Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu ameingia ofisini kwa mara ya kwanza jana baada ya kuapishwa
juzi na Rais Jakaya Kikwete huku akitangaza kuanza na watumishi wote
walioidhalilisha Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujihusisha kwa njia
moja ama nyingine na majangili.
Nyalandu aliyepandishwa kuwa waziri kamili baada
ya kujiuzulu kwa aliyekuwa akiishika nafasi hiyo, Balozi Khamis
Kagasheki akizungumza jana alisema, kwa mara ya kwanza lazima taswira
nzuri ya wizara ionekane na kitakachofanyika ni kuwashughulikia
watumishi wasio waaminifu.
Akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake, Mahmoud
Mgimwa, Nyalandu alisema, watumishi wa wizara hiyo watakaoonekana kwenda
kinyume cha utendaji kazi na kuchafua taswira ya wizara yake,
watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kutimuliwa kazi.
“Harakati za kupambana na majangili itakuwa ndiyo kaulimbiu yangu na mwenzangu,” alisema Nyalandu.
Alisema kwa kuanzia, wizara yake inawasaka watu
watatu waliohusika na kuua faru na kuchukua pembe zake katika Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Waziri Nyalandu akitoa taarifa za kuuawa kwa faru huyo Jumamosi iliyopita alisema, faru huyu aliuawa na majangili usiku huo.
“Hifadhi ya Serengati ina faru 32 pamoja na faru
watano walioletwa na mradi maalumu, unaosimamiwa na Rais Jakaya Kikwete
kutoka Afrika Kusini, ila faru mmoja kati ya hao watano aliuawa mwaka
juzi.”
Jana Nyalandu alisema, katika kupambana na
ujangili wamekamilisha rasimu ya awali ya kubadili Idara ya Wanyamapori
kuwa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania itakayosaidia kuinua morali ya
wafanyakazi ili wafanye kazi za kupambana na majangili katika mazingira
yenye hatari nyingi katika maisha yao.
Kwa upande wake Mgimwa alisema, watafanya kazi kwa
bidii na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha kuwa wizara hiyo inakuwa
ya kwanza na ya mfano katika Mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) kwa kuhakikisha sekta ya utalii inachangia zaidi ya asiliamia 23
ya pato la taifa kwa mwaka.
0 comments:
Post a Comment