MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombere-Mwiru, alisema
kuwa aliwahi kuvuliwa wadhifa wa ukuu wa mkoa kwa sababu ya kutofautia
kimtazamo na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kingunge ambaye anawakilisha kundi la waganga wa tiba asili,
alikumbushia tukio hilo juzi katika semina ya waandishi wa habari
iliyofanyika mjini hapa katika Ukumbi wa Msekwa, naye akiwa mmoja wa
watoa mada.
Akijibu swali la mwandishi wa gazeti hili la kwanini amegeuka
mlalamishi wa kukosoa viongozi wenzake wa sasa wakati amekuwa sehemu ya
serikali kwa awamu zote nne bila kutimiza wajibu wake, Kingunge alisema
kuwa amekuwa akikosoa na wakati fulani iliwahi kumgharimu.
“Wakati fulani nikiwa mkuu wa mkoa, nilipingana na Mwalimu Nyerere
nikikataa katiba isibadilishwe kwa manufaa ya watu fulani, basi
nikafukuzwa ukuu wa mkoa. Hivyo si kweli kwamba sikukosoa, hata sasa
naendelea,” alisema.
Katika mada yake kuhusu mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya, alisema
kuwa nchi zinazopata fursa ya kuandika upya katiba zake, zinapaswa
kujikita kuandika katiba bora zitakazoweza kuwa na misingi ya kukuza
uchumi wa kujitegemea.
“Maisha yetu yameegemea uamuzi wa wenzetu. Tumepigania uhuru ili
tujitawale lakini bado ni tegemezi na kama nchi iko hivyo halafu nafasi
ya kuandika Katiba mpya inakuja mnapanga safu za vyeo haina maana,”
alisema
0 comments:
Post a Comment