Showing posts with label siasa. Show all posts
Showing posts with label siasa. Show all posts

Friday, 11 April 2014

MNYIKA ASHINIKIZA KUPATA HATI YA MUUNGANO

Filled under:

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, John Mnyika, amesema atawasilisha hoja kuzuia shughuli za Bunge hilo kuendelea mpaka wajumbe watakapopatiwa hati halisi ya Muungano.

Mnyika, ambaye ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya wajenzi na kusema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo kwa vile hadi sasa serikali haijatoa hati halisi ya Muungano ingawa ni muhimu wajumbe waione.

Alikumbusha kuwa baada ya kupitishwa kwa Kanuni za Bunge alitaka kanuni ziruhusu wajumbe wa Bunge wapewe nyaraka wanazotaka katika utendaji wao wa kazi.

“Niliposema hivyo, Mbunge wa Simanjiro Ole Sendeka, alisemama na kupinga na akasema huyu Mnyika anataka kudai hati ya Muungano, naomba kanuni hiyo isiwepo”alisema.

Alisema Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alisimama na kusema kuwa hati hiyo ipo katika Sheria ya Muungano, lakini hakuna hati halisi wakati taarifa zingine zikisema kuwa ipo Umoja wa Mataifa.

“Hata hivyo baada ya kanuni hiyo kupita, nilimwandikia barua Katibu wa Bunge kuomba hati halisi ya muungano, lakini hadi sasa hivi ninavyozungumza sijapewa hati hiyo.“
Alisema msingi wa Rasimu ya Katiba ni Hati ya Muungano na kwamba umefika wakati sasa wajadili rasimu huku wakiwa na hati halisi.

“Hawa CCM wanadai uwazi kwa kukataa kura ya siri sasa inabidi waonyeshe mfano kwa kuweka wazi Hati ya Muungano, wakikomaa tutawashtaki kwa wananchi,” alisema.

Posted By Unknown04:47

Wednesday, 9 April 2014

NYANGWINE KUWASHITAKI MAKADA WA CCM WANAOMHUJUMU JIMBONI

Filled under:



VURUGU na kampeni chafu zinazofanywa na baadhi ya makada wa CCM wanaojipanga kuwania ubunge katika jimbo la Tarime, zimechukua sura mpya.

Hatua hiyo imetokana na mbunge wa jimbo hilo Nyambari Nyangwine (pichani), kuweka bayana kuwa atawasilisha malalamiko kwa uongozi wa CCM ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.

Juzi, baadhi ya wanachama wa CCM wilayani Tarime, walilalamikia kampeni chafu  zinazofanywa na baadhi makada na kusababisha makundi ambayo ni hatari kwa Chama.

Hata hivyo, baadhi ya makada hao ambao baadhi wametajwa kuungwa mkono na baadhi ya viongozi wa CCM wilayani humo, wamekuwa wakieneza siasa chafu za ukabila, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni hatari.

Makada hao ambao baadhi walishindwa kwenye kura za maoni, ambapo sasa wameanza kujipanga upya lakini wakitumia njia ambazo ni kinyume na taratibu za CCM.

Taarifa ya Nyangwine kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa atawasilisha malalamiko yake ikiwa ni pamoja na kuwataja kwa majina makada hao.

Imesema kuwa makada hao wamekuwa wakieneza siasa za chuki zenye lengo la kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Hata hivyo, alisema kamwe hatishwi na makada hao kwa kuwa baadhi waligombea mara kadhaa na kushindwa hivyo jimbo hilo kutawaliwa na wapinzani kwa miaka 10.

Alisema CCM ni chama chenye demokrasia na kinajali haki za kila mwanachama katika kuwania uongozi, lakini kina taratibu zake ambazo ni lazima zifuatwe ikiwa ni pamoja na kusbiri muda mwafaka wa kufanya kampeni na si kuwahujumu waliopo madarakani.

“Nitawasilisha malalamiko yangu rasmi kwa uongozi wa chama ngazi zote hadi kwa Katibu Mkuu wetu (Abdulrahaman Kinana), sasa hivi ni wakati wa kutekeleza Ilani za Chama kwa wananchi si kufanya kampeni ili kukwamisha kazi.

“Waniache nitumikie wananchi walionichagua na muda ukifika waje tupambane kwa hoja ndani ya Chama, haya wanayoyafanya sasa hivi ni uhuni na kutaka kurejesha makundi ambayo mwisho wa siku yatakigharimu chama chetu.

“Baadhi ya wanaoendesha siasa hizi chafu ni wanasiasa ambao wameishiwa sera na goigoi na ndio sababu wameshindwa mara kadhaa kwenye uchaguzi,” alisema Nyangwine kwenye taarifa yake.

Posted By Unknown03:14

Monday, 7 April 2014

VIONGOZI WANNE WA CHADEMA KUJIVUA UONGOZI NA UANACHAMA

Filled under:



Viongozi wanne wa CHADEMA toka ngazi ya Wilaya na Kata katika Mkoa a Arusha wameachia nyadhifa zao na kujitoa uanachama wa chama hicho.
Viongozi hao, Amani Torongey (Mwenyekiti Monduli), Revocatus Parapara (Mwenyekiti Ngorongoro), Gerald Majengo (Mwenyekiti Kata ya Terati) na Prosper Mfinanga (Katibu Mwenezi Kata ya Olorien) wamekutana na wanahabari kueleza kuwa wameamua kuwa raia wa kawaida kutokana na kutokupewa fedha za kuendesha chama.

Pia, wamedai kutokuwa na uhuru wa kuchangia hoja wakati wa mikutano mbalimbali na iwaapo wakichangia, wakibainika, hufukuzwa katika nyadhifa zao.

Posted By Unknown11:01

TAMKO LA AWALI LA CHADEMA KUPINGA UCHAGUZI MDOGO WA CHALINZE

Filled under:


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinatoa tamko la awali kwa umma kuhusu ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia uchaguzi, zilizofanyika kwenye mchakato wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Chalinze, ambao umehitimishwa Aprili 6, mwaka huu, kwa wapiga kura wa jimbo hili kupiga kura;

Ukiukwaji huo ni kama ifuatavyo;
  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuongeza wapiga kura wapya kinyume cha sheria
Kinyume kabisa na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu cha 15(5), kinachosema; 

“Kwa madhumuni ya kifungu hiki, Tume itapitia upya daftari la kudumu la taifa la wapiga kura mara mbili kati ya kipindi kinachoanza mara baada ya uchaguzi mkuu na tarehe inayofuatia siku ya uteuzi,”

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekiuka kifungu hiki cha sheria kwa kufanya kile wanachoita wao ni ‘uhakiki wa mwaka 2014’ wa daftari ambao wanadai lengo lake lilikuwa ni kupunguza idadi ya wapiga kura waliokufa au kuhama au kuandikishwa mara mbili, lakini badala ya wapiga kura kupungua, uhakiki huo uliofanywa na tume bila kushirikisha wala kuwataarifu wananchi wa Jimbo la Chalinze, umeongeza idadi ya wapiga kura wapya katika jimbo hili kwenye uchaguzi huu mdogo.

Vile vile, kutokana na kitendo hicho cha NEC kuongeza idadi ya wapiga kura wapya kwenye daftari kimesababisha kuongezeka kwa vituo vya kupigia kura tofauti na ilivyokuwa mwaka 2010, ambapo Jimbo la Chalinze lilikuw ana jumla ya vituo 286 na sasa vimekuwa 288.
  • Kutangaza matokeo kinyume cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi
Msimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Chalinze, katika kufanya majumuisho ya kura, alienda kinyume cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kwa kutangaza matokeo ya jumla bila kufanyika majumuisho ya kituo kimoja baada ya kingine, kama sheria inavyomtaka.

Kitendo hicho kilikuwa kinyume na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu 80(3), kinachosema;

“Baada ya taarifa zote za matokeo na masanduku ya kura yaliyo na karatasi za kura za uchaguzi wa bunge kupokelewa kutoka vituo vya kupigia kura katika jimbo, Msimamizi wa Uchaguzi, baada ya kuamua uhalali wa kura zozote zenye mgogoro na kabla ya kujumlisha kura hizo, atatangaza kwa sauti matokeo ya kila kituo cha kupigia kura katika jimbo kimoja baada ya kingine.”

Badala yake, Msimamizi wa Uchaguzi alitangaza matokeo ya jumla kwa kila kata, bila kufanyika kwa majumuisho kama sheria inavyotaka, jambo ambalo linapelekea matokeo yaliyotangazwa kutokuwa halali kisheria, huku yakitofautiana na matokeo tuliyonayo kwa mujibu wa fomu za matokeo.
  • Matumizi ya rasilimali za umma kuibeba CCM na mgombea wake
Tangu mwanzo wa kampeni CCM, kinyume cha sheria zinazosimamia uchaguzi, wametumia rasilimali za umma kumfanyia kampeni mgombe wao, kushawishi na kuelekeza wapiga kura.

Kuna mifano mingi katika suala hili; upo ushahidi unaonesha kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa akifika jimboni hapa kwa kutumia magari ya serikali na watumishi wa umma, ambapo alihusika kufanya kampeni za ‘mtu kwa mtu’.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Ally Mohamed Shein, ambaye alikuja Chalinze kwenye mkutano wa ufungaji wa kampeni za chama chake huko Miono, naye alitumia rasilimali za umma, k.m; magari na watumishi (wakiwemo kutoka vyombo vya ulinzi na usalama), waliokuwa kwenye msafara wake, kufanya kampeni za chama cha siasa, kushawishi na kuelekeza wapiga kura, kinyume kabisa na sheria na taratibu za uchaguzi.

Mama Salma Kikwete ambaye ni kiongozi mwandamizi wa CCM, kwa muda takriban wote wa kampeni alikuwa akitumia rasilimali za umma kama vile magari (yaliyokuwa na namba za ikulu) na watumishi, kufanya kampeni za kumnadi mgombea wa chama chake.
  • CCM kufanya kampeni siku ya uchaguzi
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alifanya kampeni siku ya kupiga kura, akiwa kwenye kituo cha kupigia kura, ambapo alinukuliwa na na kutangaazwa moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari, akisema yeye amempigia kura mgombea wa CCM.

Kitendo hicho cha Rais Kikwete ambacho kililenga kufanya kampeni, kushawishi na kuelekeza wapiga kura, ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi, kifungu cha 104 (1), ambacho kinasema;

“Hakuna mtu atakayefanya mkutano siku ya kupiga kura au; ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika uchaguzi unaendelea, au mahali popote ndani ya eneo la mita 200 ya jengo hilo…kuonesha upendeleo au nembo nyingine inayoonesha kuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi.”

Kifungu cha 104 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kinasema;
“Mtu yeyote atakwenda kinyume na kifungu hiki, atakuwa amefanya kosa…”
  • Vishawishi vya rushwa kwa ajili ya kujitoa
Kinyume na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu cha 91B, ambacho kinasema; “Mtu yeyote atakayemshawishi au kumsababisha mtu mwingine kujitoa kuwa mgombea katika uchaguzi kwa kupewa malipo, ukuwadi wa malipo au ahadi ya malipo na mtu yeyote….atakuwa amefanya kosa la rushwa na iwapo atatiwa hatiani atatumikia kifungo kisichozidi miaka mitano,” mgombea wa CCM aliwatumia makuwadi wake kumshawishi mgombea wa CHADEMA ajitoe kwa ahadi ya kupatiwa cheo atakachokuwa tayari, kati ya ukuu wa mkoa au wilaya, mahali popote nchini.

Imetolewa leo Bagamoyo, Aprili 7, 2014 na;
John Mrema
Mkuu wa Operesheni ya Uchaguzi Mdogo-Chalinze

Posted By Unknown10:56

Sunday, 6 April 2014

MATOKEO YA AWALI JIMBO LA CHALINZE

Filled under:

 
Uchaguzi wa mdogo wa Jimbo la Chalinze umefanyika huku ukigubikwa na kasoro kadhaa, ikiwa ni pamoja na watu wachache kujitokeza vituoni kupiga kura, wapiga kura kulalamika ‘kupokwa’ vitambulisho vyao, vituo kuwa majumbani kwa watu, huku pia kukiwa na hofu ya vurugu.
Kasoro hizo zilijidhihirisha jana wakati wapiga kura shughuli ya upigaji kura ilipokuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ambapo wananchi wa Chalinze walikuwa wakipiga kura mbunge wao, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki mapema mwaka huu.
Gazeti hili liliweza kuzunguka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura ambapo lilishuhudia idadi ya watu wachache wakiwa wamejitokeza kutimiza haki na wajibu wao wa kikatiba wa kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Katika kituo cha kupigia kura, Ofisi ya Maji Changa namba 2, hadi muda wa kufunga vituo ukiwa umebakia nusu saa, walikuwa wamejitokeza wapiga kura 75 kati ya 328 walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Kituo hicho, kilikuwa miongoni mwa vituo kadhaa vilivyokuwa majumbani mwa watu, kikiwa katika nyumba ya Mzee Issa Mbogo, kinyume cha sheria ya uchaguzi.
Katika kituo cha Tukamisasa hadi muda wa kufunga vituo ukiwa unakaribia mwisho, yalikuwa yametukika madaftari mawili pekee, kati ya madaftari sita ambayo yalipaswa kuwa kituoni hapo, ambapo kila daftari linajumuisha wapiga kura 50.
Mbali ya vituo kama hivyo ambavyo viko maeneo ya vijijini, hata vituo vilivyokuwa kata za mjini kama Builingu, pia hazikuwa na wapiga kura wengi.
Mathalani Kituo cha Ofisi ya Mtendaji Namba 2; waliopiga kura walikuwa 64 kati ya wapiga kura 383, Namba 3; waliopiga kura ni 62 kati ya 383.
Kata nyingine ya Pera ambayo pia iko maeneo ya mjini, Kituo cha Shule ya Msingi Namba 1; waliopiga kura ni 88, kati ya walioandikishwa 443, Kituo cha Pera Shule ya Msingi Namba 2; waliopiga kura ni 100 kati ya wapiga kura 443.
Kituo cha Chamulungu Namba 1; waliopiga kura 100 kati ya 336, huku Chamulungu II wakipiga kura 88 kati ya 325.
Wapiga kura kupokwa vitambulisho
Baadhi ya wapiga kura katika kata ya Ubena, walitoa malalamiko yao wakimtuhumu Katibu wa CCM Tawi la Lulenge kwamba alifika majumbani mwao wakati wanaume hawapo na kuchukua vitambulisho vya kupigia kura akisema kuwa anakwenda kuandikisha namba zao.
Akizungumza kwa uchungu mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la alisema kuwa kitendo hicho hicho si sahihi na akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua stahiki.
“Hapa unavyoniona nimeshindwa kupiga kura hadi sasa…jina langu na namba yangu vipo kwenye daftari kwenye kituo kile pale, lakini sina kitambulisho. Juzi natafuta kitambulisho change, mke wangu ananiambia alikuja Rajab Said ambaye ni Katibu wa Tawi la CCM Lulenge, eti alikwenda kuandikisha namba zetu.
“Hadi muda huu ninaokuambia, hajarudisha vitambulisho kwa sababu siko peke yangu, kuna wengine kama 9 hivi ninawafahamu nao pia vimechukuliwa,” alisema Simon Pojoro.
Kwa upande wake Said akijibu tuhuma hizo, Said alisema kuwa madai hayo si kweli nay eye hajui suala hilo wala hakuhusika kwa namna yoyote kwa wapiga kura kukosa haki yao ya kuchagua mbunge wao, akisema huo ni uzushi.
Tuhuma za gari ya CCM ‘kumwinda’ mgombea wa CHADEMA
Wakati huo huo, akizungumzia mwenendo wa uchaguzi huo, mgombea ubunge wa CHADEMA, Mathayo Torongey alisema kuwa gari aina ya Land Cruiser ‘hard top’, T 630 BFJ, inayomilikiwa na CCM, ilikuwa ikimfuatilia kila mahali alikokwenda wakati akipita maeneo mbalimbali kukagua vituo, kama sheria inavyomruhusu.
“Tena bahati nzuri nimefika hapa kupita kwenye hiki kituo nimeikuta hii gari, hii ndiyo imekuwa ikinifuatilia tangu asubuhi. Wamekuja pale Mdaula akashuka kijana mmoja...yule pale…akiwa na sime na nondo, tulipomshtukia akarudi ndani ya gari akabadili nguo akavua tisheti ya bluu aliyokuwa nayo akavaa koti hilo la kijeshi kama mnavyomuona hapo,” alisema Torongey huku akionesha gari na huyo mtu.
“Tunashukuru kuwa kulikuwa na polisi pale, tuliwapatia taarifa naona wamechukua hatua, tumelikuta gari hili likiwa liko hapa na hawa askari, lakini nashangaa hawajapelekwa kituoni na unawasikia wanavyozungumza kwa jeuri mbele ya polisi,” aliongeza.
Mbele ya waandishi wa habari, gari ile iliyokuwa na watu wengi ndani, huku kuionekana silaha mbalimbali na bendera ya CCM, iliruhusiwa kuondoka maeneo hayo, ikiamriwa ielekee kituoni (bila kusindikizwa na polisi), ambapo kiongozi mmoja, ambaye ni katibu wa chama hicho wilaya moja ya Iringa, akijigamba kwa kusema ‘tutakwenda kituoni baada ya kumaliza kazi zetu.”
Matokeo ya awali
Kata ya Pera; Malivundo Ofisi ya Mtendaji; CCM 77, CHADEMA 2, CUF , AFP 1, NRA 1.
Kimbugi; CCM 11, CHADEMA 1, CUF 0, AFP 0, NRA 0
Magange Ofisi ya Kitongoji; CCM 101, CHADEMA 1, NRA 0, AFP 0
Pingo Shule ya Msingi Namba 1; CCM 31, CHADEMA 1, CUF 1, NRA 0, AFP 0  
Pingo Ofisi ya Kitongoji Namba 2; CCM 61, CHADEMA 4, CUF 2, AFP 1, NRA 0

Pingo Namba 1; CCM 66, CHADEMA 0, NRA 0, AFP 0

Posted By Unknown12:06

UCHAGUZI JIMBO LA CHALINZE,CCM YAZIDI KUONGOZA

Filled under:


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya mrisho Kikwete akisoma karatasi ya kupigia kura kabla ya kupia kura kumchagua Mbunge wa Jimbo la Chalinze kwenye kituo cha kupigia kura cha Zahanati Msoga.
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye chumba cha kupigia kura wakati wa kupiga kura za kumchagua Mbunge mpya wa Jimbo la Chalinze.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipiga kura yake ya kumchagua Mbunge mpya wa Jimbo la Chalinze.
 Mama Salma Kikwete akiweka kura yake kwenye sanduku la kupigia kura kwenye kituo cha Zahanati Msoga.
 Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha AFP Ndugu Ramadhani Mgaya akizungumza na waandishi wa habarai nje ya kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata namba 1na kusema kuwa Chama chake kitakubali matokea yeyote na pia kama watashindwa watajipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2015.
 Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze Ndugu Mathayo Torongey akizungumza na baadhi ya mawakala alipotembelea kituo cha Ofisi Mtendaji Kata namba 1, Bwilingu.
 Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze Ndugu Ridhiwani Kikwete akihakiki taarifa zake kabla ya kupiga kura kwenye kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata namba 3 Bwilingu, Chalinze.
Aziza mtoto wa mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ndugu Ridhiwani Kikwete akimsaidia Baba yake kuweka kura kwenye sanduku la kura ,Ridhiwani alipigia kura yake kwenye kata ya Bwilingu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Jimbo la Chalinze Ndugu Samuel Salianga akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata Bwilingu na kutoa tathmini ya jinsi zoezi linavyoendelea na kufafanua mambo mbali mbali yanayohusu uhalali wa wagombea kupiga kura popote ndani ya jimbo la uchaguzi.


wananchi  wa  jimbo la Chalinze   wamemaliza  kupiga  kura  hivi  punde  na  tayari  baadhi ya  vituo  matokeo  yameanza  kujulikana  huku  katika matokeo hayo ambayo  si rasmi mgombea  wa CCM Ridhiwani  Jakaya  Kikwete  anaendelea  kuongoza huku  vyama  vingine  vikimfuata kwa mbali  zaidi .

Hata  hivyo  zoezi   hilo  limefanyika katika  hali ya amani na utulivu na hadi  sasa  wananchi  wameendelea  kusubiri  matokeo  hayo kwa hamu  kubwa na baadhi ya  vituo  ambavyo  matokeo  yameanza  kujulikana  wafuasi wa CCM  wameanza  kushangilia .

Mbali ya  wafuasi wa CCM  kuonyesha  kuanza kushangilia  bado  wafuasi  wa  vyama  vikuu kama Chadema  na CUF  wameendelea  kujipa matumaini makubwa ya  kushida  katika  uchaguzi  huo na  kuwa  mwisho  wa zoezi la kuhesabu kura ndipo watakapo jua  mbichi na  mbivu  katika mchakato  huo 


 Tayari  Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha AFP Bw Ramadhani Mgaya ametangaza  msimamo  wa  chama  chake   baada ya matokeo hayo  kutangazwa kwa kudai kuwa atakuwa  tayari  kukubali matokeo hata kama atashindwa  katika  uchaguzi huo .

