Monday 23 December 2013

DK.MGIMWA AZUSHIWA KIFO

Filled under:



WAKATI mawaziri wanne wameng’olewa na wengine walioitwa mizigo wanatarajiwa kutimuliwa wakati wowote, Rais Jakaya Kikwete yupo katika wakati mgumu wa kusaka warithi wa nafasi hizo,

Ugumu wa kusaka warithi wa mawaziri hao, umeongezeka zaidi jana baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa kuzushiwa kifo kutokana na afya yake kuzorota.

Hata hivyo, uvumi huo ulioenezwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi na kupitia mitandao ya kijamii, haukuwa sahihi, lakini taarifa zaidi kuhusu afya za Waziri Mgimwa zinasema kuwa atahitaji muda mrefu kupumzika, hivyo nafasi yake lazima izibwe na waziri mwingine kutokana na unyeti wake.

Mawaziri walioondolewa madarakani ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi).

Kuondolewa kwa mawaziri hao pia kunaelezwa kumelenga kumnusuru Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akitajwa kwa kushindwa kuwasimamia mawaziri walio chini yake.

Kuondoka kwa mawaziri hao, kutamsaidia au kumwongezea mzigo Rais Kikwete kutimiza mapendekezo ya Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyotaka awaondoe mawaziri saba iliyowaita ‘mizigo’.

Wadadisi wa mambo ya siasa, wanasema kuwa mazingira ya kupata baraza jipya la mawaziri, yanampa wakati mgumu sana Rais Kikwete kufanya uamuzi wa nani aingie na nani atoke.

Jina la mbunge mpya wa kuteuliwa na rais, Dk. Asha Rose Migiro, limekuwa likitajwa mara nyingi kwamba hatua ya kuingizwa ndani ya Bunge hivi karibuni, huenda kuna nia ya kutaka kumteua kuwa mmoja wa mawaziri, na sasa baada ya kutemwa kwa mawaziri hao wanne turufu inaelekezwa kwake kuwa miongoni mwa watakaoziba moja ya nafasi.

Hata hivyo, duru nyingine za siasa zinasema nafasi ya Dk. Migiro kuteuliwa kushika wizara yoyote ni finyu kutokana na ukweli kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinamhitaji sana kwenye sekretarieti ambako anaongoza Idara ya Mambo ya Nje.

Chini ya utaratibu mpya, mjumbe wa sekretarieti, haruhusiwi kuwa waziri na ndiyo maana Januari Makamba, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alilazimika kuachia nafasi ya ujumbe wa sekretarieti mara baada ya kuteuliwa kuingia katika Baraza la Mawaziri.

Inaelezwa kuwa tangu alipoingia kwenye sekretarieti, Dk. Migiro kwa kutumia uzoefu wake mambo ya kimataifa amekuwa kiungo kikubwa kwa CCM na mataifa ya nje.

Mjumbe mwingine wa sekretarieti anayetajwa kuwamo kwenye baraza jipya ni Mwigulu Nchemba ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu CCM Bara.

Majina mengine yanayotajwa miongoni mwa wabunge ni pamoja na Dk. Khamis Kigwangala, Peter Serukamba ambaye ameonyesha uwezo mkubwa tangu alipochaguliwa kuongoza Kamati ya Bunge ya Miundombinu, ingawa nafasi yake kwenye baraza jipya inaelezwa kuathiriwa na uhusiano wake na Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Katika majina hayo, yapo pia majina ya waliojiita wapambanaji wa ufisadi kama Anne Kilango Malecela, James Lembeli na wabunge wengine mwiba kwa CCM kama Kangi Lugola na Deo Filikunjombe.

0 comments:

Post a Comment