MAJIBU/MAELEZO YA PINGAMIZI LILILOWEKWA NA BWANA FABIAN L.
SKAUKI DHIDI YANGU MIMI MATAYO M.TORONGEY MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE
KUPITIA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
UTANGULIZI
Kwa mujibu wa ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa
Tanzania (1977) inaeleza wazi kuwa ili mtu ateuliwe kuwa mgombea ubunge ni
lazima awe na sifa zifuatazo;
(i) Awe raia wa Tanzania (ii) Awe ametimiza umri
wa miaka ishirini na moja (iii) Awe anajua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au
Kiingereza (iv) Awe ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha
siasa (v) Awe hajatiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa
kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya
Uchaguzi.
Aidha, Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania 1977; hata kama mtu ana sifa zote za kugombea hataruhusiwa
kugombea Ubunge kama ;
(i) Ni raia wa nchi nyingine; au (ii) Kwa mujibu wa
Sheria iliyotumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitishwa rasmi
kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili; au (iii) Amehukumiwa na Mahakama yoyote
katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa
muda usiozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote
linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au (iv) Katika kipindi cha
miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa
adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja
sheria ya maadili ya viongozi wa Umma; au
(v) Siyo mwanachama na siyo Mgombea
aliyependekezwa na chama cha siasa; au (vi) Ikiwa mtu huyo ana maslahi yoyote
katika mikataba na serikali ya Jamhuri ya Muungano au serikali ya mapinduzi
Zanzibar wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalumu kwa mujibu washeria
iliyotungwa na Bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo; au (vii) Ameshika madaraka
ya Afisa Mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano,
isipokuwa madaraka ambayo Rais anaweza au anatakiwa kukabidhi kwa Mbunge kwa
Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, au sheria iliyotungwa na Bunge; au
(viii) Kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa
yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote, mtu huyo amezuiliwa kuandikishwa kama
Mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge. (ix) Ni mgombea Urais
/Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, kwa mujibu wa masharti kwa
vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa
na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 5.3 kimeweka masharti ya Uteuzi wa
Mgombea Ubunge na kuweka kama ifuatavyo;
(i) Awe amedhaminiwa na wapiga kura
wasiopungua ishirini na tano waliojiandikisha kupiga kura katika Jimbo hilo.
(ii) Mgombea haruhusiwi kujidhamini yeye mwenyewe (iii) Awe na dhamana ya
shilingi 50,000/= (iv) Awe ametoa tamko la kisheria mbele ya hakimu kwamba
anazo sifa zinazotakiwa ili kugombea Ubunge Vilevile, kwa mujibu wa masharti
kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 6.0 kimeweka utaratibu wa
Pingamizi dhidi ya uteuzi wa Mgombea Ubunge: Na Kifungu cha 6.3, kimeweka
sababu za kuweka Pingamizi kuwa ni: (i) Maelezo yaliyopo katika fomu ya uteuzi
hayatoshi kumtambulisha Mgombea; (ii) Fomu ya Uteuzi haitimizi au
haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sharia; (iii) Kutokana na
maelezo yaliyoandikwa katika fomu ya uteuzi ni dhahiri kwamba Mgombea uchaguzi
hana sifa zinazotakiwa;
(iv) Uthibitisho wa Msimamizi wa Uchaguzi unaopaswa
kutolewa haukutolewa; (v) Mgombea hana sifa zote zinazotakiwa; (vi) Hakuna
uthibitisho kuwa Mgombea amelipa dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=);
na (vii) Hakuna picha ya Mgombea. (viii) Mgombea hakujaza fomu Na.10 kuthibisha
kuwa ataheshimu na kutekeleza maadili ya Uchaguzi. Baada ya utangulizi huo hapo
juu ambao unaonyesha dhahiri kuwa hapakuwa na sababu yoyote ya mimi kuwekewa
pingamizi na Mgombea ubunge wa Chama cha CUF, kwani hakufuata masharti ya
Katiba, Sheria na maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kwetu
kama wagombea, kwani aliamua kutunga mambo ambayo yapo nje ya utaratibu na
hayakidhi haja, hayakufuata Katiba, matakwa ya kisheria na hata maelekezo
yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Nayasema yote haya kutokana na
ukweli kuwa mimi nimekidhi sifa zote za kuwa Mgombea Ubunge na nimetimiza
masharti yote yaliyowekwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Kutokana na barua yako ya tarehe 13 Machi, 2014 yenye kumbukumbu
namba HWB/E.50/21/76 nalazimika kujibu pingamizi hilo kwa mujibu wa kifungu cha
sheria ya Uchaguzi sura Na.343 kifungu Na.40 (5) kuhusu pingamizi, hata kama
halina nguvu kwa mujibu wa katiba, sheria na maelekezo ya Tume ya taifa ya uchaguzi
hoja kwa hoja kama ifuatayvo.