Mgaya  ambae amekuwa  mwanasiasa wa kwanza  wa  vyama  vya  upinzani  kuueleza umma kuwa  yupo  tayari  kwa  matokeo  hayo na  kutangaza  kujipanga kwa mwakani 2015  .

Wakati  mgombea  huyo wa AFP akieleza  hayo kwa upande wa  mgombea wa CCM Ridhiwan Kikwete  yeye  leo amefanya  kituko  cha karne  baada ya  kujipigia  kura  katika zoezi hilo na kisha  karatasi hiyo ya  kupigia  kura  kumpa mtoto  wake  mwenye  miaka  chini ya minne kuitumbukiza katika kisanduku  cha kuhifadhia kura 

uchaguzi  huo  unafanyika  kufuatia  kifo cha  aliyekuwa  mbunge wa jimbo  hilo kupitia  CCM Marehemu  Said Bwanamdogo aliyefariki  dunia mwanzoni mwa mwaka  huu .

Posted By Unknown11:29

Monday, 31 March 2014

KAMILI:MWENYEKITI WA CCM ALIHUSIKA KUNITESA

Filled under:



Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Rose Kamili, aliyedai ametekwa na kuteswa wakati wa uchaguzi mdogo mkoani Iringa, amemtuhumu Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Jessica Msambatavangu kuwa anahusika na mashambulizi dhidi yake.

Kamili alidai alitekwa, kupigwa na kujeruhiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga uliofanyika mapema mwezi huu.

 Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari  mjini Dodoma, siku moja baada ya kula kiapo cha kuwa mjumbe wa bunge maalum la katiba, alisema akiwa vijijini alikokwenda kusambaza mawakala wa  kusimamia uchaguzi wa  Kalenga, alitekwa na watu asiowafahamu ambao walimwingiza kwenye gari na hadi ofisi za CCM mkoani  Iringa.

“Nilipofikishwa katika ofisi hizo nilianza kushushiwa kipigo kikali hata kabla sijashushwa kwenye gari. Nilipelekwa  katika moja ya ofisi na kukutana  Mwenyekiti wa CCM Msambatavangu na kumtambua,”alisema.

Alieleza kusikitishwa na hatua ya mwanamke mwenzake  akimfanyia visa hivyo.
Alisema kuwa Msambatavangu aliamuru aletwe baunsa ambaye ndiye aliyeanza kumpa kipigo kikali huku kiongozi huyo akisisitiza apigwe  zaidi.

Alisema  baada ya kupigwa kwa zaidi ya dakika 20, lilikuja gari la polisi na  wakamweleza kuwa wamefika mahali hapo kwa ajili ya kumwokoa na kumchukua kumpeleka kituoni.

Kamili alisema  alipofikishwa polisi hali yake ilianza kuwa mbaya  ndipo  walipomwandikia fomu namba tatu  (PF3) na kumkimbiza  kwenye  matibabu.

Alisema anasikitishwa kuwa hata baada ya kumtaja mbaya wake polisi, mwenyekiti huyo hajakamatwa na badala yake yupo ndani ya bunge la katiba huku kukiwa hakuna hata jalada alilofunguliwa dhidi ya kiongozi huyo.

Aidha Kamili alilituhumu Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa upendeleo wa dhahiri na kutojali madhila yaliyompata.

“Tangu nijeruhiwe hakuna tamko lolote  lililotolewa na uongozi wa Bunge kuhusiana tatizo lililonikuta, licha ya kuwa Spika ni mwanamke.”

Alisema mbali na kutoa tamko, hakuna msaada wowote wa kitabibu alioupata kutoka bungeni, lakini wabunge wa CCM wanapougua  bunge linakuwa mstari wa mbele kutoa huduma.

Umoja wa wabunge wanawake wa vyama vya Upinzani wametoa tamko la kulaani kitendo hicho na kuitaka Serikali ichukue hatua haraka kushungulikia tatizo hilo.

Akitoa tamko hilo mbele ya wandishi wa Habari, Mwenyekiti wa wabunge hao, Suzan Lyimo alisema kuwa kitendo alichofanyiwa mwanamke mwenzao ni kibaya kinachowakatisha  wanawake tamaa.

Posted By Unknown06:16

Monday, 24 March 2014

KINGUNGE:NILIWAHI KUVULIWA WADHIFU WA UKUU WA MKOA

Filled under:



MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombere-Mwiru, alisema kuwa aliwahi kuvuliwa wadhifa wa ukuu wa mkoa kwa sababu ya kutofautia kimtazamo na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kingunge ambaye anawakilisha kundi la waganga wa tiba asili, alikumbushia tukio hilo juzi katika semina ya waandishi wa habari iliyofanyika mjini hapa katika Ukumbi wa Msekwa, naye akiwa mmoja wa watoa mada.

Akijibu swali la mwandishi wa gazeti hili la kwanini amegeuka mlalamishi wa kukosoa viongozi wenzake wa sasa wakati amekuwa sehemu ya serikali kwa awamu zote nne bila kutimiza wajibu wake, Kingunge alisema kuwa amekuwa akikosoa na wakati fulani iliwahi kumgharimu.

“Wakati fulani nikiwa mkuu wa mkoa, nilipingana na Mwalimu Nyerere nikikataa katiba isibadilishwe kwa manufaa ya watu fulani, basi nikafukuzwa ukuu wa mkoa. Hivyo si kweli kwamba sikukosoa, hata sasa naendelea,” alisema.

Katika mada yake kuhusu mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya, alisema kuwa nchi zinazopata fursa ya kuandika upya katiba zake, zinapaswa kujikita kuandika katiba bora zitakazoweza kuwa na misingi ya kukuza uchumi wa kujitegemea.

“Maisha yetu yameegemea uamuzi wa wenzetu. Tumepigania uhuru ili tujitawale lakini bado ni tegemezi na kama nchi iko hivyo halafu nafasi ya kuandika Katiba mpya inakuja mnapanga safu za vyeo haina maana,” alisema

Posted By Unknown21:23

HATUTAKUBALI KUJADILI RASIMU NYINGINE

Filled under:

