Friday 14 February 2014

PROF.TIBAIJUKA ATANGAZA OPERESHENI KUBWA YA BOMOABOMOA

Filled under:



WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametangaza kiama kwa wananchi waliojitwalia na kumiliki ardhi kinyume cha sheria.
 
Tibaijuka alisema kuanzia wiki ijayo wataendesha operesheni kubwa ya kubomoa nyumba na majengo ya watu waliojenga kwenye maeneo ya wazi au  yasiyoruhusiwa.

Aliitoa kauli hiyo jana wakati wa ufunguzi wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari kuhusu elimu ya sera na sheria zinazosimamia sekta ya ardhi.

Katika semina hiyo iliyoandaliwa na wizara yake, Profesa Tibaijuka alisema kazi ya bomoabomoa hiyo wataifanya kwa weledi mkubwa zaidi na kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

“Tuliweka mabango ya kutoa notisi katika maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa, lakini wahusika walikaidi, sasa tutavunja hayo majumba na wale waliosema kuwa nimekwisha kisiasa nataka niwahakikishie kwamba sijaisha,” alisema.

Waziri Tibaijuka pia aliwaonya baadhi ya matajiri wanaotumia mahakama kuweka pingamizi ili kuzuia wasichukuliwe hatua, akisema safari hii watafuata taratibu zote za kuvunja  kwanza na atakayeshitaki wakutane mahakamani.

“Hizo kuta nilizoziona maeneo ya Mbezi na maeneo mengine tutazivunja bila kumwangalia mtu usoni. Hao wenye hati pandikizi wala hatutabembelezana nao bali tutakutana mahakamani baada ya kuvunja,’’ alitamba waziri huyo.

Kuhusu hatua za kuwachukulia baadhi ya watendaji wa wizara hiyo wanaokiuka taratibu na kugawa ardhi na hati kinyemela, alisema kuwa ameweka mfumo mzuri wa kuondoa mianya ya rushwa ili kila kitu kifanyike kwa uwazi.

“Nilisema kwamba mfumo uliopo sasa si mzuri kwani watendaji wa ardhi hawako chini ya wizara yetu bali wako chini ya halmashauri (Tamisemi) ambapo ilikuwa vigumu kuwabana.

“Ili kuwasaidia watendaji hawa wasiingie kwenye mitego ya rushwa, tumeweka mfumo mzuri ambapo sasa kamishna wa ardhi hataweza kujifungia mwenyewe ofisini na kuandika hati peke yake bila wenzake kujua anafanya nini,” alisema.

Alibainisha kuwa kamishna wa ardhi sasa atalazimika kumshirikisha katibu mkuu na watendaji wengine kuhusu hati anayotaka kuitoa kwa mhusika.

Waziri Tibaijuka alijisifu kuwa amedumu katika wizara hiyo licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya wizara zaidi ya mara mbili, na hivyo akasema kuwa atahakikisha pia wasaidizi wake nao wanadumu kwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Mapema akizungumza katika semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Selassie Mayunga, alisema kuwa hivi sasa wameweka mkakati wa kupima kila kipande cha ardhi nchini.

“Tutakwenda kijiji kwa kijiji, wilaya kwa wilaya tukianzia Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambapo kila mtu atapimiwa eneo lake na kukabidhiwa hati yake ya umiliki.

“Katika maeneo ya wafugaji tutaainisha sehemu za majosho na malisho ili kuondoa usumbufu wa wafugaji kuvamia wakulima. Lengo ni kuhakikisha migogoro ya ardhi nchini inakomeshwa,” alisema.

Aliongeza kuwa licha ya wizara yake kuwa na nia thabiti ya kutatua na ikiwezekana kumaliza migogoro ya ardhi nchini, wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa fedha.
Alibainisha kuwa kama wangekuwa wanatengewa bajeti kubwa ya kupima na kugawa ardhi, matatizo na migogoro mingi inayotokea hivi sasa isingepata nafasi.

chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment