Taarifa ya Mbunge wa Nzega kwa Umma
Kuhusiana na Upotoshaji Uliofanywa na Taasisi ya Tanzania Chamber of
Minerals and Energy (TCME)
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega imesikitishwa na kufadhaishwa na
taarifa ya uongo na isiyo na uzalendo hata chembe, iliyotolewa na
taasisi ya TCME siku ya tarehe 26, Machi, 2014. Hii imedhihirisha kuwa,
hawajui wanalolifanya ama wanatumiwa vibaya na watu wenye maslahi ovu
kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Nzega na wa Tanzania kwa Ujumla.
Taarifa za namna hii hazina maksudi mengine zaidi ya kusababisha chuki
na mfarakano usio na sababu za msingi baina ya makundi ambayo yangepaswa
kufanya kazi pamoja kutafuta suluhu ya mgogoro huu.
Mbunge wa Nzega amekuwa ni mtu anayependa kutoa fursa ya mazungumzo na
wabia wote wa maendeleo jimboni kwake na yuko tayari
kusikilizana na yeyote yule, inashangaza ni kwa nini wadaua hawatumii
vizuri fursa hizi kwa faida ya wote.
Mbunge wa Nzega ni muwekezaji yeye mwenyewe binafsi na anatambua umuhimu
wa wawekezaji kwa ukuaji uchumi na maendeleo ya jamii ya watu wake, na
ndiyo maana amekuwa siku zote mstari wa mbele kuvutia wawekezaji
mbalimbali katika jimbo lake. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) si mchukia
wawekezaji hata kidogo. Yeye ni mtetezi wa haki za kila mtu, hata za
askari polisi na magereza.
Tamko la Shrikisho la Wachimbaji na Watafutaji Madini na Nishati
Tanzania (TCME) lingepaswa kuwa la ukweli na lenye weledi wa kutosha,
lakini inasikitisha limekuwa ni tamko lisilo na uadilifu na hata chembe
ya ukweli. Hata kama taasisi hii inawawakilisha na kuwatetea mabepari,
isitetee uongo na dhulma ya wazi. Inapaswa ifahamu kuwa, Ubepari
utakaoweza kufanya kazi Tanzania ni ubepari wenye sura ya kijamaa,
unaothamini utu, udugu na umoja wetu.
Kwanza, Kwamba, Mbunge aliongoza maandamano haramu kuelekea eneo la
Mwanshina, si kweli. Ukweli ni kwamba, Mbunge wa Nzega na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, Dr. Hamisi Kigwangalla, hakuongoza
maandamano yoyote yale siku ile bali alifanya mkutano halali, na alikuwa
na ratiba ya mikutano miwili jimboni mwake katika Kata zake mbili, Kata
ya Nzega Ndogo (Kijiji cha Zogolo) na Kata ya Lusu(Kitongoji cha
Mwashina), ambayo ni maeneo yanayohusisha mgodi wa wachimbaji wadogo
wadogo wa Mwanshina.
Mikutano hii ilitolewa taarifa polisi na mamlaka nyingine mbali mbali
wilayani Nzega, kwa mujibu wa Sheria, na Ofisi ya Mbunge iliomba na
kupewa ulinzi halali wa polisi. Baada ya kumaliza Mkutano mmoja,
wananchi pamoja na Mbunge wao waliazimia waelekee kwenye Mkutano wa
pili, yaani eneo la Mwanshina, na walitembea kwa miguu wakiongozwa na
polisi, na hakukuwa na vurugu, matusi na wala dalili yoyote ile ya
uvunjifu wa amani ama uharibifu wa mali za watu. Kama kwenu watu wa
Shrikisho kutembea kwa miguu ni Maandamano basi hamuelewi mfanyalo,
maana hata waendao mazishini, harusini, watokao uwanjani kuangalia
mpira, ama watokao misikitini ama makanisani, ama kwenye mikutano ya
mahubiri, ama jaji/hakimu anavyotoka na mahakama kwenda kuangalia eneo
la tukio huwa ni kwa makundi, basi na wao ni waandamanaji!
Pili, Kwamba “Ni vizuri jamii ikajulishwa kwamba eneo lililovamiwa na
wachimbaji wadogo linamilikiwa na kampuni ya uchimbaji na utafiti wa
madini ya Resolute (Tanzania) Limited, ambao wana leseni halali ya
kuchimba madini katika eneo hilo, leseni namba SML19/97)”, inasema
taarifa yao. Kauli hii ni ya mtu asiyejua sheria ya ardhi ya Tanzania,
na kama huu ndiyo uelewa wenu haishangazi kwa ninyi kutoa tamko la uongo
na upotoshaji namna hii. Resolute ‘hamiliki’ eneo la Mwanshina,
anamiliki leseni ya kuchimba dhahabu tu! Eneo la Mwanshina ni mali ya
wananchi wakazi wa eneo lile, waliozaliwa pale na ndiyo maana hata yeye
hakuliweka kwenye uzio wa maeneo yake. Na ndiyo maana hata leo hii
akitaka kuchimba pale hawezi kufanya hivyo zaidi ya kutumia nguvu za
jeshi la polisi tu. Na hichi ndicho kitakachopingwa na wananchi siku
zote.
Tatu, katika taarifa ya TCME wanasema “Kitendo cha Kiongozi cha
kuhamasisha wachimbaji wadogo kuvunja sheria ni mfano mbaya sana kwa
jamii yetu na ni kitendo hatarishi kwa amani na utulivu”. Ni vema TCME
wakataja ni kiongozi gani amehamasisha wachimbaji wadogo wadogo wavunje
sheria?
Ni lini, wapi na kwa kauli ipi alihamasisha uvunjani huo wa sheria? Ni
Mbunge aliyeenda kuwasikiliza wananchi waliofukuzwa kuchimba ama ni
Naibu Waziri Nishati na Madini, Mhe. Stephen Massele, Mkuu wa Mkoa wa
Tabora, Ndg. Fatma Mwassa, na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Ndg. Bituni
Msangi, waliowarudisha wachimbaji hawa katika eneo lile na baada ya wiki
2 tu kuwaondoa? Wananchi hawa walianza kuchimba dhahabu eneo lile mwezi
Desemba mwaka 2013, wakazuiliwa na serikali mwezi wa kwanza na walitii
agizo hilo. Mbunge aliongea na Naibu Waziri na wakakubaliana kuwa
atazungumza na Resolute wazirudishe leseni za eneo la Mwanshina kwa
serikali hata kabla hazijamaliza muda wake, kwa kuwa wao wanaondoka na
hawachimbi tena dhahabu pale, ili Serikali iwakatie wananchi leseni zao
na kwamba wajiunge kwenye vikundi na SACCOS ili muda ukifika tu wapewe!
Je, ni nani hasa aliyewarudisha wachimbaji hawa kwenye eneo la
‘Resolute’ kabla ya utaratibu huu kukamilika? Na wakati anawarudisha
aliwasiliana na Mbunge? Wakati anawarudisha hakujua kuwa hawana leseni
na kwamba eneo lile ‘linamilikiwa na Resolute’? Ni kwa nini tena
aliyewarudisha, akawaacha wakawekeza ‘vijisenti’ vyao, na baada ya muda
wa wiki mbili hata hawajafika popote anakuja anawaondoa tena? Ni nani
atawalipa fidia ya nguvu, muda, na mitaji yao waliyowekeza pale? Ama
uwekezaji wa watanzania maskini hauna maana kabisa kwenu? Wenye maana ni
utafiti wa Resolute tu? Resolute mwenyewe alipokuja takriban miaka 15
iliyopita alikuta wenyeji wakichimba, mbona wao hawakulindwa dhidi yake?
Maana na wao si walitafiti na kugundua uwepo wa dhahabu eneo lile na
wakaanza kuchimba kabla yake?
Hivi ni wapi wachimbaji wadogo wadogo wamepewa maeneo yao na wanachimba
dhahabu nchini mwao huku wakiwa na leseni? Ni kule Rwamgasa, Mwime ama
Mwabomba? Kule wametumia vigezo gani kuwaruhusu watumie leseni za
Barrick na mashirika mengine, na hapa Nzega wanawakataliaje? Ama ni
kudhirisha madai kwamba kuna baadhi ya viongozi wa serikali wana maslahi
yao na hili eneo la Mwanshina?
Hakuna anayekataa uwekezaji mkubwa kwenye maeneo yetu bali hakuna
atakayekubali wawekezaji wachukue kila kitu na wenyeji wakose kabisa.
Hakuna atakayekubali wenyeji wanyanyaswe na wapoteze mali yao kwa sababu
kuna maslahi ya viongozi wachache. Miaka 15 iliyopita walipoteza mali
yao na hawakulipwa fidia, leo hii hatutakubali wadhulumiwe tena!
Mwisho, rai yetu ni kwamba, viongozi wa Serikali watumie busara na
hekima ya hali ya juu mara zote panapotokea migogoro baina ya wawekezaji
na walalahoi ili kuondoa dhana kwamba wawekezaji wana thamani zaidi ya
wenyeji, badala ya nguvu za kijeshi, uonevu, mabavu na vitisho, hususan
kwenye mgogoro kama huu ambapo kwa kiasi kikubwa ni viongozi wa Serikali
waliouanzisha kwa kuzuia uchimbaji pale awali, na kisha kuruhusu bila
kufuata sheria.
Aidha Serikali iwafutie kesi wachimbaji wote wadogo wadogo na Raia
waliokamatwa wakipita eneo lile siku hiyo bila kujua nini kimetokea
pale, kwa vile tunaamini hakuna kosa walilofanya na pengine ni uonevu
kuwashitaki hao wachache waliokamatwa. Pia, ni busara Serikali ikaongeza
kasi ya kutafuta suluhu ya jambo hili kwa kuwapatia wachimbaji wadogo
wadogo leseni kama makubaliano ya awali yalivyokuwa na pia mwongozo wa
uchimbaji wenye tija na ufanisi.
Imetolewa na,
Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega.
Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB).
Machi 28, 2014.