Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Rasimu ya Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameondoka kwa hasira katika
kikao cha bunge hilo kinachoendelea mjini Dodoma.
Hasira yao inatokana na madai kwamba maoni ya
wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya yamekuwa
yakipuuzwa.
Wajumbe wa bunge hilo ambao ni
kutoka upande wa upinzani chini ya umoja unaojulikana kama UKAWA, yaani
Umoja wa Katiba ya Wananchi, wameamua kutoka nje kupinga kile
wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka
muungano wa muundo wa serikali tatu kama yalivyopendekezwa katika rasimu
ya katiba hiyo.
Kilio cha mwananchi
Akichangia katika kikao cha bunge hilo Jumatano
jioni, mmoja wa wajumbe Profesa Ibrahim Lipumba amelalamikia kauli za
ubaguzi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe, hususan wanaotaka muundo wa
muungano wa serikali mbili, alieleza sababu za kutaka serikali tatu kuwa
zitasaidia kutatua matatizo yaliyopo katika muundo wa sasa.
Hata hivyo hakusita kupinga kile anachokiita kauli za ubaguzi kutoka kwa wajumbe wanaopinga mawazo ya wachache bungeni humoi.
"Hatuwezi kuwa kama kundi la wapiganaji
linalohamamisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatulikubali,
hatulikubali, hatulikubali, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi
tunawaachia muendelee na kikao chao.Ahsanteni sana".
Mara baada ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.
Hata hivyo, kikao cha bunge hilo kiliendelea
baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo kusema idadi ya wajumbe
waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.
Muundo wa serikali
Wanaounga mkono muundo wa serikali tatu,
wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa kutatua masuala
yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za muungano, hivyo
kudhoofisha muungano huo.
Hata hivyo wajumbe wanaounga mkono serikali
mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu ni kuvunja muungano
wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha serikali ya
tatu.
Bunge hilo lenye zaidi ya wajumbe mia sita
linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza
la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa na rais wa Tanzania
kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Wajumbe 191 kutoka upinzani walitoka nje ya
bunge kupinga mwenendo wa bunge hilo katika kujadili rasimu ya katiba
mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment