Thursday 25 September 2014

WARAKA WA MLIMANDAGO ALIVYOMCHAFUA DIALO KWA KUMLIPUA LOWASA

Filled under:

NAIBU Waziri wa zamani wa Maji, Anthony Diallo, amesema dhana inayojengwa kwamba Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria ulifanikishwa kwa nguvu ya aliyekuwa Waziri, Edward Lowassa, ni potofu na afadhali angetajwa yeye.

Katika mazungumzo na Raia Mwema yaliyofanyika mjini Mwanza wiki hii na ambayo yatachapishwa katika gazeti dada la hili la Raia Tanzania kesho, Diallo ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, ameweka wazi kwa kila hatua kuhusu mradi huo.

Kimsingi, Diallo ameeleza kwamba mradi huo wa maji ulitokana na ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa mwaka 2000 na kama ingekuwa sifa ni bora zingeenda kwake.

“Kwanza kuna vitu viwili. Cha kwanza miradi yote inayolipiwa na kodi za wananchi ni jukumu la serikali iliyoko madarakani, sidhani anaweza kutokea mtu mmoja kudai kwamba nilifanikisha hiki.
Ukienda kwa staili hiyo ndiyo watu wanasema ile dhana ya wabunge kuwa mawaziri inaleta haya matatizo kwamba mtu anavutia kwake akiwa na nia fulani, sasa hao wanaodai kwamba walifanya hivi definitely lazima ujue kwamba wana nia fulani, wanataka kuwavutia wapiga kura kwamba wao wanawajali sana.

Sitakueleza mambo ambayo ni siri ya Baraza la Mawaziri, siwezi kuitoa, lakini moja ni kwamba mradi huo ulikuwa ahadi ya Rais Mkapa, mwaka 2000 wakati anaomba kura kipindi cha pili, alipopita Shinyanga na Kahama alisema lazima tufanye chini juu tutajenga mradi wa maji kuelekea huko kutoka Ziwa Victoria.

Sasa ngoma ilikuwa ni pesa zitapatikana wapi, mwaka 2002 tukaanza mazungumzo makali sana na nchi hizi zilizo kwenye Bonde la Nile, na bahati nzuri mimi ndiye nilihudhuria vikao vyote, mpaka tukafika mahali tukauvunja ule mkataba wa Misri na Uingereza, kwa sababu walikuwa wanatuzuia tusitumie maji ya Ziwa Victoria na hiyo mikutano yote nimehudhuria mimi, Addis Ababa. Na nimshukuru sana waziri mwingine aliyenisaidia, maana nilikuwa vocal sana, Martha Karua wa Kenya, aliyekuwa Waziri wa Maji wakati huo,”

alisema Diallo.

Kauli hii ya Diallo ni ya kwanza kutamkwa hadharani kuhusiana na mradi huo ambao mara nyingi
umekuwa ukitajwa na wapambe wa Lowassa kuwa kati ya kete zake muhimu ndani ya chama chake kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Wapambe hao wamekuwa wakisema ni Lowassa aliyeusukuma na kuusimamia tangia kwenye mchakato wa kuondoa tatizo la maji kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa, hasa Shinyanga na Kahama.

Katika mazungumzo hayo, Diallo alieleza ya kuwa akiwa Naibu Waziri chini ya Lowassa, namna alivyoshiriki katika kila hatua kabla ya kuhamishwa wizara.

“Baada ya hapo ikaja ngoma kwamba huu mradi utapate pesa kutoka wapi. Mimi nikafanya utafiti mdogo nikagundua kwamba tusingeweza kupata hela za wahisani kokote kwa sababu World Bank (Benki ya Dunia) jamaa wa Misri wamejaa hata IMF (Shirika la Fedha Duniani) kote kule wamejaa.

Lakini pia tukakumbuka miaka ya 1960 tulipokazana kuchukua haya maji kwenye mradi ule wa Wendele, nchi za Scandinavia zikazuia kwamba tusichukue maji Ziwa Victoria badala yake wakasema tuchimbe malambo, yakaja matrekta mengi na kwa sababu tulikuwa hatuna ufundi matrekta hayo mengi yamekuja kukusanywa kwenye vyuma chakavu, kama unakumbuka kulikuwa na katapila karibu kila kijiji mengi yamekuja kukusanywa kama vyuma chakavu. Kwa hiyo ilikuwa ni tabu sana pesa mtapata wapi.

