Friday, 17 January 2014

LIYUMBA ASHINDA KESI YA KUKUTWA NA SIMU GEREZANI

Filled under:



Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana ilimuachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, dhidi ya tuhuma za kukutwa na simu ya mkononi gerezani isivyo halali baada ya ushahidi wa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi dhaifu na kushindwa kuthibitisha mashtaka hayo.
Hukumu hiyo ilisomwa saa 3:25 asubuhi na Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando.

Hakimu Mmbando alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na uliotolewa na upande wa Jamhuri ulikuwa na udhaifu na kwamba umeshindwa kuishawishi mahakama kuhusu tuhuma zinazomkabili Liyumba.

“Upande wa Jamhuri ulitoa simu waliyodai kumkuta nayo gerezani kwa kuitambulisha na siyo kielelezo... na simu hiyo ilitolewa na mwendesha mashtaka (wakati huo Elizabeth Kaganda) badala ya shahidi kuiomba mahakama kupokea simu hiyo,” alisema.

Alisema mahakama haiwezi kufanya maamuzi kwa kutumia kitu kilichotambulishwa badala yake wanatumia vielelezo mbalimbali katika kutoa maamuzi yake.

“Katika kesi hii kiini kikubwa ni simu ya mkononi aina ya Nokia yenye rangi nyeusi anayodaiwa kukutwa nayo mshtakiwa... lakini kumbukumbu za mahakama hazionyeshi kama ni kielelezo katika kuthibitisha tuhuma hizo,” alisema Hakimu Mmbando.

Hakimu huyo alisema kutokana na udhaifu na upelelezi wa kizembe dhidi ya kesi hiyo, mahakama imeona mshtakiwa hana hatia na inamwachia huru.

Septemba 8, mwaka 2011 Liyumba lifikishwa mahakamani hapo baada ya kutenda kosa wakati akiwa gerezani akitumikia kifungo cha miaka miwili kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Ilidaiwa kuwa Julai 27, mwaka 2011, alikutwa na simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 ya rangi nyeusi iliyokuwa inatumia laini namba 0653-004662 pamoja na namba ya utambulisho ya simu (IMEI) 356273/04/276170/3.

0 comments:

Post a Comment