Saturday 1 March 2014

FID Q:MBALI NA MZIKI NAJIHUSISHA NA MADINI

Filled under:



Kati ya mamia ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya maarufu Tanzania, ni mwanamuziki mmoja pekee aliyehudhuria katika Tamasha la Sauti za Busara 2014, lililotajwa na Kituo cha Utangazaji cha CNN kuwa ni tamasha lenye nguvu barani Afrika.
Huyu siyo mwingine bali ni Fareed Kubanda (Fid Q), aliyekuwapo mjini Zanzibar kwa siku mbili kushuhudia tamasha hilo lililokuwa la siku nne, lililofanyika katika wiki ya pili ya Februari mwaka huu, Viwanja vya Ngome Kongwe visiwani humo.
Ikumbukwe kuwa Fid Q alianza shughuli za muziki miaka ya 1990. Alitoa wimbo wake wa kwanza mwaka 2000 ulioitwa; Huyu na Yule, alioimba na Mr Paul. Wimbo huu ulirekodiwa na Prodyuza maarufu nchini,  Master Jay katika Studio za MJ Records na kumpa heshima kubwa msanii huyo.
Starehe ilifanya mahojiano na  Fid Q ambaye pamoja na mambo mengine aliweka wazi sababu za yeye kuwapo katika tamasha hilo, kilichomvutia huku akiweka wazi kuhusu biashara ya madini aliyodaiwa kuanza kuifanya mwishoni mwa mwaka jana.
Swali: Nini kimekuvutia ukaamua kuhudhuria katika tamasha hili?
Fid Q: Mimi ni mtu ninayependa kujifunza zaidi, nimeona hili ni tamasha kubwa na zuri kwangu kujifunza. Kubwa zaidi ni kutaka kujua wenzetu wanafanyaje muziki. Huwezi kukaa tu na kwenda kupiga muziki staili moja kila siku; ili ujue, ni vyema ukajifunza kutoka kwa watu unaowaamini.
Swali: Kupitia wanamuziki wa muziki wa asili kutoka mataifa mbalimbali katika Sauti za Busara, unadhani unaweza kupata uzoefu wa kutosha?
Fid Q: Wasanii wote wa mataifa mbalimbali waliofanikiwa hasa Nigeria, wamekuwa wakichukua vionjo kutoka katika muziki wa asili, kisha wakileta katika muziki wa kizazi kipya, inapatikana ladha ya kipekee, ndiyo maana leo unawaona kina P Square wanatamba, walianza kujifunza na kutumia vionjo kutoka katika muziki wa asili.
Swali: Unadhani nini kinachowafanya wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutohudhuria tamasha hili?
Fid Q: Hawapo tayari kujifunza. Mimi nimewahi kutumbuiza katika tamasha hili, ninajua. Huku hakuna ubabaishaji, msanii unatakiwa uimbe kwa sauti yako jukwaani, walio wengi hili hawaliwezi. Idadi kubwa ya wasanii wamezoea kuimba kwa ‘playback’, (kuweka cd ya ala), ndiyo maana hata waandaaji wanashindwa kuwaalika, muziki tunaofanya sisi ni ule wa wenzetu, lakini tunashindwa kuuwakilisha ipasavyo, tumezoea kuimba kwa ‘playback’.
Swali: Unadhani kuna umuhimu gani kwa wasanii kuimba ‘live’ (kwa sauti zao wenyewe pasipo kutegemea CD)?
Fid Q: Ina faida zake. Kwanza inakutangaza na pia unaonekana wewe ni msanii halisi. Haya ndiyo wanayohitaji kuyaona watu wanaoujua muziki, watu wanaohudhuria matamasha ya kimataifa ni wengi, hawawezi kusikiliza kitu walichokisikia kwao, wanapenda kusikia kitu kipya kitakachowateka
Swali: Unadhani ni kwa nini muziki wa asili unapendwa na wageni kuliko wazawa?
Fid Q: Tatizo ni kwamba Watanzania hawapendi wala kuuthamini utamaduni wao. Kinachosikitisha, tamasha kama hili kubwa Afrika, wamejaa wazungu, wanapenda utamaduni wao na hata wapo tayari kujifunza juu ya utamaduni wa watu wengine.
Swali: Kwa nini mwaka huu hukushiriki kwenye tamasha hili?
Fid Q: Waliniita na kutaka nishiriki, lakini sikuwa tayari na ratiba zangu na sikudhani kama nitapata muda, hivyo niliona ni vyema nikikaa pembeni baada ya kupata muda nikaona nije kushiriki tu kama mtazamaji.
Swali: Uliwahi kueleza kwamba unafanya biashara ya madini, tujuze biashara yako inaendeleaje?
Fid Q: Ha ha ha ha; mimi ni dalali tu kwenye ile biashara, mbali na kupata fedha. Ila nimeingia katika biashara ya madini ya Ruby ili kukuza kipato changu.  Unajua huwezi kufanya muziki peke yake, lazima muda mwingine ujikite katika biashara zitakazokuletea faida na kipato kikubwa ili uweze kufanya maendeleo zaidi katika maisha.
Swali: Nani hasa mhusika katika biashara hiyo?
Fid Q: Kwa bahati mbaya sitaweza kumtaja kutokana na makubaliano yetu, lakini ni mfanyabiashara mkubwa tu wa madini Arusha. Mimi nimeingia kati kama dalali, ni fursa kwangu na kwa kuwa nafahamiana na watu wengi ninaweza kufanya vizuri biashara hii.
Swali: Ni mafanikio gani uliyoyapata kupitia biashara hii?
Fid Q: Napata faida kubwa sana, ambayo imeniwezesha  kuanza kufanya mambo kadhaa ya kimaendeleo, ambayo sitakuwa tayari kuyaweka wazi kwa sasa, lakini mambo yakiwa mazuri na kukamilika kwa mipango yangu, wananchi watajua tu.
Swali: Mashabiki wako watarajie nini kutoka kwako?
Fid Q: Nipo ‘chimbo’ nikitayarisha kazi na Prodyuza P Funk, ambaye ni prodyuza wangu wa albamu yangu ya kwanza ‘Vina Mwanzo, Kati na Mwisho’.

0 comments:

Post a Comment