Nikaja na wazo kwamba kwanini tusiombe pesa kwa Rais, tutumie pesa zetu wenyewe, wakati huo pesa za makusanyo ya kodi zilianza kupanda sana. Basi tukamwandikia barua Rais, tukamwambia uwezekano wa kupata funding ni mdogo sana, kwa hiyo akakubali tutumie pesa zetu wenyewe.

Wakati ule huo mradi ulikadiriwa kumalizika kwa bilioni 27. Mimi nikaja na wazo pale wizarani, nikawaambia kwa pesa hiyo huu mradi hauwezi kuisha , kwanini tusilishawishi Baraza la Mawaziri tufanye kwa awamu, tukaandika mradi wetu na matarajio yote tukakubaliwa.

Ili tujenge kwanza pampu na lile tenki la Ihelele (kijiji kando ya ziwa unakoanzia mradi huo) hiyo ilikuwa awamu ya kwanza bilioni 27 zingeishia hapo. Nikawa nawatania wizarani kwamba tukishafikisha maji pale (Ihelele) hakuna Wizara itakayopinga tusichukue hela kuyapeleka maji mbele.

Awamu ya pili ilikuwa umeme tutaupata wapi, kwa sababu pale (kwenye chanzo cha maji) ni porini tu, mara ya kwanza tukakubaliana kwamba tujenge sub station (kituo kidogo) lakini Tanesco hawakuwa waangalifu sana ule mradi tukaliwa, kwa sababu waliweka nguzo na nyaya ambazo ni sub standard (chini ya kiwango) zisingeweza kuendesha yale mapampu.

Tukaja na wazo la kuchukua umeme Kahama Mining, ikadibi tufanye hivyo, zile nguzo za awali zikatelekezwa. Hapo serikali tulikula hasara, ingawa si mbaya kwa sababu tulikuwa tunafanya kitu kinaitwa learning curve na watalamu wetu hawakuwa wazuri kiasi hicho.

Idea ya pili niliyoitoa mimi, nilikuwa mtu wa kwanza kuleta ule utaratibu wa design and build, nikawaambia hapa tukitaka tuweke feasibility study (upembuzi yakinifu), tutazeekea hapo mradi hautakamilika.

Kwa hiyo mkandarasi tutakayempa atakuwa ana design, tunaipitia design (michoro) yake na consultant (mtaalam mshauri) tutakuwa tumeshamuweka tunakubaliana anajenga ili mradi tunajua bei haiwezi kuvuka hapo.

Hata mkimuuliza Waziri Lowassa (Edward Lowassa Waziri wa Maji wakati huo) anakumbuka. Ule mradi ulikuwa mikononi mwangu, yeye alikuwa anashughulikia DAWASA. Tulikubaliana kugawana mimi nisimamie mradi wa Shinyanga yeye asimamie DAWASA, nilikuwa na maamuzi yote.

Huo mradi ndiyo ulikuwa hivyo, lakini ku- single out (huwezi kusema) kwamba nani aliukubali au aliukataa, ninajua waliokuwa wanaupinga lakini siwezi kusema ni nani kwa sababu ilikuwa ni siri, uamuzi wa Baraza la Mawaziri ni siri,” 
alisema Diallo.

Septemba mwaka jana, Lowassa alinukuliwa katika vyombo vya habari akieleza kwamba wakati alipopendekeza mradi huo wa maji kwenye Baraza la Mawaziri wakati wa enzi ya Mkapa, ni mawaziri wawili tu ndiyo waliomuunga mkono.

Akizungumza katika Kanisa la AICT mjini Kahama, Shinyanga, Lowassa alinukuliwa akiwataja mawaziri waliomuunga mkono kuwa ni Jakaya Kikwete ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati huo na Muhammed Seif Khatib aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Muungano).




Katibu mwenezi mkoa wa Shinyanga ndugu Emmanuel Mlimandago


0 comments:

Post a Comment