MAJIBU YA HOJA ZA PINGAMIZI LA FABIAN LEONARD
SKAUKI:
1. HOJA YA KWANZA; Kwamba mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimejaza
taarifa za uongo kwenye fomu zangu kuwa kazi ninayoifanya ni BIASHARA na kusema
kuwa ni taarifa za uongo kwa kuwa sikuweka vielelezo vya kuonyesha kuwa mimi
ninafanya kazi hiyo, na kuwa sijulikani ninafanya kazi gani .
MAJIBU YA HOJA YA KWANZA : Pingamizi
na sababu zilizotolewa na Mgombea wa chama cha wananchi CUF Bwana Fabian
L.Skauki hazina mashiko na kuwa yeye ameamua kukupotosha kuwa mimi sio
mfanyabiashara kwa kuwa sikuweka vielelezo, japo ni wazi kuwa sikupaswa kuweka
vielelezo vyovyote kwani fomu haikuwa inanitaka kuweka vielelezo vya aina
yoyote kama ambavyo hata yeye hakuweka vielelezo kuwa anafanya shughuli gani.
Ninasikitika kuwa hata wewe Msimamizi umekubaliana na hoja hii dhaifu ya
pingamizi na kunitaka mimi kuijibu wakati unajua wazi kuwa haina mshiko wala
mantiki kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. Naambatanisha leseni yangu ya
Biashara yenye jina langu namba B.No. 01299270 iliyotolewa tarehe 19/09/2011 na
huo ni uthibitisho kuwa mimi ni mfanya biashara (kielelezo A)
2.HOJA YA PILI:
Kwamba, mimi Mathayo Torongey sijui kusoma wala kuandika Kiswahili au
Kiingereza, na kwamba nimedanganya na hivyo sina sifa za kuwa Mgombea Ubunge.
MAJIBU YA HOJA YA PILI; Kwanza, nieleze wazi kuwa nimesikitishwa sana na tuhuma
hizi ambazo zina lengo la kunichafua mbele ya jamii na Taifa kwa ujumla, zina
lengo la kuichafua jamii ya watanzania kutoka familia za wakulima na wafugaji,
watu ambao wana kipato kidogo na ambao wanaishi vijijini kuwa ni watu wa hovyo
na hawajui kusoma wala kuandika, ni tuhuma za kuwadhalilisha watanzania ambao
ni kutoka jamii za wananchi wa vijijini wanaotafuta fursa ya kuchaguliwa kwamba
ni watu wa wanaoomba nafasi wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, kwa kweli
nasikitika sana kwa hili na lilikuwa tusi ambalo msimamizi wa uchaguzi
hukupaswa kulipokea. Aidha, nashindwa kutoa ushahidi hapa kwani hata wewe
umeziamini tuhuma hizi kuwa mimi sijui kusoma wala kuandika na ndio maana
ukanitaka nizijibu, japo ni ukweli ulio wazi kuwa sahihi yangu kwenye fomu
haikuwa ya "kuweka dole gumba" niliweka sahihi kwa kuandika na mbele
yako na sikuandikiwa. Pili; Yafaa mgombea huyu pamoja na wale wote waliomtuma
wakatoa ushahidi wake kwako kuwa mimi Mathayo Mang'unda Torongey sijui kusoma
wala kuandika, na hii itamsaidia kuaminika mbele ya jamii ya wananchi wa
Chalinze ambao anataka kuwaongoza. Hata hivyo naomba nitoe majibu mbele yako
kwa maandishi na kwa kusoma kitu ambacho wewe utataka nisome na kuandika ili
uwe uthibitisho kwako kuwa najua kusoma na kuandika .
