MAONI YA WAJUMBE
WALIO WACHACHE WA KAMATI NAMBA SITA YA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUHUSIANA
NA SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA ZA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
(Kwa mujibu wa Kanuni 32 (4) ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014)
UTANGULIZI
Sura ya Kwanza na Sura
ya Sita za Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndizo
msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Hii ni kwa sababu Sura hizi
mbili zinazungumzia mfumo na muundo wa Muungano. Katika Sura ya Kwanza,
mfumo na muundo wa Muungano unatajwa kwenye Ibara ya 1 na Ibara ya 2 na
kwa upande wa Sura ya Sita, sura nzima inahusu Muundo wa Jamhuri ya
Muungano.
Katika kufikia maamuzi
ya Kamati Namba Sita, wajumbe waligawanyika, na katika Ibara ya 1 na ya 3
ya Sura ya Kwanza na Ibara zote za Sura ya Sita, sharti la kupata
theluthi mbili za wajumbe wote wa kamati kutoka Tanzania Bara na
theluthi mbili za wajumbe wote wa Kamati kutoka Zanzibar lilishindwa
kufikiwa.
Maoni haya ya wajumbe
walio wachache yametokana na maoni ya wajumbe sita (6) kutoka Zanzibar
na wajumbe sita (6) kutoka Tanganyika.
MAONI, SABABU NA HOJA KUHUSU IBARA YA 1 YA SURA YA KWANZA
Mjadala mkubwa kuhusu
Ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza ulihusu mfumo na muundo wa Muungano iwapo
ni wa Shirikisho, kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu, au ni Muungano
uliounda Nchi Moja (Unitary State), kama ilivyodaiwa na wajumbe walio
wengi kwenye Kamati.
Maoni na msimamo wa
wajumbe walio wachache ni kukubaliana na maoni ya Watanzania walio wengi
waliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ni SHIRIKISHO na wala si MUUNGANO ULIOUNDA NCHI
MOJA (UNITARY STATE).
Tunasema hivyo kwa
sababu ya hoja za kitaaalamu zilizofanyiwa utafiti na wataalamu mabingwa
wa sheria wa ndani na nje ya Tanzania, tafsiri za vifungu vya Mkataba
wa Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
pamoja na hali halisi ya uendeshaji wa Muungano ilivyo.
MAONI YA WATAALAMU WA SHERIA:
Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar uliundwa kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi
wa nchi hizo mbili, Rais Julius Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais
Abeid Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambayo yamo kwenye Mkataba
wa Muungano. Wataalamu mbali mbali ambao ni mabingwa wa sheria wa ndani
na nje ya Tanzania wamefanya uchambuzi wa Mkataba huo na pia Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na wamekuja na hitimisho kwamba
Muungano huu ni Shirikisho. Tunawanukuu wachache hapa chini:
- Profesa Issa Shivji katika kitabu chake, Tanzania: The Legal Foundations of the Union,
kilichochapishwa mwaka 1990 na kurejewa tena mwaka 2009 anasema baada
ya kuufanyia uchambuzi wa kina Mkataba wa Muungano ameridhika kwamba
Mkataba huo umeanzisha Shirikisho. Kwa maneno yake mwenyewe Profesa
Shivji anasema kwamba ukiyaangalia Makubaliano ya Muungano kutoka upande
wa Zanzibar na upande wa Tanganyika na kwa ujumla wao, “… msingi wa Shirikisho ndiyo wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano yanaweza kutafsiriwa kwa usahihi kama Katiba ya Shirikisho.” Kwengineko kwenye kitabu hicho hicho, Profesa Shivji anasema kwamba: “Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba Makubaliano ya Muungano siyo Katiba ya Muungano wa Nchi Moja (Unitary Constitution).”
- Waandishi Earl E. Seaton na S.T. Maliti katika kitabu chao, Tanzania Treaty Practice kilichochapishwa
mwaka 1973 walikubali kwamba Makubaliano ya Muungano yaliunda Katiba ya
Shirikisho na siyo Katiba ya Muungano wa Nchi Moja (Unitary State).
- Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Muungano unaundwa, Wolfango Dourado, katika Waraka wake aliouita, The Consolidation of the Union: A Basic Re-Appraisal,
ambao aliutoa mwaka 1983 wakati wa mjadala wa marekebisho ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano, alibainisha kwamba Makubaliano ya Muungano
hayakuunda Muungano wa Nchi Moja bali yaliunda “Shirikisho la Kweli” (A
True Federation).
- Profesa B. P. Srivastava katika waraka wake wa mwaka 1984, The Constitution of the United Republic of Tanzania 1977: Some Salient Features, Some Riddles ameandika kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una sura ya Shirikisho.
- Profesa Palamagamba Kabudi katika utafiti wake uliopelekea kutunukiwa Shahada ya Uzamili (Masters Theses) ambao unaitwa, International Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar: A Federal or Unitary State? naye amefikia hitimisho kwamba Makubaliano ya Muungano yameunda Shirikisho na siyo Muungano wa Nchi Moja.
- Profesa Yash Ghai,
aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Kenya na
ambaye ni bingwa wa sheria anayeheshimika duniani, katika utangulizi wa
toleo jipya la kitabu cha Profesa Issa Shivji kilichochapishwa upya
mwaka 2009, ameandika kwamba, “Tanzania inakidhi vigezo vingi rasmi vya
Shirikisho.”
Hayo ni maoni ya
wataalamu waliobobea katika fani ya Sheria ambayo hayawezi kupuuzwa kwa
sababu tu ya misimamo ya kisiasa ya kikundi fulani cha watu ndani ya
Tanzania ambao wanataka kulazimisha ionekane kwamba Makubaliano ya
Muungano yaliunda Nchi Moja.
MITAZAMO YA VIONGOZI WAKUU WA KISIASA:
Hoja na mtazamo kwamba
Makubaliano ya Muungano yameanzisha Shirikisho na siyo Muungano wa Nchi
Moja yametolewa pia na baadhi ya viongozi wa juu wa kisiasa wa hapa
nchini. Tuchukue mifano miwili tu hapa:
- Tume ya Mabadliko ya
Katiba katika Randama ya Rasimu ya Katiba inamnukuu Mwalimu Julius
Nyerere akiuambia mkutano maalum wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM
uliofanyika Dodoma kati ya tarehe 24 – 30 Januari, 1984 kuwa, “…
Muungano wa Tanzania ukiuangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa Shirikisho
lakini ukiuangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni Serikali Moja.”
Pamoja na kutetea muundo
wa Serikali mbili, Mwalimu Julius Nyerere anaonekana wazi kuelewa
kwamba mantiki ya nchi mbili zinapoungana ni kuwa na Shirikisho la
Serikali Tatu. Katika kitabu chake alichokichapisha mwaka 1994, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, anasema:
“Nchi zinapoungana na
kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa
mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na nchi mpya
inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa
pili, kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali
ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya
mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale
ambayo yakibaki katika mamlaka za nchi zilizoungana, basi kwa kweli
nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa
nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani…
Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa na nchi moja yenye serikali
tatu, serikali ya shirikisho na serikali mbili za awali zilizoungana
kuzaa nchi mpya moja.”
Lakini Mwalimu Julius
Nyerere hakuishia hapo tu. Ana hoja nzuri sana kuwajibu wale wanaohoji
kwamba ukiwa na Serikali Tatu, mbili za nchi washirika na moja ya
Shirikisho, hiyo Serikali ya Shirikisho itakuwa na eneo gani la kutawala
na nchi yake itatoka wapi. Mwalimu Nyerere anapozungumzia muundo wa
Shirikisho la Afrika Mashariki pale litakapofikiwa anasema:
“Kama jambo hilo
lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo
ingezaliwa ungekuwa ni wa Shirikisho; ama shirikisho la Nchi Tatu zenye
Serikali Nne, au Shirikisho la Nchi Nne lenye Serikali Tano. Kwa kweli
hata kesho nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa
ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye
Serikali Mbili – ya Zanzibar na Tanganyika – kuliko Tanzania yenye
Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar.”
Suala la kujiuliza iwapo
wale wanaohoji kama ukiwa na Serikali Tatu ndani ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, hiyo ya tatu eneo lake litakuwa lipi, nadhani
kwa mantiki hiyo hiyo wangemuuliza Mwalimu Nyerere kama kungekuwa na
Shirikisho la Afrika Mashariki linaloshirikisha Nchi Nne (kwa maana ya
Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar) zenye Serikali Tano, hiyo
Serikali ya Tano ambayo itakuwa na Shirikisho eneo lake litakuwa lipi?
Bila shaka, eneo lake ni eneo lote la nchi nne kwa pamoja lakini mamlaka
yake yatakuwa yanahusu yale mambo ya Shirikisho tu. Huyo ni Mwalimu
Nyerere. Sasa tumgeukie kiongozi mwengine aliyewahi kushika madaraka ya
juu kabisa Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano.
- Aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, katika kitabu chake, The Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – Miaka 30 ya Dhoruba alichokichapisha mwaka 1994 amesema wazi kwamba:
“Ibara za Mkataba wa
Muungano ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu na serikali shiriki
katika Muungano kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani mfumo wa Shirikisho
ambao kuna mgawiko wa mahakama, baraza la kutunga sheria na urais baina
ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na kila Serikali ikiwa na
nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”
IBARA YA 1 (1) NA 1(3) KUHUSIANA NA HATI YA MAKUBALIANO YA MUUNGANO KUWA NDIYO MSINGI MKUU WA MUUNGANO
Ibara ya 1(1) na (1(3)
za Rasimu zinafanya rejea kwenye Hati ya Makubaliano ya Muungano na
kutamka kwamba Hati hiyo ndiyo “msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania”. Kama tunakiri kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano ndiyo
msingi mkuu wa Muungano, hatuna budi kurudi katika historia yake, jinsi
ulivyofikiwa, kujua maudhui yake, na kuona utekelezaji wake umekwenda
vipi.
Kama tulivyokwisha kuona
kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliundwa kupitia Mkataba wa
Muungano wa 1964 (Articles of Union). Mkataba huu, kwa kutumia ushahidi
wa picha, ulitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius
Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani
Karume, kwa niaba ya nchi zao mbili katika Ikulu ya Zanzibar, tarehe 22
Aprili, 1964.
Mkataba wa Muungano wa
1964 (Articles of Union between the Republic of Tanganyika and the
People’s Republic of Zanzibar) ni Mkataba wa Kimataifa (an international
treaty) na ndiyo maana kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kiingereza
(English Common Law System) zilizokuwa zikifuatwa na Zanzibar na
Tanganyika wakati huo na hadi leo uliweka sharti katika kifungu cha
(viii) kwamba unapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la
Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likishirikiana na Baraza lake
la Mawaziri ili kuupa nguvu za kisheria ndani ya nchi mbili hizo.
Hoja ya kwanza
inayojitokeza hapa na ambayo imeshindwa kupatiwa majibu hadi leo ni
kushindwa kupatikana kwa nakala halisi (original copy) ya Mkataba huo
ikiwa na saini za Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume
wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hoja hii imeibuliwa ndani ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano na pia katika Mahkama Kuu ya Zanzibar ambako
Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, zimeshindwa kutoa nakala hiyo licha ya kuahidi
kufanya hivyo.
Yalikuwepo maelezo
kwamba nakala halisi ya Mkataba wa Muungano ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumbukumbu za Umoja huo kujiridhisha
kwamba nchi mbili hizi zimeungana. Hata hivyo, kumbukumbu za Umoja wa
Mataifa zinaonesha kwamba maelezo hayo si ya kweli.
Kumbukumbu za Umoja wa
Mataifa zinaonesha kwamba siku moja baada ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kutangazwa, yaani tarehe 27 Aprili 1964,
Mwanasheria Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. C.A.
Stavropoulos alimwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. U Thant,
waraka wa kiofisi uliohusu ‘Uanachama Katika Umoja wa Mataifa wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’ Kwa mujibu wa Bw. Stavropoulos,
waraka wake ulitokana na taarifa za vyombo vya habari zilizoonyesha
kwamba Tanganyika na Zanzibar, ‘ambazo kabla zilikuwa wanachama tofauti wa Umoja wa Mataifa’,
zilikuwa zimeungana na kuunda dola moja yenye uwakilishi wa pamoja nchi
za nje. Kwa vile Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikuwa hazijapeleka taarifa rasmi Umoja wa
Mataifa juu ya Muungano wa nchi zao, Bw. Stavropoulos alipendekeza
kwamba “mwakilishi wa Tanganyika ataarifiwe juu ya haja ya kupata
tamko rasmi kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano … kuhusu
kuanzishwa kwa Jamhuri hiyo … na hati mpya za utambulisho wa mwakilishi
mmoja kutoka Jamhuri (ya Muungano). (Itakuwa vizuri vile vile kwa
mwakilishi husika kutupatia nakala ya makubaliano yaliyopelekea Muungano
huo.)”
Ijapokuwa tarehe 6 Mei,
1964, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ilipeleka taarifa ya maandishi iliyodai kuambatanisha nakala ya
Hati ya Makubaliano ya Muungano, kuna mashaka ya msingi kama kweli Hati
hiyo ilipelekwa Umoja wa Mataifa. Hii ni kwa sababu, tarehe 14 Mei,
1964, yaani wiki moja tu baadaye na takriban wiki tatu baada ya
Muungano, Bw. Stavropoulos alimwandikia Deputy Chief de Cabinet wa
Umoja wa Mataifa Bw. Jose Rolz-Bennett kumwelekeza apeleke ujumbe wa
simu ya maandishi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuhusu masharti
ya kusajili Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja
wa Mataifa kama inavyotakiwa na Ibara ya 102 ya Mkataba wa Umoja wa
Mataifa (United Nations Charter). “… Serikali inayosajili inatakiwa
kuwasilisha kwa Sekretarieti nakala moja ya Makubaliano iliyothibitishwa
kwamba ni nakala ya kweli na kamili … nakala mbili za ziada na taarifa
inayohusu tarehe na namna ya kutiliwa nguvu Makubaliano hayo.”
Baada ya sarakasi yote
hiyo, sasa kuna uthibitisho kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano
haijawahi kusajili Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti
ya Umoja wa Mataifa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Andrei
Kolomoets, ambaye ni Afisa Habari za Kisheria katika Kitengo cha
Mikataba ya Kimataifa ndani ya Ofisi inayoshughulika na Mambo ya Sheria
kwenye Umoja wa Mataifa, alipoulizwa na mtafiti mmoja, alijibu kwa
maandishi tarehe 25 Machi, 2009 kwamba:
“Hakuna ushahidi wowote
kwamba Mkataba wa Muungano ulisajiliwa kwenye Sekretarieti ya Umoja wa
Mataifa. Kama ungesajiliwa, kungelikuwa na kumbukumbu kwenye kitengo cha
hifadhi ya kumbukumbu na kungekuwa na shahada ya kusajiliwa ikiwa
imeambatanishwa. Nimeangalia, hakuna kitu hicho.”
Kuonekanwa kwa nakala
halisi ya Mkataba huo ni muhimu sana katika kujiridhisha uhalisia wa
kile kilichokubaliwa baina ya nchi hizi mbili. Hilo ni suala la msingi
ili kumaliza mabishano ya kisheria na kisiasa juu ya nini hasa Rais
Nyerere na Rais Karume walikubaliana kwa niaba ya nchi zao.
