapo mmoja wao atakuwa ni msaidizi mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake za kiutendaji kwa Zanzibar na, kwa cheo cha Rais wa Zanzibar, atakuwa ndiye Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar, na mwengine atakuwa ni msaidizi mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake za kiutendaji kwa Tanganyika na Kiongozi wa Shughuli za Serikali ndani ya Bunge.”

Mbali ya Ibara hiyo kuitambua Tanganyika na kumtaja Makamu wa Pili wa Rais kama Msaidizi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika majukumu yake ya kiutendaji kwa upande wa Tanganyika, sheria nyingi zilizotungwa kati ya 1964 na 1977 ziliendelea kutumia jina la Tanganyika.

Kwa hakika, jina la Tanganyika kama jina la nchi moja kati ya nchi mbili zilizounda Muungano lilifutwa na Katiba ya 1977; ijapokuwa Katiba hiyo hiyo ya 1977 (pamoja na marekebisho yake yote yaliyofanyika hadi sasa) bado inaendelea kuitambua Tanganyika. Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili inayofanya rejea kwenye Ibara ya 98(1)(a) ya Katiba na kutaja mambo ambayo maamuzi yake yanahitaji theluthi mbili ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano inataja mojawapo ya mambo hayo kuwa ni:
“Sura ya 500, (Toleo la 1965), Sheria ya kuthibitisha Tanganyika kuwa Jamhuri, ya mwaka 1962.”

Iwapo Sheria hiyo inaendelea kutambuliwa na hata kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, je, ni Jamhuri ipi iliyozaliwa 1962 ambayo kuibadilisha kunahitaji theluthi mbili ya Wabunge wote kama si Jamhuri ya Tanganyika?

UVUNJWAJI WA MKATABA WA MUUNGANO

Mbali na suala la muundo wa Muungano, maeneo mengine mengi yanayogusa msingi wa Mkataba wa Muungano yaliendelea kuvunjwa na Tanganyika ikivaa koti la Serikali ya Muungano.

Mambo ya Muungano na Mamlaka ya Zanzibar:

Kifungu cha (iv) cha Mkataba wa Muungano kiliorodhesha mambo 11 tu ambayo ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kuwa mambo ya Muungano. Hata hivyo, kipindi cha miaka 50 ya Muungano kimeshuhudia mambo hayo yakiongezwa isivyo halali kwa kutumia chombo kisicho na mamlaka ya kufanya hivyo yaani Bunge la Muungano na sasa kufikia 22 lakini ukiyanyumbua yanafikia 31. Mfano unakuta kifungu kimoja cha 11 kinayaweka pamoja mambo manne ambayo ni Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu. Kwa lugha ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, anasema ni makontena 22 yenye mambo 31 ya Muungano. Ikumbukwe kwamba kila hatua ya kuongeza mambo ya Muungano maana yake ni kuchukua mamlaka ya Zanzibar na kuyahamishia kwa Serikali ya Muungano ambayo kama tulivyokwisha onesha kwa hakika hasa ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika koti la Muungano.

Mambo ya awali ya Muungano ambayo yanatajwa katika kile tunachoambiwa ndiyo Hati ya Makubaliano ya Muungano ni kumi na moja (11) na ni haya yafuatayo:

(i)             Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(ii)             Mambo ya Nje.
(iii)            Ulinzi.
(iv)            Polisi.
(v)             Mamlaka juu ya Hali ya Hatari.
(vi)            Uraia.
(vii)           Uhamiaji.
(viii)           Mikopo na Biashara ya Nje.
(ix)            Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(x)            Kodi ya Mapato na Kodi ya Mashirika, Ushuru wa Forodha na Kodi ya Bidhaa.
(xi)              Bandari, Usafirishaji wa Anga, Posta na Simu.
Mambo yaliyoongezwa juu ya Makubaliano ya Muungano ya asili, yaani, yale kumi na moja (11) ni haya, kama yanavyoelezwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano:-
(xii)             Mambo yote yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti); mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
(xiii)           Leseni za Viwanda na Takwimu.
(xiv)          Elimu ya Juu.
(xv)           Maliasili ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa za mafuta, na gesi asilia.
(xvi)           Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
(xvii)          Usafiri na Usafirishaji wa Anga.
(xviii)        Utafiti.
(xix)          Utabiri wa Hali ya Hewa.
(xx)           Takwimu.
(xxi)           Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
(xxii)          Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo.

Ukiondoa mambo hayo, yapo pia mambo mengine ya ziada ambayo yameingizwa katika Muungano kwa Bunge tu kutunga sheria kwa kutumia Ibara ya 64(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 na kutangaza kwamba zitatumika hadi Zanzibar. Mfano wa masuala kama hayo ni Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Utawala Bora na Haki za Bianadamu. Yapo baadhi yake kwa mfano Usafiri wa Baharini ambapo Zanzibar ilikataa kutekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge (The Merchant Shipping Act) na hatimaye ikatunga sheria yake yenyewe kuhusiana na suala hilo (The Maritime Transport Act).

Lakini kuendelea kupora mamlaka ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano hakukuishia hapo. Kwa kutumia mwanya wa uanachama mmoja wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki; dhamana juu ya mambo mengine kumi na tatu (13) yamechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano bila ya ridhaa ya Zanzibar. Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeweka mambo kumi na saba (17) yanayosimamiwa na Jumuiya hiyo lakini kati ya hayo, kwa upande wa Tanzania, ni mambo manne (4) tu ndiyo yaliyo katika mambo ya Muungano na hivyo kuwemo katika mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mambo hayo manne (4) ni haya yafuatayo:
  1. Ushirikiano katika mambo ya Fedha na Uchumi (Monetary and Financial Co-operation);
  2. Uhuru wa Mtu kwenda atakapo, Uhuru wa Huduma za Kazi, na Haki ya Ukaazi (Free Movement of Persons, Labour Services, Right of Establishment and Residence);
  3. Mahusiano na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa na Washirika wa Maendeleo (Relations with other Regional and International Organisations and Development Partners); na
  4. Ushirikiano katika Mambo ya Siasa (Cooperation in Political Matters).
Ukiondoa mambo hayo manne (4), mambo mengine kumi na tatu (13) yaliyomo katika Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki si mambo ya Muungano na hivyo ni dhamana ya mamlaka ya Zanzibar lakini yameporwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kujitwisha dhamana ya kuyasimamia katika Jumuiya hiyo. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
  1. Ushirikiano katika Kufungua Milango ya Biashara na Ukuzaji wake (Cooperation in Trade Liberalisation and Development);
  2. Ushirikiano katika Maendeleo ya Uwekezaji na Viwanda (Cooperation in Investment and Industrial Development);
  3. Ushirikiano katika Uwekaji Viwango, Uhakika wa Ubora, na Upimaji (Cooperation in Standardisation, Quality Assurance, Meteorology and Testing);
  4. Ushirikiano katika Miundombinu na Huduma (Cooperation in Infrastructure and Services);
  5. Ushirikiano katika Uendezaji wa Rasilimali Watu, Sayansi na Teknolojia (Cooperation in the Development of Human Resources, Science and Technology);
  6. Kilimo na Uhakika wa Chakula (Agriculture and Food Security);
  7. Ushirikiano katika Usimamizi wa Mazingira na Maliasili (Cooperation in Environment and Natural Resources Management);
  8. Ushirikiano katika Usimamizi wa Utalii na Wanyamapori (Cooperation in Tourism and Wildlife Management);
  9. Afya na Masuala ya Kijamii na Kiutamaduni (Health, Social and Cultural Activities);
  10. Uimarishaji wa Nafasi ya Wanawake katika Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii (Enhancing the Role of Women in Socio-Economic Development);
  11. Masuala ya Sheria na Mahkama (Legal and Judicial Affairs);
  12. Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia (The Private Sector and the Civil Society);
  13. Ushirikiano katika Maeneo mengine (Cooperation in other Fields).
Ni wapi Serikali ya Jamhuri ya Muungano imepata mamlaka ya kuyasimamia mambo haya kumi na tatu (13) ambayo ndiyo msingi wa mamlaka ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano? Jibu la mkato lingekuwa ni kwamba ukishaingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki basi umeingia katika mamalaka juu ya Mambo ya Nje. Lakini kama jibu hilo litakuwa sahihi maana yake ni kwamba ukiingia katika Mambo ya Nje, Zanzibar itakuwa haina chake – mambo yake yote yatakuwa chini ya Muungano – na katika hali halisi hivyo ndivyo ilivyo.

Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais:

Mbali na dhoruba hizo dhidi ya Mkataba wa Muungano, rungu jengine kubwa dhidi ya Mkataba wa Muungano lilikuwa ni kuvunjwa kwa masharti ya kifungu (iii)(b) cha Mkataba huo ambacho kiliweka utaratibu wa Rais wa Zanzibar kuwa mmojawapo wa Makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Sharti hili liliwekwa makusudi kabisa ili kuweka kiungo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na pia kumhakikishia Rais wa Zanzibar dhamana na uwezo wa kusimamia maslahi ya Zanzibar kwa mambo ya Muungano ambayo Zanzibar imeyatoa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Uhakikisho huu ulitupiliwa mbali na kuvunjwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano bila ya kujali kwamba yalikuwa ni masharti muhimu ya Mkataba wa Muungano ukiwa ni Mkataba wa Kimataifa ulioziunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Lililo baya zaidi ni kwamba katika kufanya hivyo hata yale masharti ya kuhitajika kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wanaotoka Zanzibar na theluthi mbili ya Wabunge wote wanaotoka Tanzania Bara halikuzingatiwa. Hansard ya Majadiliano ya Bunge ya Mkutano wa Ishirini (Sehemu ya Pili)  ya tarehe 25 Aprili, 1995 – 3 Mei, 1995 yanamnukuu aliyekuwa Spika wa Bunge, Mhe. Pius Msekwa, katika ukurasa wa 958, akielekeza:

“… Orodha za Wabunge mlizonazo za mwezi Februari zinaonyesha, idadi halisi ya Wabunge ni 245, baada ya Ndugu Mrema kupoteza Ubunge, idadi halisi ya Wabunge ni 244. Theluthi mbili ya Wabunge 244 ni 163, hiyo idadi ndiyo ya chini inayotakiwa kupitisha Muswada wa Kikatiba. Na kwa sura iliyoletwa ni theluthi mbili ya Bunge Zima siyo theluthi mbili ya kila upande, kwa hiyo tutapiga kura kutafuta theluthi mbili ya Bunge Zima, nafikiri hiyo imeeleweka. Sasa tufanye uamuzi ile hatua ya kwanza kama nilivyosema.”
Maelekezo haya yalipokuwa yakitolewa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano alikuwa ni Mhe. Andrew Chenge ambaye leo hii ni Mjumbe wa Bunge hili Maalum la Katiba. Maelekezo hayo yalitolewa kinyume na masharti ya Ibara ya 98(1)(b) ambayo imetaja mambo yaliyoorodheshwa kwenye Orodha ya Pili ya Nyongeza ya Pili ya Katiba kama mambo yanayohitaji theluthi mbili za kila upande. Orodha ya Pili kwenye jambo namba tano (5) inataja kuwa ni “Madaraka ya Serikali ya Zanzibar”. Hakuna mtu makini atakayebisha kwamba kumuondolea Rais wa Zanzibar ambaye ndiye Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar nafasi yake ya kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ni kuathiri “Madaraka ya Serikali ya Zanzibar”. Lakini bado sharti la theluthi mbili za kila upande lilipuuzwa.

Kipindi cha Mpito kuwa cha Mwaka Mmoja:

Kifungu cha (vii) cha Mkataba huo kinataka Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mashauriano na makubaliano na Makamu wa Rais ambaye pia ni Rais wa Zanzibar kuunda Tume ya Katiba kwa lengo la kutayarisha rasimu ya Katiba ya Kudumu ya Muungano na baadaye kuifikisha rasimu hiyo mbele ya Bunge la Katiba (Constituent Assembly) litakalokuwa na wajumbe kwa idadi watakayokubaliana kutoka Zanzibar na Tanganyika. Hatua hii muhimu sana kikatiba ilitakiwa itekelezwe ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tokea tarehe ya Muungano. Hadi ilipokuja hatua hii ya sasa ya kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hakuna Tume ya Katiba iliyoundwa wala Bunge la Katiba lililoundwa na kuitishwa kwa madhumuni ya kupitisha Katiba ya Kudumu ya Muungano. Kilichofanyika ni kuwa mwezi mmoja kabla ya kumalizika mwaka mmoja uliotakiwa, Bunge la Muungano lilitakiwa na Mwalimu Julius Nyerere kupitisha sheria ya kuahirisha kwa muda usiojulikana tarehe ya kutekelezwa kwa hatua hii. Nani alimpa madaraka hayo Mwalimu Nyerere na Bunge la Muungano kubadilisha masharti ya Mkataba wa Muungano ambao ni Mkataba wa Kimataifa wakati Mkataba huo haukutoa fursa kwa chombo chochote kubadilisha masharti yaliyomo?

Wengine wanadai kwamba sharti hili lilitekelezwa mwaka 1977 pale Mwalimu Julius Nyerere alipoitangaza Kamati ya Watu 20 iliyoundwa na TANU na ASP kutayarisha Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa pia imepewa mamlaka ya kuandaa Rasimu ya Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano na baadaye kulitangaza Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa ndilo Bunge la Katiba. Kila mmoja anajua kwamba Kamati hii haikuandaa rasimu hiyo bali ilipewa tu Rasimu iliyokwisha tayarishwa. Na hata pale Mswada wa Katiba hiyo ulipowasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo liliitwa ndiyo Bunge Maalum la Katiba mjadala haukuzidi muda wa saa mbili na ulikuwa zaidi wa kupongeza na kushangilia tu. Hivi kweli mtu makini anaweza kusema kwamba utaratibu ule ulikuwa ni utekelezaji wa masharti ya kifungu cha (vii) cha Mkataba wa Muungano?

MATATIZO YATOKANAYO NA KIINI CHA TATIZO

Kiini cha tatizo la msingi la Muungano ambalo ni muundo wake unaotokana na tafsiri potofu ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ndicho kimepelekea kujitokeza kwa matatizo mengine katika miaka 50 hii na ambayo yanaongezeka kila kukicha.

Mtu anapoangalia matatizo au hizi zinazoitwa kero atagundua kuwa karibu yote yanatokana aidha kwa mshirika mmoja (mara nyingi Zanzibar) kutokuuamini au kuutilia shaka upande mwengine, au mshirika wa pili (mara nyingi Tanganyika ikivaa koti la Muungano) kuamini kwamba ina haki ya moja kwa moja kuamua na kutekeleza mambo fulani bila ya kulazimika kupata ridhaa ya upande wa pili ambao inahisi kama imeubeba tu (au kwa lugha ya Mhe. Pius Msekwa ni “invited guest” yaani mgeni mwalikwa). Ukiangalia kwa undani utagundua kuwa tatizo linarudi kwenye muundo. Zanzibar haifahamu mamlaka ya Muungano katika Serikali ya Muungano yanaishia wapi ambapo mamlaka kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa ajili ya Tanganyika yanaanza. Tanganyika nayo kwa kuwemo kwake katika Serikali ya Muungano kunaifanya ishindwe kufahamu ni vipi na wapi Zanzibar inapata mamlaka ya kuhoji mambo ambayo yameshatamkwa kwamba ni ya Muungano hata kama hayakuwemo katika Mkataba wa asili wa Muungano.  Hali hii inaonekana katika kila kile kinachoitwa “Kero za Muungano”.

Mifano inaweza kutolewa kwa takriban mambo yote, lakini tuchukue mifano ya mambo matatu yafuatayo yanayozusha malalamiko:
  1. Umilikaji wa Mafuta na Gesi asilia.
  2. Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano.
  3. Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.
Umilikaji wa Mafuta na Gesi asilia

Kwanza, kuingizwa kwake katika orodha ya mambo ya Muungano (kama ilivyo kwa mambo mengi yaliyoongezwa baadaye) hakukufuata taratibu za Serikali ya Muungano (ambayo pia ni Serikali ya Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano) kuishauri na kupata ridhaa ya Zanzibar. Pili, Zanzibar inataka kujua ikiwa mafuta yanapaswa kuwa suala la Muungano na hivyo mapato yatakayopatikana yanufaishe pande zote mbili, kwa nini madini mengine yanayopatikana Bara kama vile dhahabu, almasi au tanzanite hayakufanywa pia kuwa ya Muungano na hivyo kunufaisha pande mbili pia? Kwa hivi sasa, ambapo si mambo ya Muungano, mapato yake yanaponufaisha Tanganyika peke yake, yanaingia katika mfuko (account) upi wa matumizi? Tatu, kwa miaka isiyopungua tisa (9) sasa, Tanganyika imekuwa ikivuna gesi asilia huko Songosongo na Mnazi Bay na kwa miaka miwili sasa imekuwa ikivuna gesi asilia kwa wingi katika maeneo ya bahari iliyopakana na Mtwara lakini pamoja na kutajwa suala hilo kuwa la Muungano, Zanzibar haijafaidika na chochote kutokana na mapato yake. Nne, ikiwa mapato yatakayopatikana kutokana na mafuta na gesi asilia yataingia katika mfuko wa Muungano, kuna uhakika gani wa kutumika kwa shughuli za Muungano tu wakati hakuna mifuko tofauti ya fedha kwa shughuli za Muungano na zile za Tanganyika zisizo za Muungano?

Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano

Je, mtu anaposema Zanzibar haichangii gharama za uendeshaji wa vyombo na taasisi za Muungano kwa sababu tu Serikali ya Zanzibar haitoi fungu la fedha na kuliingiza katika Serikali ya Muungano, Tanganyika ambayo hata Serikali haina inachangia vipi na kiasi gani? Ikiwa mchango wake unatolewa na Serikali ya Muungano, kwani hii siyo serikali ya shirika ambapo Zanzibar pia ni mbia? Vipi basi Zanzibar itakiwe ichangie mara mbili kwa kutumia hadhi mbili tofauti? Na ikichangia (iwapo itachangia), ina uhakika upi kwamba itakachotoa hakitatumiwa na Serikali ya Muungano kwa shughuli za Tanganyika zisizo za Muungano ikitumia mamlaka yake kwa madhumuni hayo? Vivyo hivyo, kwa mapato yatokanayo na vyombo na taasisi za Muungano, tunajua Zanzibar inapata mgao wake na kiasi chake kimewekwa wazi (ingawa kwa sasa ni mapato ya TRA yanayokusanywa Zanzibar; na pia gawio kutoka Benki Kuu (BOT) ambalo nalo kiwango chake hakikubaliki kwa Wazanzibari). Zipo mamlaka nyengine za Kimuungano zinazoingiza mapato na ambazo Zanzibar haipewi chochote kutoka kwake zikiwemo TCRA, TCAA, TPC, TTCL, na TPDC kwa kutaja chache. Masuala zaidi yanakuja: Yale mapato yanayobaki katika Serikali ya Muungano, kuna kipi cha kuonesha mpaka wa matumizi yake kwa mambo ya Muungano na kwa shughuli za Tanganyika zisizo za Muungano? Uadilifu na uwajibikaji wa matumizi yatokanayo na mgao huu wa mapato utaonekana vipi?

Ukweli hasa kuhusiana na suala la uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano ulipatikana kufuatia kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Commission) ambayo iliajiri wataalamu (consultants) kutoka taasisi inayoheshimika duniani yaPriceWaterhouseCoopers kuangalia suala hilo. Ripoti ya Wataalamu ilitolewa Agosti 2006 na kufanyiwa kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini hadi leo imekaliwa na Serikali ya Muungano bila shaka baada ya kutoa picha isiyopendeza kwa upande wa Tanganyika kuhusiana na hali halisi ya vipi uendeshaji wa Muungano ulivyo. Wataalamu wa Kampuni ya PriceWaterhouseCoopers walifanya uchambuzi halisi wa mambo yepi ni ya Muungano na yepi ni ya Tanganyika na yepi ni ya Zanzibar na gharama za uendeshaji wa kila moja. Baada ya orodha kupatikana, watafiti wakatafuta matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa muda wa kiasi cha miaka 10 iliyopita. Watafiti hao walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Muungano halisi. Mwishowe, wakalinganisha iwapo mapato yanakidhi matumizi au yana nakisi (upungufu)? Taarifa ya Tume ya ya Pamoja ya Fedha inayoitwa “Mapendekezo ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato na Kuchangia Gharama za Muungano” ya Agosti, 2006 inaeleza kwenye ukurasa wa 18:

“Uchambuzi unaonyesha kuwa mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi matumizi ya Muungano na kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu zinaonyesha kuwa kiasi kidogo cha mapato hayo kimekuwa kinagharimia matumizi ya Muungano. Kwa mfano, uwiano huu ulikuwa ni Sh. 360,679.87 milioni kati ya Sh. 1,030,513.9 milioni sawa na asilimia 35 mwaka 1999/2000, Sh. 468,450.76 milioni kati ya Sh. 1,801,733.7 milioni sawa na asilimia 26 mwaka 2002/03, na Sh. 636,078.94 milioni kati ya Sh. 2,271,710.5 milioni sawa na asilimia 28 mwaka 2003/04.

Uchambuzi unaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha ziada ya mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika kugharimia mambo yasiyo ya Muungano. Viwango hivi kwa mwaka 1999/2000 vilikuwa ni Sh. 39,822.7 milioni sawa na asilimia 5.9 kwa SMZ na Sh. 631,714.4 milioni sawa na asilimia 94.1 kwa Tanzania Bara. Viwango hivi vilibadilika kwa kiasi kikubwa kwa mwaka wa fedha 2003/04 ambapo kwa SMZ kilishuka hadi Sh. 37,053.3 milioni sawa na asilimia 2.3, na Sh. 1,588,494.1 milioni sawa na asilimia 97.7 kwa SMT.”

Ukweli huu unaonesha hata kama kungekuwa na Serikali Tatu kusingekuwa na haja yoyote kwa Serikali ya Zanzibar na ile ya Tanganyika kulipia fedha za ziada kama wahusika watatunza na kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ya mambo ya Muungano halisi badala ya yale ya Tanganyika kuchanganywa na ya Muungano.  Mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika yalipotengwa nje ya yale ya Muungano, gharama za mambo ya Muungano zimejidhihirisha wazi bila ya kujificha na kuonesha kwamba zinaweza kulipiwa kupitia mapato ya mambo ya Muungano pekee na ziada kubaki. Lakini hili limekuwa rahisi kwa kukubali ukweli kwamba kuna mafungu matatu ya mapato na matumizi katika Serikali zetu mbili. Mafungu hayo ni la SMZ kwa mambo yake yasiyo mambo ya Muungano, la Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na la Serikali ya Muungano inayofanya kazi za Tanganyika kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano.

Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano

Wananchi wengi wa Tanganyika wanahoji vipi Zanzibar iliyo ndogo na ambayo ina watu milioni 1.3 inawakilishwa na wabunge wa kuchaguliwa 50 wakati Dar es Salaam yenye wananchi wengi zaidi ina wabunge wa kuchaguliwa 7 tu? Wabunge hawa wanashiriki mijadala yote ya Bunge ikiwemo ya mambo yasiyo ya Muungano (ambayo kwa usahihi yatakuwa ni mamlaka ya Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano yanayosimamiwa na Serikali ya Muungano). Wanapata wapi uhalali wa kufanya hivyo wakati Wazanzibari hawapangiwi shughuli hizo (kwa mfano elimu, afya, kilimo, maji, umeme, habari, michezo, biashara, viwanda, serikali za mitaa n.k.) na Serikali ya Muungano wala hawasimamiwi katika mambo hayo na Bunge la Muungano? Uko wapi mpaka wa mamlaka ya Wazanzibari katika ushiriki wa Bunge hilo wakati wao wana Serikali yao inayopanga na Baraza la Wawakilishi lao linalosimamia mambo yao kama hayo yasiyo ya Muungano?

Mifano hii inatosha kuonesha kwamba takriban matatizo yote yanatokana na mkanganyiko na mgongano wa maslahi kati ya pande mbili ambao nao unasababishwa na mfumo usio wazi kuhusiana na mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano zinazotambuliwa katika Mkataba wa Muungano. Kwa lugha nyepesi, matatizo haya ya Muungano takriban yote yanatokana na tatizo la msingi la Tanganyika kuvaa koti la Muungano.

