Wednesday, 12 March 2014

WABUNGE 40 WA CHADEMA KUWEKA KAMBI KALENGA

Filled under:



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ataongoza wabunge 40 wa chama hicho kwenda kuongeza nguvu katika kampeni za lala salama za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.

Uchaguzi mdogo wa Kalenga unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo, Machi 16 mwaka huu kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Dk William Mgimwa, huku mchuano mkali ukionekana kuwa kati ya Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Habari ambazo zililifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Mbowe jana zinasema, wabunge hao watatawanywa katika kata za Jimbo la Kalenga na watakuwa katika maeneo hayo hadi Jumapili.

Akizungumza kutoka mjini Dodoma, Mbowe alithibitisha kwamba ataongoza wabunge 40 wa chama chake kwenda Kalenga ili kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi huo mdogo.
Hata hivyo, Mbowe alisema safari hiyo itazingatia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
“Kama mnavyofahamu tupo hapa Dodoma ambako tuna jukumu la kitaifa, kwa hiyo hatuwezi kuondoka tukaacha jukumu hili, tunaangalia jinsi ratiba ilivyokaa ili pale tutakapopata fursa hiyo tuweze kuitumia kwenda Kalenga,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunafahamu kwamba baada ya kupitisha Kanuni za Bunge Maalumu, kuna kazi kubwa ya kuwaapisha wabunge, inaweza kuchukua siku mbili au tatu hivi, kwa hiyo sisi tutatumia siku hizo kwa wabunge wetu kwenda kuhakikisha ushindi unapatikana Kalenga.”
Alisema wabunge hao kabla ya kuondoka watashiriki katika uchaguzi wa viongozi wakuu wa Bunge la Katiba; Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti. Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge hilo, uchaguzi wa viongozi hao unatarajiwa kufanyika leo na kesho.
Mapema Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema baada ya kuwasili, wabunge hao watapiga kambi katika jimbo hilo hadi uchaguzi utakapofanyika.
Tayari wabunge wawili wa chama hicho, Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Godbless Lema (Arusha) wapo Kalenga tangu Ijumaa iliyopita wakimnadi mgombea wa Chadema, Grace Tendega. Ofisa Habari wa 

Chadema, Tumain Makene alisema Mbowe anatarajiwa kuwasili leo Iringa akitokea Dodoma.
“Mwenyekiti wetu anatarajia kuwasili mjini hapa kesho (leo) akiwa na wabunge wengine 26, wanakuja kupiga kambi hadi utakapofanyika uchaguzi Jumapili,” alisema Makene.
Katika hatua nyingine, Lema aliwatoa shaka wananchi wa Kalenga kutokuwa na hofu kuhusu usalama wa kura watakazozipiga, kwa kuwa chama hicho kimeimarisha ulinzi baada ya kura kupigwa. Lema alisema Chadema kimewapeleka watu zaidi ya 1,000 ambao wametawanywa vijijini na kwamba wengine kutoka Mara, Arusha na mikoa mingine wanaendelea kuwasili kuungana na wenzao.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kalenga, Pudenciana Kisaka alisema maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika na kwamba anatarajia kutoa matokeo ya uchaguzi huo haraka iwezekanavyo.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damiani Lubuva akizungumza jana kwa simu, alisema yupo safarini kuelekea Iringa, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu na amani.

“Nipo safarini, uchaguzi utafanyika katika hali ya kawaida kama ilivyofanyika kwa chaguzi zingine zilizopita,” alisema.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, RamadhanI Mungi alisema jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa kwa makosa mbalimbali yanayohusishwa na vitendo vya uhalifu katika mchakato wa uchaguzi huo. Alisema baadhi ya majalada ya kesi husika yameshafikishwa kwa Mwanasheria wa Serikali kwa ajili ya wahusika kupelekwa mahakamani.
“Wapo watu tunawashikilia, ni wengi lakini orodha kamili nitaitoa Ijumaa. Wapo ambao tayari majalada yao tumeyafikisha kwa Mwanasheria wa Serikali na wakati wowote watafikishwa mahakamani,” alisema Mungi na kuongeza:
“Wengine bado tunakusanya ushahidi wa makosa yao, pindi utakapokamilika tutauwasilisha kwa Mwanasheria kwa hatua zaidi.”
Mungi alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na taarifa za matukio ya kupigwa kwa Paroko wa makanisa ya Ordthodox, Padri Constantino Mbilinyi, kuchomwa kisu kwa Katibu wa Vijana wa Chadema, Kata ya Luhota, Richard Mawata na kupigwa kwa Mohamed Kunambi ambaye ni dereva wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba.
Pia kumekuwapo na vitendo vya kuchanwa kwa mabango na bendera za vyama katika jimbo hilo.

0 comments:

Post a Comment