Hata tukichukulia kwamba
kile tulichoaminishwa kwamba ndiyo Hati ya Makubaliano ya Muungano kuwa
ni sahihi, hoja ya pili inazuka kuhusu utekelezwaji wa matakwa ya
uthibitishaji (the want of ratification) wa Mkataba huo kwa upande wa
Zanzibar. Upo ushahidi wa kutosha kwamba Bunge la Tanganyika lilikutana
na kuuridhia Mkataba huo tarehe 25 Aprili, 1964. Kwa upande mwengine,
hakuna ushahidi wowote kwamba Baraza la Mapinduzi likishirikiana na
Baraza la Mawaziri la Zanzibar lilikaa kuuridhia Mkataba huo kwa
kupitisha Sheria ya Kuthibitisha (Ratification Decree) kama ilivyotakiwa
na Mkataba wenyewe. Kwa hakika ushahidi ulioibuliwa na Prof. Issa
Shivji katika kitabu chake, Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Unionkilichochapishwa
mwaka 2008 umeweka wazi pasina chembe ya wasiwasi kwamba Mkataba huo
haujaridhiwa na upande wa Zanzibar hadi hii leo. Profesa Shivji anaeleza
kwamba:
“Uhalisi wa mambo ni
kwamba ushahidi wote unaelekeza kwenye ukweli kwamba kile kinachodaiwa
kuwa ni Sheria ya Zanzibar ya kuridhia Hati ya Makubaliano ya Muungano
iliandaliwa na kuandikwa na maofisa wa sheria wa Tanganyika wakiwa ndani
ya Tanganyika. Maofisa hao wa sheria walikuwa wakijua mahitaji na
matakwa yote ya utungaji wa sheria kama yalivyokuwa katika Sheria za
Kikatiba za Zanzibar za wakati ule kwa sababu wamezitaja kwenye kifungu
kidogo cha 2 cha kifungu cha 7 cha Sheria hiyo. Uhalisi wa mambo kwamba
masharti hayo hayakutekelezwa ulitokana na ukweli wa kisiasa uliokuwepo
wakati huo, mkubwa na muhimu kuliko yote ukiwa ni kwamba Baraza la
Mapinduzi kwa ujumla halikuukubali Muungano. Hapana shaka kwamba
Muungano ‘ulilazimishwa’. Kwa hivyo, maofisa wa sheria wa kigeni wa
Serikali ya Tanganyika (ambao katika kadhia hii walisadifia pia kuwa ni
marafiki wa Nyerere) walitumia mbinu na hila ya kisheria ya kuchapisha
Sheria ya Kuridhia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964,
waliyoitengeneza wao, kwenye Gazeti Rasmi la Jamhuri ya Muungano kama
Taarifa ikiwa na saini ya [Kaimu Mshauri Mkuu wa Sheria wa Tanganyika]
Fifoot. Taarifa kwamba Sheria ile ilitungwa na ‘Baraza la Mapinduzi la
Zanzibar likishirikiana na Baraza la Mawaziri’ ilikuwa ni ya uongo. Kwa
hivyo, mamlaka husika za Zanzibar hazikuridhia, kisheria na kiuhalisia,
Hati ya Mapatano ya Muungano.”
Ukiachilia mbali hoja
hizo, na kwa msingi wa hoja tukichukulia kwamba Mkataba huo ni halali,
bado ukitazama kwa jicho la sheria, utaona kiini cha matatizo ya
Muungano kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano (Articles of
Union) wa 1964. Suala kubwa lililoumiza na linaloendelea kuumiza vichwa
vya wengi na hivyo kuendelea kuulizwa ni mfumo gani wa Muungano
ulikusudiwa kuwekwa na Mkataba huu? Ni muungano wa moja kwa moja
(unitary) au wa shirikisho (federal)?
Mfumo uliopo sasa ambao
ulianza kutekelezwa 1964 ni ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya
Muungano na ile ya Zanzibar. Tanganyika haikuwekewa serikali yake
tofauti; madaraka yake kwa yale mambo yasiyo ya Muungano yalielezwa
kwamba yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali hiyo hiyo ya Jamhuri ya
Muungano. Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu umeendelea
kuhojiwa na hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio
yaliyomo katika Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.
Mkataba wa Muungano
wenyewe hauelezi bayana aina au mfumo wa muungano inaouanzisha lakini
uko wazi kuhusiana na mgawanyo wa madaraka (distribution of power) inaouweka na idadi ya mamlaka (number of jurisdictions) zitakazokuwepo. Ibara ya (iii) (a) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Baraza la Kutunga Sheria na Mamlaka ya Utendaji’ (Legislature and Executive) ndani ya na kwa ajili ya Zanzibar ikiwa na mamlaka kamili (exclusive authority) kuhusiana
na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa Zanzibar. Kwa upande
mwengine, Ibara ya (iv) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Bunge na Mamlaka ya
Utendaji’ (Parliament and Executive)ya Jamhuri ya Muungano
ikiwa na mamlaka kamili katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano
kuhusiana na mambo ya Muungano na, pia, ikiwa na mamlaka kamili ndani
ya, na kwa ajili ya Tanganyika kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya
Muungano kwa Tanganyika. Kwa hivyo, katika sehemu ya pili, mamlaka mbili
tofauti zimechanganywa pamoja.
Mjadala mkubwa na mkali umekuja kuhusiana na tafsiri ya Ibara hiyo ya (iv) na kule kuchanganya kwake mamlaka mbili hizo.
Haya si masuala ya
kisheria tu kama ambavyo baadhi yetu wanataka tuamini (ingawa nayo ni
muhimu mno kama ilivyodhihirika hivi karibuni), bali pia ni masuala ya
kisiasa kwa vile yanahusisha uwezo wa maamuzi, madaraka na mamlaka, na
zaidi mchango wa gharama za uendeshaji na mgawanyo wa rasilimali na
mapato kati ya wahusika wakuu. Mambo haya, katika uzoefu wa nchi za
wenzetu, ndiyo yaliyopelekea kuvunjika kwa miungano yao kwani huzaa
kutiliana shaka na kutokuaminiana. Kwa vile yanachukua sura ya kisiasa
(kutokana na sababu nilizozitaja), haya hayana chama wala itikadi. Kama
alivyowahi kusema Prof. Issa Shivji mwaka 1994 kwenye makala yake ‘The Union: Hopes and Fears’ iliyochapishwa katika gazeti la The Family Mirror (Dar es Salaam), First Issue, January 1994, uk. 5:
“Ultimately, the
question of the Union is primarily a political question and no amount of
rhetoric about blood and cultural ties will matter when it comes to
realpolitik.”
Yaani, “Mwisho wa yote,
suala la Muungano linabakia kimsingi kuwa ni suala la kisiasa, na
inapofikia kwenye siasa hasa, hotuba na kauli kali za jazba kuhusiana na
mahusiano ya damu na ya kidugu, zote hazitafaa kitu.”
Kwa hakika, kinyume na
inavyojaribiwa kuoneshwa na wengi kwamba Tanganyika imepoteza kila kitu
katika muundo huu wakati Zanzibar imekabidhi sehemu tu ya madaraka yake,
muundo wa Serikali mbili umepelekea wengi kuamini kwamba kilichofanyika
ni kiini macho tu kwani ni Zanzibar iliyokabidhi sehemu muhimu ya
mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi
na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa
Tanganyika na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya
Muungano. Na haya si maoni ya ngumbaru (kwa kutumia lugha ya
Mwalimu Julius Nyerere) bali ni maoni ya watu wazito wakiwemo aliyekuwa
Spika wa Bunge na baadaye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa
Pius Msekwa ambaye alisema kwa jinsi mambo yalivyofanyika, Zanzibar
inaonekana kama vile ni ‘invited guest’ (mgeni aliyealikwa) katika Muungano (Rejea Pius Msekwa (1994) ‘The State of the Union’ –Paper presented to a Seminar on the State of the Union, Mkonge Hotel, Tanga 25 – 27 February, 1994). Naye msomi mashuhuri ulimwenguni, Prof. Ali Mazrui katika makala yake ‘Imperialism after the Empire: Lessons from Uganda and Tanzania’ iliyochapishwa katika gazeti la The Sunday Nation (Nairobi),
May 22, 1994 alisema baada ya Muungano, Zanzibar imepoteza kila kitu
muhimu wakati Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania huku ikiwa
na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo yake ya Taifa,
wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa Mataifa.
MAPENDEKEZO:
Ibara ya 1:
Jina la Muungano
Muungano huu umetokana
na Jamhuri mbili kuungana kwa hiyari. Jamhuri hizo ni Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Jina la awali lililotajwa katika
Mkataba wa Muungano la muungano wa jamhuri hizi mbili lilikuwa ni
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jina hili baadaye tarehe
28 Oktoba, 1964 lilibadilishwa na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Tarehe 2 Novemba, 1964, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kwenye Umoja wa Mataifa ukapeleka taarifa ya
kubadilisha jina hilo lakini taarifa hiyo haikuwa na saini na badala
yake ikagongwa mhuri wa Jamhuri ya Tanganyika, ambayo tumefanywa tuamini
kwamba ilishafutika tokea tarehe 26 Aprili, 1964. Tunachojiuliza ni upi
uhalali wa taarifa hiyo iliyopelekwa Umoja wa Mataifa na Jamhuri ya
Tanganyika, nchi ambayo tunaambiwa haikuwepo tena tarehe 2 Novemba,
1964?
Tunaelewa kwamba tarehe 3
Desemba, 1964 ikiwa ni takriban wiki sita tokea jina la ‘Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania’ lilipoanza kutumika, ulipelekwa Mswada wa Sheria
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kubadilisha jina hilo. Suala
linalokuja hapa ni kwamba: Je, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipata
wapi mamlaka ya kubadilisha jina rasmi la ‘Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar’ ambalo ndilo jina lililotajwa katika Sheria ya
Kuridhia Hati ya Makubaliano ya Muungano (Sheria Nam. 22 ya 1964) wakati
Hati yenyewe ya Makubaliano haikutoa mamlaka kwa chombo chochote
kubadilisha masharti yaliyomo kwenye Hati hiyo?
Wakati umefika sasa wa
kurudisha jina linaloakisi msingi wa Muungano wenyewe ambao umetokana na
nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na pia kuutambua na kuukiri ukweli
huo.
Hata ukiangalia mifano
ya nchi nyingine zilizoungana, jina la miungano huweka bayana kwamba
zilizoungana ni zaidi ya nchi moja. Kwa mfano, Muungano wa Nchi (states)
za Marekani unaitwa kwa kiingereza United States of America (USA), ule uliokuwa Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti ukiitwa Union of Soviet Socialist Republics (USSR) na ule Muungano wa Falme za Kiarabu unaitwa United Arab Emirates (UAE).
Ili kuondosha dhana
iliyojengeka kwamba muungano wa jamhuri zetu mbili umeunda nchi moja na
kuzifuta nchi zetu, Katiba Mpya inapaswa kuweka jina linalotambua msingi
huo na historia hiyo. Hivyo basi, jina jipya liwe ni Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar na kwa kiingereza The Federal Republics of Tanganyika and Zanzibar.
Ibara ya 1, maneno ya mwisho yanayosomeka “ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru” yaondoke.
Muungano haukukusudia kufuta uhuru wa nchi zilizoungana na hatuamini
kwamba kwa kukubali kuingia katika muungano, nchi washirika
zilisalimisha uhuru wao. Kinachozungumzwa katika utangulizi wa Mkataba
wa Muungano wa 1964 ni mahusiano au maingiliano ya watu (furthering that
association and strengthening of these ties) na siyo kusalimisha
mamlaka au kufuta uhuru wa nchi washirika (associating states).
Kwa vyovyote vile, Uhuru
wa Tanganyika uliopatikana tarehe 9 Desemba, 1961 na ambao
unasherehekewa hadi leo na Uhuru wa Zanzibar uliopatikana kwa njia ya
Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ambayo yanaadhimishwa hadi leo, uko
pale pale na nchi zetu mbili hazikuwa na maana ya kusalimisha uhuru huo
kwa kuingia kwenye Muungano baina yao.
Isitoshe, maelezo
yaliyomo kwenye Ibara ya 1 yanayosomeka kwamba “Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili” siyo sahihi.
Kilichoundwa kupitia Muungano huu ni SHIRIKISHO na siyo NCHI. Hakuna
kifungu chochote katika Mkataba wa Muungano ambacho kinazifuta nchi za
Tanganyika na Zanzibar. Kwa hakika, maneno “Tanzania ni nchi moja na
ni Jamhuri ya Muungano” yaliyomo kwenye Ibara ya 1 ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ya mwaka 1977, ni maneno mapya yaliyoingizwa mwaka 1984
wakati wa marekebisho ya Katiba hiyo. Hayakuwemo kwenye Katiba ya Muda
ya 1964; hayakuwemo kwenye Katiba ya Muda ya 1965; na wala hayakuwemo
kwenye Katiba ya mwaka 1977 (kabla ya kufanyiwa marekebisho makubwa
mwaka 1984).
Katiba ya Muda ya 1964,
Ibara ya 1 ilisema: “Tanganyika and Zanzibar is one United Sovereign
Republic” ambayo tafsiri yake ni: “Tanganyika na Zanzibar ni Jamhuri
huru moja iliyoungana”. Katiba ya Muda ya 1965, Ibara ya 1 ilisema:
“Tanzania is a United Sovereign Republic” ambayo tafsiri yake ni:
“Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano”. Na Katiba ya 1977 (kabla ya
marekebisho ya mwaka 1984) , Ibara ya 1 ilisema: “Tanzania ni Jamhuri
ya Muungano”.
Kwa hivyo, Ibara ya 1 inapaswa isomeke kama ifuatavyo:
“1.-(1)
Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho ambalo
limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar ulioundwa kupitia Hati ya Makubaliano ya Muungano
baina ya nchi hizo mbili tarehe 26 Aprili, 1964.
(2) Shirikisho
la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la kidemokrasia
linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu,
kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu, na
lisilofungamana na dini ijapokuwa raia wake wana imani zao za dini.
(3) Hati ya
Makubaliano ya Muungano baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar iliyorejewa katika ibara ndogo ya (1), ndiyo msingi
mkuu wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar na Katiba hii,
kwa kadiri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano
hayo.”
Pendekezo la kuongeza Ibara ndogo mpya ya 1(4):
Mkataba wa Muungano
(Articles of Union) wa 1964 umeweka wazi katika Utangulizi wake kwamba
muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hatua ya mwanzo kuelekea Umoja wa
Afrika ambapo inaelezwa:
“WHEREAS the
Governments of the Republic of Tanganyika and of the Peoples’ Republic
of Zanzibar being mindful of the long association of the peoples of
these lands and of their ties of kinship and amity, and being desirous
of furthering that association and strengthening of these ties and of
furthering the unity of African peoples have met and considered the
union of the Republic of Tanganyika with the Peoples Republic of
Zanzibar;”
Hata sasa tunapojadili
Katiba Mpya, hoja kubwa inajengwa kwamba muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ni mwanzo tu wa kufikia muungano mkubwa zaidi wa nchi za Afrika
Mashariki na hatimaye wa nchi zote za Afrika.
Iwapo malengo hayo ni ya
dhati na si propaganda tu za kisiasa ni muhimu basi msingi huu
ukazingatiwa katika Katiba Mpya ili kufuta ile dhana kwamba muungano huu
ulikuwa na dhamira moja tu ya kuimeza Zanzibar na kuifanya sehemu ya
Tanganyika mpya iliyopewa jina la Tanzania.
Rasimu ya Katiba kama ilivyo sasa haitoi fursa wala haioneshi kama kuna uwezekano wa nchi nyengine kujiunga na Muungano huu. Je,
ile dhana ya kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hatua ya
mwanzo tu ya muungano mkubwa zaidi wa nchi za Afrika na ambayo inatajwa
pia kama ni mojawapo ya sababu za kuunda muungano huu katika maelezo ya
utangulizi wa Mkataba wa Muungano wa 1964 kwa maneno “and being desirous
of… furthering the unity of African peoples”, sasa haipo tena?
