Chama cha NCCR-Mageuzi kitafanya Uchaguzi Mkuu wake Januari 18
mwaka huu, huku Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na Katibu Mkuu
wake, Samwel Ruhuza wakijitosa tena kutetea nafasi zao.
Chama hicho kilisema Mbatia ambaye amekuwa
mwenyekiti wa chama hicho tangu mwaka 2000 na Ruhuza 2009, pamoja na
viongozi wengine wanatetea nafasi zao kwa kuwa Katiba na kanuni za chama
hicho hazijaweka ukomo wa uongozi.
Vigogo wengine wa chama hicho waliojitosa kuwania
uongozi ni mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, Faustine Sungura
(Mjumbe wa Halmashauri Kuu), Danda Juju (Msaidizi wa Mwenyekiti- Taifa),
Leticia Ghati (Katibu wa Wanawake Taifa) na Mosena Nyambabe (Kaimu
Katibu Mkuu).
Mbatia ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, atachuana na
Charles Makofila (37) ambaye ni mlemavu wa viungo. Kwa sasa Makofila
ni Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Katavi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu
Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe alisema Mkutano Mkuu ndiyo
utakaowachagua viongozi hao, utajadili katiba ya chama hicho na kufanyia
marekebisho baadhi ya vifungu vyake kama itaona inafaa.
“Hata rasimu ya Katiba imependekeza ukomo wa
uongozi, sitaki kulizungumzia kiundani suala hili, lakini huenda
likajadiliwa na Mkutano Mkuu. Maana hata taasisi na mashirika mbalimbali
yamekuwa na utaratibu wa kuwa na ukomo wa uongozi,” alisema.
Alisema nafasi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo
ni Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti (Bara), Makamu Mwenyekiti
(Zanzibar), Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Naibu Katibu Mkuu
(Zanzibar), Mweka Hazina, Wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa na
Makamishna wa Mikoa. “Uchaguzi wa majimbo tumeshamaliza na Januari 18
utafanyika Mkutano Mkuu ambao utawachagua Mwenyekiti, Makamu wake wawili
(Bara na Zanzibar)” alisema na kuongeza;
“Wajumbe 12 wa Halmashauri Kuu, wajumbe wanane
wanawake kutoka Zanzibar na Bara, wajumbe wawili kutoka makundi maalumu
na wengine wawili wawakilishi wa vijana.”
Alisema watakaoibuka washindi katika uchaguzi huo
moja kwa moja watakuwa wameunda Halmashauri Kuu Mpya ambayo Januari 19,
itawachagua Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu (Bara na Zanzibar) na mweka
hazina wa chama.
Watakaochuana kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti
(Bara) ni Ghati, Anyimike Mwasakalali, Rakia Abubakar Hassan na Danda,
huku Haji Ambar Khamis ambaye ni Makamu Mwenyekiti Zanzibar akikosa
mpinzani katika nafasi hiyo.
Kwa nafasi ya Katibu Mkuu wapo Nyambabe, Rehema
Sam na Ruhuza, wanaowania nafasi ya Naibu Katibu Mkuu (Bara) ni Martin
Mung’ong’o, Sungura na Machali.
Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) wapo Ameir Mshindani Ali na Mussa Kombo Mussa.Katika mkutano huo Nyambabe alifafanua sakata la mbunge wa chama hicho
Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye Desemba 17, mwaka 2011,
Halmashauri Kuu ya chama hicho ilimvua uanachama, hivyo kupoteza sifa ya
kuwa mbunge.
“Chama kimeshamalizana na Kafulila tangu Julai mwaka jana, kwa sasa Kafulila ni mbunge kamili wa NCCR,” alisema.
“Chama kimeshamalizana na Kafulila tangu Julai mwaka jana, kwa sasa Kafulila ni mbunge kamili wa NCCR,” alisema.
0 comments:
Post a Comment