Monday 24 March 2014

MKUMBO:UHALALI WA KITAFITI WA MAONI YA WANANCHI TUME YA WARIOBA

Filled under:



BUNGE la Katiba linatarajiwa kuanza kazi yake wiki hii baada ya kukamilisha na kupitisha kanuni zake na hatimaye kuchagua Mwenyekiti atakayeliongoza. Kazi kubwa ya Bunge hili ni kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba ambayo hatimaye itapigiwa kura na wananchi.

Wabunge wana vigezo viwili vya kuwasaidia kufanya uamuzi wao katika ibara mbalimbali za rasimu inayopendekezwa na Tume ya Warioba. Kigezo cha kwanza ni kutumia kile tunachoweza kukiita uamuzi kwa mujibu wa utashi wa kisiasa (political based decision making). Kigezo cha pili ni kile tunachoweza kukiita uamuzi kwa mujibu wa ushahidi wa kisayansi (evidence based decision making). Vigezo vyote vinapatikana kikamilifu katika ripoti na nyaraka mbalimbali za Tume ya
Warioba. Ni matumaini yangu kwamba kila mjumbe katika Bunge hili atazisoma nyaraka zote zilizomo katika Tume ya Warioba kwa ukamilifu wake kabla hajaanza kuchangia. Kwa kweli ningekuwa Mwenyekiti wa Bunge hili ningehimiza kila mjumbe asitoe mchango wake kabla hajasoma nyaraka hizi, ambazo kwa ujumla wake zipo zaidi ya saba.

Katika makala haya ninatoa mchango wangu kwa kuanisha uhalali wa kisayansi kuhusu maoni ya wananchi yaliyopo katika ripoti ya Tume ya Warioba. Kuna nyaraka mbili katika Ripoti ya Tume ya Warioba kuhusu maoni ya wananchi. Nyaraka ya kwanza ni ile inayoanisha maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyaraka ya pili ni ile inayoanisha maoni ya Mabaraza ya Katiba kuhusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika maoni yote haya umetolewa uchambuzi wa kitakwimu (quantitative analysis) na uchambuzi wa kihoja (qualitative analysis). Ninajadili uhalali wa kitafiti juu ya aina mbili hizi za maoni, nikianza na uhalali wa kitafiti kuhusu matokeo ya kitakwimu.

Msingi wa utafiti wa kitakwimu (quantitative research) ni idadi ya walioshiriki katika utafiti husika na jinsi washiriki hawa walivyopatikana. Kikubwa kabisa kinachoangaliwa katika utafiti wa kitakwimu ni jinsi wa washiriki walivyopatikana. Ili matokeo ya utafiti wa kitakwimu yaweze kuheshimika na kukubalika, na yaonekana kwamba yanawakilisha maoni ya watu katika eneo husika ambao hawakushiriki katika utafiti huo, ni sharti kwamba washiriki wapatikane kwa njia ya kinasibu (random sampling). Sasa kwa vigezo hivi tuangalie uhalali wa takwimu zilizopo katika ripoti ya Tume ya Warioba katika suala la muundo wa Muungano, ambalo ndilo suala tata kuliko yote katika Rasimu ya Katiba.

Kwa mujibu wa takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (nyaraka ya nne katika ripoti ya Tume), idadi ya wananchi waliotoa maoni kuhusu jambo hili ni 47,820, wakiwemo 26,625 kutoka Tanzania Bara na 19,351 kutoka Zanzibar. Waliotaka serikali tatu walikuwa ni asilimia 37.2 (takribani watu 17,789), waliotaka serikali mbili walikuwa ni asilimia 29.8 (takribani watu 14,250) na waliotaka Muungano wa mkataba walikuwa ni asilimia 25.3 (takribani watu 12,098). Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 60.2 ya watu wote waliotoa maoni (takribani watu 11,649) walitaka Muungano wa mkataba na kwa upande wa Tanzania Bara asilimia 61.3 (takribani watu 16,321) walitaka serikali tatu. Kwa takwimu hizi wananchi walio wengi wa pande zote mbili za Muungano walioshiriki kutoa maoni kuhusu muundo wa Muungano walikuwa hawataki serikali mbili.

Sasa ni nini uhalali wa takwimu hizi kitafiti? Kama nilivyoeleza hapo juu, katika kupata uhalali wa matokeo ya utafiti takwimu (quantitative research) tunaangalia idadi ya walioshiriki na jinsi ambavyo washiriki hawa walipatikana. Pamoja na kwamba idadi ya walioshiriki kutoa maoni kuhusu Muungano inaonekana kuwa ni ndogo, kitafiti idadi hii ni kubwa sana. Sampuli nyingi duniani katika utafiti wa maoni (opinion poll) huwa na idadi isiyozidi watu 5,000. Kwa hiyo kwa Tume kuwafikia watu zaidi ya 40,000 ni idadi kubwa sana.

