Wednesday 23 July 2014

TAARIFA RASMI ILIYOTOLEWA NA POLISI KUHUSU KUTUPWA VIUNGO VYA BINADAMU MAENEO YA BONDE LA BWENI

Filled under:

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE

22/07/2014

WATU WANANE WAKIWEMO MADAKTARI WASHIKILIWA NA KUHOJIWA NA JESHI LA POLISI KUTOKANA NA KUTUPWA VIUNGO VYA BINADAMU MAENEO YA BONDE LA MBWENI MPIJI ENEO LA BUNJU 


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu wanane na kuwahoji kuhusu tukio la kupatina kwa viungo vya binadamu vilivyogundulika katika maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji ambapo mifuko ya plastiki ipatayo 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu yaligundulika. Polisi walipata taarifa 21/07/2014 jioni kutoka kwa wasamaria wema na ndipo jopo la wapelelezi likiongozwa na Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ACP. Camilius Wambura walifika hapo majira ya saa 1.00 usiku.

Walipofika katika tukio waligundua mifuko ipatayo 85 mieusi yenye viungo vya aina mbali mbali vya binadamu kama vile Vichwa, Miguu, Mikono, Mioyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbali mbali ya binadamu. Viungo hivyo havikuwa na uvundo au harufu ya aina yoyote na vilionekana kwamba vimekaushwa na kukakamaa. Katika eneo hilo pia vilikutwa vifaa vinavyotumika hospitali kama vile mipira ya kuvaa mikononi (gloves) mifuko miwili iliyotumika ,nguo maalum (apron) zipatazo 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.

Wananchi wasiopungua 1,000 walifika katika eneo hilo la tukio lakini hakuna aliyekuwa na taarifa sahihi. Viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Aidha jopo la Wapelelezi chini ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ACP. Japhari Mohamed walianza uchunguzi mara moja kwa kusaidiana na Daktari wa Jeshi la Polisi anayehusika na uchunguzi wa miili ya binadamu (Forensic Doctor) ambaye kwa pamoja walishirikiana na madaktari wengine kutoka hospitali wa Taifa Muhimbili.

Hatimaye uchunguzi wa kina ulibaini kwamba viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika Maabara ya Chuo Kikuu Madaktari IMTU jijini D’Salaam. Baada ya kugundulika hivyo Polisi wamewakamata na sasa wanaendelea kuwahoji watu wanane ambao wanasadikiwa kuhusika na miili hiyo ikiwa ni pamoja na baadhi ya madaktari wa IMTU. IMTU (International Medical and Technolegical University) ni chuo Kikuu cha Madaktari ambacho pia hufanya mafunzo ya udakitari kwa vitendo (practical). Jeshi la Polisi Kanda Maalum litamuhusisha Mkemia Mkuu wa Serikali na hatimaye mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi jalada litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zake ili sheria ichukue mkondo wake.

S. H. KOVA

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

0 comments:

Post a Comment