Thursday, 6 February 2014

SAFARI YA NKAMIA TOKA UANDISHI WA HABARI MPAKA NAIBU WAZIRI

Filled under:



Ni siku chache tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amuapishe Juma Nkamia kuitumika Serikali kama Naibu Waziri katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Kwa taaluma, Naibu Waziri Nkamia (Pichani) ni mwanahabari ambaye amesomea na kufanya kazi ya habari kwa kipindi kirefu kabla ya kuingia katika Ubunge ambao umemuwezesha kuteuliwa kuwa waziri.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika wizara hiyo,   Nkamia alisema anamshukuru  Rais Kikwete kwa kumteua na kumpa dhamana hiyo na kuahidi kuwa atasaidiana na Waziri wa wizara hiyo kutimiza majuku ya wizara katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya nne.

“Kama kiongozi mwenye mamlaka ndani ya wizara hii, nipo tayari kushirikiana na viongozi wenzangu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Idara zote zinazounda wizara hiyo”, alisema.

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inaundwa na idara kuu nne za kisekta ambazo ni Idara ya Habari, Idara ya Vijana, Idara ya Maendeleo ya  Utamaduni na Idara ya Maendeleo ya  Michezo.

Kwa kuwa tasnia ya habari ni miongoni mwa idara zilizo chini ya wizara hii, Nkamia alisema kuwa yupo tayari kushirikiana na wadau wa habari ikiwemo kusimamia maslahi ya waandishi wa habari nchini.

“Ukitaka kujua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa habari katika nchi yeyote ile, jaribu kuvifanya  vyombo hivyo kuanzia redio, televisheni na magazeti visifanye kazi hata kwa muda wa saa moja tu uone ni hasara kiasi gani na hatari kiasi gani zitatokea katika nchi ile” alisema Nkamia.

 Alisema anaheshimu na anatambua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini na atafanya nao kazi vizuri kwa kipindi chote atakachokuwa wizarani hapo.

Alisema kuwa anatambua kuwa  waandishi wa habari wanafanya  kazi katika mazingira magumu wakati wa kutekeleza majukumu yao ikiwemo  tatizo la “ukanjanja” na lugha mbalimbali zinozotolewa juu yao.

Amaeahidi kushirishirikiana na viongozi na wadau wa habari kuhakikisha kinaundwa chombo (bodi) kitakachosimamia maslahi ya waandishi wa habari.

Bodi itakayoundwa itasaidia kusimamia tasnia ya habari na kuhakikisha habari zinazoandikwa zitakuwa kwa maendeleo, manufaa na maslahi ya taifa na kuhakikisha inawajengea heshima waandishi wenyewe kwa kazi zao wanazofanya kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na ya nchi.

Naibu Waziri Nkamia ametoa rai kwa wadau wote wa habari kushirikiana ili kufanikisha uundwaji wa sheria ya habari. Alisema “Sheria hii ikikamilika itasaidia kuboresha baadhi ya changamoto za wanahabari ikiwemo ajira zao na mafao yao ya sasa na uzeeni”.

Nkamia amepewa wadhifa huo baada ya Rais Dkt. Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri katika kuziba nafasi zilizoachwa na mawaziri wanne waliojiuzulu na mmoja aliyefariki mwanzoni mwa mwezi huu.

Nkamia ni mkongwe aliyebobea katika taaluma ya uandishi wa habari akiwa amefanya kazi na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Aliajiriwa kwa mara ya kwanza na  Redio ya Taifa (Radio Tanzania Dar es Salaam) mnamo Oktoba 10, 1994 kama mwandishi msaidizi. Alifanya kazi RTD kwa muda wa miaka tisa hadi 2003  alipojiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Akiwa BBC Nkamia alifanya mambo mengi mazuri yaliyomjengea heshima mwenyewe na taifa. Ikizingatiwa kuwa Nkamia  alipenda sana kutangaza habari za michezo, alifanikiwa kutangaza mechi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Kama mwandishi wa habari za michezo, Nkamia alikuwa Mwafrika na Mtanzania wa kwanza kutangaza mchezo wa mpira wa miguu wa ligi ya Uingereza kwa lugha ya Kiswahili.

Kutokana na umahiri wake katika kutangaza habari za michezo, Nkamia aliaminiwa kutangaza mchezo wa fainali ya ligi ya Uingereza mwaka 2006 kati ya Manchester United na Arsenal  na mwaka huo huo, BBC ilimpa tena jukumu la kutangaza mechi ya fainali ya Ligi ya klabu bingwa ya Ulaya kati ya Arsenal na Barcelona.

Mwaka 2006 Nkamia alirudi nyumbani Tanzania na kujiunga na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambapo alifanyakazi kama mwandishi na mhariri hadi 2009.

Mwaka 2009 hadi 2010 Nkamia alifanya kazi ya uandishi katika shirika la utangazaji la Sauti ya Amerika (VOA) inayomilikiwa na Taasisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kazi ambayo aliifanya kwa mwaka mmoja.

Mwaka 2010 Nkamia alitambua na kuitikia dhamiri yake ya kuitumikia nchi yake katika mambo ya siasa hivyo aliamua kurudi Tanzania kuomba ridhaa ya wana Kondoa Kusini awe mwakilishi wao bungeni na Kamati Kuu ya chama chake, Chama cha Mapinduzi, ikapitisha jina lake kuwa mgombea ubunge wa chama hicho jimboni humo.

Nkamia anasema, kwa kuwa alikuwa anafanya kazi na watu, wapo waliomshagaa kuacha kazi ya maslahi zaidi na kurudi nyumbani. Miongoni mwa hao ni Dkt. Shaka Ssali mtangazaji na mmoja wa  wanahabari maarufu duniani aliyeuliza  Nkamia anafanya nini katika karne yenye changamoto ya ajira duniani kuacha kazi yenye mshahara na maslahi makubwa na kwenda kwenye siasa.

Anasema kwake jibu la swali hilo lilikuwa rahisi kuwa ni Uzalendo wa nchi kwanza ndiyo maana aliamua kurudi  kutoa mchango wake kwa maendeleo ya watu wake wa Kondoa Kusini na nchi kwa ujumla.

Kwa kuzingatia ukomavu na weledi alionao kwenye taaluma ya habari, ndiyo maana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ameamini na kumpa dhamana ili asaidiane  na Waziri mwenye dhamana katika Wizara hiyo, Fenella Mukangara, kuiongoza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Nkamia amechukua nafasi hiyo badala ya Mhe. Amosi Makalla aliyehamishiwa Wizara ya Maji.

Wengine waliowahi kushika nafasi ya Naibu Waziri katika wizara hiyo ni Dkt. Makongoro Mahanga, N. Nswanzungwanko, Joel Bendera, Dkt. Emmanuel Nchimbi na Dkt.Fenella Mukangara ambaye sasa ni waziri wa wizara hiyo.   

Juma Nkamia ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto sita wa familia ya Mzee Selemani Nkamia na Mwanaidi Ndwata. Anatokea eneo la kanda ya Kati katika mkoa wa Dodoma wilayani Kondoa. Ni  baba wa familia mwenye mke mmoja Bi Amina na watoto wawili ambao ni Kassi mwenye umri wa miaka 13 anayesoma kidato cha pili Shule ya Sekondari ya Wavulana Fezza na Hassani mwenye umri wa miaka saba anayesoma darasa la pili katika shule hiyo hiyo.

Kwa sasa Nkamia anaendelea kujiimarisha kielimu akiwa anasoma katika chuo Kikuu cha Dodoma

0 comments:

Post a Comment