 
Bunge Maalumu la Katiba sasa lipo katika hati hati ya kuendelea kutokana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutangaza kuwa hawatakuwa tayari kujadili rasimu tofauti na iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba bungeni.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni, viongozi wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu, walisema wataitetea rasimu hiyo, ndani ya Bunge na kwenye Kamati.
“Rais Jakaya Kikwete amekuja bungeni siyo kufungua Bunge la Katiba bali kaja na mapendekezo ya rasimu ya CCM, sisi tutajadili rasimu ya wananchi ya Jaji Joseph Warioba ambayo inazungumzia muundo wa Muungano wa Serikali tatu,” alisema Profesa Lipumba.
Kutokana na msimamo huu wa Ukawa huenda Bunge litakwama kwani kwa mapendekezo ya CCM yenye Muundo wa Muungano wa Serikali mbili ni lazima kuandikwa upya Rasimu ya Katiba au kufanyika mabadiliko makubwa.
Profesa Lipumba alisema katika majadiliano juu ya rasimu, Ukawa watajikita kutumia Rasimu ya Katiba waliyopewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo imeeleza mapendekezo kwa nini yamefikiwa katika kila hoja,” alisema.
Hata hivyo, alisema wamesikitishwa sana na Rais Jakaya Kikwete, badala ya kufungua Bunge alijikita katika kuchambua rasimu na kuikosoa tume aliyoiunda mwenyewe.
“Rais Jakaya Kikwete siyo tu amemdhalilisha Jaji Warioba pamoja na wajumbe wa Tume, bali amewadhalilisha wananchi waliotoa maoni kwani hata takwimu alizotoa za kupinga rasimu siyo za kweli,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema muundo wa Serikali tatu ndio mawazo ya wananchi ambayo yamekusanywa na watu wenye heshma wakiwapo Jaji Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais na Jaji Augustino Ramadhani ambaye pia amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kauli za Rais badala ya kuimarisha umoja zimewagawa Watanzania kwani ametoa vitisho ambavyo havina sababu hasa kwa Wapemba bila kujua kuna Wanyamwezi wanaoishi Zanzibar.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo, alisema kwa kauli ya juzi ya Rais Kikwete, kutangaza kuwapatia Zanzibar; watu, ardhi, mamlaka kamili na kusimamia uhusiano wa kimataifa ni kuvunja rasmi Muungano,
Mbatia alisema Rais Kikwete pia amewagawa Watanzania katika kauli zake ikiwa ni pamoja na ile ya Wapemba kwa kulima vitunguu katika Jimbo la Kibakwe kana kwamba ni makosa.
Alisema wamesikitishwa na Rais kuacha kufungua Bunge badala yake katumia taarifa potofu za mitaani kuligawa Bunge na kuwadhalilisha wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hakuna asiyejua sasa tupo katika mgogoro mkubwa wa kikatiba, Zanzibar tayari ni nchi kamili kutokana na mabadiliko ya 10 ya katiba yao waliyoyafanya mwaka 2010 baada ya kupitisha dhana ya kuwa Zanzibar ni nchi,” alisema.
Mbowe
Mbowe alisema Rais amevunja maridhiano na hata kushindwa kusikiliza maoni ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Seneta Amos Wako kuwa maoni ya wananchi yaheshimiwe.
Alisema Serikali ya Kenya ilichakachua maoni, ilichakachua rasimu na kusababisha vurugu kubwa jambo ambalo linaweza kutokea kwa Tanzania.
“CCM wasijidanganye kwa wingi wao bungeni hakika katika hili tutatetea madai na maoni ya wananchi hadi mwisho,” alisema

Posted By Unknown03:02

Saturday, 15 March 2014

MAJIBU/MAELEZO YA PINGAMIZI LILILOWEKWA NA BWANA FABIAN L. SKAUKI DHIDI YANGU MIMI MATAYO M.TORONGEY MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE KUPITIA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

Filled under:

 
 MAJIBU/MAELEZO YA PINGAMIZI LILILOWEKWA NA BWANA FABIAN L. SKAUKI DHIDI YANGU MIMI MATAYO M.TORONGEY MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE KUPITIA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