Kuna haja ya kuzingatia
utaratibu kama ule uliomo katika kifungu cha 3(1) cha Mkataba wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki ambao unatoa uhuru na fursa kwa nchi nyengine
yoyote kujiunga iwapo itakubaliana na masharti yaliyowekwa.
Tunapendekeza kuwepo kwa
Ibara Ndogo mpya ya 1(4) itakayoruhusu nchi nyengine ikitaka kujiunga
na Shirikisho hili iweze kufanya hivyo, alimradi tu wanakubaliana na
masharti ya Katiba hii; na kifungu hicho kisomeke kama ifuatavyo:
“1(4).- Nchi
yoyote inaweza kuomba kujiunga katika Shirikisho la Jamhuri za
Tanganyika na Zanzibar ikiwa nchi hiyo itatimiza masharti yaliyowekwa
katika Katiba hii, na kwa ridhaa ya Serikali na Bunge la Tanganyika na
Serikali na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na ridhaa ya
Serikali na Bunge la Shirikisho.”
Ibara ya 2:
Eneo la Shirikisho na Mipaka ya Zanzibar na Tanganyika
Katika eneo hili, Kamati
Namba Sita ilikubaliana jinsi ya kuiandika upya Ibara ya 2 kwa msingi
wa kutambua kwamba eneo la Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar ni eneo lote la Tanganyika ikijumuisha na sehemu yake ya bahari
na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha na sehemu yake ya bahari na maeneo
yao yatakayoongezwa.
Mbali na kutaja eneo la
Shirikisho, Katiba Mpya ni lazima itamke bayana na kwa uwazi kabisa na
kutambua na kuheshimu mipaka ya nchi washirika (Zanzibar na Tanganyika)
kama ilivyokuwa kabla ya siku ya Muungano tarehe 26 Aprili, 1964. Hili
ni muhimu katika kuheshimu mamlaka ya nchi washirika katika kusimamia
mambo yasiyo ya Muungano katika maeneo yao.
Baada ya hapo, Katiba ya
Zanzibar na Katiba ya Tanganyika (itakayotungwa baada ya kupata Katiba
mpya ya Muungano) kila moja iweke wazi mipaka yake.
Jambo zuri ni kwamba
wakati zinaungana, Zanzibar na Tanganyika zilikuwa tayari ni nchi zenye
mamlaka kamili zikiwa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na hivyo kila
moja ilikuwa na mipaka yake inayoeleweka ambayo ilitajwa katika Katiba
za Uhuru za Tanganyika na Zanzibar.
Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1961 inafafanua eneo la Tanganyika kupitia Ibara ya 89(1) yenye tafsiri kama ifuatavyo:
“Tanganyika” means the
territory that, immediately before the ninth day of December, 1961, was
comprised in the Trust Territory of Tanganyika under United Kingdom
administration;
Yaani “Tanganyika” maana
yake ni eneo ambalo, mara kabla ya tarehe 9 Desemba, 1961,
lilijumuishwa kwenye Eneo la Amana la Tanganyika lililokuwa chini ya
utawala wa Uingereza;
Na kwa upande wa
Zanzibar, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1963 inafafanua eneo la Zanzibar
kupitia Ibara ya 136 yenye tafsiri kama ifuatavyo:
“The State of Zanzibar”
means the Islands of Zanzibar, Pemba and Latham including the
territorial waters thereof, and any islets within those waters;
Yaani “Dola ya Zanzibar”
maana yake ni visiwa vya Unguja, Pemba na Latham pamoja na eneo lake la
bahari, na visiwa vyovyote vidogo vilivyomo kwenye eneo hilo la bahari;
SEHEMU YA PILI:
Ibara ya 8:
Mamlaka na Utii wa Katiba
Ibara hii inapaswa
itamke wazi kwamba Ukuu wa Katiba hii utahusika na mambo ya Muungano tu
kama yalivyo kwenye Nyongeza ya Katiba. Hivyo basi, Ibara Ndogo ya 8(1)
mwishoni iongezewe maneno, “kwa kadiri yatakavyohusika na utekelezaji wa mambo ya Muungano”.
Kwa msingi huo huo,
Ibara Ndogo ya 8(4) inapaswa iongezewe maneno kwamba sheria, mila,
desturi au uamuzi ambao hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya
Katiba hii utakuwa batili “kwa kadiri utakavyokuwa unahusu utekelezaji wa mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa kwenye Nyongeza ya Katiba hii”.
Hili ni muhimu kwa
sababu katika Rasimu ya Katiba Mpya kuna suala la Haki za Binadamu
(ambalo tutalitolea maoni makhsusi tutakapofikia kujadili Sura ya Nne ya
Rasimu ya Katiba). Ibara ya 8(3) isipobainisha wazi kwamba sheria,
mila, desturi au uamuzi unaokusudiwa ni kuhusiana na mambo ya Muungano
tu, utekelezaji wake unaweza ukaja ukaleta mtafaruku hasa ikizingatiwa
sehemu ya mfumo wa sheria wa nchi mshirika mmoja (Zanzibar) inatambua
sheria za kiislamu katika mambo ya kifamilia na mfumo huo umewekewa
Mahkama ya Qadhi ambayo uwezo wake unatambuliwa ndani ya Katiba ya
Zanzibar.
Mahkama mara nyingi
hutafsiri mfumo wa ulinzi wa haki za binadamu katika kila nchi kulingana
na mazingira ya nchi husika. Mfumo huu usipowekwa wazi unaweza kuja
kusababisha migongano au mitafaruku isiyo na sababu baina ya mamlaka ya
Shirikisho na mamlaka ya nchi washirika na kwa madhumuni ya maelezo haya
inakusudiwa zaidi Zanzibar.
SURA YA SITA YA RASIMU – MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO
Sura ya Sita yenye ibara
tisa kuanzia Ibara ya 60 hadi 69 inahusu muundo wa Muungano. Ni maoni
yetu kwamba ili kufahamu maoni ya wajumbe walio wachache kuhusiana na
muundo wa Muungano, ni vizuri kwanza kujikumbusha hali halisi ya
Muungano ilivyo katika miaka hamsini iliyopita ili kujua ni muundo upi
unaweza kutuondoa katika hali iliyopo sasa.
MISUKOSUKO KATIKA MUUNGANO
Muungano wa Zanzibar na
Tanganyika umepita katika masaiba kadhaa tokea kuasisiwa kwake miaka 50
iliyopita lakini mtikisiko ulioukumba katika siku za karibuni ni mkubwa
sana. Ni mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu ambapo suala
linaloulizwa ni iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika baadhi ya
mambo, je, Zanzibar na Tanganyika zimejifuta na hivyo kupoteza hadhi
zake kama nchi? Hilo limekuwa ndiyo suala kubwa linaloulizwa na wananchi
wa Tanganyika na Zanzibar hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kutamka Bungeni kwamba Zanzibar si nchi.
Hakuna awezaye kubisha
kwamba tokea kuasisiwa kwake, Muungano huu umejengeka kutokana na
misingi ya khofu, kutiliana shaka na kutokuaminiana baina ya pande mbili
zinazouunda, ambako wakati mwengine kumepelekea hata kutishia uhai wa
Muungano wenyewe.
Muungano umekuwa gumzo
kuu katika takriban kila mjadala wa katiba na siasa katika nchi yetu.
Umejitokeza na kujionyesha hivyo katika mwaka wa mwanzo wa Muungano
kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi
kwa upande wa Tanganyika na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa
upande wa Zanzibar, kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
mwaka 1964 – 1966, wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU kuunda
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, katika mjadala wa marekebisho ya
Katiba wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar
Sheikh Aboud Jumbe, wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi Maalim
Seif Sharif Hamad na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake 6 mwaka
1988, katika harakati za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na
Muungano huo mwaka 1989/90, wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi
mwaka 1991, katika sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za
Kiislamu (OIC) mwaka 1993, wakati wa mjadala wa G-55 kudai kuanzishwa
kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, katika mjadala
wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano mwaka 1994/95, wakati
wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na karibuni kabisa
kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar,
harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki na pia baada ya
kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984
yaliyofanywa mwaka 2010.
Ukiondoa kuibuka kwake
katika mijadala mikubwa ya kikatiba na kisiasa nchini, kwa upande
mwengine katika uendeshaji wa shughuli za Serikali za kila siku,
“matatizo na vikwazo kadhaa ya kiutawala na kiutendaji” vimekuwa
vikiripotiwa kila mara kwamba vinakwamisha uimarishaji wa Muungano.
Tume na Kamati kadhaa
zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na kupendekeza njia za
kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda Tume na Kamati
zifuatazo, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala haya:
- Kamati ya Mtei
- Tume ya Jaji Francis Nyalali (1991)
- Kamati ya Shellukindo (1994)
- Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
- Kamati ya Jaji Mark Bomani (1995)
- Kamati ya Jaji Robert Kisanga (1998)
- Kamati ya ‘Harmonization’
- Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
- Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
- Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) ya 1997
- Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman)
- Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
- Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje
- Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001
- Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
- Kamati ya Mafuta
- Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
- Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
- Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu
- Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
- Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa (2004)
Ukiacha Tume, Kamati na
Ripoti hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya
Pamoja ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri Kiongozi wa
Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao ulitarajiwa uwe
ndiyo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa
Muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa. Utaratibu huu uliachwa kwa
muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya
Kikwete alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa
Serikali yake huko Ngurdoto, Arusha mwezi Februari, 2006. Mikutano hiyo
sasa imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na
Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais
kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mikutano, Makongamano,
Semina na Warsha vimefanywa kujadili masuala haya na kupendekeza hatua
za kuchukuliwa. Wasomi na wanafunzi wamefanya tafiti kadhaa na kujipatia
shahada na stashahada hadi ngazi ya Ph.D juu ya Muungano lakini bado
matatizo yako pale pale na yanaongezeka kila kukicha.
Yanayoonekana na
kuelezwa kama matatizo, mapungufu, dosari, kasoro na, kwa msamiati wa
sasa, kero yamekuwa ndiyo yale kwa yale. Kwa mtazamo wetu, sababu kuu
mojawapo iliyotufikisha hapa ni muundo wa Muungano wa Serikali Mbili
uliopo sasa na kitendo cha Tanganyika kuvaa koti la Muungano.
MKATABA WA MUUNGANO HAUJAFUTA SERIKALI YA TANGANYIKA
Katika makubaliano ya
kimataifa yaliyounda Muungano, ambayo kama tulivyoonesha hapo juu
uhalisia wake umezua mashaka makubwa kutokana na kutoonekana kwa Hati ya
Makubaliano ya Muungano, lakini hata tukichukulia kuwa hicho
kinachodaiwa kuwa Makubaliano ya Muungano kuwa ndicho, basi hakuna
kifungu hata kimoja ndani yake kilichotoa au kuagiza kwamba Serikali ya
Tanganyika ifutwe. Serikali ya Tanganyika, kama ilivyo ile ya Zanzibar,
imelindwa na kifungu cha (v) kinachosomeka kwamba: “The existing laws of Tanganyika and of Zanzibar shall remain in force in their respective territories…”. Kinachosemwa hapa ni kwamba “Sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kufanya kazi na kuwa na nguvu katika maeneo yao.”
Wataalamu wa katiba na
sheria wanafahamu kwamba katiba ndio sheria mama ya sheria zote za nchi.
Hivyo Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na Serikali
yake iwepo, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya
Muungano. Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike
katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye
Muungano kama ambavyo Katiba (au kabla ya hapo Dikrii za Kikatiba –Constitutional Decrees) na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa yale mambo ambayo si ya Muungano. Hiyo ndio tafsiri ya ‘maeneo yao’.
Wazanzibari wanafahamu
kwamba Katiba na Serikali ya Tanganyika vimefutwa kwa makusudi na
Mwalimu Julius Nyerere na Bunge la Tanganyika ili kujipa nafasi kuitumia
Serikali ya Muungano, kama kwamba ndio Serikali ya Tanganyika. Lengo ni
hatimaye kuiuwa Serikali ya Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa
na jina jipya la Tanzania lenye mipaka mipya, yaani kuwa nchi moja
yenye Serikali Moja.
Hiyo ndio ghilba
iliyofanywa na viongozi wa Tanganyika mara baada ya kutiwa saini
makubaliano. Kwa kusaidia kufichuwa ukweli wa hadaa hii, ni vyema
ikaangaliwa Sheria Na. 22 ya mwaka 1964 inayoitwa “Union of Tanganyika and Zanzibar Act, 1964.” Sheria
hii ilipitishwa na Bunge la Tanganyika Aprili 25, 1964, siku moja kabla
Muungano kuanza kufanya kazi. Ilikusudiwa kuthibitisha kukubalika
Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar upande wa Tanganyika(ratification). Kifungu cha (viii) cha Makubaliano ya Muunganokinaagiza ifanyike hivyo kwa pande zote mbili za Muungano.
Inasikitisha kusoma katika kifungu Na. 2 cha sheria hiyo kwamba:
“existing law” means
the written and unwritten law as it exists immediately before the Union
Day … but does not include the Constitution of Tanganyika insofar as it
provides for the government of the Republic of Tanganyika or any
declaration or law, or any provision thereof, which expires with effect
from commencement of the interim Constitution;”
(“Sheria iliyopo maana
yake ni sheria iliyoandikwa na isiyoandikwa kama ilivyo kabla tu ya siku
ya Muungano… lakini haijumuishi Katiba ya Tanganyika kwa mintaraf ya
kuiweka kwake Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika au tamko au sheria, au
kifungu chochote ambacho kinafutika kwa kuanza kufanya kazi Katiba ya
Muda).”
Kwa hivyo, wakati Bunge la Tanganyika linapitisha sheria ya kuridhia (ratify) kuwepo
kwa Muungano kwa upande wa Tanganyika, sheria hiyo ilianza kuvunja
masharti ya vifungu vya makubaliano hayo. Mfano mwengine ni kifungu Na. 7
cha sheria hiyo kinachosema:
“7. On the
commencement of the interim Constitution of the United Republic, the
Constitution of Tanganyika shall cease to have effect for the government
of Tanganyika as a separate part of the United Republic”.
(“Itapoanza kufanya kazi
Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Tanganyika itasita
kuwa na nguvu kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika kama sehemu nyengine
ya Jamhuri ya Muungano.”)
Kwa maneno mengine,
sheria ambazo zilitakiwa zitumike Tanganyika kwa mambo ambayo si ya
Muungano zilipewa maana mpya kwamba eti zisijumuishe Katiba ya
Tanganyika.
Jambo moja lililo wazi,
pamoja na hatua hii ya kuifuta Katiba ya Tanganyika, ni kwamba kule
kuendelea kutambua kuwepo kwa sheria nyengine za Tanganyika bado
kunamaanisha kuwepo kwa mamlaka ya Tanganyika ambako sheria hizo kwa
mambo yote yasiyo mambo ya Muungano ziliendelea na zinaendelea kutumika
hadi leo.
Zaidi, inapaswa
ifahamike kwamba kufuta Katiba ya Tanganyika kulikofanywa na vifungu vya
sheria hii hakukubadilisha makubaliano yaliyokwishatiwa saini kati ya
Serikali mbili zilizounda Muungano, yaliyosema kwamba sheria za nchi
mbili hizi zitaendelea kutumika katika maeneo yao.
Bunge la Tanganyika, na hata Bunge la sasa la Muungano, halikuwa na
mamlaka kutafsiri vifungu vya Mkataba wa Muungano ambao ni mkataba wa
kimataifa.
Utaratibu wa kisheria ni
kwamba kama Mkataba ulitakiwa kutafsiriwa basi mkataba huo ulipaswa
kutoa tafsiri ya vifungu vyake, tafsiri ambayo ingepaswa iwe sehemu ya
Mkataba huo. Na wala makubaliano yale hayakufuta wadhifa wa Rais wa
Tanganyika. Si hivyo tu, bali pia Katiba ya Muungano ambayo ilitakiwa
iwe ya muda tu kwa mwaka mmoja (interim) ilikuwa ni ile ya Tanganyika iliyofanyiwa marekebisho kwa ajili ya kutumika kwa Serikali ya Muungano.
Haikuruhusiwa kutumika
kuiongoza Tanganyika kwa sababu Tanganyika ilikuwa na Katiba yake na
Rais wake. Mwalimu Nyerere alikuwa na vyeo viwili, Rais wa Jamhuri ya
Muungano kwa mujibu wa Makubaliano na Katiba ya Muungano na Rais wa
Tanganyika kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika, kama alivyokuwa Mzee
Karume ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu
wa Makubaliano na Katiba ya Muungano na akaendelea kubaki kuwa Rais wa
Zanzibar kwa mujibu wa Dikirii za Katiba ya Zanzibar (Constitutional Decrees).
Hivyo ndivyo makubaliano
yalivyokuwa na ndivyo yalivyopaswa yawe hadi hii leo. Waliobadilika ni
watu tu. Kufanya vyenginevyo ni kinyume na makubaliano yale na ndio
sababu ya migogoro ya Muungano.
Hatua zote za kuepusha
Serikali ya Tanganyika kuwepo zilifanywa kwa makusudi kabisa, ili
itumike Serikali ya Muungano kama ndio Tanganyika. Katika Sheria ile Na.
22 ya 1964, Rais wa Tanganyika amejipa madaraka ya kutunga na kutoa
maagizo yanayohusu Muungano kwa kutumia amri (Decrees) za Sheria ya Tanganyika.
Siku moja tu baada ya kupitishwa Sheria Na. 22 ya 1964, Rais Julius Nyerere alitoa Amri za Rais (Decrees) mbili zilizotokana na kifungu cha 5(2), cha 7(2) na (3), na cha 10 vya Sheria hiyo Na. 22 ya 1964, yaani The Provisional Transitional Decree 1964, na ile ya Interim Constitution Decree 1964 ambazo zilifanya mabadiliko makubwa ya Muungano nje ya yale makubaliano yaliyokuwemo katika Mkataba wa Muungano.
Miongoni mwa mambo
yaliyodhihirisha kuwa hakukuwa na nia njema katika Muungano huu tokea
awali ni pale watumishi wa Serikali ya Tanganyika wote, bila kujali kama
wanashughulikia mambo ya Muungano au mambo yasiyo ya Muungano,
walipopandishwa vyeo kwa pamoja na kufanywa watumishi wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano kama kifungu cha 3(1) cha Provisional Transitional Decree kinavyosema:
“Every person who
holds office in the service of the Republic of Tanganyika immediately
before the Union Day, shall on the Union Day be deemed to have been
elected, appointed or otherwise selected to the corresponding office in
the service of the United Republic.”
Yaani kila mtumishi wa Serikali ya Tanganyika mara kabla ya siku ya Muungano kufumba na kufumbuwa (au tuseme kwa mtindo wa abra cadabra) anakuwa mara moja mtumishi wa Serikali ya Muungano kuanzia siku ya Muungano.
Vivyo hivyo, kifungu cha 6(1) cha Provisional Transitional Decree kinasema
mara tu baada ya kuanza Muungano, Mahkama ya Tanganyika na Majaji wake
wote nao watakuwa ndio Mahkama na Majaji wa Jamhuri ya Muungano kinyume
na Makubaliano ya Muungano. Hati ya Makubaliano ya Muungano na hata
Katiba ya Jamhuri ya Muungano mpaka leo hazitambuwi Mahkama kama ni
suala la Muungano (ukiondoa Mahkama ya Rufaa, ambayo nayo kuongezwa
kwake kama jambo la Muungano kumejaa utatanishi). Nembo ya Tanganyika
inatumika kama nembo ya Jamhuri ya Muungano, Wimbo wa Taifa wa
Tanganyika unatumika kama Wimbo wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano na Idara
ya Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika inachukuliwa kama Idara ya
Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.
Haya yote hayamo na ni
kinyume na Makubaliano ya Muungano ya 1964. Yote haya na kile kifungu
cha 7 cha Sheria Na. 22 ya 1964 kinachofuta kuwepo kwa Serikali ya
Tanganyika hayakubadilisha na wala hayana mahusiano na Makubaliano ya
Muungano ya 1964. Yote haya yalifanywa na Rais Julius Nyerere kwa
maslahi ya Tanganyika nje ya Mkataba wa Muungano.
Aliyekuwa Spika wa Bunge
na baadaye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Pius Msekwa,
analifahamu vyema suala hili. Katika waraka wake alioutoa kwenye Semina
kuhusu Muungano hapo Hoteli ya Mkonge, Tanga tarehe 25—27 Februari 1994
anasema:
“The Transitional
Decree, 1964 published on 01/05/64, transferred persons who were holding
office in the public service of the Republic of Tanganyika to the
corresponding office in the public service of the United Republic of
Tanzania. By the same decree the High Court of Tanganyika also became
the High Court of United Republic of Tanzania and the public seal of
Tanganyika became public seal of the United Republic.”
Athari za hatua hizi kwa
Zanzibar ziko wazi. Tanganyika imejigeuza Tanzania na imechukua mamlaka
ya mambo muhimu ya Zanzibar huku ikijipa hadhi ya kuwa juu ya Serikali
ya Zanzibar kinyume na Mkataba wa Muungano.
Hii ndiyo siri ya
viongozi wa Tanganyika wanaoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano
kung’ang’ania mfumo wa Serikali mbili na kukataa kata kata mabadiliko
yoyote ya mfumo huo kwani Tanganyika inanufaika nao kwa kuwa yenyewe
ndiyo imekuwa ‘Muungano’. Hili limethibitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, katika hotuba yake ya
uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum. Kukubali muundo wa
Serikali tatu ni kuzifanya Tanganyika na Zanzibar ziwe na hadhi na
fursa sawa katika Muungano, jambo ambalo Tanganyika hailitaki maana
kulikubali ni kukubali kupoteza fursa zote inazozipata hivi sasa kwa
kujikweza kwake na kujifanya kuwa ndiyo ‘Muungano’.
Ushahidi wa wazi wa hoja
hii ni kwamba mtu anapoangalia taasisi zote za Muungano zilizoundwa
chini ya Katiba au sheria za Muungano ambazo zinazikutanisha Serikali
mbili zilizopo sasa, ataona kuwa wajumbe wanaowakilisha upande wa
Serikali ya Muungano wote ni kutoka Tanganyika. Hoja inayojitokeza ni
kwamba Serikali ya Muungano ni ya shirika ambapo Zanzibar ni sehemu ya
ushirika huo, kwa nini basi wajumbe wanaowakilisha Serikali hiyo ya
Muungano watoke upande wa Tanganyika peke yake? Jawabu ni rahisi.
Serikali ya Muungano kwa hakika ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika
koti la Muungano.
Katiba ya Muda ya 1965 na ya 1977 zaitambua Tanganyika
Kuthibitisha zaidi
kwamba Tanganyika haikufutwa na wala haikufutika kupitia Makubaliano ya
Muungano ya 1964, mtu ataona kwamba bado inatambuliwa hata katika
Katiba ya Muda ya 1965 na hata kuwekewa Mkuu wake wa kushughulikia mambo
yanayoihusu kama ambavyo Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Zanzibar
anayeshughulikia mambo yanayoihusu.
Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Muda ya 1965 inaeleza kwamba:
“13.-(1) There shall be
two Vice-Presidents of the United Republic (who shall be styled the
First Vice-President and the Second Vice-President respectively), one of
whom shall be the principal assistant of the President in the discharge
of his executive functions in relation to Zanzibar and, under the style
of President of Zanzibar, the head of the Executive for Zanzibar, and
the other shall be the principal assistant of the President in the
discharge of his executive functions in relation to Tanganyika and the
leader of Government business in the National Assembly.”
Tafsiri yake kwa Kiswahili ni kwamba:
“13.-(1) Kutakuwa na
Makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano (ambao wataitwa Makamu wa
Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais), ambapo mmoja wao atakuwa ni
msaidizi mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake za kiutendaji kwa
Zanzibar na, kwa cheo cha Rais wa Zanzibar, atakuwa ndiye Kiongozi wa
Serikali ya Zanzibar, na mwengine atakuwa ni msaidizi mkuu wa Rais
katika kutekeleza kazi zake za kiutendaji kwa Tanganyika na Kiongozi wa
Shughuli za Serikali ndani ya Bunge.”
Mbali ya Ibara hiyo
kuitambua Tanganyika na kumtaja Makamu wa Pili wa Rais kama Msaidizi
Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika majukumu yake ya kiutendaji
kwa upande wa Tanganyika, sheria nyingi zilizotungwa kati ya 1964 na
1977 ziliendelea kutumia jina la Tanganyika.
Kwa hakika, jina la
Tanganyika kama jina la nchi moja kati ya nchi mbili zilizounda Muungano
lilifutwa na Katiba ya 1977; ijapokuwa Katiba hiyo hiyo ya 1977 (pamoja
na marekebisho yake yote yaliyofanyika hadi sasa) bado inaendelea
kuitambua Tanganyika. Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili
inayofanya rejea kwenye Ibara ya 98(1)(a) ya Katiba na kutaja mambo
ambayo maamuzi yake yanahitaji theluthi mbili ya Wabunge wote wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano inataja mojawapo ya mambo hayo kuwa ni:
“Sura ya 500, (Toleo la 1965), Sheria ya kuthibitisha Tanganyika kuwa Jamhuri, ya mwaka 1962.”
Iwapo Sheria hiyo
inaendelea kutambuliwa na hata kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ya 1977, je, ni Jamhuri ipi iliyozaliwa 1962 ambayo kuibadilisha
kunahitaji theluthi mbili ya Wabunge wote kama si Jamhuri ya Tanganyika?
UVUNJWAJI WA MKATABA WA MUUNGANO
Mbali na suala la muundo
wa Muungano, maeneo mengine mengi yanayogusa msingi wa Mkataba wa
Muungano yaliendelea kuvunjwa na Tanganyika ikivaa koti la Serikali ya
Muungano.
Mambo ya Muungano na Mamlaka ya Zanzibar:
Kifungu cha (iv) cha
Mkataba wa Muungano kiliorodhesha mambo 11 tu ambayo ndiyo
yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika
kuwa mambo ya Muungano. Hata hivyo, kipindi cha miaka 50 ya Muungano
kimeshuhudia mambo hayo yakiongezwa isivyo halali kwa kutumia chombo
kisicho na mamlaka ya kufanya hivyo yaani Bunge la Muungano na sasa
kufikia 22 lakini ukiyanyumbua yanafikia 31. Mfano unakuta kifungu
kimoja cha 11 kinayaweka pamoja mambo manne ambayo ni Bandari, Usafiri
wa Anga, Posta na Simu. Kwa lugha ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe.
Othman Masoud Othman, anasema ni makontena 22 yenye mambo 31 ya
Muungano. Ikumbukwe kwamba kila hatua ya kuongeza mambo ya Muungano
maana yake ni kuchukua mamlaka ya Zanzibar na kuyahamishia kwa Serikali
ya Muungano ambayo kama tulivyokwisha onesha kwa hakika hasa ni Serikali
ya Tanganyika iliyojivika koti la Muungano.
Mambo ya awali ya
Muungano ambayo yanatajwa katika kile tunachoambiwa ndiyo Hati ya
Makubaliano ya Muungano ni kumi na moja (11) na ni haya yafuatayo:
(i) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(ii) Mambo ya Nje.
(iii) Ulinzi.
(iv) Polisi.
(v) Mamlaka juu ya Hali ya Hatari.
(vi) Uraia.
(vii) Uhamiaji.
(viii) Mikopo na Biashara ya Nje.
(ix) Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(x) Kodi ya Mapato na Kodi ya Mashirika, Ushuru wa Forodha na Kodi ya Bidhaa.
(xi) Bandari, Usafirishaji wa Anga, Posta na Simu.
Mambo yaliyoongezwa juu
ya Makubaliano ya Muungano ya asili, yaani, yale kumi na moja (11) ni
haya, kama yanavyoelezwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano:-
(xii) Mambo
yote yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali
(pamoja na noti); mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo
yanayohusika na fedha za kigeni.
(xiii) Leseni za Viwanda na Takwimu.
(xiv) Elimu ya Juu.
(xv) Maliasili
ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya
petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa za mafuta, na gesi
asilia.
(xvi) Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
(xvii) Usafiri na Usafirishaji wa Anga.
(xviii) Utafiti.
(xix) Utabiri wa Hali ya Hewa.
(xx) Takwimu.
(xxi) Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
(xxii) Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo.
Ukiondoa mambo hayo,
yapo pia mambo mengine ya ziada ambayo yameingizwa katika Muungano kwa
Bunge tu kutunga sheria kwa kutumia Ibara ya 64(4) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ya 1977 na kutangaza kwamba zitatumika hadi Zanzibar. Mfano
wa masuala kama hayo ni Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Utawala Bora na
Haki za Bianadamu. Yapo baadhi yake kwa mfano Usafiri wa Baharini ambapo
Zanzibar ilikataa kutekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge (The Merchant Shipping Act) na hatimaye ikatunga sheria yake yenyewe kuhusiana na suala hilo (The Maritime Transport Act).
Lakini kuendelea kupora
mamlaka ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano hakukuishia hapo. Kwa
kutumia mwanya wa uanachama mmoja wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika
Mashariki; dhamana juu ya mambo mengine kumi na tatu (13) yamechukuliwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano bila ya ridhaa ya Zanzibar. Hali hiyo
inatokana na ukweli kwamba Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
umeweka mambo kumi na saba (17) yanayosimamiwa na Jumuiya hiyo lakini
kati ya hayo, kwa upande wa Tanzania, ni mambo manne (4) tu ndiyo yaliyo
katika mambo ya Muungano na hivyo kuwemo katika mamlaka ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano. Mambo hayo manne (4) ni haya yafuatayo:
- Ushirikiano katika mambo ya Fedha na Uchumi (Monetary and Financial Co-operation);
- Uhuru wa Mtu kwenda
atakapo, Uhuru wa Huduma za Kazi, na Haki ya Ukaazi (Free Movement of
Persons, Labour Services, Right of Establishment and Residence);
- Mahusiano na Jumuiya
za Kikanda na Kimataifa na Washirika wa Maendeleo (Relations with other
Regional and International Organisations and Development Partners); na
- Ushirikiano katika Mambo ya Siasa (Cooperation in Political Matters).
Ukiondoa mambo hayo
manne (4), mambo mengine kumi na tatu (13) yaliyomo katika Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki si mambo ya Muungano na hivyo ni dhamana ya
mamlaka ya Zanzibar lakini yameporwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
na kujitwisha dhamana ya kuyasimamia katika Jumuiya hiyo. Mambo hayo ni
haya yafuatayo:
- Ushirikiano katika Kufungua Milango ya Biashara na Ukuzaji wake (Cooperation in Trade Liberalisation and Development);
- Ushirikiano katika Maendeleo ya Uwekezaji na Viwanda (Cooperation in Investment and Industrial Development);
- Ushirikiano katika
Uwekaji Viwango, Uhakika wa Ubora, na Upimaji (Cooperation in
Standardisation, Quality Assurance, Meteorology and Testing);
- Ushirikiano katika Miundombinu na Huduma (Cooperation in Infrastructure and Services);
- Ushirikiano katika
Uendezaji wa Rasilimali Watu, Sayansi na Teknolojia (Cooperation in the
Development of Human Resources, Science and Technology);
- Kilimo na Uhakika wa Chakula (Agriculture and Food Security);
- Ushirikiano katika Usimamizi wa Mazingira na Maliasili (Cooperation in Environment and Natural Resources Management);
- Ushirikiano katika Usimamizi wa Utalii na Wanyamapori (Cooperation in Tourism and Wildlife Management);
- Afya na Masuala ya Kijamii na Kiutamaduni (Health, Social and Cultural Activities);
- Uimarishaji wa
Nafasi ya Wanawake katika Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii (Enhancing
the Role of Women in Socio-Economic Development);
- Masuala ya Sheria na Mahkama (Legal and Judicial Affairs);
- Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia (The Private Sector and the Civil Society);
- Ushirikiano katika Maeneo mengine (Cooperation in other Fields).
Ni wapi Serikali ya
Jamhuri ya Muungano imepata mamlaka ya kuyasimamia mambo haya kumi na
tatu (13) ambayo ndiyo msingi wa mamlaka ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya
Muungano? Jibu la mkato lingekuwa ni kwamba ukishaingia katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki basi umeingia katika mamalaka juu ya Mambo ya Nje.
Lakini kama jibu hilo litakuwa sahihi maana yake ni kwamba ukiingia
katika Mambo ya Nje, Zanzibar itakuwa haina chake – mambo yake yote
yatakuwa chini ya Muungano – na katika hali halisi hivyo ndivyo ilivyo.
Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais:
Mbali na dhoruba hizo
dhidi ya Mkataba wa Muungano, rungu jengine kubwa dhidi ya Mkataba wa
Muungano lilikuwa ni kuvunjwa kwa masharti ya kifungu (iii)(b) cha
Mkataba huo ambacho kiliweka utaratibu wa Rais wa Zanzibar kuwa
mmojawapo wa Makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Sharti hili
liliwekwa makusudi kabisa ili kuweka kiungo baina ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na pia kumhakikishia
Rais wa Zanzibar dhamana na uwezo wa kusimamia maslahi ya Zanzibar kwa
mambo ya Muungano ambayo Zanzibar imeyatoa kwa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano.
Uhakikisho huu
ulitupiliwa mbali na kuvunjwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano bila ya
kujali kwamba yalikuwa ni masharti muhimu ya Mkataba wa Muungano ukiwa
ni Mkataba wa Kimataifa ulioziunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar. Lililo baya zaidi ni kwamba katika kufanya hivyo
hata yale masharti ya kuhitajika kuungwa mkono na theluthi mbili ya
Wabunge wote wanaotoka Zanzibar na theluthi mbili ya Wabunge wote
wanaotoka Tanzania Bara halikuzingatiwa. Hansard ya Majadiliano ya Bunge
ya Mkutano wa Ishirini (Sehemu ya Pili) ya tarehe 25 Aprili, 1995 – 3
Mei, 1995 yanamnukuu aliyekuwa Spika wa Bunge, Mhe. Pius Msekwa, katika
ukurasa wa 958, akielekeza:
“… Orodha za Wabunge
mlizonazo za mwezi Februari zinaonyesha, idadi halisi ya Wabunge ni 245,
baada ya Ndugu Mrema kupoteza Ubunge, idadi halisi ya Wabunge ni 244.
Theluthi mbili ya Wabunge 244 ni 163, hiyo idadi ndiyo ya chini
inayotakiwa kupitisha Muswada wa Kikatiba. Na kwa sura iliyoletwa ni
theluthi mbili ya Bunge Zima siyo theluthi mbili ya kila upande, kwa
hiyo tutapiga kura kutafuta theluthi mbili ya Bunge Zima, nafikiri hiyo
imeeleweka. Sasa tufanye uamuzi ile hatua ya kwanza kama nilivyosema.”
Maelekezo haya
yalipokuwa yakitolewa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano alikuwa ni Mhe. Andrew Chenge ambaye leo hii ni Mjumbe wa Bunge
hili Maalum la Katiba. Maelekezo hayo yalitolewa kinyume na masharti ya
Ibara ya 98(1)(b) ambayo imetaja mambo yaliyoorodheshwa kwenye Orodha
ya Pili ya Nyongeza ya Pili ya Katiba kama mambo yanayohitaji theluthi
mbili za kila upande. Orodha ya Pili kwenye jambo namba tano (5) inataja
kuwa ni “Madaraka ya Serikali ya Zanzibar”. Hakuna mtu makini
atakayebisha kwamba kumuondolea Rais wa Zanzibar ambaye ndiye Kiongozi
wa Serikali ya Zanzibar nafasi yake ya kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano ni kuathiri “Madaraka ya Serikali ya Zanzibar”. Lakini bado
sharti la theluthi mbili za kila upande lilipuuzwa.
Kipindi cha Mpito kuwa cha Mwaka Mmoja:
Kifungu cha (vii) cha
Mkataba huo kinataka Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mashauriano na
makubaliano na Makamu wa Rais ambaye pia ni Rais wa Zanzibar kuunda Tume
ya Katiba kwa lengo la kutayarisha rasimu ya Katiba ya Kudumu ya
Muungano na baadaye kuifikisha rasimu hiyo mbele ya Bunge la Katiba
(Constituent Assembly) litakalokuwa na wajumbe kwa idadi
watakayokubaliana kutoka Zanzibar na Tanganyika. Hatua hii muhimu sana
kikatiba ilitakiwa itekelezwe ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tokea
tarehe ya Muungano. Hadi ilipokuja hatua hii ya sasa ya kuunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, hakuna Tume ya Katiba iliyoundwa wala Bunge la
Katiba lililoundwa na kuitishwa kwa madhumuni ya kupitisha Katiba ya
Kudumu ya Muungano. Kilichofanyika ni kuwa mwezi mmoja kabla ya
kumalizika mwaka mmoja uliotakiwa, Bunge la Muungano lilitakiwa na
Mwalimu Julius Nyerere kupitisha sheria ya kuahirisha kwa muda
usiojulikana tarehe ya kutekelezwa kwa hatua hii. Nani alimpa madaraka
hayo Mwalimu Nyerere na Bunge la Muungano kubadilisha masharti ya
Mkataba wa Muungano ambao ni Mkataba wa Kimataifa wakati Mkataba huo
haukutoa fursa kwa chombo chochote kubadilisha masharti yaliyomo?
Wengine wanadai kwamba
sharti hili lilitekelezwa mwaka 1977 pale Mwalimu Julius Nyerere
alipoitangaza Kamati ya Watu 20 iliyoundwa na TANU na ASP kutayarisha
Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa pia imepewa mamlaka ya kuandaa
Rasimu ya Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano na baadaye kulitangaza
Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa ndilo Bunge la Katiba. Kila mmoja
anajua kwamba Kamati hii haikuandaa rasimu hiyo bali ilipewa tu Rasimu
iliyokwisha tayarishwa. Na hata pale Mswada wa Katiba hiyo
ulipowasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo liliitwa
ndiyo Bunge Maalum la Katiba mjadala haukuzidi muda wa saa mbili na
ulikuwa zaidi wa kupongeza na kushangilia tu. Hivi kweli mtu makini
anaweza kusema kwamba utaratibu ule ulikuwa ni utekelezaji wa masharti
ya kifungu cha (vii) cha Mkataba wa Muungano?
MATATIZO YATOKANAYO NA KIINI CHA TATIZO
Kiini cha tatizo la msingi la Muungano ambalo ni muundo wake unaotokana na tafsiri potofu ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ndicho kimepelekea kujitokeza kwa matatizo mengine katika miaka 50 hii na ambayo yanaongezeka kila kukicha.
Mtu anapoangalia
matatizo au hizi zinazoitwa kero atagundua kuwa karibu yote yanatokana
aidha kwa mshirika mmoja (mara nyingi Zanzibar) kutokuuamini au kuutilia
shaka upande mwengine, au mshirika wa pili (mara nyingi Tanganyika
ikivaa koti la Muungano) kuamini kwamba ina haki ya moja kwa moja kuamua
na kutekeleza mambo fulani bila ya kulazimika kupata ridhaa ya upande
wa pili ambao inahisi kama imeubeba tu (au kwa lugha ya Mhe. Pius Msekwa
ni “invited guest” yaani mgeni mwalikwa). Ukiangalia kwa undani
utagundua kuwa tatizo linarudi kwenye muundo. Zanzibar haifahamu mamlaka
ya Muungano katika Serikali ya Muungano yanaishia wapi ambapo mamlaka
kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa ajili ya Tanganyika yanaanza.
Tanganyika nayo kwa kuwemo kwake katika Serikali ya Muungano kunaifanya
ishindwe kufahamu ni vipi na wapi Zanzibar inapata mamlaka ya kuhoji
mambo ambayo yameshatamkwa kwamba ni ya Muungano hata kama hayakuwemo
katika Mkataba wa asili wa Muungano. Hali hii inaonekana katika kila
kile kinachoitwa “Kero za Muungano”.
Mifano inaweza kutolewa kwa takriban mambo yote, lakini tuchukue mifano ya mambo matatu yafuatayo yanayozusha malalamiko:
- Umilikaji wa Mafuta na Gesi asilia.
- Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano.
- Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.
Umilikaji wa Mafuta na Gesi asilia
Kwanza, kuingizwa kwake
katika orodha ya mambo ya Muungano (kama ilivyo kwa mambo mengi
yaliyoongezwa baadaye) hakukufuata taratibu za Serikali ya Muungano
(ambayo pia ni Serikali ya Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano)
kuishauri na kupata ridhaa ya Zanzibar. Pili, Zanzibar inataka kujua
ikiwa mafuta yanapaswa kuwa suala la Muungano na hivyo mapato
yatakayopatikana yanufaishe pande zote mbili, kwa nini madini mengine
yanayopatikana Bara kama vile dhahabu, almasi au tanzanite hayakufanywa
pia kuwa ya Muungano na hivyo kunufaisha pande mbili pia? Kwa hivi sasa,
ambapo si mambo ya Muungano, mapato yake yanaponufaisha Tanganyika peke
yake, yanaingia katika mfuko (account) upi wa matumizi? Tatu,
kwa miaka isiyopungua tisa (9) sasa, Tanganyika imekuwa ikivuna gesi
asilia huko Songosongo na Mnazi Bay na kwa miaka miwili sasa imekuwa
ikivuna gesi asilia kwa wingi katika maeneo ya bahari iliyopakana na
Mtwara lakini pamoja na kutajwa suala hilo kuwa la Muungano, Zanzibar
haijafaidika na chochote kutokana na mapato yake. Nne, ikiwa mapato
yatakayopatikana kutokana na mafuta na gesi asilia yataingia katika
mfuko wa Muungano, kuna uhakika gani wa kutumika kwa shughuli za
Muungano tu wakati hakuna mifuko tofauti ya fedha kwa shughuli za
Muungano na zile za Tanganyika zisizo za Muungano?
Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano
Je, mtu anaposema
Zanzibar haichangii gharama za uendeshaji wa vyombo na taasisi za
Muungano kwa sababu tu Serikali ya Zanzibar haitoi fungu la fedha na
kuliingiza katika Serikali ya Muungano, Tanganyika ambayo hata Serikali
haina inachangia vipi na kiasi gani? Ikiwa mchango wake unatolewa na
Serikali ya Muungano, kwani hii siyo serikali ya shirika ambapo Zanzibar
pia ni mbia? Vipi basi Zanzibar itakiwe ichangie mara mbili kwa kutumia
hadhi mbili tofauti? Na ikichangia (iwapo itachangia), ina uhakika upi
kwamba itakachotoa hakitatumiwa na Serikali ya Muungano kwa shughuli za
Tanganyika zisizo za Muungano ikitumia mamlaka yake kwa madhumuni hayo?
Vivyo hivyo, kwa mapato yatokanayo na vyombo na taasisi za Muungano,
tunajua Zanzibar inapata mgao wake na kiasi chake kimewekwa wazi (ingawa
kwa sasa ni mapato ya TRA yanayokusanywa Zanzibar; na pia gawio kutoka
Benki Kuu (BOT) ambalo nalo kiwango chake hakikubaliki kwa Wazanzibari).
Zipo mamlaka nyengine za Kimuungano zinazoingiza mapato na ambazo
Zanzibar haipewi chochote kutoka kwake zikiwemo TCRA, TCAA, TPC, TTCL,
na TPDC kwa kutaja chache. Masuala zaidi yanakuja: Yale mapato
yanayobaki katika Serikali ya Muungano, kuna kipi cha kuonesha mpaka wa
matumizi yake kwa mambo ya Muungano na kwa shughuli za Tanganyika zisizo
za Muungano? Uadilifu na uwajibikaji wa matumizi yatokanayo na mgao huu
wa mapato utaonekana vipi?
Ukweli hasa kuhusiana na
suala la uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato
yanayotokana na Muungano ulipatikana kufuatia kuundwa kwa Tume ya Pamoja
ya Fedha (Joint Finance Commission) ambayo iliajiri wataalamu (consultants) kutoka taasisi inayoheshimika duniani yaPriceWaterhouseCoopers kuangalia
suala hilo. Ripoti ya Wataalamu ilitolewa Agosti 2006 na kufanyiwa kazi
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini hadi leo imekaliwa na
Serikali ya Muungano bila shaka baada ya kutoa picha isiyopendeza kwa
upande wa Tanganyika kuhusiana na hali halisi ya vipi uendeshaji wa
Muungano ulivyo. Wataalamu wa Kampuni ya PriceWaterhouseCoopers walifanya
uchambuzi halisi wa mambo yepi ni ya Muungano na yepi ni ya Tanganyika
na yepi ni ya Zanzibar na gharama za uendeshaji wa kila moja. Baada ya
orodha kupatikana, watafiti wakatafuta matumizi halisi ya bajeti ya
vifungu hivyo kwa muda wa kiasi cha miaka 10 iliyopita. Watafiti hao
walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu
cha mambo ya Muungano halisi. Mwishowe, wakalinganisha iwapo mapato
yanakidhi matumizi au yana nakisi (upungufu)? Taarifa ya Tume ya ya
Pamoja ya Fedha inayoitwa “Mapendekezo ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato na Kuchangia Gharama za Muungano” ya Agosti, 2006 inaeleza kwenye ukurasa wa 18:
“Uchambuzi unaonyesha
kuwa mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi matumizi ya
Muungano na kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu zinaonyesha kuwa kiasi
kidogo cha mapato hayo kimekuwa kinagharimia matumizi ya Muungano. Kwa
mfano, uwiano huu ulikuwa ni Sh. 360,679.87 milioni kati ya Sh.
1,030,513.9 milioni sawa na asilimia 35 mwaka 1999/2000, Sh. 468,450.76
milioni kati ya Sh. 1,801,733.7 milioni sawa na asilimia 26 mwaka
2002/03, na Sh. 636,078.94 milioni kati ya Sh. 2,271,710.5 milioni sawa
na asilimia 28 mwaka 2003/04.
Uchambuzi unaonyesha
kuwa kiasi kikubwa cha ziada ya mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika
kugharimia mambo yasiyo ya Muungano. Viwango hivi kwa mwaka 1999/2000
vilikuwa ni Sh. 39,822.7 milioni sawa na asilimia 5.9 kwa SMZ na Sh.
631,714.4 milioni sawa na asilimia 94.1 kwa Tanzania Bara. Viwango hivi
vilibadilika kwa kiasi kikubwa kwa mwaka wa fedha 2003/04 ambapo kwa SMZ
kilishuka hadi Sh. 37,053.3 milioni sawa na asilimia 2.3, na Sh.
1,588,494.1 milioni sawa na asilimia 97.7 kwa SMT.”
Ukweli huu unaonesha
hata kama kungekuwa na Serikali Tatu kusingekuwa na haja yoyote kwa
Serikali ya Zanzibar na ile ya Tanganyika kulipia fedha za ziada kama
wahusika watatunza na kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ya
mambo ya Muungano halisi badala ya yale ya Tanganyika kuchanganywa na ya
Muungano. Mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika yalipotengwa nje
ya yale ya Muungano, gharama za mambo ya Muungano zimejidhihirisha wazi
bila ya kujificha na kuonesha kwamba zinaweza kulipiwa kupitia mapato ya
mambo ya Muungano pekee na ziada kubaki. Lakini hili limekuwa rahisi
kwa kukubali ukweli kwamba kuna mafungu matatu ya mapato na matumizi
katika Serikali zetu mbili. Mafungu hayo ni la SMZ kwa mambo yake yasiyo
mambo ya Muungano, la Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na la
Serikali ya Muungano inayofanya kazi za Tanganyika kwa mambo yasiyokuwa
ya Muungano.
Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano
Wananchi wengi wa
Tanganyika wanahoji vipi Zanzibar iliyo ndogo na ambayo ina watu milioni
1.3 inawakilishwa na wabunge wa kuchaguliwa 50 wakati Dar es Salaam
yenye wananchi wengi zaidi ina wabunge wa kuchaguliwa 7 tu? Wabunge hawa
wanashiriki mijadala yote ya Bunge ikiwemo ya mambo yasiyo ya Muungano
(ambayo kwa usahihi yatakuwa ni mamlaka ya Tanganyika kwa mambo yasiyo
ya Muungano yanayosimamiwa na Serikali ya Muungano). Wanapata wapi
uhalali wa kufanya hivyo wakati Wazanzibari hawapangiwi shughuli hizo
(kwa mfano elimu, afya, kilimo, maji, umeme, habari, michezo, biashara,
viwanda, serikali za mitaa n.k.) na Serikali ya Muungano wala
hawasimamiwi katika mambo hayo na Bunge la Muungano? Uko wapi mpaka wa
mamlaka ya Wazanzibari katika ushiriki wa Bunge hilo wakati wao wana
Serikali yao inayopanga na Baraza la Wawakilishi lao linalosimamia mambo
yao kama hayo yasiyo ya Muungano?
Mifano hii inatosha
kuonesha kwamba takriban matatizo yote yanatokana na mkanganyiko na
mgongano wa maslahi kati ya pande mbili ambao nao unasababishwa na mfumo
usio wazi kuhusiana na mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka tatu za
Muungano zinazotambuliwa katika Mkataba wa Muungano. Kwa lugha nyepesi,
matatizo haya ya Muungano takriban yote yanatokana na tatizo la msingi
la Tanganyika kuvaa koti la Muungano.
HALI HALISI YA MFUMO WA MUUNDO WA SERIKALI MBILI ULIOPO SASA NA JINSI ULIVYOSHINDWA KUTATUA MATATIZO YA MUUNGANO
Kwa madhumuni ya kuelewa
msingi wa matatizo yanayoukabili Muungano katika muundo uliopo sasa ni
muhimu sana kufanya uchambuzi wa kina wa maeneo yafuatayo:
- Mfumo Uliopo Sasa na Udhaifu Wake
- Maeneo Muhimu ya Kuzingatiwa
- Mfumo wa Sasa na Udhaifu Wake
Mfumo wa Sasa una mambo 8 ya kuzingatia
I. Misingi ya Muungano na Utaifa;
II. Mgawanyo wa Mambo ya Muungano na Yasiyo ya Muungano;
III. Utaratibu wa Kutunga Sera kwa Mambo ya Muungano;
IV. Utaratibu wa Kutunga Sheria za Muungano;
V. Bajeti na Fedha za Muungano;
VI. Usimamizi wa Mambo ya Muungano;
VII. Matumizi ya Rasilimali za Muungano
VIII. Udhaifu wa Jumla wa Mfumo uliopo
- Misingi ya Muungano na Utaifa
- Kanuni ya Kwanza ya
Muungano ni kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitokana na muungano
wa Dola mbili huru zilizokuwa na mamlaka kamili na ambazo zilikuwa
wanachama wa Umoja wa Mataifa. Muungano haukutokana na nchi moja au
majimbo ya kiutawala.
- Kanuni ya Pili ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni
kuwa kutokana na mazingira ya kihistoria, kijiografia na kidemografia,
haiwezekani kuwa na Muungano wa Serikali moja. Mheshimiwa Rais Mkapa
amelifafanua vizuri sana suala hili katika Hotuba yake ya Miaka 40 ya
Muungano (Uk. 31-32 wa Hotuba yake). Hivyo kwa vyovyote vile, kwa
Kanuni hii, Zanzibar itabaki kuwa na utambulisho wake;
- Kanuni ya Tatu ya
Msingi ni kuwa Muungano una Mamlaka Tatu; Mamlaka ya Muungano, Mamlaka
ya Zanzibar na Mamlaka ya Tanganyika kama ilivyofafanuliwa na Hati ya
Muungano na Ibara ya Nne ya Katiba ya Muungano;
- Kanuni ya Nne ya
Msingi ya Muungano ni, kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili, Orodha ya Pili
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Washirika wa Muungano wanao uhuru na
fursa ya kujadili na kukubaliana kuendelea kuwepo au kutokuwepo kwa
Muungano. Utaratibu wa maamuzi katika suala hili ni theluthi mbili ya
kura za Wabunge wa kila upande wa Muungano.
- Kanuni ya Tano ya
Msingi ya Muungano ni usawa katika maamuzi yanayohusu mambo ya
Muungano; INGAWA kwa sasa Kanuni hii haitekelezwi kabisa na ndio moja ya
kiini cha matatizo ya Muungano;
- Kanuni ya Sita ni
haki ya pande mbili za Muungano katika ushiriki wa uendeshaji wa mambo
ya Muungano; kwa sasa Kanuni hii pia haifuatwi kabisa nayo pia ni moja
ya mizizi ya matatizo ya Muungano.
Pamoja na kuwepo misingi hiyo bayana, Katiba ya sasa haitamki wazi misingi muhimu ya Muungano kwa ufasaha na uwazi.
Katiba ya baadhi ya Nchi
kama vile, Switzerland imetamka bayana nani washirika wa Muungano wao
na hadhi zao na haki zao kama washirika wa Muungano. Katiba ya Brazil
imetamka bayana washirika wa Muungano wao na hadhi zao. Katiba ya Urusi
imetamka bayana Washirika wa Muungano wao na hadhi zao.
Katiba pia haiweki
bayana msingi wa Muungano katika kulinda msingi wa kuwa ni Muungano wa
nchi mbili huru zenye mazingira maalum na hivyo kuendelea kulinda
mazingira hayo. Katiba ya Marekani kwa mfano inakataza State moja
kugawanywa na pia kuungana na kuwa State moja.
Kwa upande wa sauti sawa
katika maamuzi, msingi huu sio tu kuwa haupo bayana bali Katiba ya sasa
inahalalisha kutokuwepo kwake. Imeweka masharti ya wazi yanayovunja
Msingi huu wa Muungano kwa kulipa Baraza la Mawaziri mamlaka pekee ya
kuamua kuhusu Sera za Muungano na Bunge mamlaka ya kupitisha Sheria za
Muungano (kwa mambo yote yaliyoainishwa katika Nyongeza ya Kwanza kuwa
ni Mambo ya Muungano) kwa wingi wa Kura tu.
Kwa upande wa haki
katika ushiriki wa uendeshaji wa Mambo ya Muungano, masharti pekee ya
Katiba ni haki ya kila upande kutoa Rais au Makamu wa Rais. Hata hivyo
kwa mfumo wa sasa Rais wa Muungano na Makamu wa Rais hawana uhusiano wa
moja kwa moja na Serikali ya Zanzibar. Uhusiano uliopo ni wa kisiasa
zaidi kwa vile wanatoka Chama kimoja. Kama watatoka vyama tofauti
kimsingi hapatakuwa na pahala pa kuwakutanisha viongozi wa Serikali ya
Muungano na wa Serikali ya Zanzibar.
Hivyo moja ya kasoro kubwa za Muungano wa sasa ni kutowekwa bayana misingi ya Muungano, kuivunja na kuhalalisha kuvunjwa kwake.
- Mgawanyo wa Mambo ya Muungano na Yasiyo ya Muungano
- Mambo ya Muungano
kwa mujibu wa ibara ya 4 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977 yametajwa
katika Nyongeza ya Kwanza. Mambo hayo ni kama yafuatayo:
i. Katiba ya Muungano
ii. Mambo ya Nje
iii. Ulinzi
iv. Usalama
v. Polisi
vi. Hali ya Hatari
vii. Uraia
viii. Uhamiaji
ix. Mikopo ya Nje
x. Biashara
xi. Utumishi katika Serikali ya Muungano
xii. Kodi ya Mapato
xiii. Forodha (Ushuru)
xiv. Kodi ya Bidhaa (excise)
xv. Bandari
xvi. Usafirishaji wa Anga
xvii. Posta
xviii. Simu
xix. Sarafu
xx. Mabenki
xxi. Fedha za Kigeni
xxii. Leseni za Viwanda
xxiii. Takwimu
xxiv. Elimu ya Juu
xxv. Mafuta yasiyosafishwa
xxvi. Gesi asilia
xxvii. Baraza la Mitihani
xxviii. Usafiri wa Anga
xxix. Utafiti
xxx. Mahkama ya Rufaa
xxxi. Usajili na Shughuli za Vyama vya Siasa
- Matatizo ya mgawanyo wa Mambo ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano ni pamoja na:
i. Kukosekana
tafsiri ya mipaka (scope) ya mambo ya Muungano. Mfano ni suala la simu-
siku za nyuma, Shirika la Posta na Simu ndio lilokuwa jambo la Muungano
kwani Zanzibar haikuruhusiwa kuwa na Shirika lake la Posta wala la Simu
kwa vile hilo ni jambo la Muungano. Hata hivyo, baada ya kubinafsishwa
Zanzibar kwanza haikupewa hisa hata moja katika Kampuni ya TTCL wala
gawio katika biashara zilizotokana na TTCL. Aidha, Zanzibar hadi leo,
ukiachia kutoa Mjumbe wa Bodi katika Shirika la Posta, haitambuliwi kama
mshirika au mbia katika Shirika hilo. Jambo hili linazua hoja ya wazi
kuwa nini jambo la Muungano katika suala la Simu na Posta halifahamiki.
Hivi sasa suala la Muungano linaonekana limebaki kuwa ni udhibiti wa
Simu na Posta kupitia Tanzania Communication Regulatory Authority
(TCRA). Hata hivyo, ukiwachia Zanzibar kutoa Mjumbe wa Bodi haina faida
nyengine inayopata kwani mapato yote ya TCRA yanakwenda Serikali ya
Muungano. Mabenki pia, ilikuwa na biashara NBC sasa ni udhibiti tu.
Elimu ya Juu tafsiri yake nayo haijulikani imeanzia wapi na kuishia
wapi;
ii. Tafsiri ya Mahkama ya Rufaani ya Tanzani katika Kesi ya Machano Khamis na wenzake 17 (“KESI
YA UHAINI”) imebainisha wazi kuwa Orodha ya Mambo ya Muungano ni ndefu
zaidi kuliko ilivyo katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba. Aidha,
inaonesha kuwa mambo ya Muungano hayajulikani hasa ni mangapi.
iii. Kwa kupitia
Mambo ya Nje, hakuna lisilokuwa la Muungano. Tatizo zaidi ni kuwa kwa
mlango huu wa Mambo ya Nje, mambo yote ni ya Muungano au Tanganyika
pekee (Mfano ni suala la Mpira- TFF na ushiriki wa FIFA). Sababu kubwa
ya matatizo haya ni kuwa Taasisi zisizokuwa za Muungano za Tanganyika
ndizo zilizojichukulia mamlaka ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano nje
ya Tanzania kwa mambo ambayo si ya Muungano. Hili ni kasoro ya msingi
kwa vile uwakilishi huo ni batili kisheria. Kwanza, Taasisi hizo hazina
uwezo wa kuiwakilisha Zanzibar kwa vile si mambo ya Muungano. Kwa
mantiki hiyo, vyombo na taasisi hizo wanapokwenda nje ya Tanzania
wanaiwakilisha Tanganyika pekee jambo ambalo si halali. Kwa mfano sasa
hivi TFF ni mwanachama wa FIFA kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Ni wazi kwamba uwanachama huo ni batili kwa vile hawana
mamlaka ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
- Utaratibu wa Kutunga Sera kwa Mambo ya Muungano.
- Kwa mujibu wa ibara ya 53(2) ya
Katiba, mamlaka ya Kutunga Sera za Serikali ya Jamhuri ya Muungano yamo
mikononi mwa Baraza la Mawaziri la Muungano. Katiba haikutenganisha
baina ya sera kwa mambo ya Muungano na sera kwa mambo yasiyo ya
Muungano. Aidha, Katiba haikuweka utaratibu wa aina yoyote ya
kuishirikisha Zanzibar katika maamuzi yanayohusu sera za mambo ya
Muungano. Mbali ya Katiba hakuna sheria wala utaratibu rasmi uliowekwa
kwa ajili hiyo. Hoja ya baadhi ya watu ni kuwa Zanzibar inashirikishwa
kwa vile kuna mawaziri kutoka Zanzibar na pia Rais wa Zanzibar katika
Baraza la Mawaziri la Muungano. Hoja hii haina msingi kwa vile:
i. mawaziri
wanaotoka Zanzibar hawajaenda kuiwakilisha Zanzibar katika Baraza la
Mawaziri na hata Rais wa Zanzibar yumo kama Mjumbe wa Baraza la
Mawaziri. Kwa sababu hiyo wanabanwa na Kanuni za maamuzi ya Baraza la
Mawaziri ambamo muamuzi hasa ni Rais na Wajumbe wote wa Baraza ni
washauri wake. Aidha, wanabanwa na Kanuni ya uwajibikaji wa pamoja
ambapo Waziri haruhusiwi kulipinga jambo liloamuliwa na Baraza la
Mawaziri.
ii. Mawaziri
wanaotoka Zanzibar waliomo katika Baraza la Mawaziri la Muungano hawana
uhusiano wowote na Serikali ya Zanzibar. Hawana njia na wala hawapaswi
kutafuta maoni ya Zanzibar katika utekelezaji wa kazi zao.
