WAKATI Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akijipanga kuanza
ziara katika mikoa kadhaa nchini kujibu mapigo ya tuhuma dhidi yake
zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kwenye ziara ya Operesheni M4C Pamoja Daima, mbunge huyo
ameibuka na DVD inayowananga viongozi wa CHADEMA.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa DVD hizo zitasambazwa kwenye
mikoa na maeneo yote atakayofanya mikutano ya hadhara mbunge huyo, kama
moja ya harakati na mikakati ya kujisafisha na tuhuma za usaliti
zinazomkabili ndani ya chama.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa DVD hizo
zinatengenezwa kwenye kampuni moja iliyopo eneo la Kariakoo ambayo
imepewa tenda ya kuchapa nakala 10,000 na kampuni nyingine zaidi ya
tatu, nazo zimepewa tenda ya kuchapa DVD hizo kwa idadi tofauti.
Hata hivyo jambo la kushangaza ni kwamba katika jaradio la DVD hizo
kuna rangi ya njano, nyeupe, bluu nyepesi, bluu nzito pamoja na bendera
ya taifa.
Rangi zilizotumika kwenye jaradio hilo hazina uhusiano na rangi za bendera ya CHADEMA wala chama chochote cha siasa nchini.
Mbali ya jaradio hilo kupambwa na rangi hizo, pia limepambwa na picha
kadhaa za mikutano aliyopata kuifanya mwanasiasa huyo katika maeneo
mbalimbali na nyakati tofauti nchini, huku picha kubwa ikimwonyesha
Zitto akiwa amevalia suti huku akitabasamu.
Jaradio hilo pia limezungukwa na maandishi mbalimbali ambayo yanasomeka:
‘Uadilifu, Uzalendo na Uwajibikaji, ndio silaha yetu katika
kutetea wanyonge na maskini wote wa Tanzania, tuungane kwa pamoja.’
‘Tanzania Kwanza’
Maandishi mengine makubwa yanamtambulisha mbunge huyo ambayo nayo yanasomeka:
‘Zitto Zuberi Kabwe, Mtetezi wa Wanyonge, Tumaini la Maskini wa Tanzania”
Jaradio hilo pia limeweka mawasiliano ya mbunge huyo ya simu ya mkononi, barua pepe, Facebook na Twitter.
Hakuna maelezo yanayoonyesha kama DVD hizo zinauzwa au zinatolewa bure.
Ndani ya DVD
DVD hizo ambazo nakala tunayo, zinaonyesha picha ya mikutano ya
hadhara ya mbunge huyo aliyoifanya mkoani Kigoma mara baada ya Kamati
Kuu (CC) ya CHADEMA kumvua nyadhifa zake na Mahakama Kuu kushikilia
hatima ya uanachama wake baada ya kukabiliwa na tishio la kuvuliwa
uanachama.
Kwa mujibu wa DVD hizo, katika moja ya mikutano ya mkoani Kigoma,
Zitto anasikika akiuambia umati wa wafuasi wake waliofurika kumsikiliza
akieleza chanzo cha mgogoro wake na CHADEMA ni msimamo wake wa kuhoji
hesabu za fedha za vyama vya siasa, kikiwemo CHADEMA na kumuagiza
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya uhakiki.
Kama ambavyo amepata kukaririwa mara kwa mara, Zitto ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
anasema CHADEMA ilimtaka awajulishe kwanza kabla ya kumuagiza CAG
kufanya ukaguzi ili kutoa fursa ya kuweka hesabu zao vizuri.
DVD hiyo pia inamuonyesha Zitto akisema sababu nyingine ya ugomvi
wake na CHADEMA ni dhamira yake ya kutaka kuwania uenyekiti wa CHADEMA,
nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai na
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wafuasi wake, baadhi wakiwa na
mabango ya kumsifia, Zitto anasema hajawahi kupewa fedha na CCM
kuisaliti CHADEMA na kuongeza kwamba atakuwa wa mwisho kutoka ndani ya
chama hicho alichojiunga nacho akiwa na umri wa miaka 16.
Dk. Kitila Mkumbo naye yumo
DVD hiyo pia inamuonyesha aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Baraza
Kuu la CHADEMA, Dk. Kitila Mkumbo, akieleza sababu za yeye kutaka
kujiuzulu kabla ya Kamati Kuu kuamua kumvua uanachama.
Dk. Kitila pia anaonekana kwenye DVD hiyo akielezea waraka
ulioandikwa na Samson Mwigamba ambao ulinaswa ukielezea mikakati ya
kutaka kuung’oa uongozi wa Mbowe kwenye nafasi ya uenyekiti.
Kwa mujibu wa habari hizo, lengo la ziara ya Zitto ni kujibu mapigo
ya CHADEMA, hasa katika maeneo ambayo baadhi ya makada na viongozi wa
chama hicho wamepita na kuzungumzia hatima yake kisiasa, hasa walipojibu
maswali ya wananchi kuhusu sakata lake kuvuliwa uongozi kwa tuhuma za
usaliti, na hatimaye Zitto kwenda mahakamani kuzuia chama kujadili
uanachama wake.
Katika kesi ya msingi, Zitto aliyewahi kuwa maarufu akiwa kiongozi wa
CHADEMA, anaomba arudishiwe nyadhifa zake zote, na apatiwe nakala za
uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ili aweze kukata rufaa Baraza Kuu.
0 comments:
Post a Comment