Friday, 11 April 2014

MNYIKA ASHINIKIZA KUPATA HATI YA MUUNGANO

Filled under:

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, John Mnyika, amesema atawasilisha hoja kuzuia shughuli za Bunge hilo kuendelea mpaka wajumbe watakapopatiwa hati halisi ya Muungano.

Mnyika, ambaye ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya wajenzi na kusema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo kwa vile hadi sasa serikali haijatoa hati halisi ya Muungano ingawa ni muhimu wajumbe waione.

Alikumbusha kuwa baada ya kupitishwa kwa Kanuni za Bunge alitaka kanuni ziruhusu wajumbe wa Bunge wapewe nyaraka wanazotaka katika utendaji wao wa kazi.

“Niliposema hivyo, Mbunge wa Simanjiro Ole Sendeka, alisemama na kupinga na akasema huyu Mnyika anataka kudai hati ya Muungano, naomba kanuni hiyo isiwepo”alisema.

Alisema Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alisimama na kusema kuwa hati hiyo ipo katika Sheria ya Muungano, lakini hakuna hati halisi wakati taarifa zingine zikisema kuwa ipo Umoja wa Mataifa.

“Hata hivyo baada ya kanuni hiyo kupita, nilimwandikia barua Katibu wa Bunge kuomba hati halisi ya muungano, lakini hadi sasa hivi ninavyozungumza sijapewa hati hiyo.“
Alisema msingi wa Rasimu ya Katiba ni Hati ya Muungano na kwamba umefika wakati sasa wajadili rasimu huku wakiwa na hati halisi.

“Hawa CCM wanadai uwazi kwa kukataa kura ya siri sasa inabidi waonyeshe mfano kwa kuweka wazi Hati ya Muungano, wakikomaa tutawashtaki kwa wananchi,” alisema.

0 comments:

Post a Comment