- Baadhi ya mifano ya kutoshirikishwa Zanzibar katika kuandaa sera za Mambo ya Muungano na athari zake ni kama yafuatayo:
i. Katika
maandalizi ya mfumo mpya wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Zanzibar
haikushirikishwa tokea awali. Ililetewa tu rasimu ya Sheria katika
hatua za mwisho za maandalizi. Hata baada ya kutoa maoni katika hatua
hii, maoni hayo hayakusikuzingatiwa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni
kuwepo Mkuu wa TRA Zanzibar mwenye hadhi ya Kamishna kama ilivyo kwa
Jeshi la Polisi na Uhamiaji. Matokeo yake baada ya Sheria kupitishwa
TRA iliteua Naibu Kamishna kutoka Tanganyika kuja kufanya kazi
Zanzibar. Serikali ya Zanzibar ilimkataa ofisa huyo na kueleza wazi
kuwa haiko tayari kushirikiana naye na hatimaye aliondolewa na kuteuliwa
mtu mwengine kutoka Zanzibar.
ii. Wakati wa
maandalizi ya mfumo mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Zanzibar,
katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi ilitoa mapendekezo kadhaa ambayo
yote hayakuzingatiwa na mfumo na Sheria ikapitishwa bila ya kuwepo
mapendekezo ya Zanizibar;
iii. Katika
maandalizi ya Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing
Authority) maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa, na hata pale Naibu Waziri
wa Maliasili kutoka Zanzibar, Mheshimiwa Mwalimu Haji Ameir, ambaye
alikuwa pia Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi kulieleza Bunge kuwa
maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa katika Sheria hiyo, bado Bunge
lilipitisha Sheria hiyo ambayo ilikaa miaka zaidi ya kumi bila
kutekelezwa kwa vile Zanzibar ilikataa kutoa ushirikiano hadi pale
mawazo yake yatapozingatiwa. Utekelezaji wa Sheria hii ulikuwa Kero ya
Muungano ya muda mrefu.
iv. Katika
maandalizi ya Sera ya Mambo ya Nje, Zanzibar ililetewa rasimu ya Sera
hiyo itoe maoni. Baraza la Mapinduzi liliunda Kamati kuipitia na
kuandaa maoni ambayo yalikubaliwa na Baraza la Mapinduzi. Hata hivyo,
takriban maoni yote ya BLM yalikataliwa na hayakuzingatiwa katika Sera
hiyo.
v. Katika
maandalizi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Zanzibar pia ilitakiwa kutoa
maoni tu na ikafanya hivyo kupitia Kamati ya BLM. Hata hivyo, maoni
hayo hayakuzingatiwa. Hata pale Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ulipokaribia kutiwa saini, Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, aliandika
Waraka mrefu wa maoni ya Zanzibar kuhusiana na Jumuiya ya Afrika
Mashariki, lakini maoni hayo hadi leo hayakuzingatiwa.
Hiyo ni baadhi ya mifano
michache ya namna Zanzibar ilivyokuwa haikushirikishwa katika
maandalizi ya Sera za Msingi za masuala ya Muungano hata pale ilipotoa
maoni ya maandishi. Sababu kubwa ni kuwa mfumo wa sasa wa Muungano
inaupa mamlaka yote ya maamuzi Serikali ya Muungano na mamlaka hayo
yamekuwa yakitumiwa kwa maslahi ya upande mmoja tu wa Muungano;
Tanganyika.
- Athari ya mfumo
uliopo katika utungaji wa Sera za Muungano ni kuwa Sera za Muungano
zinazingatia mahitaji, mazingira na matakwa ya upande mmoja tu wa
Muungano. Aidha, baadhi ya sera hizo zina athari kubwa kwa uchumi na
maendeleo ya Zanzibar.
- Mfumo wa Kutunga Sheria za Muungano
Mfumo wa kutunga Sheria za Muungano una matatizo kadhaa kama yafuatayo:
- Maandalizi ya Sheria ni ya upande mmoja. Zanzibar baadhi ya wakati huletewa kutoa maoni juu ya Mswada ulokwisha andaliwa.
- Kwa mujibu wa ibara ya 98,
mambo yote yaliomo katika Orodha ya Mambo ya Muungano, Sheria zake
zinapitishwa kwa wingi wa kura katika Bunge. Kutokana na Idadi ya
Wabunge wa Zanzibar, ina maana Sheria hizo zina ridhaa ya upande mmoja
tu wa Muungano.
- Sheria
nyingi za Muungano zinazingatia Sheria nyengine, mazingira na taratibu
za Tanganyika pekee. Mfano usajili wa wataalamu kama vile wanasheria,
wahandisi huzingatia taratibu za Tanganyika na bila kuzitambua taratibu
ziliopo Zanzibar.
- Fedha za Muungano na Bajeti
- Kwa mujibu wa Ibara ya 133 na 134 za Katiba ya Muungano, utaratibu
wa fedha za Muungano upo chini ya Tume ya Pamoja ya Fedha. Tume ndiyo
inayotakiwa iandae mapendekezo ya kuchangia fedha za kuendesha shughuli
za Muungano na kugawana ziada ya mapato ya Muungano. Tume imetajwa
katika Katiba tokea mwaka 1984, Sheria ya Kuanzishwa ikapitishwa mwaka
1996 lakini Tume ikaundwa mwaka 2003. Tume imetoa mapendekezo mwaka
2006 hadi leo SMT haijayafanyia kazi mapendekezo hayo. Kwa muhtasari
tu, kila jambo la Muungano lina mapato na gharama. Ukichukua mapato ya
Muungano kutokana na vyanzo vya Muungano na matumizi ya mambo ya
Muungano kama kuna ziada bila shaka kwa utaratibu wa sasa Zanzibar
haipati ziada hiyo. Ni dhahiri hilo ndio liloifanya Serikali ya
Muungano isiwe na haraka katika kuunda Tume na katika kutekeleza
mapendekezo ya Tume.
- Ibara hizo za Katiba
zinaweka sharti la kuwepo Akaunti ya Pamoja ya Fedha ambayo ndio
itawekwa mapato ya Muungano na kutoa matumizi ya Muungano. Sharti hilo
halijatekelezwa.
- Mfumo wa Bajeti ya
Serikali ya Muungano kwa sasa hautenganishi Mambo ya Muungano na mambo
yasiyo ya Muungano. Hivyo mapato ya Muungano yanatumika pia kuendesha
mambo yasiyo ya Muungano. Inawezekana pia mapato yasiyo ya Muungano
yanatumika kuendesha mambo ya Muungano. Lakini kwa kuzingatia utafiti
wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC), mapato ya Muungano ni makubwa kuliko
matumizi ya Muungano, ni wazi kuwa mapato ya Muungano ndiyo yanayotumika
kuendesha mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika.
- Sera
za kodi na fedha kwa sasa zinazingatia zaidi mahitaji ya bajeti ya
Serikali ya Muungano na sio pande mbili za Muungano. Kwa kutokuwepo
bajeti pekee ya Muungano kunachangia jambo hilo.
- Usimamizi wa Mambo ya Muungano
- Ngazi ya Baraza la Mawaziri: Mambo ya Muungano kwa utaratibu wa
sasa yanasimamiwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano ambalo
pia kwa mujibu wa ibara ya 34 ya Katiba, ndilo linasimamia mambo yasiyo
ya Muungano kwa Tanganyika. Usimamizi ni pamoja na kutoa maamuzi ya
kisera, kibajeti na kiuendeshaji. Ingawa wapo mawaziri kutoka Zanzibar
katika Baraza la Mawaziri na wengi wanachukulia kuwa ndio wawakilishi wa
Zanzibar lakini kwa utaratibu wa Baraza la Mawaziri hawapaswi kuwa
wawakilishi wa Zanzibar.
- Ngazi ya Mawizara:
Kwa utaratibu wa sasa, mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano
yamechanganywa katika baadhi ya Mawizara. Mfumo huu unafanya upande
mmoja wa Tanganyika uone kwamba mambo yote ya Muungano ni sehemu tu ya
mambo ya Tanganyika. Hivyo, hakuna tofauti katika maamuzi na wa
usimamizi. Mfumo huu umeondoa kabisa dhana ya kuwa mambo ya Muungano ni
ya pamoja yanayohitaji usimamizi wa pamoja na wa kushauriana.
- Ngazi ya Taasisi za
Muungano: Taasisi takriban zote za Muungano hazina sura ya Muungano
katika usimamizi na uongozi. Mfano mzuri ni Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) ambayo ukiwachia Wajumbe wawili wa Bodi hakuna
uwakilishi mwengine wa Zanzibar. Kwa madhumuni yote chombo hichi hakina
tofauti na taasisi yoyote nyengine isiyokuwa ya Muungano ya
Tanganyika. Mifano hiyo ipo kwa Benki Kuu, Mamlaka ya Usafiri wa Anga,
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) n.k.
- Utatuzi wa Migogoro na Kero
i. Mifano ya Migogoro na Kero:
- Fursa za Kodi:
Miongoni mwa mgogoro mkubwa uliopo baina ya Zanzibar na Serikali ya
Muungano ni ile ya Zanzibar kutumia fursa za sera za kodi kwa uchumi
wake. Zanzibar iliwahi kuandaa sheria ya Offshore companies na ilitumia
fedha nyingi kuajiri wataalam wa fani hiyo. Ingawa Serikali ya
Muungano ilikubaliana na sera hizo, lakini hatimaye ilikataa wakati
Mswada wa Sheria hiyo upo katika hatua ya Kamati ya Baraza la
Wawakilishi na bila ya kutoa sababu yoyote ya msingi. Aidha, Zanzibar
ilianzisha maeneo huru ya Uchumi (EPZ) na baadhi ya viwanda kama vile
cha madirisha maalum ya aluminium na mafuta ya kupikia vilianzishwa.
Hata hivyo, viwanda hivyo vilishindwa kuendelea na kazi kutokana na TRA
kukwamisha bidhaa zao kila wanaposafirisha kupitia bandari ya Dar es
salaam. Hatimaye viwanda vyote hivyo vilifungwa. Mgogoro mwengine
mkubwa ni wa Kodi ya Mapato (PAYE) ambao ingawa mazungumzo yalianza
tokea mwaka 1996, makubaliano yalifikiwa mwaka 2011. Pamoja na
makubaliano hayo, Serikali ya Muungano ilichelewesha utekelezaji kwa
makusudi kwa mwaka mmoja zaidi na kuikosesha Zanzibar zaidi ya shilingi
bilioni 18 ambazo imekataa kuzilipa.
- Suala la Benki Kuu:
Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa badala ya Bodi ya Sarafu ya Afrika
Mashariki ambayo Zanzibar ilikuwa na hisa za asilimia 11. Pamoja na
fedha nyengine, Benki Kuu ilianzishwa kutokana na malipo ya fedha za
Zanzibar kutoka Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Na hata kama
haikuwa hivyo, kwa vile Benki Kuu imechukua nafasi ya Bodi ya Sarafu,
Zanzibar ilipaswa kuwa na maslahi yale yale ambayo iliyapoteza katika
Bodi ya Sarafu. Mzozo huo ambao uliibuka mwaka 1994, haujaweza kupatiwa
ufumbuzi mpaka leo.
- Suala la Tume ya Pamoja ya Fedha: Tume
ya Pamoja ya Fedha ilianzishwa na Katiba ya Muungano mwaka 1984. Hata
hivyo, sheria ya kuunda Tume hiyo ilipitishwa mwaka 1996. Tume yenyewe
ikaundwa rasmi mwaka 2003; miaka 19 tokea Katiba iweke sharti la kuundwa
Tume hiyo. Tume ilitoa mapendekezo ya awali ya utaratibu wa kuchangia
na kugawana mapato ya Muungano tokea mwaka 2006 hadi leo Serikali
yaMuungano imeshindwa kutoa maoni yake juu ya mapendekezo ya Tume.
Aidha, kutokana na kuchelewa huko Akaunti ya Pamoja ya Fedha ambayo
ndiyo inayotakiwa kuwekwa mapato na kutoa matumizi ya Muungano
haijaanzishwa. Hivyo bajeti ya Muungano kwa muda wote huu inaendeshwa
kinyume na maelekezo ya Katiba.
- Masuala ya uwekezaji:
Uwekezaji katika baadhi ya sekta ndani ya Zanzibar yanategemea idhini
ya Serikali ya Muungano. Mfano wa sekta hizo ni simu na usafiri wa
anga. Zantel ilipowekeza Zanzibar iliwekewa vikwazo vingi na Tume ya
Mawasiliano (TCC) na hata Waziri aliyekuwa akisimamia sekta hiyo kwa
wakati huo Mheshimiwa William Kusila hadi kupelekea kuondolewa kwake na
kuja Mheshimiwa Enerst Nyanda. Mzozo huu ulipelekea Zanzibar kudai ITU
iirejeshee namba yake ya kimataifa ya 259 ili ijitoe katika kutumia namba ya kimataifa ya Tanzania ya 255 ili
iwekeze mradi wa simu wa Zantel. Baada ya hatua hiyo na kuondolewa
Waziri Kusila ndio mzozo huo ukatatuka. Katika suala la ndege, Mamlaka
ya Usafiri wa Anga ya Tanzania iliwahi kuzuia Zanzibar kuanzisha
Zanzibar Airline kwa madai kuwa ATC ndio Shirika la Ndege pekee la
Tanzania. Hata hivyo, mamlaka hiyo ilikuja kuruhusu Precision Air na
hatimaye makampuni mengine binafsi.
- Masuala ya Afrika Mashariki: Suala hili limeelezwa kwa urefu sehemu nyengine katika Waraka huu.
- Masuala ya Uanachama wa FIFA: Suala hili nalo limezungumzwa kwa urefu katika uchambuzi wa mambo ya Muungano.
- Suala la hisa katika mashirika ya Muungano yaliyobinafsishwa:
Yapo mashirika kadhaa ambayo yalikuwa yakijulikana kama ya Muungano na
ambayo yamebinafsishwa au kuundwa upya. Katika hatua hiyo, Zanzibar
ilipaswa kupewa hisa zake katika mashirika hayo lakini haijafanyika
hivyo hata baada ya Serikali mbili kukubaliana kulifanyia kazi na hata
baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mhe. John Malecela kutoa maelekezo ya
kuliharakisha. Miongoni mwa mashirika hayo ni ATCL, TTCL na NBC.
- Suala la Mafuta na Gesi asilia:
Mgogoro juu suala hili ulianza baada ya Antrim ya Canada kutaka kufanya
utafiti wa mafuta Zanzibar baada ya kupewa kibali na TPDC mwaka 1996.
Wakati huo wafadhili wakiongozwa na Canada walikuwa wameigomea Zanzibar
na bila ya Serikali ya Muungano kuchukua hatua yoyote ya kidiplomasia.
Zanzibar iliamua kuikatalia Antrim kufanya kazi hiyo Zanzibar na
hatimaye kuamua kutaka suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika
Orodha ya Mambo ya Muungano. Ingawa Zanzibar imeweka bayana uamuzi huo
kwa kupitishwa na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi na pia
kwa kupitisha Sera ya Nishati, lakini Serikali ya Muungano imeshindwa
kuchukua hatua kutekeleza matakwa hayo ya Zanzibar. Kwa upande mwengine
Serikali ya Muungano imekuwa ikiendeleza kwa kasi juhudi za uendelezaji
shughuli za utafutaji wa mafuta na uchimbaji wa gesi. Kwa upande wa
gesi hadi leo hakuna utaratibu wa kugawana mapato ya rasilimali hiyo
ambayo ni ya Muungano. Mgogoro huu umechangia kwa sehemu kubwa kuleta
hisia dhidi ya Muungano kwa wananchi wa Zanzibar hasa kwa vile viongozi
wa kambi zote mbili za kisiasa wanakubaliana katika suala hili.
ii. Udhaifu wa Mfumo wa sasa katika utatuzi wa migogoro ya Muungano:
Kama tulivyoona kwamba ipo migogoro mikubwa na msingi ambayo mingine
inatishia hata uhai na uimara wa Muungano lakini utatuzi wake ama haupo
au ni dhaifu. Hii inatokana na upande mmoja wa Muungano kuwa na mamlaka
yote na mwisho katika kuamua masuala ya Muungano. Hivyo, hata pale
unapofanya makosa hakuna mfumo mbadala wa kupata ufumbuzi. Kwa ufupi
mfumo wa sasa wa utatuzi wa migogoro ya Muungano ni sawa na refarii kuwa
pia mchezaji. Si mfumo na wala haufai kabisa kwa vile haufanyi kazi.
Ni kiini cha matatizo ya Muungano na umekuwa ukitumika vibaya na upande
mmoja na kwa kiasi kikubwa sana umedhoofisha Muungano.
- Matumizi ya Rasilimali za Muungano
- Miundombinu ya Taasisi za Muungano: Kwa
kawaida, uwekezaji wa rasilimali za Taifa una faida kubwa katika kukuza
uchumi wa nchi. Ni kwa sababu hizo ndio maana Jumuiya zote za kiuchumi
zina mfumo wa kugawana kwa haki baina ya wanachama faida za uwekezaji
huo. Uwekezaji huo mara nyingi uko katika mfumo wa ujenzi wa
miundombinu ya taasisi za Muungano hasa Makao Makuu ya taasisi hizo.
Uwekezaji unapowekwa unatoa fursa nyingi katika eneo husika. Kwa upande
wa Muungano wa Tanzania, uwekezaji umewekwa katika upande mmoja tu wa
Muungano na hivyo kutoa fursa kwa upande huo wa Tanganyika. Mfano wa
uwekezaji huo ni pamoja na Benki Kuu, Posta, TCRA, TCCA, TCU, COSTECH
nk.
- Ajira:
Muungano wenye haki na usawa unazingatia sana mgawanyo wa ajira katika
taasisi za Muungano kwa pande zote za Muungano katika ngazi zote za
Utendaji na za kawaida. Mfumo wa sasa wa Muungano hilo halizingatiwi
hata kidogo. Baya zaidi ni kuwa hata kwa taasisi za Muungano ziliopo
Zanzibar kama vile Benki Kuu waajiriwa wengi wanatoka Tanganyika.
- Udhaifu wa Jumla wa Mfumo Uliopo
i. Udhaifu wa Katiba: Katiba yenyewe ina udhaifu kama ilivyoainishwa hapo awali ambayo kwa ufupi ni kama yafuatayo:
ii. kukosa misingi ya wazi ya Muungano,
iii. maamuzi yote ya msingi ya Muungano kufanywa na upande mmoja,
iv. kukosa usawa, haki na fursa zilizo sawa kwa pande mbili;
v. kuchanganywa mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano;
vi. Kukosa mfumo wa mashirikiano na mashauriano baina ya pande mbili;
vii. Kukosa mfumo wa utatuzi wa migogoro na kero za Muungano;
viii. Rasilimali za Muungano kutotumika kwa haki baina ya pande mbili za Muungano.
Udhaifu wa Mfumo wa Serikali Mbili:
Mfumo wa Serikali Mbili umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa una udhaifu
mkubwa katika kuendesha Muungano wa Tanzania na pia katika kusimamia
Muungano unaoweza kuhimili mageuzi ya kisiasa. Miongoni mwa kasoro za
Msingi za Mfumo wa Serikali mbili uliopo ni kama zifuatavyo:
i. Umegeuza
mmoja wa Washirika wa Muungano (Zanzibar) kuwa ni sehemu ya nchi
(political subdivision or a Province of a sovereign country) na kumvika
Mshirika mwengine (Tanganyika) kuwa ni Taifa kamili lenye mamlaka yote
kwa kubadili jina tu na kuwa Tanzania;
ii. Umenyan’ganya
mamlaka yote kutoka kwa Washirika wa Muungano na kuukabidhi upande
mmoja wa Muungano na kutoa fursa ya upande mmoja kutumia mamlaka hayo
kadri upendavyo na kwa maslahi yake tu;
iii. Umeondoa
misingi ya Muungano kwa kukosa kiungo baina ya pande mbili za
Muungano. Mfumo uliopo wa Serikali mbili umeshindwa kufanya kazi wakati
Chama kimoja kinatawala Serikali zote mbili. Hatudhani kama unaweza
kufanya kazi kama yatatokea mabadiliko ya chama;
iv. Mfumo
uliopo wa Serikali mbili unajenga mazingira ya kuwa na Serikali na Rais
wa Muungano ambaye hana uhalali upande mmoja wa Muungano (Zanzibar).
Hii ni kwa sababu Chama kinachoongoza Serikali ya Muungano na Rais wa
Muungano anaweza wasipate kiti wala kura Zanzibar na bado ikawa Serikali
ya Muungano na Rais wa Muungano. Huu ni ushahidi wa wazi kuwa mfumo wa
Serikali mbili haujengi usawa wa ridhaa ya pande mbili bali unajenga
mazingira ya upande mmoja kuwa mkubwa na sehemu ya pili kuwa sehemu tu
ya utawala (dominion). Mfumo huu unaondoa msingi mmoja wa haki ya watu
wa Zanzibar kujitawala na kuendesha mambo yao kwani hawana mamlaka ya
kuchagua kiongozi wanayemtaka wala sera wanazotaka za kuongoza masuala
ya Muungano. Mfumo huu unayafanya mambo ya Muungano kuwa ni ya upande
mmoja na upande huo ndio wenye haki na ridhaa ya kuchagua kiongozi na
sera wanazotaka kuhusiana na masuala ya Muungano sawa na yale mambo
ambayo si ya Muungano.
v. Mfumo
wa Serikali mbili uliopo unaufanya Muungano utegemee zaidi mazingira ya
kisiasa. Mabadiliko yoyote ya kisiasa yatayobadili vyama vinavyotawala
Serikali mbili yanaweza kuutia Muungano katika mashaka makubwa ya
kuendelea kuwepo kwani itategemea zaidi masikilizano ya vyama badala ya
misingi ya Katiba.
Mambo Muhimu ya Kuzingatiwa
- Kulinda
Msingi Mama wa Muungano kwamba ni Muungano wa Nchi Mbili Huru zenye
mazingira tofauti sana ya kijiografia, kidemografia na kiuchumi.
- Kuweka msingi wa kuwa na Muungano wa kweli hata kama itakuwa ni kwa maeneo machache;
- Kuweka bayana misingi muhimu ya Muungano ambayo imeelezwa hapo awali;
- Kulinda maslahi ya kiuchumi ya washirika wa Muungano kwa kutoa uhuru katika maeneo ambayo ni nyenzo za kiuchumi kwa kila upande;
- Kulinda haki ya watu
wa kila upande kujiamulia kubaki kuwemo katika Muungano au kutoka kwa
masharti yatayohakikisha kuwa kweli huo ni uamuzi wa watu wote wa upande
huo na sio wa wachache;
- Kuwepo mfumo bayana wa kugawana haki za mali na kugawana dhima na kulipana madai ya muda mrefu baina ya pande mbili.
MAPENDEKEZO YA KUREKEBISHA IBARA ZA SURA YA SITA
Kutokana na maelezo,
hoja na sababu tulizozitaja hapo juu, Wajumbe walio wachache tunaona
hakuna njia nyengine zaidi ya kubadili muundo wa Muungano kwa kuanzisha
Shirikisho la Serikali Tatu kama walivyopendekeza wananchi walio wengi
kupitia maoni yao waliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo, pamoja na
kukubaliana na pendekezo la msingi la kuwa na Shirikisho la Serikali
Tatu kama yalivyo kwenye Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba, tunapendekeza
marekebisho yafuatayo ili kuufanya muundo huo uweze kufanya kazi vizuri
zaidi kwa maslahi na manufaa ya wananchi wa Tanganyika na Zanzibar.
Ibara ya 60:
Kama tulivyotangulia kueleza, jina la muungano huu liwe ni “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar” ili
kuweka bayana kwamba muungano huu ni wa Jamhuri mbili ambazo ni Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Kwa msingi huo basi,
katika Sura hii na katika sehemu zote za Katiba kila ilipotajwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania iandikwe Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.
Ibara ya 62:
Ibara 62(3) inasema
kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, inaweza kutekeleza
jambo lolote lilio chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Tanganyika.
Maelezo:
Ingawa serikali hizi zinaweza kukubaliana kushirikiana, lakini
ushirikiano unapaswa uwe ni kwa pande mbili (two-way). Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyikazinaweza kukubaliana
kushirikiana na kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, na vile vile zinaweza
kutekeleza jambo lolote lililo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano,
kwa makubaliano. Mamlaka ya Serikali ya Shirikisho yatakuwa ni kuhusu
mambo ya Muungano tu kama yalivyoorodheshwa kwenye Nyongeza ya Katiba.
Maudhui yaliyomo kwenye Ibara Ndogo ya 62(3) yanaingilia mamlaka ya
Serikali za nchi washirika kwa mambo yasiyo ya Muungano. Namna
ilivyoelezwa katika Ibara hii, inaipa fursa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano kujiingiza katika mambo yasio ya Muungano ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, na si kinyume chake.
Huu ni mlango wa nyuma kuingilia mamlaka ya Serikali nyengine, na inafaa
uzibwe.
Pendekezo ni kwamba ama Ibara ya 62(3) ifutwe au iandikwe upya na isomeke:
“62(3).- Bila
kuathiri au kukiuka masharti ya Ibara hii, Serikali ya Shirikisho,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, zinaweza
kushirikiana na kutekeleza jambo lolote lililo chini ya mamlaka yao kwa
mujibu wa masharti ya makubaliano ya kimkataba baina yao na pia
kuanzisha taasisi zenye maslahi ya pamoja.”
Ibara ya 63:
Ibara ya 63 inahusu
Mambo ya Muungano ambayo yametajwa katika Nyongeza (Schedule) ya Rasimu
ya Katiba. Tunapendekeza Orodha hiyo iangaliwe upya pale utakapofika
wakati wa kuijadili.
Ibara ya 65:
Ibara ya 65 imeandikwa
kwa lengo la kuonesha kwamba nchi washirika sasa watakuwa na udhibiti wa
ushirikiano wa kimataifa katika yale mambo yasiyo ya Muungano. Hata
hivyo, Ibara hiyo haitaweza kutekelezeka kwa sababu ni Hati za Kisheria
(Legal Instruments) zinazoanzisha jumuiya, taasisi na mashirika ya
kimataifa ndizo zinazoweka sharti la nchi kuwa na mamlaka kamili
(sovereign state) ili kuweza kukubalika kuwa mwanachama. Mfano mzuri ni
jitihada za Zanzibar kupitia ZFA kutaka kujiunga na Shirikisho la Soka
Duniani (FIFA). Inaeleweka
kwamba michezo si suala la Muungano na ni sehemu ya mambo ambayo
Zanzibar inapaswa kuwa na mamlaka kamili (exclusive jurisdiction) kwa
mujibu wa Mkataba wa Muungano wa 1964 na hata kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Hata hivyo, FIFA kupitia barua
yake kwa ZFA ya tarehe 21 Juni, 2010 yenye Kumb. Nam. SG/TRE/PCO
imeeleza kwamba sababu ya kuikatalia Zanzibar kujiunga na Shirikisho
hilo ni kukosa sifa ya kuwa na mamlaka kamili (sovereignty) na kwamba
Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.
Hali kama hiyo inahusu
mashirika kama WHO kwa sekta ya afya, UNESCO kwa sekta za elimu na
utamaduni, FAO na IFAD kwa sekta ya kilimo, UNEP kwa sekta ya mazingira,
na sasa hata OIC kwa maendeleo ya kiuchumi.
Kwa msingi huo, masharti
ya Ibara hiyo ya 65 yanabaki ni pambo (cosmetic) tu lakini hayawezi
kutekelezeka bila ya nchi washirika kuwa na mamlaka kuhusiana na
mahusiano ya kimataifa.
Pendekezo ni
Ibara ya 65 kuandikwa upya kwa kutamka wazi kwamba Nchi Washirika
zitakuwa na mamlaka kamili katika masuala ya uhusiano na ushirikiano wa
kimataifa kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano.
Ibara ya 67:
Makao Makuu ya Muungano:
Ibara 67(2) inataja Makao Makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano,
lakini haielezi yatakuwa wapi – itakuwa ni ofisi tu chini ya mamlaka ya
Nchi Mshirika mmojawapo, au katika miji tofauti kugawanya makao makuu ya
Urais, Bunge na Mahakama, kama ilivyo Afrika Kusini; au Mji Mkuu wa
Muungano, kama Brasilia (Brazil) au Islamabad (Pakistan).
Maelezo:
Kwa muda wa miaka hamsini ya Muungano taasisi zote za Muungano
zimejengwa Tanganyika na kuiwacha Zanzibar katika hali ya ukiwa. Katika
vyuo na taasisi za elimu ya juu zisizopungua 20 za umma ziliopo
Tanzania, hakuna hata moja iliyojengwa Zanzibar. Tunataka kuona kuwa
Makao Makuu ya Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar sasa yawe
na sura ya Shirikisho la kweli.
Kwa upande mwengine,
neno “Waziri Mkaazi” halileti taswira nzuri na pia halieleweki vyema.
Kimsingi Waziri Mkaazi anapaswa kuitwa kwa dhamana yake ambapo ni Waziri
wa Nchi Washirika anayeshughulikia mambo ya Muungano.
Ibara ya 68:
Ibara ya 68(1): Serikali
ya Shirikisho kimsingi inapata uhalali wake kutoka kwa Serikali za nchi
washirika na siyo moja kwa moja kutoka kwa wananchi. Kwa upande
mwengine uhalali na msingi wa mamlaka ya Serikali za nchi washirika
unapaswa kuachwa kwa nchi washirika wenyewe kwa utaratibu utakaoelezwa
kwenye Katiba za nchi zao.
Ibara ya 68 (2): Masuala
ya kugatua madaraka (devolution) kwa serikali za mitaa hayaihusu
Serikali ya Shirikisho na hivyo hayapaswi kuwemo kwenye Katiba ya
Shirikisho kwa sababu masuala ya serikali za mitaa si mambo ya Muungano.
Hayo ni mambo ya nchi washirika na yanapaswa kuwemo kwenye Katiba za
nchi washirika kwa utaratibu ambao kila nchi itaona unafaa.
Ibara ya 69:
Ibara ya 69 inahusu
Wajibu wa Kulinda Muungano na inasisitiza kwamba Viongozi Wakuu (Rais wa
Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa
Tanganyika na Rais wa Zanzibar) wataapa “kuutetea na kuudumisha
Muungano.”
Maelezo:
Ibara hii haijengi msingi muhimu wa Muungano wa watu ambao ni kuwa na
muungano wa hiyari na badala yake inaufanya Muungano uonekane kama vile
ni jambo linaloshurutishwa. Isitoshe, kwa nini tunasisitiza na
kung’ang’ania suala la Muungano tu? Viongozi Wakuu wanatakiwa walinde
nchi zao, demokrasia, haki za wananchi wote, Katiba, na mambo mengi
mengine. Hata kama Muungano usingekuwepo, bado wangetakiwa kuapa kulinda
nchi na katiba zao. Rasimu hii tayari imeweka kipengele juu ya uwepo na
uwezekano wa kutokuwepo kwa Muungano kwa kura ya maoni (“opt-out
clause”- Ibara 119(e), na hivyo kuonesha kuna uhalali wa kufikiri juu ya
tukio hilo. Ikitokea mgogoro wa kikatiba, na ikafika wakati hawa
viongozi wakilazimika kusema Muungano hauwezi kuendelea, basi kwa nini
wafungwe midomo kwa woga wa uhaini? Suala la “Kuwapo wa Jamhuri ya
Muungano” linaweza kuondolewa pia hata kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano inayotumika sasa ya mwaka 1977, Ibara ya 98(1)(b) na
linatajwa kwenye Orodha ya Pili ya Nyongeza ya Pili.
Pendekezo:
Inatosha kusema kwamba Viongozi Wakuu waliotajwa katika Ibara ya 69
wataapa kulinda Nchi na Katiba ambayo inajumuisha mambo yote
yanayohusika.
= mwisho =