UTANGULIZI  
       Kwa mujibu wa ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania (1977) inaeleza wazi kuwa ili mtu ateuliwe kuwa mgombea ubunge ni lazima awe na sifa zifuatazo; 
(i) Awe raia wa Tanzania (ii) Awe ametimiza umri wa miaka ishirini na moja (iii) Awe anajua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza (iv) Awe ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa (v) Awe hajatiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi. 
Aidha, Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977; hata kama mtu ana sifa zote za kugombea hataruhusiwa kugombea Ubunge kama ;
(i) Ni raia wa nchi nyingine; au (ii) Kwa mujibu wa Sheria iliyotumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili; au (iii) Amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda usiozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au (iv) Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa Umma; au 
(v) Siyo mwanachama na siyo Mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; au (vi) Ikiwa mtu huyo ana maslahi yoyote katika mikataba na serikali ya Jamhuri ya Muungano au serikali ya mapinduzi Zanzibar wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalumu kwa mujibu washeria iliyotungwa na Bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo; au (vii) Ameshika madaraka ya Afisa Mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa madaraka ambayo Rais anaweza au anatakiwa kukabidhi kwa Mbunge kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, au sheria iliyotungwa na Bunge; au (viii) Kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote, mtu huyo amezuiliwa kuandikishwa kama Mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge. (ix) Ni mgombea Urais /Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    Aidha, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 5.3 kimeweka masharti ya Uteuzi wa Mgombea Ubunge na kuweka kama ifuatavyo;
(i) Awe amedhaminiwa na wapiga kura wasiopungua ishirini na tano waliojiandikisha kupiga kura katika Jimbo hilo. (ii) Mgombea haruhusiwi kujidhamini yeye mwenyewe (iii) Awe na dhamana ya shilingi 50,000/= (iv) Awe ametoa tamko la kisheria mbele ya hakimu kwamba anazo sifa zinazotakiwa ili kugombea Ubunge Vilevile, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 6.0 kimeweka utaratibu wa Pingamizi dhidi ya uteuzi wa Mgombea Ubunge: Na Kifungu cha 6.3, kimeweka sababu za kuweka Pingamizi kuwa ni: (i) Maelezo yaliyopo katika fomu ya uteuzi hayatoshi kumtambulisha Mgombea; (ii) Fomu ya Uteuzi haitimizi au haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sharia; (iii) Kutokana na maelezo yaliyoandikwa katika fomu ya uteuzi ni dhahiri kwamba Mgombea uchaguzi hana sifa zinazotakiwa; 
(iv) Uthibitisho wa Msimamizi wa Uchaguzi unaopaswa kutolewa haukutolewa; (v) Mgombea hana sifa zote zinazotakiwa; (vi) Hakuna uthibitisho kuwa Mgombea amelipa dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=); na (vii) Hakuna picha ya Mgombea. (viii) Mgombea hakujaza fomu Na.10 kuthibisha kuwa ataheshimu na kutekeleza maadili ya Uchaguzi. Baada ya utangulizi huo hapo juu ambao unaonyesha dhahiri kuwa hapakuwa na sababu yoyote ya mimi kuwekewa pingamizi na Mgombea ubunge wa Chama cha CUF, kwani hakufuata masharti ya Katiba, Sheria na maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kwetu kama wagombea, kwani aliamua kutunga mambo ambayo yapo nje ya utaratibu na hayakidhi haja, hayakufuata Katiba, matakwa ya kisheria na hata maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Nayasema yote haya kutokana na ukweli kuwa mimi nimekidhi sifa zote za kuwa Mgombea Ubunge na nimetimiza masharti yote yaliyowekwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na barua yako ya tarehe 13 Machi, 2014 yenye kumbukumbu namba HWB/E.50/21/76 nalazimika kujibu pingamizi hilo kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya Uchaguzi sura Na.343 kifungu Na.40 (5) kuhusu pingamizi, hata kama halina nguvu kwa mujibu wa katiba, sheria na maelekezo ya Tume ya taifa ya uchaguzi hoja kwa hoja kama ifuatayvo.
MAJIBU YA HOJA ZA PINGAMIZI LA FABIAN LEONARD SKAUKI: 
1. HOJA YA KWANZA; Kwamba mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimejaza taarifa za uongo kwenye fomu zangu kuwa kazi ninayoifanya ni BIASHARA na kusema kuwa ni taarifa za uongo kwa kuwa sikuweka vielelezo vya kuonyesha kuwa mimi ninafanya kazi hiyo, na kuwa sijulikani ninafanya kazi gani .
MAJIBU YA HOJA YA KWANZA : Pingamizi na sababu zilizotolewa na Mgombea wa chama cha wananchi CUF Bwana Fabian L.Skauki hazina mashiko na kuwa yeye ameamua kukupotosha kuwa mimi sio mfanyabiashara kwa kuwa sikuweka vielelezo, japo ni wazi kuwa sikupaswa kuweka vielelezo vyovyote kwani fomu haikuwa inanitaka kuweka vielelezo vya aina yoyote kama ambavyo hata yeye hakuweka vielelezo kuwa anafanya shughuli gani. Ninasikitika kuwa hata wewe Msimamizi umekubaliana na hoja hii dhaifu ya pingamizi na kunitaka mimi kuijibu wakati unajua wazi kuwa haina mshiko wala mantiki kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. Naambatanisha leseni yangu ya Biashara yenye jina langu namba B.No. 01299270 iliyotolewa tarehe 19/09/2011 na huo ni uthibitisho kuwa mimi ni mfanya biashara (kielelezo A) 
2.HOJA YA PILI: Kwamba, mimi Mathayo Torongey sijui kusoma wala kuandika Kiswahili au Kiingereza, na kwamba nimedanganya na hivyo sina sifa za kuwa Mgombea Ubunge. 
MAJIBU YA HOJA YA PILI; Kwanza, nieleze wazi kuwa nimesikitishwa sana na tuhuma hizi ambazo zina lengo la kunichafua mbele ya jamii na Taifa kwa ujumla, zina lengo la kuichafua jamii ya watanzania kutoka familia za wakulima na wafugaji, watu ambao wana kipato kidogo na ambao wanaishi vijijini kuwa ni watu wa hovyo na hawajui kusoma wala kuandika, ni tuhuma za kuwadhalilisha watanzania ambao ni kutoka jamii za wananchi wa vijijini wanaotafuta fursa ya kuchaguliwa kwamba ni watu wa wanaoomba nafasi wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, kwa kweli nasikitika sana kwa hili na lilikuwa tusi ambalo msimamizi wa uchaguzi hukupaswa kulipokea. Aidha, nashindwa kutoa ushahidi hapa kwani hata wewe umeziamini tuhuma hizi kuwa mimi sijui kusoma wala kuandika na ndio maana ukanitaka nizijibu, japo ni ukweli ulio wazi kuwa sahihi yangu kwenye fomu haikuwa ya "kuweka dole gumba" niliweka sahihi kwa kuandika na mbele yako na sikuandikiwa. Pili; Yafaa mgombea huyu pamoja na wale wote waliomtuma wakatoa ushahidi wake kwako kuwa mimi Mathayo Mang'unda Torongey sijui kusoma wala kuandika, na hii itamsaidia kuaminika mbele ya jamii ya wananchi wa Chalinze ambao anataka kuwaongoza. Hata hivyo naomba nitoe majibu mbele yako kwa maandishi na kwa kusoma kitu ambacho wewe utataka nisome na kuandika ili uwe uthibitisho kwako kuwa najua kusoma na kuandika . 
3. HOJA YA TATU: Kwamba, mimi Mathayo Torongey nimedanganya kwa kughushi/kufoji sahihi za wadhamini walionidhamini kuwa Mgombea na kuwa sahihi zote zimefojiwa na hazifanani na zile zilizokuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuwa sahihi zote hizi zimesainiwa na mtu mmoja ambaye sio mhusika . 
MAJIBU YA HOJA YA TATU: Kwanza, nieleze wazi kuwa nilipokamilisha kujaza fomu zangu na kudhaminiwa na wadhamini 25 kwa mujibu wa sheria , nilikuja ofisini kwako na tukakagua kwa pamoja majina ya wadhamini wote waliokuwepo kwenye fomu zangu na nilikuja na shahada zote za wapiga kura ambao walinidhamini na wewe ulizikagua na kuridhika kuwa walikuwa ni wapiga kura sahihi na saini zao zilikuwa sahihi na uliandika hilo kama uthibitisho wako kwenye fomu zangu za uteuzi na ndio maana uliniteua kuwa mgombea . Pili, Namshangaa mweka Pingamizi kwa kuja na tuhuma kuwa saini za wapiga kura zinatofautiana na saini zilizoko kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura ,hii ni kutokana na ukweli kuwa kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura hakuna saini za wapiga kura isipokuwa saini zipo kwenye vitambulisho vya wapiga kura, na vitambulisho hivyo niliviwasilisha kwako na wewe kama msimamizi wa uchaguzi baada ya kukagua vitambulisho hivyo uliridhika kuwa saini za wadhamini wangu zilikuwa sahihi na ndio maana uliniteua kuwa Mgombea na kuweka "uthibitisho wako" katika kifungu F. kwa maandishi kwenye fomu zangu za uteuzi. Naomba kunukuu maelezo yako uliyoyaandika kwenye fomu yangu ya uteuzi tarehe 12.03.2014 saa 9.05 Alasiri kama ifuatavyo; 