3. HOJA YA TATU: Kwamba,
mimi Mathayo Torongey nimedanganya kwa kughushi/kufoji sahihi za wadhamini
walionidhamini kuwa Mgombea na kuwa sahihi zote zimefojiwa na hazifanani na
zile zilizokuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuwa sahihi zote
hizi zimesainiwa na mtu mmoja ambaye sio mhusika .
MAJIBU YA HOJA YA TATU:
Kwanza, nieleze wazi kuwa nilipokamilisha kujaza fomu zangu na kudhaminiwa na
wadhamini 25 kwa mujibu wa sheria , nilikuja ofisini kwako na tukakagua kwa
pamoja majina ya wadhamini wote waliokuwepo kwenye fomu zangu na nilikuja na
shahada zote za wapiga kura ambao walinidhamini na wewe ulizikagua na kuridhika
kuwa walikuwa ni wapiga kura sahihi na saini zao zilikuwa sahihi na uliandika
hilo kama uthibitisho wako kwenye fomu zangu za uteuzi na ndio maana uliniteua
kuwa mgombea . Pili, Namshangaa mweka Pingamizi kwa kuja na tuhuma kuwa saini
za wapiga kura zinatofautiana na saini zilizoko kwenye Daftari la kudumu la
wapiga kura ,hii ni kutokana na ukweli kuwa kwenye Daftari la kudumu la wapiga
kura hakuna saini za wapiga kura isipokuwa saini zipo kwenye vitambulisho vya
wapiga kura, na vitambulisho hivyo niliviwasilisha kwako na wewe kama msimamizi
wa uchaguzi baada ya kukagua vitambulisho hivyo uliridhika kuwa saini za
wadhamini wangu zilikuwa sahihi na ndio maana uliniteua kuwa Mgombea na kuweka
"uthibitisho wako" katika kifungu F. kwa maandishi kwenye fomu zangu
za uteuzi. Naomba kunukuu maelezo yako uliyoyaandika kwenye fomu yangu ya
uteuzi tarehe 12.03.2014 saa 9.05 Alasiri kama ifuatavyo;
‘(i) Nimekagua majina
yote ya waliomdhamini mgombea aliyetajwa hapa naninathibitisha kwamba wote
wameandikishwa kuwa wapiga kura katika Daftari la kudumu la wapiga kura katika
Jimbo la Chalinze' Tatu, Mweka pingamizi anatakiwa kuthibitisha kwako kuwa
saini hizo zimeghushiwa kwani ni ukweli ulio wazi kuwa kwa mujibu wa sheria za
nchi yetu kughushi ni kosa la Jinai na hivyo ushahidi wake huo unaweza
kuwasilishwa mbele ya vyombo vya dola kwa hatua zaidi. Nne, mweka pingamizi ana
wajibu wa kuthibitisha kuwa saini hizo zinafanana zote kwani ni ukweli uliowazi
kuwa saini za wadhamini wangu hazifanani kutokana na kuwa wapo wadhamini ambao
waliweka "dole gumba" kuthibitisha saini zao na wengine
walisaini kwa maandishi, sasa
kufanana anakosema ni kwa aina gani? Kwamba alama ya dole gumba ina fanana na
saini ya kuandika?! Tano, yafaa mweka pingamizi na wale wote ambao
walishirikiana naye kuweka hoja hii katika pingamizi hili kujitokeza na kueleza
kwa uwazi lengo la kuweka pingamizi hili ambalo ni la kutungwa na lenye nia ovu
dhidi yangu, Chama changu na Wananchi wote wa Jimbo la Chalinze.
