Friday 12 September 2014

SITTA ASHAMBULIWA KAMA MWEWE

Filled under:


Samuel Sitta
Mpango wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta wa kutaka ya wajumbe wake walioko nje ya nchi kupiga kura kupitisha Katiba inayopendekezwa, umepingwa na wasomi, ukielezwa ni kinyume na kanuni za Bunge na sheria za nchi.

Wasomi hao, wanaharakati na wanasiasa wamesema Tanzania haina utaratibu wa raia wake kupiga kura wakiwa nje ya nchi na kwamba hiyo ni mbinu ya kufanya udanganyifu.
Juzi, Sitta alisema wajumbe wa Bunge hilo watakaokuwa nje ya nchi kwa sababu zozote, ikiwamo ya matibabu na Hijja, watapiga kura hukohuko mara upigaji kura utakapoanza Septemba 26, mwaka huu na kuwataka wajumbe hao kuacha mawasiliano yao watakapokuwa nje na kwamba uongozi wa Bunge umeanza kufanya mawasiliano na balozi mbalimbali za Tanzania, ili wawepo watumishi wake watakaokula kiapo cha kisheria kusimamia kazi hiyo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema suala la Watanzania kupiga kura wakiwa nje ya nchi halimo kwenye kanuni zinazoongoza Bunge hilo na ni vizuri utaratibu huo ukaachwa.
Alisema anachokiona sasa ni Bunge kuendelea kupoteza fedha za wananchi wakati hakuna maridhiano huku uamuzi ukiwa umefikiwa kwamba Katiba Mpya itapatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Hata kanuni za mabunge ya Jumuiya za Madola ambazo sisi tunazifuata ikitokea mjumbe anaumwa anapelekwa kwenye ukumbi wa Bunge kupiga kura, kura haipigwi sehemu yoyote.
“Hata katika Bunge la Uingereza ikionekana mjumbe anatakiwa kupiga kura lakini anaumwa atapelekwa ukumbini kwa msaada wa uongozi wa Bunge, ili aweze kutimiza haki yake ya kidemokrasia lakini haki hiyo haiwezi kumfuata huko aliko.
“Sitta analichukulia suala la Katiba kama lake binafsi, utaratibu wa kupiga kura za kificho haukubaliki kwa sababu utasababisha uchakachuaji,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema Tanzania haina utaratibu wa raia wake kupiga kura wakiwa nje ya nchi.
Mwanasheria huyo alisema kinachofanywa na Sitta kinaonyesha namna Bunge la Katiba linavyolazimisha mchakato huo.
“Kituo pekee cha wajumbe wa Bunge Maalumu kupiga kura ni ndani ya Ukumbi wa Bunge na si vinginevyo. Kinachofanywa na Sitta ni kuwahadaa Watanzania, mtu anaumwa atapigaje kura wakati hata kwenye majadiliano hakuwapo? Unalipigia kura jambo ambalo umeshiriki kwenye majadiliano,” alisema.

Alisema Tanzania haina utaratibu wa raia wake kupiga kura wakiwa nje ya nchi na kwamba endapo Serikali inataka kuuruhusu basi ifanye hivyo.

0 comments:

Post a Comment