KANISA la Moravian kupitia Kamati yake ya Mpito ya Jimbo la Misheni
Mashariki imemwandikia barua Msajili wa Vyama na Taasisi za Dini
aliyepo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupuuza taarifa alizopewa za
Mkutano Mkuu wa Taifa uliofanywa na kundi lenye mgogoro katika kanisa
hilo.
Mkuu wa Mawasiliano, Mahusiano, Uandishi na Uratibu wa kanisa hilo,
Mchungaji Emmaus Mwamakula, alisema hayo jana alipozungumza na
waandishi wa habari kuhusu mkutano huo batili uliofanyika Desemba 26
hadi 28, mwaka jana ambao ulitolewa tamko na Askofu wa Jimbo la Kusini,
Lusekelo Mwakafwila.
Alisema walimtaka msajili huyo kurejea maelezo ambayo wamekuwa
wakimpa kwa njia ya e-mail pamoja na nyaraka mbalimbali walizompatia
kutoka uongozi wa Kanisa la Moravian duniani kuhusiana na mgogoro wa
kanisa katika jimbo hilo.
Mwamakula alisema mgogoro uliopo katika kanisa hilo unatokana na uchu
wa madaraka kwa baadhi ya viongozi ambapo Mwakafwila na wenzake
walibuni tuhuma za uongo dhidi ya Mwenyekiti wa Jimbo hilo, Mchungaji
Clement Fumbo, kwa lengo la kumchafua pamoja na watendaji wengine,
jambo ambalo wameshindwa kulithibitisha mpaka sasa.
“Tunapenda kuifahamisha ofisi yako kuwa mkutano mkuu ulioitishwa na
Askofu Lusekelo Mwakafwila ni batili kwa mujibu wa kanuni na taratibu
za Kanisa la Moravian na hivyo uongozi uliochaguliwa kutokana na
mkutano huo ni batili,” alisema.
Alisema pamoja na uongozi wa Moravian duniani kumpa nafasi ya
kusuluhisha jambo hilo Askofu Mwakafwila, bado alivuruga kwa makusudi
hatua muhimu zilizokuwa zimefikiwa za kupatanisha kanisa hilo.
Alitoa wito kwa viongozi wa kanisa hilo na hata wale wa madhehebu
mengine ya Kikristo kukemea kwa nguvu vitendo vya kuchochea fujo ndani
ya nyumba za ibada.
0 comments:
Post a Comment