4. HOJA YA NNE; Hoja ya mweka pingamizi iliyonihusu mimi Mgombea wa chama cha demokrasia na
maendeleo (CHADEMA) ilidai kuwa nimeshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya
kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake nimedhaminiwa na wadhamini 28
ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura halali wa jimbo la CHALINZE, na
kwamba Taarifa zao na namba zilizojazwa hazifanani. Hivyo nabakiwa na wadhamini
halali 21 ambao kisheria hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria. Majina ya
wadhamini hao ambao hawakidhi matakwa ya kisheria na namba zao kutajwa kuwa
ni:-
1. HABIBU ALLY SAIDI - 16886275 2. MOHAMMED RAMADHANI - 30376567 3.
ABDULKADIR ALLY - 49264905 4. SHABANI SULEYMAN - 16984045 5. JUMA MRISHO -
48759563 6. RAJABU ALLY - 16872368 7. MANENO MIRAJI - 16872059
MAJIBU YA HOJA
YA NNE (4). Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimekidhi vigezo na masharti ya
wadhamini wote 25 wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria kama nilivyo orodhesha
kwenye fomu ya wadhamini na hivyo basi pingamizi namba nne lililowekwa na
mgombea ubunge wa chama cha The Civic United Front (CUF) Kuwa Bwana HABIBU ALLY
SAIDI mwenye namba 16886275 kuwa sio mdhamini halali, nikiri kuwa ni kweli sio
mdhamini wangu halali; Mdhamini wangu halali ni Bwana HABIBU ALLY DAUDI mwenye
namba 16886275. Na vilevile ni kweli kwamba Bwana MOHAMMED RAMADHANI mwenye
‘30376567' si mdhamini wangu halali, Mdhamini wangu halali ni Bwana MOHAMMED
RAMADHANI mwenye namba 30576567.
Pia napenda kukuthibitishia bila chembe ya
shaka kuwa Bwana ABDULKADIR ALLY mwenye namba 49264905 aliyezaliwa wilaya ya
Bagamoyo tarehe 17/04/1974 ni mdhamini wangu halali aliye andikishwa tarehe 02.
03. 2010 kwenye kituo cha shule ya msingi Mkoko kata ya Msata halmashauri ya
Bagamoyo mkoa wa Pwani. Hata hivyo amesema Bwana SHABANI SULEYMAN mwenye namba
16984045 si mdhamini wangu halali, Napenda kuthibitishia kuwa mdhamini wangu
halali ni Bwana SHABANI SELEMANI mwenye namba 16984045 na si Bwana SHABANI
SULEYMAN. Hata hivyo, nadhibitisha kuwa Bwana JUMA MRISHO mwenye namba
48759563, aliyesema sio mdhamini wangu halali ni halali kwani amezaliwa tarehe
04.04.1981 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Msinune halmashauri
ya Bagamoyo mkoa wa Pwani na shahada yake ya kupigia kura imeandikishwa kwenye
kituo cha shule ya msingi Msinune, hivyo ni mdhamini wangu halali na amekidhi
vigezo vya kunidhamini sawa na Bwana RAJABU ALLY mwenye namba 16872368
aliyezaliwa tarehe 28.09.1979 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha
Kiwangwa mkoa wa Pwani naye ni mdhamini halali aliyejiandikisha kwenye kituo
cha Kibaoni ofisini; Kama ilivyo kwa mdhamini halali Bwana MANENO MIRAJI mwenye
namba 16872059 aliyezaliwa wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa mkoa Pwani na
kaandikishwa kituo cha Kibaoni Ofisini.
Muweka pingamizi angekuwa sahihi Kama
ningekuwa sijatoa uthibitisho kwa msimamizi wa uchaguzi. Hoja yake ingekuwa na
uzito unao bebwa na kifungu 6.3 (iv) kwenye kitabu cha tume ya taifa ya
uchaguzi cha maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa urais,
ubunge na madiwani kinasema, "Uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi
unaopaswa kutolewa haukutolewa". Lakini kwenye fomu namba 88 F ukurasa 8, "UTHIBITISHO
WA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI" msimamizi wa uchaguzi kwenye F( i) amekiri
kukagua na kuthibitisha ya kuwa wadhamini wote walioandikishwa kuwa wapiga kura
katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jimbo la CHALINZE ni halali.
