JESHI la Polisi wilayani Nzega, mkoani Tabora limemkamata na
kumuachia kwa masharti Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangallah, kwa
madai ya kuongoza maandamano ya wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao
wanapinga kufungwa kwa machimbo ya Mwashina, yaliyo jirani na mgodi wa
Resolute Tanzania Limited.
Mbunge huyo alikamatwa majira ya saa 10:00 jioni juzi baada ya kufanya maandamano yasiyo na kibali yaliyoanza saa saba mchana.
Kabla ya hapo mbunge huyo alifanya mkutano wa hadhara na wachimbaji
hao katika Kijiji cha Nzega Ndogo wilayani humo ambapo alielezwa
matatizo ya kufungwa kwa machimbo hayo na Kamishna wa Madini nchini,
Paulo Masanja, bila kujali gharama walizoingia wachimbaji hao.
Katika mkutano huo wachimbaji hao walidai ni vema serikali iangalie
haki zao zilizotumika kwenye uendeshaji na uchimbaji wa mashimo hayo
kuliko kuwafungia bila kujali ingawa eneo hilo liko ndani ya leseni ya
mgodi wa Resolute.
Hata hivyo katika hoja hiyo mbunge huyo aliwataka wachimbaji hao
kudai haki yao kwa kufuata taratibu bila kujali tofauti zao kisiasa,
kikabila na kidini na badala yake wawe kitu kimoja.
Dk. Kigwangallah aliwaambia wachimbaji hao haki zao ziko mikononi
mwao hivyo ni uamuzi wao kudai haki na yeye kama mwakilishi wao yuko
nyuma yao mpaka pale haki yao itakapopatikana.
Aidha, wachimbaji hao walimwomba mbunge huyo kuambatana nao kwenye
maandamano ya amani kutoka Kijiji cha Nzega Ndogo kwenda Mwashina yalipo
machimbo yaliyofukiwa umbali wa zaidi ya kilomita tatu kujionea hali
halisi.
Kufuata hali hiyo, wachimbaji hao walianza maandamano ambayo
yaliungwa mkono na mbunge huyo hadi Kijiji cha Mkwajuni kabla ya kufika
Mwashina, ambapo polisi waliibuka na kuyasambaratisha kwa mabomu ya
machozi.
Katika purukushani hizo polisi walimkamata Dk. Kigwanhallah na
kumjeruhi mtu mmoja kwa risasi ya moto kwenye paji la uso, ambapo
waliondoka naye kwenye gari pamoja na mbunge huyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda, alisema Dk.
Kigwangallah alikamatwa na kuachiwa huru ili akamalizie kazi zake kama
mjumbe wa Bunge la Katiba.
0 comments:
Post a Comment