Uchaguzi wa mdogo wa
Jimbo la Chalinze umefanyika huku ukigubikwa na kasoro kadhaa, ikiwa ni pamoja
na watu wachache kujitokeza vituoni kupiga kura, wapiga kura kulalamika
‘kupokwa’ vitambulisho vyao, vituo kuwa majumbani kwa watu, huku pia kukiwa na
hofu ya vurugu.
Kasoro hizo
zilijidhihirisha jana wakati wapiga kura shughuli ya upigaji kura ilipokuwa
ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ambapo wananchi wa Chalinze
walikuwa wakipiga kura mbunge wao, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa
mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki mapema mwaka huu.
Gazeti hili liliweza
kuzunguka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura ambapo lilishuhudia idadi ya
watu wachache wakiwa wamejitokeza kutimiza haki na wajibu wao wa kikatiba wa
kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Katika kituo cha
kupigia kura, Ofisi ya Maji Changa namba 2, hadi muda wa kufunga vituo ukiwa
umebakia nusu saa, walikuwa wamejitokeza wapiga kura 75 kati ya 328
walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Kituo hicho, kilikuwa miongoni
mwa vituo kadhaa vilivyokuwa majumbani mwa watu, kikiwa katika nyumba ya Mzee
Issa Mbogo, kinyume cha sheria ya uchaguzi.
Katika kituo cha
Tukamisasa hadi muda wa kufunga vituo ukiwa unakaribia mwisho, yalikuwa
yametukika madaftari mawili pekee, kati ya madaftari sita ambayo yalipaswa kuwa
kituoni hapo, ambapo kila daftari linajumuisha wapiga kura 50.
Mbali ya vituo kama
hivyo ambavyo viko maeneo ya vijijini, hata vituo vilivyokuwa kata za mjini
kama Builingu, pia hazikuwa na wapiga kura wengi.
Mathalani Kituo cha
Ofisi ya Mtendaji Namba 2; waliopiga kura walikuwa 64 kati ya wapiga kura 383,
Namba 3; waliopiga kura ni 62 kati ya 383.
Kata nyingine ya Pera
ambayo pia iko maeneo ya mjini, Kituo cha Shule ya Msingi Namba 1; waliopiga
kura ni 88, kati ya walioandikishwa 443, Kituo cha Pera Shule ya Msingi Namba
2; waliopiga kura ni 100 kati ya wapiga kura 443.
Kituo cha Chamulungu
Namba 1; waliopiga kura 100 kati ya 336, huku Chamulungu II wakipiga kura 88
kati ya 325.
Wapiga kura kupokwa
vitambulisho
Baadhi ya wapiga kura
katika kata ya Ubena, walitoa malalamiko yao wakimtuhumu Katibu wa CCM Tawi la
Lulenge kwamba alifika majumbani mwao wakati wanaume hawapo na kuchukua
vitambulisho vya kupigia kura akisema kuwa anakwenda kuandikisha namba zao.
Akizungumza kwa
uchungu mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la alisema kuwa
kitendo hicho hicho si sahihi na akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua
stahiki.
“Hapa unavyoniona
nimeshindwa kupiga kura hadi sasa…jina langu na namba yangu vipo kwenye daftari
kwenye kituo kile pale, lakini sina kitambulisho. Juzi natafuta kitambulisho
change, mke wangu ananiambia alikuja Rajab Said ambaye ni Katibu wa Tawi la CCM
Lulenge, eti alikwenda kuandikisha namba zetu.
“Hadi muda huu
ninaokuambia, hajarudisha vitambulisho kwa sababu siko peke yangu, kuna wengine
kama 9 hivi ninawafahamu nao pia vimechukuliwa,” alisema Simon Pojoro.
Kwa upande wake Said
akijibu tuhuma hizo, Said alisema kuwa madai hayo si kweli nay eye hajui suala
hilo wala hakuhusika kwa namna yoyote kwa wapiga kura kukosa haki yao ya
kuchagua mbunge wao, akisema huo ni uzushi.
Tuhuma za gari ya CCM
‘kumwinda’ mgombea wa CHADEMA
Wakati huo huo,
akizungumzia mwenendo wa uchaguzi huo, mgombea ubunge wa CHADEMA, Mathayo
Torongey alisema kuwa gari aina ya Land Cruiser ‘hard top’, T 630 BFJ,
inayomilikiwa na CCM, ilikuwa ikimfuatilia kila mahali alikokwenda wakati akipita
maeneo mbalimbali kukagua vituo, kama sheria inavyomruhusu.
“Tena bahati nzuri
nimefika hapa kupita kwenye hiki kituo nimeikuta hii gari, hii ndiyo imekuwa
ikinifuatilia tangu asubuhi. Wamekuja pale Mdaula akashuka kijana mmoja...yule
pale…akiwa na sime na nondo, tulipomshtukia akarudi ndani ya gari akabadili
nguo akavua tisheti ya bluu aliyokuwa nayo akavaa koti hilo la kijeshi kama
mnavyomuona hapo,” alisema Torongey huku akionesha gari na huyo mtu.
“Tunashukuru kuwa
kulikuwa na polisi pale, tuliwapatia taarifa naona wamechukua hatua, tumelikuta
gari hili likiwa liko hapa na hawa askari, lakini nashangaa hawajapelekwa
kituoni na unawasikia wanavyozungumza kwa jeuri mbele ya polisi,” aliongeza.
Mbele ya waandishi wa
habari, gari ile iliyokuwa na watu wengi ndani, huku kuionekana silaha
mbalimbali na bendera ya CCM, iliruhusiwa kuondoka maeneo hayo, ikiamriwa
ielekee kituoni (bila kusindikizwa na polisi), ambapo kiongozi mmoja, ambaye ni
katibu wa chama hicho wilaya moja ya Iringa, akijigamba kwa kusema ‘tutakwenda
kituoni baada ya kumaliza kazi zetu.”
Matokeo ya awali
Kata ya Pera;
Malivundo Ofisi ya Mtendaji; CCM 77, CHADEMA 2, CUF , AFP 1, NRA 1.
Kimbugi; CCM 11,
CHADEMA 1, CUF 0, AFP 0, NRA 0
Magange Ofisi ya
Kitongoji; CCM 101, CHADEMA 1, NRA 0, AFP 0
Pingo Shule ya Msingi
Namba 1; CCM 31, CHADEMA 1, CUF 1, NRA 0, AFP 0
Pingo Ofisi ya
Kitongoji Namba 2; CCM 61, CHADEMA 4, CUF 2, AFP 1, NRA 0
Pingo Namba 1; CCM 66, CHADEMA 0, NRA 0, AFP 0
0 comments:
Post a Comment