Friday, 14 February 2014

JE UNAELEWA CHANZO CHA VALENTINE'S DAY NA NINI UNATAKIWA UFANYE

Filled under:



Februari 14 kila mwaka, dunia nzima imekuwa ikisherehekea Siku ya Wapendanao, maarufru kama ‘Valentine’s Day’, kwa wengi wao kutumiana zawadi za maua, kadi na nyinginezo, ambazo hufungwa ndani ya maboksi mekundu.

Katika miaka ya karibuni, sikukuu hii imepata umaarufu zaidi nchini kwa kuifanya kuwa sherehe kubwa, ingawa bado haijatambuliwa kitaifa lakini imeonekana kuwagusa watu wengi.

Katika makala hii tungependa kuzungumzia kwa undani kuhusu sikukuu hii, ikiwamo historia na namna ambavyo inatakiwa kusherehekewa na makosa yanayofanywa katika sherehe hii kwa kizazi cha sasa.

Historia yake
Mwanzo wa kuanza kuisherehekea sikukuu hii ilikuwa ni karne ya tano, ambako Kanisa Katoliki lilieleza nia yake ya kutaka kumaliza ukuaji wa mila za wapagani ambazo wananchi wa Roma walikuwa wakizisherehekea kila mwaka tangu karne ya nne BC.

Kutokana na mila za Waroma wakati huo, walikuwa wakifanya siku ya Februari 14 aina ya kamari maalumu waliyokuwa wakiwashirikisha vijana wao wa kike na wa kiume kwa ajili ya kupeleka zawadi kwa ‘mungu wao’ waliyekuwa wakimuita kwa jina la Lupericus.

Hivyo vijana wa kike walishiriki katika kamari hiyo kwa kuweka majina yao kwenye kiboksi na kasha la vijana wa kiume na baada ya kufanya hivyo vijana wa kiume walitakiwa kuchagua majina hayo na msichana aliyebahatika kuchaguliwa na mvulana fulani, hapo huwa na mvulana huyo kwa mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi chote cha mwaka mzima hadi kamari ya mwaka unaofuata.

Kanisa halikufurahishwa kabisa na mpango huo wa kiibada za Waroma ambazo zilikuwa na nia ya kufanya mapenzi kiholela kupitia kamari na likaamua kutokomeza mila hiyo kwa kuchagua ‘mpenzi’ ambaye huozeshwa badala ya mila ya kamari ya ‘mungu Lupericus’.

Ili kufanikisha hilo, kanisa likamchagua Askofu Valentine, mtu ambaye alihukumiwa kuuawa katika karne ya 3 AD kutokana na kukaidi amri ya mtawala (Emperor Claudius).

Mtawala huyo alipiga marufu watu kuoa kwa madai kuwa wanaume wanaooa wanafanya vibaya vitani na wakati mwingine huwa hawataki kuacha familia zao na kwenda vitani.

Askofu Valentine alikuwa akipinga amri hiyo na badala yake alikuwa akiwaalika na kuwafungisha ndoa kwa siri wale waliokuwa wakihitaji kufanya hivyo.

Baada ya kubainika kufanya hivyo kisiri, aliuawa na kabla ya kuuawa alituma ujumbe wa mapenzi kwa binti wa mlinzi wa jela aliyewahi kuwa na mahusiano naye ya kimapenzi.

Ujumbe wake ulikuwa ukisomeka kwamba: ‘Kutoka kwa Valentine wako (from your Valentine)’.
Barua hiyo ilipata umaarufu na neno hilo likatumiwa na Kanisa Katoliki na kuchagua Askofu Valentine awe mfano wa kuigwa kwa wapendanao na kutokemeza ibada za kipagani za kufanya mapenzi kiholela kwa kuchagua mwanamke kwa njia ya kamari na badala yake wakishapendana wafungishwe ndoa.

Lakini kutokana na nidhamu ya kidemokrasia kuibuka katika nchi zao na watu kuacha mafunzo ya kidini na kuburuzwa na fikra za ‘uhuru’, siku hiyo ikawarejesha kule kule katika zama za wapagani kwa kuhamasisha uchafu wa zinaa nje ya ndoa.

Makosa yanayofanywa kuisherehekea
Pamoja na makusudio hayo, lakini kwa sasa kumekuwa na makosa ambayo yamegunduliwa kufanyika katika sherehe hii ambayo ni maalumu kwa wapendanao kuzidisha upendo.
Katika sikukuu hii wanaume hasa ndio wamekuwa wanaelezwa kufanya makosa ambayo wameyaona ya kawaida kwao bila ya kujali yanaathiri mahusiano yao kwa kiasi gani.

Kosa la Kwanza: Kutozungumza maneno ya hekima
Hakikisha katika siku hii unazungumza maneno ya busara ikiwa ni pamoja na kumwandikia meseji mpendwa wako za kumfurahisha kwani katika uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa wanawake wengi wanapenda kuzawadiwa kadi na kuandikiwa maneno mazuri ya mapenzi huku wakiwa sambamba na wapendwa wao.

Pili: Uchaguzi wa zawadi
Mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya mapenzi, Dk. Terri Orbuch, anasema zaidi ya asilimia 75 ya wanawake wamekuwa wakipenda kupewa zaidi. Lakini wanaume wengi wamekuwa wakishindwa kuwanunulia zawadi kutokana na fikra potofu wakidhani zawadi nzuri ni kubwa peke yake ndiyo itaweza kumpatia heshima.
Wanafikiria zawadi ni lazima ununue vitu kama magari au vito vya thamani na kumbe wanawake hufurahia zawadi za kawaida kama chocolate, kadi na maua ikiwa ni pamoja na kuambiwa maneno matamu ya kimahaba.
Ni vizuri katika siku hii kwenda dukani na kumnunulia mpendwa wako zawadi za maua mazuri, vitabu vya mahaba, DVD za mapenzi, mishumaa, chocolates na nyingine za aina hiyo.

Yakupasayo kuyafanya
Jitahidi kuonyesha tabasamu lako unapokuwa na mpenzi wako na kununua zawadi za kawaida, kwani hii humsaidia mpenzi wako hasa yule asiyekuwa na uwezo naye kukununulia kama hiyo, kwani wengi wamekuwa na mtindo wa kurudisha zawadi inayofanana na ile uliyomnunulia.
Tahadhari nyingine kwa siku hii ni kuepuka kumuonyesha mwenzako mambo ambayo unajua yataleta maudhi kwake, hivyo kufanya siku hiyo kuwa mbaya kwenu.
Suala la kuchati kwa wapendanao siku hii ni muhimu ambako linasaidia kuongeza upendo kwa wawili na hii haijalishi ni njia gani unaitumia iwe kutuma meseji za simu au barua pepe za mtandaoni au unaweza kutumia mitandao ya Facebook na Twitter, hii itamfariji hata yule aliye mbali nawe.
Wakati mwingine unaweza kutumia barua ambayo itakuwa na maneno mazuri, ikiwa sambamba na picha ambayo nyuma yake ukiwa umeiandika ujumbe mzuri wa kimahaba ikiwa ni pamoja na CD iliyojaa nyimbo za mapenzi ili asikilize ukiwa umempatia kama zawadi.

Namna ya uvaaji
Siku hii pia ina namna yake ya kuvaa ambapo kwa mwanamke ni vema ukavaa gauni jipya na fupi ambalo litamvutia mwenzio huku mwanamume yeye akitakiwa kuvaa suruali ya kitambaa na shati la mikono mirefu au mifupi na si vibaya kama utavaa tai ndogo. Pia si vibaya kuvaa suti.

0 comments:

Post a Comment