Tatizo kubwa kuhusu maoni ya wananchi katika ripoti ya Tume ya Warioba ni ukweli kwamba washiriki hawakupatikana kwa njia ya kinasibu (random sampling). Hawa ni watu waliojitolea kwenda kutoa maoni kwa hiari yao na kwa sababu zao na hawakuchaguliwa kama inavyofanyika katika tafiti za kimaoni (opinion polls). Njia hii ya kupata washiriki katika lugha ya kitafiti inaitwa ‘convenience sampling’. Hii ndio njia ya kupata washiriki ambayo inadharaulika kuliko zote katika utafiti takwimu na matokeo yatokanayo na njia hii huwa hayakubaliki kisayansi, na hakuna jarida la kitafiti makini linaloweza kukubali kuchapisha matokeo yatokanayo na maoni ya washiriki waliopatikana kwa njia hii. Ndio kusema, kisayansi, maoni ya wananchi katika ripoti ya Tume ya Warioba ni kiashiria tu (indicative) na hayawezi kutiliwa manani katika kufikia uamuzi wa maana na mkubwa.

Tungekuwa makini katika mchakato huu, tungeitisha kura ya maoni ya wananchi wote kuhusu Muungano kabla ya kuandika Katiba. Aidha, kama Tume ya Warioba ilihitaji kutumia matokeo ya utafiti takwimu katika kujenga hoja yake wangefanya utafiti wa kisayansi katika utaratibu wa ‘opinion poll’. Takwimu zilizopo katika ripoti ya Tume kwa sasa hazina uhalali wa kisayansi katika ulimwengu wa utafiti wa kitakwimu.

Ndio kusema msingi mkubwa wa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu katika ripoti ya Tume ya Warioba unapaswa kutokana na uzito wa sababu ambazo wananchi walizitoa kuhusu kwa nini wanataka muundo wa serikali tatu na sio wa serikali mbili uliozoeleka. Hivi ndiyo uhalali wa utafiti hoja (qualitative research) unavyojengwa. Utafiti hoja hauangalii idadi ya watu bali uzito wa hoja husika. Kwa maoni ya Tume, ambayo nami nakubaliana nayo, ili tuendelee na muundo wa serikali mbili itahitajika kufanyika ukarabati mkubwa sana. Serikali ya CCM ilifanya makosa makubwa kuiruhusu Zanzibar kufanya mabadiliko makubwa sana katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambayo kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya Muungano, wanadhani kwamba, kwa marekebisho haya ya Katiba ya Zanzibar, ilikuwa ni tangazo la Zanzibar kujitoa katika Muungano. Hili lilikuwa ni kosa kubwa la kisiasa, kiutawala na kisheria. Sasa hatuwezi kula keki na hapo hapo tuendelee kuwa nayo. Wataalamu wa mambo ya Muungano wanaeleza kwamba huwezi tena kuendelea na muundo wa serikali mbili bila kuifanyia ukarabati mkubwa Katiba ya Zanzibar, jambo ambalo linaonekana haliwezekani kwa sasa.

Katika ripoti yake, Tume ya Warioba imeainisha vizuri sana mlolongo wa matatizo ya muundo wa Muungano tangu enzi za kile kilichoitwa “kuchafuka kwa hali ya hewa kisiasa Zanzibar” mwaka 1984. Tume imeeleza pia sababu zilizoainishwa na Tume zingine kuanzia na Tume ya Nyalali ya Mwaka 1991 na baadaye Tume ya Kisanga ya mwaka 1998 ambazo nazo zilipendekeza muundo wa serikali tatu. Tukumbuke kwamba Tume zote hizi ziliundwa na Serikali ya CCM na ziliongozwa na majaji walioteuliwa na Rais atokanaye na serikali hiyo. Kikubwa zaidi, Tume ya Warioba iliongozwa na kada wa CCM na ndani yake walijaa makada nguli wa chama hicho, akiwemo Mzee Salim Ahmed Salim na Mzee Joseph Butiku. Ukada wa wazee hawa hautiliki shaka, lakini pia ni watu ambao utaifa na uzalendo wao kwa nchi haujawahi kutetereka. Kwa hiyo, huu msimamo wa CCM wa kung’ang’ania serikali mbili sio msimamo wa CCM ya Nyerere. Kazi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba.

- Imeandikwa na Dk Kitila Mkumbo, imenukuliwa kutoka gazeti la Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment