Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiache kumsakama Waziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwa sababu tu ya kutaka kutimiza ndoto
yake.
Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa Kilimanjaro, alisema kama ni kuonyesha nia wapo wanachama wengine
wa CCM wamefanya hivyo bila kusakamwa.
Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa wanaousaka
urais mwaka 2015, na harakati zake hizo zinaonekana kuwakera baadhi ya
viongozi wa CCM ambao wameanza kumwandama kwa maneno.
Tayari CCM kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake,
Philip Mangula na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wamekaririwa
wakisema walioanza kampeni mapema watashughulikiwa.
Hata hivyo hakuna mahali popote ambapo Lowassa
ambaye pia ni Mbunge wa Monduli amewahi kutangaza nia ya kuusaka urais
isipokuwa amesema ana ndoto ambayo iko mbioni kutimia.
Akitoa salamu zake za mwaka mpya wa 2014 jana,
Ndesamburo alisema si haki kila matamko ya viongozi wa CCM kumlenga
Lowassa pekee wakati wapo wanachama wengine ndani ya CCM.
“Wanaotangaza nia mbona wako wengi sana huko CCM na wala siyo Lowassa peke yake,” alisema na kuongeza;
“Hao wanaomnyooshea kidole Lowassa hawa wengine
hawawaoni?” alihoji Ndesamburo na kuwataka viongozi wa CCM kuacha
unafiki na kuendesha mambo kwa “double standard” (ubaguzi).
Ndesamburo alisema ukimwondoa Lowassa, wapo
wanachama wengine wa CCM wanaoshiriki kwenye harambee kanisani na
misikitini, lakini hilo haliwagusi viongozi wa CCM isipokuwa Lowassa tu.
Mbunge huyo alisema njia pekee ya kuepukana na unafiki huo wa CCM ni kuichagua Chadema yenye malengo na maisha mazuri.
0 comments:
Post a Comment