HALI HALISI YA MFUMO WA MUUNDO WA SERIKALI MBILI ULIOPO SASA NA JINSI ULIVYOSHINDWA KUTATUA MATATIZO YA MUUNGANO

Kwa madhumuni ya kuelewa msingi wa matatizo yanayoukabili Muungano katika muundo uliopo sasa ni muhimu sana kufanya uchambuzi wa kina wa maeneo yafuatayo:
  • Mfumo Uliopo Sasa na Udhaifu Wake
  • Maeneo Muhimu ya Kuzingatiwa
  1. Mfumo wa Sasa na Udhaifu Wake
Mfumo wa Sasa una mambo 8 ya kuzingatia
I.            Misingi ya Muungano na Utaifa;
II.            Mgawanyo wa Mambo ya Muungano na Yasiyo ya Muungano;
III.            Utaratibu wa Kutunga Sera kwa Mambo ya Muungano;
IV.            Utaratibu wa Kutunga Sheria za Muungano;
V.            Bajeti na Fedha za Muungano;
VI.            Usimamizi wa Mambo ya Muungano;
VII.            Matumizi ya Rasilimali za Muungano
VIII.            Udhaifu wa Jumla wa Mfumo uliopo
  1. Misingi ya Muungano na Utaifa
    1. Kanuni ya Kwanza ya Muungano ni kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitokana na muungano wa Dola mbili huru zilizokuwa na mamlaka kamili na ambazo zilikuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa.  Muungano haukutokana na nchi moja au majimbo ya kiutawala.
    2. Kanuni ya Pili ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kuwa kutokana na mazingira ya kihistoria, kijiografia na kidemografia, haiwezekani kuwa na Muungano wa Serikali moja.  Mheshimiwa Rais Mkapa amelifafanua vizuri sana suala hili katika Hotuba yake ya Miaka 40 ya Muungano (Uk. 31-32 wa Hotuba yake).  Hivyo kwa vyovyote vile, kwa Kanuni hii, Zanzibar itabaki kuwa na utambulisho wake;
    3. Kanuni ya Tatu ya Msingi ni kuwa Muungano una Mamlaka Tatu; Mamlaka ya Muungano, Mamlaka ya Zanzibar na Mamlaka ya Tanganyika kama ilivyofafanuliwa na Hati ya Muungano na Ibara ya Nne ya Katiba ya Muungano;
    4. Kanuni ya Nne ya Msingi ya Muungano ni, kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili, Orodha ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Washirika wa Muungano wanao uhuru na fursa ya kujadili na kukubaliana kuendelea kuwepo au kutokuwepo kwa Muungano.  Utaratibu wa maamuzi katika suala hili ni theluthi mbili ya kura za Wabunge wa kila upande wa Muungano.
    5. Kanuni ya Tano ya Msingi ya Muungano ni usawa katika maamuzi yanayohusu mambo ya Muungano; INGAWA kwa sasa Kanuni hii haitekelezwi kabisa na ndio moja ya kiini cha matatizo ya Muungano;
    6. Kanuni ya Sita ni haki ya pande mbili za Muungano katika ushiriki wa uendeshaji wa mambo ya Muungano;  kwa sasa Kanuni hii pia haifuatwi kabisa nayo pia ni moja ya mizizi ya matatizo ya Muungano.
Pamoja na kuwepo misingi hiyo bayana, Katiba ya sasa haitamki wazi misingi muhimu ya Muungano kwa ufasaha na uwazi.

Katiba ya baadhi ya Nchi kama vile, Switzerland imetamka bayana nani washirika wa Muungano wao na hadhi zao na haki zao kama washirika wa Muungano.  Katiba ya Brazil imetamka bayana washirika wa Muungano wao na hadhi zao.  Katiba ya Urusi imetamka bayana Washirika wa Muungano wao na hadhi zao.

Katiba pia haiweki bayana msingi wa Muungano katika kulinda msingi wa kuwa ni Muungano wa nchi mbili huru zenye mazingira maalum na hivyo kuendelea kulinda mazingira hayo.  Katiba ya Marekani kwa mfano inakataza State moja kugawanywa na pia kuungana na kuwa State moja.

Kwa upande wa sauti sawa katika maamuzi, msingi huu sio tu kuwa haupo bayana bali Katiba ya sasa inahalalisha kutokuwepo kwake.  Imeweka masharti ya wazi yanayovunja Msingi huu wa Muungano kwa kulipa Baraza la Mawaziri mamlaka pekee ya kuamua kuhusu Sera za Muungano na Bunge mamlaka ya kupitisha Sheria za Muungano (kwa mambo yote yaliyoainishwa katika Nyongeza ya Kwanza kuwa ni Mambo ya Muungano) kwa wingi wa Kura tu.
Kwa upande wa haki katika ushiriki wa uendeshaji wa Mambo ya Muungano, masharti pekee ya Katiba ni haki ya kila upande kutoa Rais au Makamu wa Rais.  Hata hivyo kwa mfumo wa sasa Rais wa Muungano na Makamu wa Rais hawana uhusiano wa moja kwa moja na Serikali ya Zanzibar.  Uhusiano uliopo ni wa kisiasa zaidi kwa vile wanatoka Chama kimoja.  Kama watatoka vyama tofauti kimsingi hapatakuwa na pahala pa kuwakutanisha viongozi wa Serikali ya Muungano na wa Serikali ya Zanzibar.

Hivyo moja ya kasoro kubwa za Muungano wa sasa ni kutowekwa bayana misingi ya Muungano, kuivunja na kuhalalisha kuvunjwa kwake.
  1. Mgawanyo wa Mambo ya Muungano na Yasiyo ya Muungano
    1. Mambo ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 4 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977 yametajwa katika Nyongeza ya Kwanza.  Mambo hayo ni kama yafuatayo:
i.      Katiba ya Muungano
ii.      Mambo ya Nje
iii.      Ulinzi
iv.      Usalama
v.      Polisi
vi.      Hali ya Hatari
vii.      Uraia
viii.      Uhamiaji
ix.      Mikopo ya Nje
x.      Biashara
xi.      Utumishi katika Serikali ya Muungano
xii.      Kodi ya Mapato
xiii.     Forodha (Ushuru)
xiv.     Kodi ya Bidhaa (excise)
xv.      Bandari
xvi.     Usafirishaji wa Anga
xvii.    Posta
xviii.    Simu
xix.     Sarafu
xx.      Mabenki
xxi.     Fedha za Kigeni
xxii.     Leseni za Viwanda
xxiii.    Takwimu
xxiv.    Elimu ya Juu
xxv.    Mafuta yasiyosafishwa
xxvi.    Gesi asilia
xxvii.   Baraza la Mitihani
xxviii.   Usafiri wa Anga
xxix.    Utafiti
xxx.     Mahkama ya Rufaa
xxxi.    Usajili na Shughuli za Vyama vya Siasa
  1. Matatizo ya mgawanyo wa Mambo ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano ni pamoja na:
i.      Kukosekana tafsiri ya mipaka (scope) ya mambo ya Muungano.  Mfano ni suala la simu- siku za nyuma, Shirika la Posta na Simu ndio lilokuwa jambo la Muungano kwani Zanzibar haikuruhusiwa kuwa na Shirika lake la Posta wala la Simu kwa vile hilo ni jambo la Muungano.  Hata hivyo, baada ya kubinafsishwa Zanzibar kwanza haikupewa hisa hata moja katika Kampuni ya TTCL wala gawio katika biashara zilizotokana na TTCL.  Aidha, Zanzibar hadi leo, ukiachia kutoa Mjumbe wa Bodi katika Shirika la Posta, haitambuliwi kama mshirika au mbia katika Shirika hilo.  Jambo hili linazua hoja ya wazi kuwa nini jambo la Muungano katika suala la Simu na Posta halifahamiki.  Hivi sasa suala la Muungano linaonekana limebaki kuwa ni udhibiti wa Simu na Posta kupitia Tanzania Communication Regulatory Authority (TCRA).  Hata hivyo, ukiwachia Zanzibar kutoa Mjumbe wa Bodi haina faida nyengine inayopata kwani mapato yote ya TCRA yanakwenda Serikali ya Muungano. Mabenki pia, ilikuwa na biashara NBC sasa ni udhibiti tu.  Elimu ya Juu tafsiri yake nayo haijulikani imeanzia wapi na kuishia wapi;

ii.      Tafsiri ya Mahkama ya Rufaani ya Tanzani katika Kesi ya Machano Khamis na wenzake 17 (“KESI YA UHAINI”) imebainisha wazi kuwa Orodha ya Mambo ya Muungano ni ndefu zaidi kuliko ilivyo katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba.  Aidha, inaonesha kuwa mambo ya Muungano hayajulikani hasa ni mangapi.

iii.      Kwa kupitia Mambo ya Nje, hakuna lisilokuwa la Muungano.  Tatizo zaidi ni kuwa kwa mlango huu wa Mambo ya Nje, mambo yote ni ya Muungano au Tanganyika pekee (Mfano ni suala la Mpira- TFF na ushiriki wa FIFA).  Sababu kubwa ya matatizo haya ni kuwa Taasisi zisizokuwa za Muungano za Tanganyika ndizo zilizojichukulia mamlaka ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano nje ya Tanzania kwa mambo ambayo si ya Muungano.  Hili ni kasoro ya msingi kwa vile uwakilishi huo ni batili kisheria.  Kwanza, Taasisi hizo hazina uwezo wa kuiwakilisha Zanzibar kwa vile si mambo ya Muungano.  Kwa mantiki hiyo, vyombo na taasisi hizo wanapokwenda nje ya Tanzania wanaiwakilisha Tanganyika pekee jambo ambalo si halali.  Kwa mfano sasa hivi TFF ni mwanachama wa FIFA kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Ni wazi kwamba uwanachama huo ni batili kwa vile hawana mamlaka ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  1. Utaratibu wa Kutunga Sera kwa Mambo ya Muungano.
    1. Kwa mujibu wa ibara ya 53(2) ya Katiba, mamlaka ya Kutunga Sera za Serikali ya Jamhuri ya Muungano yamo mikononi mwa Baraza la Mawaziri la Muungano.  Katiba haikutenganisha baina ya sera kwa mambo ya Muungano na sera kwa mambo yasiyo ya Muungano.  Aidha, Katiba haikuweka utaratibu wa aina yoyote ya kuishirikisha Zanzibar katika maamuzi yanayohusu sera za mambo ya Muungano.  Mbali ya Katiba hakuna sheria wala utaratibu rasmi uliowekwa kwa ajili hiyo.  Hoja ya baadhi ya watu ni kuwa Zanzibar inashirikishwa kwa vile kuna mawaziri kutoka Zanzibar na pia Rais wa Zanzibar katika Baraza la Mawaziri la Muungano.  Hoja hii haina msingi kwa vile:
i.       mawaziri wanaotoka Zanzibar hawajaenda kuiwakilisha Zanzibar katika Baraza la Mawaziri na hata Rais wa Zanzibar yumo kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri.  Kwa sababu hiyo wanabanwa na Kanuni za maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambamo muamuzi hasa ni Rais na Wajumbe wote wa Baraza ni washauri wake.  Aidha, wanabanwa na Kanuni ya uwajibikaji wa pamoja ambapo Waziri haruhusiwi kulipinga jambo liloamuliwa na Baraza la Mawaziri.

ii.      Mawaziri wanaotoka Zanzibar waliomo katika Baraza la Mawaziri la Muungano hawana uhusiano wowote na Serikali ya Zanzibar.  Hawana njia na wala hawapaswi kutafuta maoni ya Zanzibar katika utekelezaji wa kazi zao.
  1. Baadhi ya mifano ya kutoshirikishwa Zanzibar katika kuandaa sera za Mambo ya Muungano na athari zake ni kama yafuatayo:
i.      Katika maandalizi ya mfumo mpya wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Zanzibar haikushirikishwa tokea awali.  Ililetewa tu rasimu ya Sheria katika hatua za mwisho za maandalizi.  Hata baada ya kutoa maoni katika hatua hii, maoni hayo hayakusikuzingatiwa.  Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwepo Mkuu wa TRA Zanzibar mwenye hadhi ya Kamishna kama ilivyo kwa Jeshi la Polisi na Uhamiaji.  Matokeo yake baada ya Sheria kupitishwa TRA iliteua Naibu Kamishna kutoka Tanganyika kuja kufanya kazi Zanzibar.  Serikali ya Zanzibar ilimkataa ofisa huyo na kueleza wazi kuwa haiko tayari kushirikiana naye na hatimaye aliondolewa na kuteuliwa mtu mwengine kutoka Zanzibar.

ii.      Wakati wa maandalizi ya mfumo mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Zanzibar, katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi ilitoa mapendekezo kadhaa ambayo yote hayakuzingatiwa na mfumo na Sheria ikapitishwa bila ya kuwepo mapendekezo ya Zanizibar;

iii.      Katika maandalizi ya Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority) maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa, na hata pale Naibu Waziri wa Maliasili kutoka Zanzibar, Mheshimiwa Mwalimu Haji Ameir, ambaye alikuwa pia Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi kulieleza Bunge kuwa maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa katika Sheria hiyo, bado Bunge lilipitisha Sheria hiyo ambayo ilikaa miaka zaidi ya kumi bila kutekelezwa kwa vile Zanzibar ilikataa kutoa ushirikiano hadi pale mawazo yake yatapozingatiwa.  Utekelezaji wa Sheria hii ulikuwa Kero ya Muungano ya muda mrefu.

iv.      Katika maandalizi ya Sera ya Mambo ya Nje, Zanzibar ililetewa rasimu ya Sera hiyo itoe maoni.  Baraza la Mapinduzi liliunda Kamati kuipitia na kuandaa maoni ambayo yalikubaliwa na Baraza la Mapinduzi.  Hata hivyo, takriban maoni yote ya BLM yalikataliwa na hayakuzingatiwa katika Sera hiyo.

v.      Katika maandalizi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Zanzibar pia ilitakiwa kutoa maoni tu na ikafanya hivyo kupitia Kamati ya BLM.  Hata hivyo, maoni hayo hayakuzingatiwa.  Hata pale Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulipokaribia kutiwa saini, Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, aliandika Waraka mrefu wa maoni ya Zanzibar kuhusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini maoni hayo hadi leo hayakuzingatiwa.

Hiyo ni baadhi ya mifano michache ya namna Zanzibar ilivyokuwa haikushirikishwa katika maandalizi ya Sera za Msingi za masuala ya Muungano hata pale ilipotoa maoni ya maandishi.  Sababu kubwa ni kuwa mfumo wa sasa wa Muungano inaupa mamlaka yote ya maamuzi Serikali ya Muungano na mamlaka hayo yamekuwa yakitumiwa kwa maslahi ya upande mmoja tu wa Muungano; Tanganyika.
  1. Athari ya mfumo uliopo katika utungaji wa Sera za Muungano ni kuwa Sera za Muungano zinazingatia mahitaji, mazingira na matakwa ya upande mmoja tu wa Muungano.  Aidha, baadhi ya sera hizo zina athari kubwa kwa uchumi na maendeleo ya Zanzibar.
  1. Mfumo wa Kutunga Sheria za Muungano
Mfumo wa kutunga Sheria za Muungano una matatizo kadhaa kama yafuatayo:
  • Maandalizi ya Sheria ni ya upande mmoja. Zanzibar baadhi ya wakati huletewa kutoa maoni juu ya Mswada ulokwisha andaliwa.
  • Kwa mujibu wa ibara ya 98, mambo yote yaliomo katika Orodha ya Mambo ya Muungano, Sheria zake zinapitishwa kwa wingi wa kura katika Bunge.  Kutokana na Idadi ya Wabunge wa Zanzibar, ina maana Sheria hizo zina ridhaa ya upande mmoja tu wa Muungano.
  • Sheria nyingi za Muungano zinazingatia Sheria nyengine, mazingira na taratibu za Tanganyika pekee.  Mfano usajili wa wataalamu kama vile wanasheria, wahandisi huzingatia taratibu za Tanganyika na bila kuzitambua taratibu ziliopo Zanzibar.
  1. Fedha za Muungano na Bajeti
  • Kwa mujibu wa Ibara ya 133 na 134 za Katiba ya Muungano, utaratibu wa fedha za Muungano upo chini ya Tume ya Pamoja ya Fedha.  Tume ndiyo inayotakiwa iandae mapendekezo ya kuchangia fedha za kuendesha shughuli za Muungano na kugawana ziada ya mapato ya Muungano.  Tume imetajwa katika Katiba tokea mwaka 1984, Sheria ya Kuanzishwa ikapitishwa mwaka 1996 lakini Tume ikaundwa mwaka 2003.  Tume imetoa mapendekezo mwaka 2006 hadi leo SMT haijayafanyia kazi mapendekezo hayo.  Kwa muhtasari tu, kila jambo la Muungano lina mapato na gharama.  Ukichukua mapato ya Muungano kutokana na vyanzo vya Muungano na matumizi ya mambo ya Muungano kama kuna ziada bila shaka kwa utaratibu wa sasa Zanzibar haipati ziada hiyo.  Ni dhahiri hilo ndio liloifanya Serikali ya Muungano isiwe na haraka katika kuunda Tume na katika kutekeleza mapendekezo ya Tume.
  • Ibara hizo za Katiba zinaweka sharti la kuwepo Akaunti ya Pamoja ya Fedha ambayo ndio itawekwa mapato ya Muungano na kutoa matumizi ya Muungano.  Sharti hilo halijatekelezwa.
  • Mfumo wa Bajeti ya Serikali ya Muungano kwa sasa hautenganishi Mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano. Hivyo mapato ya Muungano yanatumika pia kuendesha mambo yasiyo ya Muungano.  Inawezekana pia mapato yasiyo ya Muungano yanatumika kuendesha mambo ya Muungano.  Lakini kwa kuzingatia utafiti wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC), mapato ya Muungano ni makubwa kuliko matumizi ya Muungano, ni wazi kuwa mapato ya Muungano ndiyo yanayotumika kuendesha mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika.
  • Sera za kodi na fedha kwa sasa zinazingatia zaidi mahitaji ya bajeti ya Serikali ya Muungano na sio pande mbili za Muungano.  Kwa kutokuwepo bajeti pekee ya Muungano kunachangia jambo hilo.
  1. Usimamizi wa Mambo ya Muungano
  • Ngazi ya Baraza la Mawaziri:  Mambo ya Muungano kwa utaratibu wa sasa yanasimamiwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano ambalo pia kwa mujibu wa ibara ya 34 ya Katiba, ndilo linasimamia mambo yasiyo ya Muungano kwa Tanganyika.  Usimamizi ni pamoja na kutoa maamuzi ya kisera, kibajeti na kiuendeshaji.  Ingawa wapo mawaziri kutoka Zanzibar katika Baraza la Mawaziri na wengi wanachukulia kuwa ndio wawakilishi wa Zanzibar lakini kwa utaratibu wa Baraza la Mawaziri hawapaswi kuwa wawakilishi wa Zanzibar.
  • Ngazi ya Mawizara:  Kwa utaratibu wa sasa, mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano yamechanganywa katika baadhi ya Mawizara.  Mfumo huu unafanya upande mmoja wa Tanganyika uone kwamba mambo yote ya Muungano ni sehemu tu ya mambo ya Tanganyika.  Hivyo, hakuna tofauti katika maamuzi na wa usimamizi.  Mfumo huu umeondoa kabisa dhana ya kuwa mambo ya Muungano ni ya pamoja yanayohitaji usimamizi wa pamoja na wa kushauriana.
  • Ngazi ya Taasisi za Muungano:  Taasisi takriban zote za Muungano hazina sura ya Muungano katika usimamizi na uongozi.  Mfano mzuri ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ukiwachia Wajumbe wawili wa Bodi hakuna uwakilishi mwengine wa Zanzibar.  Kwa madhumuni yote chombo hichi hakina tofauti na taasisi yoyote nyengine isiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika.  Mifano hiyo ipo kwa Benki Kuu, Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) n.k.
  • Utatuzi wa Migogoro na Kero

i.      Mifano ya Migogoro na Kero:
  1. Fursa za Kodi:  Miongoni mwa mgogoro mkubwa uliopo baina ya Zanzibar na Serikali ya Muungano ni ile ya Zanzibar kutumia fursa za sera za kodi kwa uchumi wake.  Zanzibar iliwahi kuandaa sheria ya Offshore companies na ilitumia fedha nyingi kuajiri wataalam wa fani hiyo.  Ingawa Serikali ya Muungano ilikubaliana na sera hizo, lakini hatimaye ilikataa wakati Mswada wa Sheria hiyo upo katika hatua ya Kamati ya Baraza la Wawakilishi na bila ya kutoa sababu yoyote ya msingi.  Aidha, Zanzibar ilianzisha maeneo huru ya Uchumi (EPZ) na baadhi ya viwanda kama vile cha madirisha maalum ya aluminium na mafuta ya kupikia vilianzishwa.  Hata hivyo, viwanda hivyo vilishindwa kuendelea na kazi kutokana na TRA kukwamisha bidhaa zao kila wanaposafirisha kupitia bandari ya Dar es salaam.  Hatimaye viwanda vyote hivyo vilifungwa. Mgogoro mwengine mkubwa ni wa Kodi ya Mapato (PAYE) ambao ingawa mazungumzo yalianza tokea mwaka 1996, makubaliano yalifikiwa mwaka 2011.  Pamoja na makubaliano hayo, Serikali ya Muungano ilichelewesha utekelezaji kwa makusudi kwa mwaka mmoja zaidi na kuikosesha Zanzibar zaidi ya shilingi bilioni 18 ambazo imekataa kuzilipa.
  1. Suala la Benki Kuu:  Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa badala ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ambayo Zanzibar ilikuwa na hisa za asilimia 11.  Pamoja na fedha nyengine,  Benki Kuu ilianzishwa kutokana na malipo ya fedha za Zanzibar kutoka Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.  Na hata kama haikuwa hivyo, kwa vile Benki Kuu imechukua nafasi ya Bodi ya Sarafu, Zanzibar ilipaswa kuwa na maslahi yale yale ambayo iliyapoteza katika Bodi ya Sarafu.  Mzozo huo ambao uliibuka mwaka 1994, haujaweza kupatiwa ufumbuzi mpaka leo.
  1. Suala la Tume ya Pamoja ya Fedha:  Tume ya Pamoja ya Fedha ilianzishwa na Katiba ya Muungano mwaka 1984.  Hata hivyo, sheria ya kuunda Tume hiyo ilipitishwa mwaka 1996.  Tume yenyewe ikaundwa rasmi mwaka 2003; miaka 19 tokea Katiba iweke sharti la kuundwa Tume hiyo.  Tume ilitoa mapendekezo ya awali ya utaratibu wa kuchangia na kugawana mapato ya Muungano tokea mwaka 2006 hadi leo Serikali yaMuungano imeshindwa kutoa maoni yake juu ya mapendekezo ya Tume.  Aidha, kutokana na kuchelewa huko Akaunti ya Pamoja ya Fedha ambayo ndiyo inayotakiwa kuwekwa mapato na kutoa matumizi ya Muungano haijaanzishwa.  Hivyo bajeti ya Muungano kwa muda wote huu inaendeshwa kinyume na maelekezo ya Katiba.
  1. Masuala ya uwekezaji:  Uwekezaji katika baadhi ya sekta ndani ya Zanzibar yanategemea idhini ya Serikali ya Muungano.  Mfano wa sekta hizo ni simu na usafiri wa anga.  Zantel ilipowekeza Zanzibar iliwekewa vikwazo vingi na Tume ya Mawasiliano (TCC) na hata Waziri aliyekuwa akisimamia sekta hiyo kwa wakati huo Mheshimiwa William Kusila hadi kupelekea kuondolewa kwake na kuja Mheshimiwa Enerst Nyanda.  Mzozo huu ulipelekea Zanzibar kudai ITU iirejeshee namba yake ya kimataifa ya 259 ili ijitoe katika kutumia namba ya kimataifa ya Tanzania ya 255 ili iwekeze mradi wa simu wa Zantel.  Baada ya hatua hiyo na kuondolewa Waziri Kusila ndio mzozo huo ukatatuka.  Katika suala la ndege, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Tanzania iliwahi kuzuia Zanzibar kuanzisha Zanzibar Airline kwa madai kuwa ATC ndio Shirika la Ndege pekee la Tanzania.  Hata hivyo, mamlaka hiyo ilikuja kuruhusu Precision Air na hatimaye makampuni mengine binafsi.
  1. Masuala ya Afrika Mashariki:  Suala hili limeelezwa kwa urefu sehemu nyengine katika Waraka huu.
  1. Masuala ya Uanachama wa FIFA:  Suala hili nalo limezungumzwa kwa urefu katika uchambuzi wa mambo ya Muungano.
  1. Suala la hisa katika mashirika ya Muungano yaliyobinafsishwa:  Yapo mashirika kadhaa ambayo yalikuwa yakijulikana kama ya Muungano na ambayo yamebinafsishwa au kuundwa upya.  Katika hatua hiyo, Zanzibar ilipaswa kupewa hisa zake katika mashirika hayo lakini haijafanyika hivyo hata baada ya Serikali mbili kukubaliana kulifanyia kazi na hata baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mhe. John Malecela kutoa maelekezo ya kuliharakisha.  Miongoni mwa mashirika hayo ni ATCL, TTCL na NBC.
  1. Suala la Mafuta na Gesi asilia:  Mgogoro juu suala hili ulianza baada ya Antrim ya Canada kutaka kufanya utafiti wa mafuta Zanzibar baada ya kupewa kibali na TPDC mwaka 1996.  Wakati huo wafadhili wakiongozwa na Canada walikuwa wameigomea Zanzibar na bila ya Serikali ya Muungano kuchukua hatua yoyote ya kidiplomasia.  Zanzibar iliamua kuikatalia Antrim kufanya kazi hiyo Zanzibar na hatimaye kuamua kutaka suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.  Ingawa Zanzibar imeweka bayana uamuzi huo kwa kupitishwa na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi na pia kwa kupitisha Sera ya Nishati, lakini Serikali ya Muungano imeshindwa kuchukua hatua kutekeleza matakwa hayo ya Zanzibar.  Kwa upande mwengine Serikali ya Muungano imekuwa ikiendeleza kwa kasi juhudi za uendelezaji shughuli za utafutaji wa mafuta na uchimbaji wa gesi.  Kwa upande wa gesi hadi leo hakuna utaratibu wa kugawana mapato ya rasilimali hiyo ambayo ni ya Muungano.  Mgogoro huu umechangia kwa sehemu kubwa kuleta hisia dhidi ya Muungano kwa wananchi wa Zanzibar hasa kwa vile viongozi wa kambi zote mbili za kisiasa wanakubaliana katika suala hili.

