Rais Jakaya Kikwete amefunga mjadala wa wafanyabiashara wazawa
wanaotaka kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa sekta ya gesi akisema
Shirika la Maendeleo la Petroli(TPDC) linajitosheleza kuwasaidia
Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo.
Katika kipindi cha miaka miwili, Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameshikilia kuwa hakuna Watanzania
wenye uwezo wa utafutaji, uchimbaji na uzalishaji, jambo ambalo
linapingwa vikali na wafanyabiashara wazawa.
Akizungumza jana wakati wa Kongamano la Viongozi
wa Dini kuhusu rasilimali ya gesi, mafuta na madini kwa ajili ya amani
na maendeleo ya taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema hakuna kampuni nchini
yenye dhamana ya kupata mikopo kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kampuni za kigeni zenye mitaji mikubwa
zinafanikiwa kupata mikopo kwa kuwa zina dhamana inayowasaidia kupata
mikopo kwenye mabenki,” alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kama kuna kampuni
za Watanzania zinatakiwa kushirikiana na wawekezaji watapaswa kufuata
taratibu zilizowekwa.
Rais Kikwete alisema uwekezaji kwenye sekta ya
mafuta ni kama mchezo wa kamari kwani mtu anaweza kuwekeza fedha nyingi
katika utafutaji wa gesi na asipate kitu.
“Ni kampuni gani Tanzania ambayo itakuwa tayari kucheza kamari?” alihoji Rais Kikwete.
Alisema ndio maana Serikali imeona ni vizuri
iandae mpango wa kuiwezesha TPDC kuingia kwenye shughuli za gesi badala
ya kuwa kutoa leseni tu.
“Tunataka siku moja TPDC iwe na uwezo wa kuwauzia
hisa Watanzania iwe kama kampuni kubwa za Statoil(Norway) na Petro
Plus(Brazil) zinazoendeshwa na Serikali zao,” alisema.
Rais Kikwete alisema baada ya kuliwezesha shirika
hilo, Watanzania watanufaika kwa kiwango kikubwa tofauti na kutoa
kipaumbele kwa kampuni binafsi za Watanzania.
Washiriki watoa maoni tofauti
Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima alipinga kongamano hilo kufanyika sasa kwani alieleza lilipaswa kufanyika miaka mitano iliyopita na sio sasa wakati ambapo shughuli za uchimbaji wa gesi zinakaribia kuanza.
Akizungumza wakati wa akisoma salamu za viongozi wa Dini ya
Kikristo katika kongamano hilo, Dk Kitima alisema kongamano kama hilo
haliwezi kubadili chochote na kinachofanyika ni kwa wawekezaji
kujifagilia njia wakati wanaelekea katika kuanza kutekeleza miradi
waliyowekeza.
“Hapa ninachoweza kusema ni kuwa wafadhili hao
wametoa fedha, wamefadhili kongamano hili ili wakianza shughuli zao
wasisumbuliwe,” alisema na kuongeza kuwa kinachofanyika sasa hakitoi
taswira nzuri kwani jamii imelishwa sumu kuwa haiwezi kufanya lolote
bila kuombaomba.
Akionekana kujibu hoja hiyo, Askofu Stephen Munga
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), aliomba kuweka sawa dhana
hiyo kwa kusema kuwa sio sahihi kuwa mkutano huo umefadhiliwa na
matajiri wa gesi na mafuta.
“Kongamano tumeandaa wenyewe baada ya baadhi ya
maaskofu wa KKKT kufika ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo
kuzungumza nae kuhusiana na uharibifu wa mazingira na akataka pia
tuzungumzie suala la gesi, ndio tukaona kuna haja ya kufanya kitu kama
hiki ambacho kinafanyika sasa,” alisema.
Naye Sheikh Aboubakary Zuberi alisema ni vizuri
watu ambao wanaishi katika maeneo ambako rasilimali zinapatikana ni
vizuri wakanufaika nazo badala ya kuwa kama ilivyo sasa jambo ambalo
haliwezi kuleta matokeo mazuri siku za mbeleni.
Alisema nchini kuna mgawanyiko mkubwa wa mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.
0 comments:
Post a Comment