Kwa
maana hiyo, udhibitisho wa msimamizi wa uchaguzi ni kwamba wadhamini wangu ni
halali hivyo hoja ya muweka pingamizi kwenye swala la wadhamini haina mashiko
na msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kupokea pingamizi hilo bali alipaswa
kulitupa kabla ya kufikiria kulileta kwangu. Hata hivyo, nichukue fursa hii
adhimu kumuelimisha muweka pingamizi wa chama cha wananchi CUF (Civic United
Front) ya kuwa majina yanaweza kufanana kwenye kituo kimoja au kituo kingine
ama kata nyingine au wilaya na mkoa mwingine lakini namba ya kadi halali ya
mpiga kura haiwezi kufafana na kadi ya mpiga kura mwingine halali, kwa mfano
kwenye kituo 00006347 kata ya Bwilungu jimbo la CHALINZE wilaya ya Bagamoyo
Mkoa wa Pwani mpiga kura HAMZA ATHUMANI mwenye shahada namba 17023223 anafanana
jina na HAMZA ATHUMANI mwenye shahada namba 1702107 sawa na Bwana BONELA
SHABANI MADEGA mwenye shahada namba 19534653 na BONELA SHABANI MADEGA mwenye
shahada namba 19525475. Hawa wote wakitazamwa kwa majina kwa jicho la muweka
pingamizi wa CUF wataonekana ni mtu mmoja au ni mapacha wakati uhalisia ni watu
tofauti wanao tofautishwa na namba za shahada zao halali za kupigia kura.
5.
HOJA YA TANO; Kuwa Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimedanganya Uraia wangu na
kuwa mimi sio Mtanzania wa kuzaliwa kwa kuwa sikuweka vielelezo vyovyote
halali.
MAJIBU YA HOJA YA TANO; Napenda kurudia kuwa huenda mweka pingamizi
ameamua kukupotosha na kuandika taarifa za uongo kwa lengo ambalo yeye na wale
wote waliomtuma wanalijua wao. Napenda kurudia kuthibitisha kama nilivyoandika
kwenye fomu zangu za kuomba uteuzi kuwa mimi ni mzaliwa wa Kijiji cha Kaloleni
katika Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania . Naomba kuweka
kielelezo "B" kuthibitisha uraia wangu wa Kuzaliwa kama ifuatavyo; 1.
Naweka nakala ya kitambulisho changu cha kuandikishwa kuwa mpiga kura katika
Jimbo la Ubungo chenye namba *46670962*. Na kwa mujibu wa sheria ya Taifa ya
Uchaguzi sura ya 343 , kifungu cha 10 (1) ‘sifa na kukosa sifa za kuandikishwa
kuwa mpiga kura na kupiga kura' kinasomeka ‘Hakutakuwa na mtu zaidi ya raia wa
Tanzania ambaye ametimiza umri wa miaka kumi na nane na ambaye hajapoteza sifa
kwa masharti ya Sheria hii au sheria nyingine yoyote ya Bunge atakayestahili
kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa mujibu wa masharti ya sheria hii' Hivyo kwa
kuwa nimekidhi vigezo vya kuwa mpiga kura ,mimi ni raia halali, naambatanisha
nakala ya shahada yangu ya Mpiga kura kama kielelezo ‘C'.
Aidha, ukisoma majibu
ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na wagombea wa
CHADEMA dhidi ya uraia wa wagombea wa CCM Sioi Sumari 2012 na Godfrey Mgimwa
2014 katika majimbo ya Arumeru Mashariki na Kalenga ,Tume iliamua kuwa jukumu
la kuthibisha /kutoa vielelezo kuhusu tuhuma za uraia wa mgombea ni kwa mtoa
tuhuma (who allegies must prove), hivyo mweka pingamizi atakiwe kuwasilisha
vielelezo vya tuhuma zake kwako ili kuthibitisha madai yake kuhusu uraia wangu.
HITIMISHO
Baada ya maelezo tajwa hapo juu na uthibitisho ambao nimeuwasilisha
kwako naomba kukujulisha kuwa mimi nina sifa zote kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuwa mgombea halali wa ubunge jimbo la Chalinze na
yafaa ukatupilia mbali pingamizi lililowekwa dhidi yangu kama jinsi ambavyo
ulipaswa kulitupilia mbali kabla hujalileta kwangu kwani lilikosa sifa na
vigezo vya kuwa pingamizi.
…………………………………
Mathayo Mang'unda Torongey
Mgombea
Ubunge wa CHADEMA jimbo la CHALINZE.
14 Machi, 2014.
0 comments:
Post a Comment