Thursday 12 December 2013

ZUMA AZOMEWA NA BAADHI YA WAOMBOLEZAJI

Filled under:



Chama Tawala cha Afrika Kusini, Africa National Congress (ANC) kimekasirishwa na kuzomewa kwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma wakati wa Ibada ya kitaifa ya heshima za mwisho kwa rais wake wa kwanza mzalendo, Mzee Nelson Mandela.

Rais Zuma alizomewa mara kadhaa na baadhi ya waomboleza waliofurika katika Uwanja wa Michezo wa FNB (Soccer City), juzi Jumanne na kuhudhuriwa na mamia ya wakuu wa nchi na Serikali pamoja na watu mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mara ya kwanza rais huyo alizomewa wakati akiingia uwanjani hapo, huku kundi jingine la watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa ANC likimshangilia, hali ambayo iliendelea wakati akitambulishwa na kila sura yake ilipoonekana kwenye televisheni kubwa zilizokuwapo uwanjani.

Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati kiongozi huyo aliposimama kuhutubia ambapo waliompinga walionyesha wazi kiasi cha kusababaisha kuchelewa kuanza kwa hutuba yake.

Makamu Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa ambaye alikuwa mmoja wa waendeshaji shughuli hiyo ya kitaifa, mara kadhaa alijaribu kukemea zomeazomea hiyo, lakini hakusikilizwa kwani wapo waliokuwa wakiimba wakati hotuba za viongozi zikiendelea.

Ramaphosa zaidi ya mara tatu alisikika akikemea kile alichokiita utovu wa nidhamu kwa baadhi ya watu waliokuwa FNB. “Tuna wageni, hebu tusijiaibishe wenyewe na tuwe na nidhamu,” alisema na kuongeza:

“Yeye (Mandela) alikuwa ni kada mwenye nidhamu, kwahiyo hebu basi tumsindikize katika hali ya kuwa na nidhamu,tuonyeshe kwamba sisi tuna nidhamu katika mazingira ya aina yoyote”.
Msemaji wa ANC,Jackson Mthembu akizungumza baada ya ibada hiyo, alisema waliokuwa wakimzomea Zuma ambaye pia ni Rais wa ANC “wameliaibisha taifa la Afrika Kusini”.

“Tukio hili halikuwa la kisiasa wala la siasa na hao waliozomea wamewaangusha Waafrika Kusini waliokuwapo uwanjani na wale waliokuwa wakifuatilia tukio hili la kihitoria kupitia vyombo vya habari,” alisema Mthembu.

Wakati Rais Zuma akizomewa, mtangulizi wake, Thabo Mbeki pamoja na viongozi wengine kadhaa wakiwamo naibu wake, Kgalema Motlante, Rais wa Zimbabwe, Robet Mugabe, Rais wa Marekani Barack Obama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kin Moon walikuwa wakishangiliwa kwa nyakati toauti.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliliambia gazeti hili kuwa Rais Zuma “anavuna alichopanda”.

“Zuma hana hata hadhi ya kusimama katika kivuli cha Mandela, naamini hata Madiba alipo anafahamu kwamba alipigania uhuru wa watu lakini wale waliofuata wakiwa watawala nchi na watu havipo katika mioyo yao,” alisema Martin Cullen mkazi wa Soweto.

0 comments:

Post a Comment