ii.      Udhaifu wa Mfumo wa sasa katika utatuzi wa migogoro ya Muungano:  Kama tulivyoona kwamba ipo migogoro mikubwa na msingi ambayo mingine inatishia hata uhai na uimara wa Muungano lakini utatuzi wake ama haupo au ni dhaifu.  Hii inatokana na upande mmoja wa Muungano kuwa na mamlaka yote na mwisho katika kuamua masuala ya Muungano.  Hivyo, hata pale unapofanya makosa hakuna mfumo mbadala wa kupata ufumbuzi.  Kwa ufupi mfumo wa sasa wa utatuzi wa migogoro ya Muungano ni sawa na refarii kuwa pia mchezaji.  Si mfumo na wala haufai kabisa kwa vile haufanyi kazi.  Ni kiini cha matatizo ya Muungano na umekuwa ukitumika vibaya na upande mmoja na kwa kiasi kikubwa sana umedhoofisha Muungano.
  1. Matumizi ya Rasilimali za Muungano
    1. Miundombinu ya Taasisi za Muungano: Kwa kawaida, uwekezaji wa rasilimali za Taifa una faida kubwa katika kukuza uchumi wa nchi.  Ni kwa sababu hizo ndio maana Jumuiya zote za kiuchumi zina mfumo wa kugawana kwa haki baina ya wanachama faida za uwekezaji huo.  Uwekezaji huo mara nyingi uko katika mfumo wa ujenzi wa miundombinu ya taasisi za Muungano hasa Makao Makuu ya taasisi hizo.  Uwekezaji unapowekwa unatoa fursa nyingi katika eneo husika.  Kwa upande wa Muungano wa Tanzania, uwekezaji umewekwa katika upande mmoja tu wa Muungano na hivyo kutoa fursa kwa upande huo wa Tanganyika.  Mfano wa uwekezaji huo ni pamoja na Benki Kuu, Posta, TCRA, TCCA, TCU, COSTECH nk.
  1. Ajira:  Muungano wenye haki na usawa unazingatia sana mgawanyo wa ajira katika taasisi za Muungano kwa pande zote za Muungano katika ngazi zote za Utendaji na za kawaida.  Mfumo wa sasa wa Muungano hilo halizingatiwi hata kidogo.  Baya zaidi ni kuwa hata kwa taasisi za Muungano ziliopo Zanzibar kama vile Benki Kuu waajiriwa wengi wanatoka Tanganyika.
  1. Udhaifu wa Jumla wa Mfumo Uliopo

i.      Udhaifu wa Katiba: Katiba yenyewe ina udhaifu kama ilivyoainishwa hapo awali ambayo kwa ufupi ni kama yafuatayo:

ii.      kukosa misingi ya wazi ya Muungano,

iii.      maamuzi yote ya msingi ya Muungano kufanywa na upande mmoja,

iv.      kukosa usawa, haki na fursa zilizo sawa kwa pande mbili;

v.      kuchanganywa mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano;

vi.      Kukosa mfumo wa mashirikiano na mashauriano baina ya pande mbili;

vii.      Kukosa mfumo wa utatuzi wa migogoro na kero za Muungano;

viii.      Rasilimali za Muungano kutotumika kwa haki baina ya pande mbili za Muungano.

Udhaifu wa Mfumo wa Serikali Mbili:  Mfumo wa Serikali Mbili umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa una udhaifu mkubwa katika kuendesha Muungano wa Tanzania na pia katika kusimamia Muungano unaoweza kuhimili mageuzi ya kisiasa.  Miongoni mwa kasoro za Msingi za Mfumo wa Serikali mbili uliopo ni kama zifuatavyo:

i.      Umegeuza mmoja wa Washirika wa Muungano (Zanzibar) kuwa ni sehemu ya nchi (political subdivision or a Province of a sovereign country) na kumvika Mshirika mwengine (Tanganyika) kuwa ni Taifa kamili lenye mamlaka yote kwa kubadili jina tu na kuwa Tanzania;

ii.      Umenyan’ganya mamlaka yote kutoka kwa Washirika wa Muungano na kuukabidhi upande mmoja wa Muungano na kutoa fursa ya upande mmoja kutumia mamlaka hayo kadri upendavyo na kwa maslahi yake tu;

iii.      Umeondoa misingi ya Muungano kwa kukosa kiungo baina ya pande mbili za Muungano.  Mfumo uliopo wa Serikali mbili umeshindwa kufanya kazi wakati Chama kimoja kinatawala Serikali zote mbili.  Hatudhani kama unaweza kufanya kazi kama yatatokea mabadiliko ya chama;

  iv.      Mfumo uliopo wa Serikali mbili unajenga mazingira ya kuwa na Serikali na Rais wa Muungano ambaye hana uhalali upande mmoja wa Muungano (Zanzibar).  Hii ni kwa sababu Chama kinachoongoza Serikali ya Muungano na Rais wa Muungano anaweza wasipate kiti wala kura Zanzibar na bado ikawa Serikali ya Muungano na Rais wa Muungano.  Huu ni ushahidi wa wazi kuwa mfumo wa Serikali mbili haujengi usawa wa ridhaa ya pande mbili bali unajenga mazingira ya upande mmoja kuwa mkubwa na sehemu ya pili kuwa sehemu tu ya utawala (dominion).  Mfumo huu unaondoa msingi mmoja wa haki ya watu wa Zanzibar kujitawala na kuendesha mambo yao kwani hawana mamlaka ya kuchagua kiongozi wanayemtaka wala sera wanazotaka za kuongoza masuala ya Muungano.  Mfumo huu unayafanya mambo ya Muungano kuwa ni ya upande mmoja na upande huo ndio wenye haki na ridhaa ya kuchagua kiongozi na sera wanazotaka kuhusiana na masuala ya Muungano sawa na yale mambo ambayo si ya Muungano.

v.      Mfumo wa Serikali mbili uliopo unaufanya Muungano utegemee zaidi mazingira ya kisiasa.  Mabadiliko yoyote ya kisiasa yatayobadili vyama vinavyotawala Serikali mbili yanaweza  kuutia Muungano katika mashaka makubwa ya kuendelea kuwepo kwani itategemea zaidi masikilizano ya vyama badala ya misingi ya Katiba.

Mambo Muhimu ya Kuzingatiwa
  1. Kulinda Msingi Mama wa Muungano kwamba ni Muungano wa Nchi Mbili Huru zenye mazingira tofauti sana ya kijiografia, kidemografia na kiuchumi.
  2. Kuweka msingi wa kuwa na Muungano wa kweli hata kama itakuwa ni kwa maeneo machache;
  3. Kuweka bayana misingi muhimu ya Muungano ambayo imeelezwa hapo awali;
  4. Kulinda maslahi ya kiuchumi ya washirika wa Muungano kwa kutoa uhuru katika maeneo ambayo ni nyenzo za kiuchumi kwa kila upande;
  5. Kulinda haki ya watu wa kila upande kujiamulia kubaki kuwemo katika Muungano au kutoka kwa masharti yatayohakikisha kuwa kweli huo ni uamuzi wa watu wote wa upande huo na sio wa wachache;
  6. Kuwepo mfumo bayana wa kugawana haki za mali na kugawana dhima na kulipana madai ya muda mrefu baina ya pande mbili.
MAPENDEKEZO YA KUREKEBISHA IBARA ZA SURA YA SITA

Kutokana na maelezo, hoja na sababu tulizozitaja hapo juu, Wajumbe walio wachache tunaona hakuna njia nyengine zaidi ya kubadili muundo wa Muungano kwa kuanzisha Shirikisho la Serikali Tatu kama walivyopendekeza wananchi walio wengi kupitia maoni yao waliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, pamoja na kukubaliana na pendekezo la msingi la kuwa na Shirikisho la Serikali Tatu kama yalivyo kwenye Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba, tunapendekeza marekebisho yafuatayo ili kuufanya muundo huo uweze kufanya kazi vizuri zaidi kwa maslahi na manufaa ya wananchi wa Tanganyika na Zanzibar.

Ibara ya 60:
Kama tulivyotangulia kueleza, jina la muungano huu liwe ni “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar” ili kuweka bayana kwamba muungano huu ni wa Jamhuri mbili ambazo ni Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Kwa msingi huo basi, katika Sura hii na katika sehemu zote za Katiba kila ilipotajwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iandikwe Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.

Ibara ya 62:
Ibara 62(3) inasema kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, inaweza kutekeleza jambo lolote lilio chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.

Maelezo: Ingawa serikali hizi zinaweza kukubaliana kushirikiana, lakini ushirikiano unapaswa uwe ni kwa pande mbili (two-way). Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyikazinaweza kukubaliana kushirikiana na kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, na vile vile zinaweza kutekeleza jambo lolote lililo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano. Mamlaka ya Serikali ya Shirikisho yatakuwa ni kuhusu mambo ya Muungano tu kama yalivyoorodheshwa kwenye Nyongeza ya Katiba. Maudhui yaliyomo kwenye Ibara Ndogo ya 62(3) yanaingilia mamlaka ya Serikali za nchi washirika kwa mambo yasiyo ya Muungano. Namna ilivyoelezwa katika Ibara hii, inaipa fursa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kujiingiza katika mambo yasio ya Muungano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, na si kinyume chake. Huu ni mlango wa nyuma kuingilia mamlaka ya Serikali nyengine, na inafaa uzibwe.

Pendekezo ni kwamba ama Ibara ya 62(3) ifutwe au iandikwe upya na isomeke:
“62(3).- Bila kuathiri au kukiuka masharti ya Ibara hii, Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, zinaweza kushirikiana na kutekeleza jambo lolote lililo chini ya mamlaka yao kwa mujibu wa masharti ya makubaliano ya kimkataba baina yao na pia kuanzisha taasisi zenye maslahi ya pamoja.”

Ibara ya 63:
Ibara ya 63 inahusu Mambo ya Muungano ambayo yametajwa katika Nyongeza (Schedule) ya Rasimu ya Katiba. Tunapendekeza Orodha hiyo iangaliwe upya pale utakapofika wakati wa kuijadili.

Ibara ya 65:
Ibara ya 65 imeandikwa kwa lengo la kuonesha kwamba nchi washirika sasa watakuwa na udhibiti wa ushirikiano wa kimataifa katika yale mambo yasiyo ya Muungano. Hata hivyo, Ibara hiyo haitaweza kutekelezeka kwa sababu ni Hati za Kisheria (Legal Instruments) zinazoanzisha jumuiya, taasisi na mashirika ya kimataifa ndizo zinazoweka sharti la nchi kuwa na mamlaka kamili (sovereign state) ili kuweza kukubalika kuwa mwanachama. Mfano mzuri ni jitihada za Zanzibar kupitia ZFA kutaka kujiunga na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Inaeleweka kwamba michezo si suala la Muungano na ni sehemu ya mambo ambayo Zanzibar inapaswa kuwa na mamlaka kamili (exclusive jurisdiction) kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano wa 1964 na hata kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Hata hivyo, FIFA kupitia barua yake kwa ZFA ya tarehe 21 Juni, 2010 yenye Kumb. Nam. SG/TRE/PCO imeeleza kwamba sababu ya kuikatalia Zanzibar kujiunga na Shirikisho hilo ni kukosa sifa ya kuwa na mamlaka kamili (sovereignty) na kwamba Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.

Hali kama hiyo inahusu mashirika kama WHO kwa sekta ya afya, UNESCO kwa sekta za elimu na utamaduni, FAO na IFAD kwa sekta ya kilimo, UNEP kwa sekta ya mazingira, na sasa hata OIC kwa maendeleo ya kiuchumi.

Kwa msingi huo, masharti ya Ibara hiyo ya 65 yanabaki ni pambo (cosmetic) tu lakini hayawezi kutekelezeka bila ya nchi washirika kuwa na mamlaka kuhusiana na mahusiano ya kimataifa.

Pendekezo ni Ibara ya 65 kuandikwa upya kwa kutamka wazi kwamba Nchi Washirika zitakuwa na mamlaka kamili katika masuala ya uhusiano na ushirikiano wa kimataifa kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano.

Ibara ya 67:
Makao Makuu ya Muungano: Ibara 67(2) inataja Makao Makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, lakini haielezi yatakuwa wapi – itakuwa ni ofisi tu chini ya mamlaka ya Nchi Mshirika mmojawapo, au katika miji tofauti kugawanya makao makuu ya Urais, Bunge na Mahakama, kama ilivyo Afrika Kusini; au Mji Mkuu wa Muungano, kama Brasilia (Brazil) au Islamabad (Pakistan).

Maelezo: Kwa muda wa miaka hamsini ya Muungano taasisi zote za Muungano zimejengwa Tanganyika na kuiwacha Zanzibar katika hali ya ukiwa. Katika vyuo na taasisi za elimu ya juu zisizopungua 20 za umma ziliopo Tanzania, hakuna hata moja iliyojengwa Zanzibar. Tunataka kuona kuwa Makao Makuu ya Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar sasa yawe na sura ya Shirikisho la kweli.

Kwa upande mwengine, neno “Waziri Mkaazi” halileti taswira nzuri na pia halieleweki vyema. Kimsingi Waziri Mkaazi anapaswa kuitwa kwa dhamana yake ambapo ni Waziri wa Nchi Washirika anayeshughulikia mambo ya Muungano.

Ibara ya 68:
Ibara ya 68(1): Serikali ya Shirikisho kimsingi inapata uhalali wake kutoka kwa Serikali za nchi washirika na siyo moja kwa moja kutoka kwa wananchi. Kwa upande mwengine uhalali na msingi wa mamlaka ya Serikali za nchi washirika unapaswa kuachwa kwa nchi washirika wenyewe kwa utaratibu utakaoelezwa kwenye Katiba za nchi zao.

Ibara ya 68 (2): Masuala ya kugatua madaraka (devolution) kwa serikali za mitaa hayaihusu Serikali ya Shirikisho na hivyo hayapaswi kuwemo kwenye Katiba ya Shirikisho kwa sababu masuala ya serikali za mitaa si mambo ya Muungano. Hayo ni mambo ya nchi washirika na yanapaswa kuwemo kwenye Katiba za nchi washirika kwa utaratibu ambao kila nchi itaona unafaa.

Ibara ya 69:
Ibara ya 69 inahusu Wajibu wa Kulinda Muungano na inasisitiza kwamba Viongozi Wakuu (Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar) wataapa “kuutetea na kuudumisha Muungano.”

Maelezo: Ibara hii haijengi msingi muhimu wa Muungano wa watu ambao ni kuwa na muungano wa hiyari na badala yake inaufanya Muungano uonekane kama vile ni jambo linaloshurutishwa. Isitoshe, kwa nini tunasisitiza na kung’ang’ania suala la Muungano tu? Viongozi Wakuu wanatakiwa walinde nchi zao, demokrasia, haki za wananchi wote, Katiba, na mambo mengi mengine. Hata kama Muungano usingekuwepo, bado wangetakiwa kuapa kulinda nchi na katiba zao. Rasimu hii tayari imeweka kipengele juu ya uwepo na uwezekano wa kutokuwepo kwa Muungano kwa kura ya maoni (“opt-out clause”- Ibara 119(e), na hivyo kuonesha kuna uhalali wa kufikiri juu ya tukio hilo. Ikitokea mgogoro wa kikatiba, na ikafika wakati hawa viongozi wakilazimika kusema Muungano hauwezi kuendelea, basi kwa nini wafungwe midomo kwa woga wa uhaini? Suala la “Kuwapo wa Jamhuri ya Muungano” linaweza kuondolewa pia hata kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotumika sasa ya mwaka 1977, Ibara ya 98(1)(b) na linatajwa kwenye Orodha ya Pili ya Nyongeza ya Pili.

Pendekezo: Inatosha kusema kwamba Viongozi Wakuu waliotajwa katika Ibara ya 69 wataapa kulinda Nchi na Katiba ambayo inajumuisha mambo yote yanayohusika.

= mwisho =

Posted By Unknown07:21