Monday 13 October 2014

TAMKO LA WAKRISTO BUKOBA KUHUSIANA NA MAUAJI PAMOJA NA UCHOMAJI WA MAKANISA

Filled under:

TAMKO LA WAKRISTO BUKOBA KUHUSIANA NA MAUAJI PAMOJA NA UCHOMAJI MAKANISA TAREHE 11/10/2014.


Baada ya tukio la kutisha la kushambuliwa kwa washirika na hatimaye kuuawa kwa mshirika na kujeruhiwa vibaya kwa mwingine kanisani Kagemu PAG; Wachungaji na viongozi wa kiroho wa Bukoba tumepokea taarifa hizi kwa mshtuko mkubwa. Tumekutana tarehe 10 Oct 2014 na kutafakari hatima ya wakristo katika eneo hili.

Matukio rejea tuliyojikumbusha ni kama ifuatavyo:

1. Kanisa la Living water pale Buyekera mlimani limechomwa moto mara.

2. Kanisa la Hofan ministries limechomwa moto pale Rugambwa.

3. Kanisa la la International assemblies of God lilipo Magoti lilichomwa moto na kuteketea.

4. Kanisa la TAG Kihwa lilichomwa moto na kuteketea.

5. Makanisa mengine maeneo ya vijijini kuchomwa moto nayo ni pamoja na Ruhanga TAG, Kakindo PAG na Kasharu EAGT.

6. Vitisho na Kushambuliwa kwa mawe wakati ibada zikiendelea mara kwa mara Kanisa la PAG Buyekera.

7. Kanisa la EAGT Kibeta kushambuliwa kwa mawe baada ya kundi la watu kuvamia kanisani miezi 3 iliyopita

8. Kanisa la Harvest kushambuliwa kwa mawe usiku na kundi la watu.

9. Jaribio la kuchomwa kisu Askofu Sesse Lazaro wakati akiwa kanisani.

10. Kifo cha kutatanisha cha Mch Jackson Kabuga wa TAG Kashabo.

Mengi ya matukio haya yameripotiwa katika vyombo vya usalama ingawa hatujapata mrejesho wowote toka vyombo hivi.

Kwa mtazamo wetu huu ni mpango uliolasimishwa wa kujenga hofu na hatimaye kukomesha uhuru wetu katika kumwabudu Mungu. Matukio haya japo yanaonekana hayahusiani lakini yamebeba maudhui inayofanana na yanatekelezwa kwa mbinu zinazofanana na inawezekana na kundi moja lenye mtandao mpana.

Kwa tamko hili tunataka yafuatayo yazingatiwe:

a. Kwa hali hii wakristo tutaweka mtandao unaojitegemea wa ki ulinzi wa nyumba za ibada, viongozi wa kiroho, na washirika wetu pamoja na hatua nyingine zozote za kiusalama tutakazoona zinafaa.

b. Tunaitaka serkali ifanye uchunguzi wa kina juu ya tukio hili na mengine yaliyotangulia na kutupatia taarifa ndani ya muda mfupi juu ya mafanikio au kukwama kwa uchunguzi.

c. Kwa Wakristo wote walioguswa na kuumizwa na tukio hili maneno la Mungu toka Rumi 8:37-39 yawe faraja yetu:

“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Amen

Tamko hili limetolewa na Wachungaji 35 waliokaa katika kikao cha dhararula PAG tarehe 10/10/2014 na kutiwa sahihi kwa niaba yao na:-

Mch Crodward Edward.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wachungaji Bukoba.

0 comments:

Post a Comment