WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema hajawahi kutoa wala kupokea rushwa.
Waziri mkuu huyo anayejipambanua kwa kupiga vita rushwa alisisitiza
kwamba katika kipindi cha miaka 20 aliyokuwa Mbunge wa Hanang’ na miaka
10 ya uwaziri mkuu wake hajawahi kupokea wala kutoa rushwa na kamwe
hawezi kufanya hivyo.
Sumaye alisema hayo alipozungumzia miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwenye mahojiano yake na kituo cha Redio Tumaini cha
jijini Dar es Salaam jana asubuhi.
Alisema anayetoa rushwa ili kupata uongozi hafai kwa kuwa akishapata
anachokipata atatumia muda mwingi kujilimbikizia mali na kukusanya fedha
za kuwahonga wapiga kura kwenye uchaguzi ujao ili aendelee kuongoza.
Kuhusu kampeni za siasa zilizoanza kwa ajili ya kuwania urais mwaka 2015 alisema ni haramu kwa kuwa zinaambatana na rushwa.
Bila kutaja jina la mtu, alisema anayefanya kampeni hizo sasa hivi
anatangaza kuwanunua wapiga kura, kitendo kinachokwenda kinyume cha
taratibu na kanuni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo mwanasiasa huyo
hafai.
“Na kama chama kitafanya mambo ya ajabu kikampitisha mtu huyo kuwa
mgombea hapo tutaachana, lakini siamini kama chama changu kitampitisha,”
alisema Sumaye akimaanisha kuondoka ndani ya CCM huku akisisitiza
kwamba muda wa kutangaza nia ya kuwania urais ukifika atasema.
Kuhusu harakati za vyama vya upinzani, Sumaye alielezea kufurahia
kazi za wanasiasa wa upande huo akisisitiza kwamba zinaifanya serikali
kuwatumikia vema wananchi.
“Mimi ni muumini wa vyama vingi na hata nilipokuwa waziri mkuu
nilitamani idadi ya wabunge wa upinzani iwe kubwa zaidi… wanaisaidia
serikali isisinzie katika utendaji wake na ndiyo kazi yao kubwa,”
alisema Sumaye.
Kwa upande mwingine alizungumzia Bunge maalumu la Katiba na
kuwashauri wabunge hao kuzingatia uzalendo wa nchi kwanza badala ya
kupeleka mapendekezo ya vyama vyao.
Pia alipendekeza uwepo wa serikali mbili huku akisisitiza kwamba
kabla ya kupitisha serikali tatu lazima kero zote za muungano
zitatuliwe.
Awali alieleza mafanikio ya uongozi wa CCM kwa miaka 37 na kutaka
maboresho zaidi kwenye huduma za jamii na kuzitaja kuwa ni afya, elimu
na mgawanyo sawa wa mapato ya nchi.
0 comments:
Post a Comment