Bunge
Maalumu la Katiba sasa lipo katika hati hati ya kuendelea kutokana na
viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutangaza kuwa
hawatakuwa tayari kujadili rasimu tofauti na iliyowasilishwa na Jaji
Joseph Warioba bungeni.
Wakizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa
bungeni, viongozi wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia,
Freeman Mbowe na Tundu Lissu, walisema wataitetea rasimu hiyo, ndani ya
Bunge na kwenye Kamati.
“Rais Jakaya
Kikwete amekuja bungeni siyo kufungua Bunge la Katiba bali kaja na
mapendekezo ya rasimu ya CCM, sisi tutajadili rasimu ya wananchi ya Jaji
Joseph Warioba ambayo inazungumzia muundo wa Muungano wa Serikali
tatu,” alisema Profesa Lipumba.
Kutokana na
msimamo huu wa Ukawa huenda Bunge litakwama kwani kwa mapendekezo ya CCM
yenye Muundo wa Muungano wa Serikali mbili ni lazima kuandikwa upya
Rasimu ya Katiba au kufanyika mabadiliko makubwa.
Profesa
Lipumba alisema katika majadiliano juu ya rasimu, Ukawa watajikita
kutumia Rasimu ya Katiba waliyopewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
ambayo imeeleza mapendekezo kwa nini yamefikiwa katika kila hoja,”
alisema.
Hata hivyo,
alisema wamesikitishwa sana na Rais Jakaya Kikwete, badala ya kufungua
Bunge alijikita katika kuchambua rasimu na kuikosoa tume aliyoiunda
mwenyewe.
“Rais Jakaya
Kikwete siyo tu amemdhalilisha Jaji Warioba pamoja na wajumbe wa Tume,
bali amewadhalilisha wananchi waliotoa maoni kwani hata takwimu alizotoa
za kupinga rasimu siyo za kweli,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema
muundo wa Serikali tatu ndio mawazo ya wananchi ambayo yamekusanywa na
watu wenye heshma wakiwapo Jaji Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na
Makamu wa Rais na Jaji Augustino Ramadhani ambaye pia amewahi kuwa Jaji
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Alisema
kauli za Rais badala ya kuimarisha umoja zimewagawa Watanzania kwani
ametoa vitisho ambavyo havina sababu hasa kwa Wapemba bila kujua kuna
Wanyamwezi wanaoishi Zanzibar.
Mbatia
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo,
alisema kwa kauli ya juzi ya Rais Kikwete, kutangaza kuwapatia Zanzibar;
watu, ardhi, mamlaka kamili na kusimamia uhusiano wa kimataifa ni
kuvunja rasmi Muungano,
Mbatia
alisema Rais Kikwete pia amewagawa Watanzania katika kauli zake ikiwa ni
pamoja na ile ya Wapemba kwa kulima vitunguu katika Jimbo la Kibakwe
kana kwamba ni makosa.
Alisema
wamesikitishwa na Rais kuacha kufungua Bunge badala yake katumia taarifa
potofu za mitaani kuligawa Bunge na kuwadhalilisha wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Hakuna
asiyejua sasa tupo katika mgogoro mkubwa wa kikatiba, Zanzibar tayari ni
nchi kamili kutokana na mabadiliko ya 10 ya katiba yao waliyoyafanya
mwaka 2010 baada ya kupitisha dhana ya kuwa Zanzibar ni nchi,” alisema.
Mbowe
Mbowe
alisema Rais amevunja maridhiano na hata kushindwa kusikiliza maoni ya
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Seneta Amos Wako kuwa maoni ya
wananchi yaheshimiwe.
Alisema
Serikali ya Kenya ilichakachua maoni, ilichakachua rasimu na kusababisha
vurugu kubwa jambo ambalo linaweza kutokea kwa Tanzania.
“CCM wasijidanganye kwa wingi wao bungeni hakika katika hili tutatetea madai na maoni ya wananchi hadi mwisho,” alisema
0 comments:
Post a Comment