Monday 24 March 2014

UMOJA WA WAKULIMA WA CHAI WAMBURUZA MAHAKAMANI JANUARY MAKAMBA

Filled under:



UMOJA wa Wakulima wa Chai (UTEGA) Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto, Tanga unatarajia kumburuza mahakamani Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.

Uamuzi wa UTEGA ulitolewa hivi karibuni katika mkutano mkuu maalumu wa UTEGA ulioitishwa kwa nia ya kutathmini njia bora za kisheria za kuhakikisha kiwanda cha chai kinafunguliwa na kudai fidia ya athari walizopata kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kufungwa.

Kwa mujibu wa UTEGA uamuzi huo unatokana na hatua ya mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknelojia, kuitisha mkutano wa hadhara  uliotoa azimio la kufungwa kwa Kiwanda cha Mponde Tea Estates kinyume cha sheria za nchi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UTEGA, William Shelukindo, alisema kwa mwaka mmoja tangu kiwanda kifungwe jitihada mbalimbali zimechukuliwa za kukinusuru zikiwemo kufanya kikao na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga.

Shelukindo alisema katika mkutano huo, Kamati ya Siasa iliagiza kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Usambara Tea Growers Association (UTEGA) kama ilivyopendekezwa na Makamba.

Shelukindo alisema kikao cha kamati ya utendaji ya UTEGA cha Septemba 14, 2013 hakikuafikiana na maagizo hayo.

“Kamati yetu ya utendaji ilipingana na wazo la Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa kwa sababu kubwa kwamba, endapo tutafanya  uchaguzi kabla ya wakati, tutakuwa tumekiuka Katiba ya UTEGA,” alisema Shelukindo.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa walifanya kikao kingine kati ya uongozi wa UTEGA, na maofisa wa Hazina (Msajili wa Hazina), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali na Msimamizi wa mali za serikali zilizouzwa (CHC) Consolidated Holdings Cooperation.

Akifafanua zaidi Shelukindo alisema kuwa kikao kilibainisha wazi kwamba suala la Kiwanda cha Chai cha Mponde ni la kisheria kwa vile kiwanda pamoja na shamba la Sakare viliuzwa na serikali kwa UTEGA, na hakuna upande wowote wenye tatizo na umoja huo.

Mwenyekiti aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, Mwenyekiti wa Lushoto Tea Company, Nawab Mulla, alifanya kikao na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, Februari 23, mwaka huu, mkoani Dodoma.

Alisema kuwa katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu alishauri kwamba kiwanda kifunguliwe kwani wakulima wa chai wanateseka sana na suala hilo linamuumiza kichwa chake.

Katika hoja hizo, ilibainika wazi kuwa kiwanda hicho kilifungwa kwa madai ya kuchochewa na Mbunge wa Bumbuli kwenye mkutano wa hadhara wa Mei  26 mwaka jana uliofanyika ndani ya kiwanja kilichopo kiwandani hapo.

Mara baada ya mkutano huo msaidizi wa mbunge alianza kusambaza fomu kwa wakulima wa chai ili wazijaze kumuunga mkono, hatua aliyoichukua ya kufunga kiwanda hicho kinachotoa huduma kwa wakulima wa chai wa vituo vya Lushoto na Korogwe.

Wajumbe hao waliiagiza Mponde Tea Estates Company Ltd, iende mahakama kupata kibali cha kufungua kiwanda ili wakulima wasiendelee kuteseka.

Kwa mujibu wa mkutano huo, mashitaka mengine ambayo wanakusudia kufungua mahakamani ni kudai fidia iliyotokana na kufungwa kiwanda hicho na kukisababishia hasara kubwa.

0 comments:

Post a Comment