UMOJA wa Wakulima wa Chai (UTEGA) Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto, Tanga unatarajia kumburuza mahakamani Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.
Uamuzi wa UTEGA ulitolewa hivi karibuni katika mkutano mkuu maalumu
wa UTEGA ulioitishwa kwa nia ya kutathmini njia bora za kisheria za
kuhakikisha kiwanda cha chai kinafunguliwa na kudai fidia ya athari
walizopata kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kufungwa.
Kwa mujibu wa UTEGA uamuzi huo unatokana na hatua ya mbunge huyo
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknelojia, kuitisha mkutano wa
hadhara uliotoa azimio la kufungwa kwa Kiwanda cha Mponde Tea Estates
kinyume cha sheria za nchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UTEGA, William
Shelukindo, alisema kwa mwaka mmoja tangu kiwanda kifungwe jitihada
mbalimbali zimechukuliwa za kukinusuru zikiwemo kufanya kikao na Kamati
ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga.
Shelukindo alisema katika mkutano huo, Kamati ya Siasa iliagiza
kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Usambara Tea Growers Association (UTEGA)
kama ilivyopendekezwa na Makamba.
Shelukindo alisema kikao cha kamati ya utendaji ya UTEGA cha Septemba 14, 2013 hakikuafikiana na maagizo hayo.
“Kamati yetu ya utendaji ilipingana na wazo la Kamati ya Siasa ya CCM
Mkoa kwa sababu kubwa kwamba, endapo tutafanya uchaguzi kabla ya
wakati, tutakuwa tumekiuka Katiba ya UTEGA,” alisema Shelukindo.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa walifanya kikao kingine kati ya
uongozi wa UTEGA, na maofisa wa Hazina (Msajili wa Hazina), Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa serikali na Msimamizi wa mali za serikali zilizouzwa
(CHC) Consolidated Holdings Cooperation.
Akifafanua zaidi Shelukindo alisema kuwa kikao kilibainisha wazi
kwamba suala la Kiwanda cha Chai cha Mponde ni la kisheria kwa vile
kiwanda pamoja na shamba la Sakare viliuzwa na serikali kwa UTEGA, na
hakuna upande wowote wenye tatizo na umoja huo.
Mwenyekiti aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, Mwenyekiti wa
Lushoto Tea Company, Nawab Mulla, alifanya kikao na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, Februari 23, mwaka huu,
mkoani Dodoma.
Alisema kuwa katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu alishauri kwamba
kiwanda kifunguliwe kwani wakulima wa chai wanateseka sana na suala hilo
linamuumiza kichwa chake.
Katika hoja hizo, ilibainika wazi kuwa kiwanda hicho kilifungwa kwa
madai ya kuchochewa na Mbunge wa Bumbuli kwenye mkutano wa hadhara wa
Mei 26 mwaka jana uliofanyika ndani ya kiwanja kilichopo kiwandani
hapo.
Mara baada ya mkutano huo msaidizi wa mbunge alianza kusambaza fomu
kwa wakulima wa chai ili wazijaze kumuunga mkono, hatua aliyoichukua ya
kufunga kiwanda hicho kinachotoa huduma kwa wakulima wa chai wa vituo
vya Lushoto na Korogwe.
Wajumbe hao waliiagiza Mponde Tea Estates Company Ltd, iende mahakama
kupata kibali cha kufungua kiwanda ili wakulima wasiendelee kuteseka.
Kwa mujibu wa mkutano huo, mashitaka mengine ambayo wanakusudia
kufungua mahakamani ni kudai fidia iliyotokana na kufungwa kiwanda hicho
na kukisababishia hasara kubwa.
0 comments:
Post a Comment