Friday 28 February 2014

MAPACHA WALIOTENGANISHWA WAWASILI SALAMA KYELA

Filled under:

Kyela. Mamia ya wakazi wa Kijiji cha Kasumulu eneo la ‘Juakali’, wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya, jana walimiminika nyumbani kwa mama wa watoto pacha, Grace Joel ili kushuhudia jinsi walivyotenganishwa baada ya kufanyiwa upasuaji nchini India hivi karibuni.

Watoto hao pacha, waliozaliwa wakiwa wameungana eneo la kiunoni, waliwasili na mama yao nyumbani kwao wilayani Kyela na kulakiwa na wanakijiji wengi.

Pacha hao, Elikana na Eliud wakiwa na baba yao, Rick Mwakyusa na mama yao, waliwasili kijijini kwa gari dogo.

Watoto na wazazi wao walifika kwenye nyumba anayoishi mzazi wa baba yao ambayo imejengwa kwa matofali ya kuchoma na kuezekwa kwa bati, lakini haina madirisha.

Miongoni mwa watu wa kwanza kushuhudia ugeni huo, alikuwa bibi wa watoto hao, Subilaga Kasekele ambaye ni mama wa Rick, akifuatana na mama mzazi wa Grace, Lide Mwakasala.


Kelele zililipuka kutoka kwa baadhi ya wanakijiji hao baada ya kupata taarifa za ujio huo na wengi waliwapokea kwa furaha kiasi cha kuwavuta hata watu kutoka vijiji vya jirani.

Mzazi wa watoto hao, Grace , akionekana mwenye furaha, alibubujikwa na machozi ya furaha na kuwashukuru wazazi wa pande zote mbili kwa maombi yao.

Akizungumzia hali yake, alimshukuru Mungu kwa kumfikisha salama Mbeya, lakini akasema ana wasiwasi na lishe ya watoto wake kwa kuwa hana uhakika wa kipato kwa kuwa hana kazi na mume wake ni dereva wa bodaboda.

“Nina wasiwasi na lishe kwa wanangu. Maisha yangu yenyewe ni ya ‘kubangaiza’, nimepanga nyumba kwa Sh.25,000 kwa mwezi, sasa baada ya hapo sijui...Nawashukuru Watanzania kwa misaada yao, lakini naomba wasiishie hapo,” alisema.

Alisema kuwa alichelewa kwenda Mbeya baada ya kuwasili Dar es Salaam kwani alikuwa akisubiri hati yake ya kusafiria pamoja na ripoti ya madaktari atakayoiwasilisha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Watoto hao walirejea nchini Februari 20 mwaka huu, ikiwa ni siku moja kabla ya kutimiza mwaka.

Baba alonga 
Baba wa watoto hao, Mwakyusa alisema hana nyumba kijijini hapo bali amepanga na walihamia eneo hilo hivi karibuni wakitokea kijiji cha mbali zaidi.

0 comments:

Post a Comment