WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, amekiri kutoa maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi
kanisani kwa madai ya kuingiwa hofu na harakati za asasi ya kidini ya
Uamsho, kufanana na za Chama cha Wananchi (CUF) za kudai Serikali ya
mkataba.
Waziri Lukuvi alitoa kauli hiyo jana bungeni, akitoa ufafanuzi wa
kauli aliyopata kuitoa katika Kanisa la Methodist wakati wa kumsimika
Askofu Mteule, Joseph Bundara.
Katika misa hiyo, Lukuvi aliwaambia waumini wa kanisa hilo kwamba
muundo wa serikali tatu utavunja Muungano na ikipitishwa, jeshi
litaingilia kati kuongoza nchi, kauli ambayo juzi ilisababisha UKAWA
wasusie Bunge.
Katika ufafanuzi wake jana bungeni Lukuvi alikiri kutoa kauli hiyo
kanisani kwa madai ya kuingiwa hofu ya kutokea ubaguzi wa kidini.
Alisisitiza kuwa hofu yake inatokana na harakati zinazofanywa na
kikundi cha Uamsho visiwani Zanzibar, kufanana na za CUF ambazo ni
kudai Serikali ya Mkataba.
Alisema uamsho imekuwa ikihusishwa na vurugu zinazotokea mara kwa
mara visiwani humo, zinazohusishwa na vuguvugu la kudai mamlaka kamili
ya Zanzibar.
Akitolea mfano, Lukuvi alisema Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel
Sitta, alipotumwa Zanzibar kupeleka Rasimu ya Katiba, rasimu hiyo
ilichukuliwa na wanauamsho na kuichanachana, kisha kuisigina mbele yake.
“Sasa niwaulize humu ndani…Uamusho ni nani…?” Wajumbe kwa wingi wao
na vigelegele wakajibu “Ni CUF”. Akauliza mara ya pili: “Uamusho ni
nani…?” akajibiwa: “ CUFUUUUU”.
“Lakini kuna swali liliulizwa hapa bungeni, CUF wakaja juu wakasema
ni Taasisi ya Kidini…sasa unaniambiaje mimi nisiwe na hofu ya kidini
wakati kuna chama cha siasa kinahusiana na Uamsho lakini ina ladha ya
kidini.
“Na kwa kuwadhihirishia hivyo, kila mara CUF na Uamsho utakapomtaja
Mwalimu Nyerere na kumtaja Karume wanakwambia alaaniwe.. lakini hizi
ndiyo sera za hao mnaowasema, sasa tunakuwaje na chama cha siasa ambacho
tayari kinajipanga kutawala Zanzibar, lakini kinaendeshwa na Sera za
Uamsho…uamsho wenyewe wanasema ni Taasisi ya Kidini, kwa nini usiwe na
wasiwasi na mihemko yote ile ya Uamsho mpaka na Bara tukatikishika, kwa
nini tusiwe na wasiwasi kwamba CUF ikichukua nchi basi Uamsho ndiyo
utatawala, kwa nini tusiwe na hofu, yametokea na sisi tumeyaona, kwa
nini wanajificha kwenye kivuli cha dini ili kufanya siasa…na kwa nini
dini imetumika vizuri sana kueneza sera za CUF za serikali tatu, na kila
wachosema CUF ndicho wanachosema uamsho?,” alihoji Lukuvi.
“Na ukishaona chama kinajitayarisha kuchukua madaraka kama ilivyo kwa
CUF, kinatumia taasisi hii yenye msimamo mkalii kueneza sera zake ni
hatari kwa mustakabali wetu, ni hatari kubwa,” alisema.
Alisema kama kweli Uamsho ni taasisi ya kidini na inatekeleza sera
ambazo zinatekelezwa na vyama vya siasa, lazima Watanzania wajiulize
kuna nini.
Alisema kuna tishio la baadhi ya watu ambao wameanza kufikiria kwamba
Wazanzibar wanafaidi sana wakiwa Tanzania Bara na kufikiria kuwafukuza
na kunyang’anya mali zao na iwapo watafanikiwa kuwanyang’anya
watawafukuza.
“Sasa baada ya Wazanzibari kuondoka, tutaanza kuangalia hawa Wachina,
hawa Wahindi na vinginevyo tutakuja hata kwenye dini, Wakristo wana
mali zaidi kuliko Waislamu.Lakini kwa Zanzibar ambayo ina dini kubwa moja na tunajua hizi dini,
kwa mfano katika dini ya Ukristo kuna dini ndogo ndogo nyingi na ndani
ya ukristo kuna watu wenye siasa kali lakini na ndani ya Uislamu kuna
watu wenye siasa kali kwa hiyo mimi nina hofu nyingine ya ubaguzi .
“Nasema kunaweza kukatokea ubaguzi wa kidini, inaweza ikatokea
ubaguzi wa kieneo kwani inaweza kutokea hata Unguja akaenda mtu akasema
Waunguja wote ondokeni hapa pamejaa, sasa hizi ni hofu zangu, mfumo huu
wa serikali mbili umetuondolea hofu hizi hatuna hofu kabisa ya maisha
haya, leo hatumfikirii Mpemba atoke au Muunguja atoke, Msukuma atoke,
hatufikirii,” alisema.
Awali kabla ya Lukuvi kutoa ufafanuzi huo, Sitta aliwaambia wabunge
kuwa amemlazimisha Lukuvi kukatiza safari yake nchini India ili atoe
ufafanuzi wa kauli alizozitoa katika Kanisa la Methodist.
Alisema amelazimika kumwita Lukuvi ambaye alikuwa akijiandaa kuondoka
nchini jana kwenda India kwa matibabu ili atoe ufafanuzi wa kauli yake
ambayo juzi ilisababisha UKAWA, wanaounga mkono serikali tatu, kususia
Bunge hilo.
Moto wa wajumbe wa UKAWA, kutoka bungeni juzi uliwashwa na Profesa
Ibrahim Lipumba ambaye alisema serikali na mawaziri wake wameanza
kampeni ya kupinga muundo wa serikali tatu unaopendekezwa na rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hoja ya Lukuvi inafanana na ile ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati wa kufungua Bunge, Machi 21, mwaka huu.
Tanzania Kwanza wamruka Lukuvi
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaojiita Tanzania Kwanza,
wamemruka Mjumbe wa Bunge hilo, William Lukuvi, kuwa kauli aliyoitoa
kanisani na kusababisha mtafaruku ndani ya bunge ni maoni yake binafsi
na si maoni ya serikali ya CCM.
Akitoa ufafanuzi jana, Kiongozi wa kundi hilo, Adam Malima, alisema
Lukuvi kama mjumbe ana uhuru wa kutoa maoni yake na kwamba aliyoyasema
ni yake na wala si ya chama wala serikali.
Kuhusu kauli za matusi, Malima alisema haoni kama kuna matusi na
kuongeza kuwa tusi kubwa ni lile alilolitoa Profesa Lipumba kwamba wote
wanaodai serikali mbili ni Interahamwe.
0 comments:
Post a Comment