‘(i) Nimekagua majina yote ya waliomdhamini mgombea aliyetajwa hapa naninathibitisha kwamba wote wameandikishwa kuwa wapiga kura katika Daftari la kudumu la wapiga kura katika Jimbo la Chalinze' Tatu, Mweka pingamizi anatakiwa kuthibitisha kwako kuwa saini hizo zimeghushiwa kwani ni ukweli ulio wazi kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kughushi ni kosa la Jinai na hivyo ushahidi wake huo unaweza kuwasilishwa mbele ya vyombo vya dola kwa hatua zaidi. Nne, mweka pingamizi ana wajibu wa kuthibitisha kuwa saini hizo zinafanana zote kwani ni ukweli uliowazi kuwa saini za wadhamini wangu hazifanani kutokana na kuwa wapo wadhamini ambao waliweka "dole gumba" kuthibitisha saini zao na wengine
walisaini kwa maandishi, sasa kufanana anakosema ni kwa aina gani? Kwamba alama ya dole gumba ina fanana na saini ya kuandika?! Tano, yafaa mweka pingamizi na wale wote ambao walishirikiana naye kuweka hoja hii katika pingamizi hili kujitokeza na kueleza kwa uwazi lengo la kuweka pingamizi hili ambalo ni la kutungwa na lenye nia ovu dhidi yangu, Chama changu na Wananchi wote wa Jimbo la Chalinze. 
4. HOJA YA NNE; Hoja ya mweka pingamizi iliyonihusu mimi Mgombea wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ilidai kuwa nimeshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake nimedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura halali wa jimbo la CHALINZE, na kwamba Taarifa zao na namba zilizojazwa hazifanani. Hivyo nabakiwa na wadhamini halali 21 ambao kisheria hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria. Majina ya wadhamini hao ambao hawakidhi matakwa ya kisheria na namba zao kutajwa kuwa ni:- 
1. HABIBU ALLY SAIDI - 16886275 2. MOHAMMED RAMADHANI - 30376567 3. ABDULKADIR ALLY - 49264905 4. SHABANI SULEYMAN - 16984045 5. JUMA MRISHO - 48759563 6. RAJABU ALLY - 16872368 7. MANENO MIRAJI - 16872059 
MAJIBU YA HOJA YA NNE (4). Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimekidhi vigezo na masharti ya wadhamini wote 25 wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria kama nilivyo orodhesha kwenye fomu ya wadhamini na hivyo basi pingamizi namba nne lililowekwa na mgombea ubunge wa chama cha The Civic United Front (CUF) Kuwa Bwana HABIBU ALLY SAIDI mwenye namba 16886275 kuwa sio mdhamini halali, nikiri kuwa ni kweli sio mdhamini wangu halali; Mdhamini wangu halali ni Bwana HABIBU ALLY DAUDI mwenye namba 16886275. Na vilevile ni kweli kwamba Bwana MOHAMMED RAMADHANI mwenye ‘30376567' si mdhamini wangu halali, Mdhamini wangu halali ni Bwana MOHAMMED RAMADHANI mwenye namba 30576567. 
Pia napenda kukuthibitishia bila chembe ya shaka kuwa Bwana ABDULKADIR ALLY mwenye namba 49264905 aliyezaliwa wilaya ya Bagamoyo tarehe 17/04/1974 ni mdhamini wangu halali aliye andikishwa tarehe 02. 03. 2010 kwenye kituo cha shule ya msingi Mkoko kata ya Msata halmashauri ya Bagamoyo mkoa wa Pwani. Hata hivyo amesema Bwana SHABANI SULEYMAN mwenye namba 16984045 si mdhamini wangu halali, Napenda kuthibitishia kuwa mdhamini wangu halali ni Bwana SHABANI SELEMANI mwenye namba 16984045 na si Bwana SHABANI SULEYMAN. Hata hivyo, nadhibitisha kuwa Bwana JUMA MRISHO mwenye namba 48759563, aliyesema sio mdhamini wangu halali ni halali kwani amezaliwa tarehe 04.04.1981 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Msinune halmashauri ya Bagamoyo mkoa wa Pwani na shahada yake ya kupigia kura imeandikishwa kwenye kituo cha shule ya msingi Msinune, hivyo ni mdhamini wangu halali na amekidhi vigezo vya kunidhamini sawa na Bwana RAJABU ALLY mwenye namba 16872368 aliyezaliwa tarehe 28.09.1979 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Kiwangwa mkoa wa Pwani naye ni mdhamini halali aliyejiandikisha kwenye kituo cha Kibaoni ofisini; Kama ilivyo kwa mdhamini halali Bwana MANENO MIRAJI mwenye namba 16872059 aliyezaliwa wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa mkoa Pwani na kaandikishwa kituo cha Kibaoni Ofisini. 
Muweka pingamizi angekuwa sahihi Kama ningekuwa sijatoa uthibitisho kwa msimamizi wa uchaguzi. Hoja yake ingekuwa na uzito unao bebwa na kifungu 6.3 (iv) kwenye kitabu cha tume ya taifa ya uchaguzi cha maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa urais, ubunge na madiwani kinasema, "Uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi unaopaswa kutolewa haukutolewa". Lakini kwenye fomu namba 88 F ukurasa 8, "UTHIBITISHO WA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI" msimamizi wa uchaguzi kwenye F( i) amekiri kukagua na kuthibitisha ya kuwa wadhamini wote walioandikishwa kuwa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jimbo la CHALINZE ni halali. 
Kwa maana hiyo, udhibitisho wa msimamizi wa uchaguzi ni kwamba wadhamini wangu ni halali hivyo hoja ya muweka pingamizi kwenye swala la wadhamini haina mashiko na msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kupokea pingamizi hilo bali alipaswa kulitupa kabla ya kufikiria kulileta kwangu. Hata hivyo, nichukue fursa hii adhimu kumuelimisha muweka pingamizi wa chama cha wananchi CUF (Civic United Front) ya kuwa majina yanaweza kufanana kwenye kituo kimoja au kituo kingine ama kata nyingine au wilaya na mkoa mwingine lakini namba ya kadi halali ya mpiga kura haiwezi kufafana na kadi ya mpiga kura mwingine halali, kwa mfano kwenye kituo 00006347 kata ya Bwilungu jimbo la CHALINZE wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani mpiga kura HAMZA ATHUMANI mwenye shahada namba 17023223 anafanana jina na HAMZA ATHUMANI mwenye shahada namba 1702107 sawa na Bwana BONELA SHABANI MADEGA mwenye shahada namba 19534653 na BONELA SHABANI MADEGA mwenye shahada namba 19525475. Hawa wote wakitazamwa kwa majina kwa jicho la muweka pingamizi wa CUF wataonekana ni mtu mmoja au ni mapacha wakati uhalisia ni watu tofauti wanao tofautishwa na namba za shahada zao halali za kupigia kura. 
5. HOJA YA TANO; Kuwa Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimedanganya Uraia wangu na kuwa mimi sio Mtanzania wa kuzaliwa kwa kuwa sikuweka vielelezo vyovyote halali. 
MAJIBU YA HOJA YA TANO; Napenda kurudia kuwa huenda mweka pingamizi ameamua kukupotosha na kuandika taarifa za uongo kwa lengo ambalo yeye na wale wote waliomtuma wanalijua wao. Napenda kurudia kuthibitisha kama nilivyoandika kwenye fomu zangu za kuomba uteuzi kuwa mimi ni mzaliwa wa Kijiji cha Kaloleni katika Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania . Naomba kuweka kielelezo "B" kuthibitisha uraia wangu wa Kuzaliwa kama ifuatavyo; 1. Naweka nakala ya kitambulisho changu cha kuandikishwa kuwa mpiga kura katika Jimbo la Ubungo chenye namba *46670962*. Na kwa mujibu wa sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 , kifungu cha 10 (1) ‘sifa na kukosa sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura na kupiga kura' kinasomeka ‘Hakutakuwa na mtu zaidi ya raia wa Tanzania ambaye ametimiza umri wa miaka kumi na nane na ambaye hajapoteza sifa kwa masharti ya Sheria hii au sheria nyingine yoyote ya Bunge atakayestahili kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa mujibu wa masharti ya sheria hii' Hivyo kwa kuwa nimekidhi vigezo vya kuwa mpiga kura ,mimi ni raia halali, naambatanisha nakala ya shahada yangu ya Mpiga kura kama kielelezo ‘C'. 
Aidha, ukisoma majibu ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na wagombea wa CHADEMA dhidi ya uraia wa wagombea wa CCM Sioi Sumari 2012 na Godfrey Mgimwa 2014 katika majimbo ya Arumeru Mashariki na Kalenga ,Tume iliamua kuwa jukumu la kuthibisha /kutoa vielelezo kuhusu tuhuma za uraia wa mgombea ni kwa mtoa tuhuma (who allegies must prove), hivyo mweka pingamizi atakiwe kuwasilisha vielelezo vya tuhuma zake kwako ili kuthibitisha madai yake kuhusu uraia wangu. 
HITIMISHO
Baada ya maelezo tajwa hapo juu na uthibitisho ambao nimeuwasilisha kwako naomba kukujulisha kuwa mimi nina sifa zote kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgombea halali wa ubunge jimbo la Chalinze na yafaa ukatupilia mbali pingamizi lililowekwa dhidi yangu kama jinsi ambavyo ulipaswa kulitupilia mbali kabla hujalileta kwangu kwani lilikosa sifa na vigezo vya kuwa pingamizi. 
………………………………… 
Mathayo Mang'unda Torongey 
Mgombea Ubunge wa CHADEMA jimbo la CHALINZE. 
14 Machi, 2014.

