Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila amepinga uhalali wa Bunge hilo ambalo amelifananisha na Mkutano Mkuu wa CCM.
Mchungaji Mtikila aliyasema hayo juzi katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma kutokana na mwenendo usioridhisha wa Bunge hilo.
Alisema Bunge hilo ni kwa ajili ya kupoteza fedha
za walipakodi zinazotumika katika kuwalipa posho wajumbe ambao hawana
kazi ya kufanya.
Alisema wajumbe wa Bunge hilo wanapoteza muda wao
kwa kupingana na misimamo ya CCM na matokeo yake ni malumbano
yasiyokuwa na tija.
“Kila siku nimekuwa nasema kuwa kinachoendelea
hapa ni usanii mtupu, kama kweli sisi ni watu wa kumwogopa Mungu, basi
tukubali kuziacha posho zetu na turudi nyumbani,” alisema Mchungaji
Mtikila.
Mchungaji Mtikila alisema inasikitisha kuona kuwa
watu wanalipwa fedha kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano Mkuu wa CCM,
chama ambacho alidai kimepanga kuisaliti nchi.
Alisema CCM kupitia wajumbe wake, kinataka
kulazimisha mchakato wa Katiba, jambo ambalo alisema ni kutengeneza bomu
kubwa kwa Taifa.
Hata hivyo, alisisitiza msimamo wake wa kwenda
mahakamani kabla ya kumalizika kwa Bunge na kwamba safari hii hakuna
atakayechomoka kwa sababu ana ushahidi wa kutosha.
“Posho hizi walizonilipa, nitazitumia katika
kutafuta haki na uhuru kamili wa Watanganyika, najua kabisa kuwa kwa
uzembe walionao, hata kama nikiwakuta majaji wabovu mahakamani, kesi
hii nashinda tena kwa urahisi,” alisema Mchungaji Mtikila.
0 comments:
Post a Comment