KWA
siku 12 za Operesheni M4C Pamoja Daima, Chama cha Dekomrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kimekitia kiwewe Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho
sasa kimelazimika kurejesha wabunge wake mikoani ili kujinusuru kutokana
na kimbunga cha operesheni hiyo.
Habari
zilizolifikia gazeti hili jana zinasema kwamba CCM imeamua kuwa wabunge
wote wasambae majimboni mwao kusafisha upepo wa M4C Pamoja Daima mara
baada ya vikao vya kamati za Bunge.
Kwa
kawaida, wabunge huwa wanaelekea bungeni Dodoma mara baada ya vikao vya
kamati za Bunge, lakini zamu hii chama kimewaelekeza wabunge, wakiwamo
mawaziri wote, kurudi mikoani kwa ajili ya kujibu mapigo ya CHADEMA
kabla ya kwenda bungeni.
Wachambuzi
wa masuala ya kisiasa wanasema uamuzi huu wa CCM ni uthibitisho wa
athari kubwa za Operesheni M4C Pamoja Daima, ambayo viongozi wa CHADEMA
wameimarisha chama na kukiweka pamoja zaidi katika kupigania maslahi ya
umma.
Katika
wiki mbili hizo, CHADEMA kimefanikiwa kufanya mikutano 206 na
kuhamasisha wananchi katika majimbo 166 ya uchaguzi, huku kikifanikiwa
kushinikiza serikali iboreshe daftari la kudumu la wapiga kura.
Hata
kabla ya CHADEMA kuhitimisha operesheni hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
ilitangaza kuboresha daftari hilo kabla ya kura ya maoni ya katiba
mpya.
Kwa
mujibu wa CHADEMA, wananchi wapatao milioni tano waliofikia umri wa
kupiga kura hawajaandikishwa, kwani serikali imekuwa inadai haina hela
za kufanyia kazi hiyo.
Viongozi
wa CHADEMA walisema wakati wa operesheni hiyo, kwamba serikali imekuwa
inagoma kuandikisha wananchi, huku ikijua ni kinyume cha sheria
kutofanya hivyo; kwani inapaswa kuboresha daftari hilo mara mbili katika
miaka mitano.
Mwenyekiti
wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, wamekuwa
wakisisitiza kuwa serikali isipofanya hivyo, chama hicho kitachukua
hatua mbadala ili kuhakikisha wananchi wanajiandikisha na wanashiriki
katika kura ya kupitisha katiba mpya.
Uchambuzi
uliofanywa na gazeti hili unaonyesha pia kwamba kupitia mikutano ya
hadhara na ya ndani, CHADEMA kimefanikiwa kuponya majeraha ya kisiasa
miongoni mwa viongozi na wanachama katika baadhi ya maeneo.
Katika
Mkoa wa Kagera kwa mfano, Mbowe alifanikiwa kupatanisha Mwenyekiti wa
Mkoa, Wilfred Lwakatare na Katibu wa Mkoa, Conchesta Rwamlaza, ambao
wamekuwa na ‘bifu’ ya muda mrefu na kutishia kugawa chama makundi
kutokana na mgogoro wa Manispaa ya Bukoba uliomng’oa aliyekuwa meya,
Anatory Amani.
Amani
alikuwa amefanikiwa kugawa CHADEMA katika makundi mawili, moja likitaka
ang’oke na jingine likiepuka kumwajibisha kwa mantiki kwamba kitendo
hicho kingemnufaisha kisiasa Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis
Kagasheki, ambaye aliunga mkono hoja ya CHADEMA ya kumng’oa Amani kwa
tuhuma za ufisadi.
Rwamlaza
ndiye alikuwa kinara wa upande wa CHADEMA uliokuwa unataka Amani
ang’oke, jambo lililosababisha upande mwingine kumtuhumu kwamba anafanya
kazi na Kagasheki.
Hata
hivyo, Mbowe alipofika Bukoba, alimshukuru Rwamlaza na madiwani wote wa
CHADEMA na CCM waliosimama kidete kumwondoa Amani, kwani msimamo wa
chama katika suala hilo unafahamika.
Baadaye
katika kikao cha ndani, aliwasuluhisha Lwakatare na Rwamlaza, mbele ya
Baraza la Mashauriano la Mkoa, umoja na amani vikarejea.
Operesheni
hiyo ilifanyika katika mikoa 22 ya Tanzania Bara na kuongeza hamasa ya
kisiasa miongoni mwa wanaCHADEMA na wananchi, huku ikisaidia kupokea
wanachama wapya kutoka vyama vingine, hasa CCM.
CHADEMA imetumia fursa hiyo pia kunadi wagombea wake wa udiwani katika kata zinazofanya uchaguzi katika maeneo mbalimbali.
Chama
hicho kilibeba ajenda tisa zikiwamo mchakato wa katiba mpya katika
hatua ya Bunge la Katiba, kura ya maoni; daftari la kudumu la
wapigakura.
Mkurugenzi
wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila, aliliambia
gazeti hili kuwa walikuwa wanafanya mikutano mitano hadi saba katika
mkoa mmoja kwa siku kwa sababu ya mfumo waliotumia.
“Kama
tungekuwa tunatumia magari kwa muda wa wiki hii moja tungekuwa tumeweza
kufika katika mkoa mmoja, na hivyo mkakati wetu wa kutembea nchi nzima
ndani ya wiki mbili usingefanikiwa.
“Na
operesheni hizi zinagharamiwa kwa asilimia kubwa na michango ya
wanachama na wafadhili wetu, na matumizi mazuri ya pesa za ruzuku ambazo
huwa tunatenga kila tukipata mwisho wa mwezi,” alisema.
Kigaila alisema kuwa wanaCHADEMA, na viongozi wa chama wapo tayari kuchangia operesheni hizo kwa kuwa wanatambua umuhimu wake.
0 comments:
Post a Comment