Posted By Unknown03:06

TUME YATOA UFAFANUZI KUHUSU DAFTARI LA WAPIGA KURA LITAKALOTUMIKA KATIKA UCHAGUZI JIMBO LA KALENGA

Filled under:

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva akisoma taarifa ya tume mbele ya waandishi wa habari inayohusu ufafanuzi kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura litakalotumika  katika uchaguzi wa ubunge jimbo la Kalenga,kulia kwake ni Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Himid Mahamoud Himid na upande wa kushoto ni Mkurugenzi wa Uchaguzi Julius Malaba.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva akibadilishana mawazo kabla ya kujibu swali kwa waandishi wa habari ambao waliuliza kuhusu mambo mbali mbali yanayohusiana na daftari la kudumu na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Himid Mahamoud Himid.
Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Jaji John Joseph Mkwawa akizungumzia suala zima la vyama kuwa makini siku ya kupiga kura kwani hakutotakiwa kuwe na alama ama kielelezo cha chama fulani katika siku hiyo,kushoto kwake ni Profesa Amon Chaligha .
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva akijadiliana suala la takwimu za daftari la kupiga kura pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndugu Julius Malaba na Dk.Sist Cariah Naibu Katibu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Tehama ambapo wapiga kura ambao taarifa zao zimetokea zaidi ya mara moja  waliondolewa kwenye daftari hilo na ni wapiga kura hao kwa idadi ni 142.
Baadhi ya maofisa wa Tume ya Uchaguzi wakisikiliza kwa makini kikao cha Tume ya Uchaguzi na Waandishi wa habari wakati wa kutoa taarifa juu ya daftari la kudumu litakalotumika kwenye uchaguzi wa ubunge Kalenga siku ya tarehe 16 Machi 2014 ambapo taarifa za uhakiki zilizofanyika  zilikuwa 149 tu na wapiga kura walioongezeka  katika daftari lililotumika  katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 ni 7 tu na sio 600 kama ilivyoripotiwa na vyombo mbali mbali vya habari.

Posted By Unknown02:59

Thursday, 13 March 2014

SAMIA SULUHU HASSAN NDIYE MAKAMU MWENYEKITI BUNGE LA KATIBA

Filled under:

 
Samia Suluhu Hassan


Samia Suluhu Hassan ndiye Makamu Mwenyekiti wa Kudumu Bunge Maalum la Katiba baada ya kupata kura 390 sawa na 74% na kumshinda mpinzani wake Amina Abdallah Amour aliyepata jumla ya kura 126 sawa na 24%. Kwa matokeo hayo, Samia Hassan ataungana na Samuel Sitta aliyechaguliwa jana kuwa Mwenyekiti wa Kudumu wa bunge hilo katika mchakato mzima wa kupata katiba…

Posted By Unknown12:54

TAARIFA YA PINGAMIZI DHIDI YA MGOMBEA WA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE

Filled under:

 
TAARIFA YA PINGAMIZI LA MGOMBEA WA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE

FABIAN LEONARD SKAUKI – MGOMBEA CHAMA CHA WANANCHI – CUF

DHIDI YA

MATHAYO MANG’UNDA TORONGEY – MGOMBEA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO - CHADEMA

13.03.2014

Mimi FABIAN L. SKAUKI, mgombea ubunge wa uchaguzi mdogo jimbo la CHALINZE kwa Ticket ya THE CIVIC UNITED FRONT (CUF) ninamwekea Pingamizi mgombea wa chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba amepoteza sifa za kuwa mgombea kwa sababu zifuatazo.

Ndugu MATHAYO. M. TORONGEY amejaza Taarifa za uongo kwenye Fomu yake kwamba kazi
 anayoifanya ni BIASHARA. Sio kweli, kwa sababu hajaweka vielelezo vya yeye kufanya hiyo kazi. Hajulikani anafanya kazi gani.

Ndugu MATHAYO .M. TORONGEY amejaza katika fomu kwamba anajua kusoma na kuandika
Kiswahili na kiingereza. Taarifa hizi ni za uongo, mgombea huyu hajui kusoma wala kuandika Kiswahili wala kiingereza, na kwamba amedanganya na amepoteza sifa za kuwa mgombea.

Ndugu MATHAYO .M.TORONGEY amedanganya kwa kughushi/kufoji sahihi za wadhamini,ambao amewaorodhesha kwenye fomu ya kuomba kuthibitishwa kuwa mgombea. Ambapo katika fomu hizo wadhamini wote sahihi zao zimefojiwa na hazifanani na zile zilizokuwepo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba sahihi zote hizi zimesainiwa na mtu mmoja ambaye sio muhusika. Hivyo anapoteza sifa ya kuendelea kuwa mgombea.

Ndugu MATHAYO.M.TORONGEY ameshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake amedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura halali wa jimbo la CHALINZE, na kwamba Taarifa zao na namba zilizojazwa hazifanani.

Hivyo anabakiwa na wadhamini halali 21 ambao kisheria hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria.

Majina ya wadhamini hao ambao hawakidhi matakwa ya kisheria na namba zao ni

JINA LA MDHAMINI *NAMBA YA KADI KURA*

HABIBU ALLY SAIDI * 16886275*

MOHAMMED RAMADHANI *30376567*

ABDULKADIR ALLY *49264905*

SHABANI SULEYMAN *16984045*

JUMA MRISHO *48759563*

RAJABU ALLY *16872368*

MANENO MIRAJI *16872059*

Wananchi wenye namba na majina hayo hapo juu waliojazwa kama wadhamini kuanzia namba 1 hadi 7 kwenye fomu yake hawana sifa za kupiga kura kwenye maeneo ambayo wamejazwa wanatokea.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba idadi halali ya wadhamini wanaobaki ukiwaondoa hao saba watabaki 21, hawakizi vigezo vya kuwa wadhamini.

Ndugu MATHAYO.M.TORONGEY amedanganya Uraia wake, na kwamba yeye si Mtanzania wa kuzaliwa ndio maana hana vielelezo halali vinavyohusu uraia wake. Hivyo anakosa sifa ya kuwa mgombea.

Hivyo ninaomba Tume ya Uchaguzi kutengua uteuzi wa mgombea wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ndugu MATHAYO.M.TORONGEY kwa kuwa anakosa sifa za yeye kuendelea kuwa mgombea.

Wako katika ujenzi wa Taifa

FABIAN LEONARD SKAUKI

……………………………………………………..
MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE.
 THE CIVIC UNITED FRONT

Posted By Unknown10:06