MKALI wa filamu za Kibongo, Jacqueline Wolper, amewashukia
wasambazaji filamu, hasa wenye asili ya Kiasia kwa kile alichodai
wanalipa kiasi kidogo cha fedha na kusababisha kuwapa hasara waandaaji
kama ilivyotokea kwake katika ‘muvi’ ya ‘After Death’.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Wolper alisema katika muvi
yake hiyo ya kwanza, alitumia gharama kubwa kuiandaa kwa imani kuwa
ingempa faida kubwa na kurudisha gharama alizotumia, lakini ikawa ndivyo
sivyo.
Alisema kuwa haoni haja ya kuendelea kupoteza fedha zake kwa lengo la
kupata faida, lakini uchache wa wasambazaji ndiyo umekuwa tatizo kubwa
la kunyonywa stahiki wanayotakiwa kupewa wahusika na kuwataka Watanzania
wazalendo, kujitokeza ili kutoa ushindani kwa lengo la kuondoa tatizo
hilo.
Wolper alimpongeza Mkurugenzi wa kampuni ya kizalendo ya 5 Effects
Film, William Mtitu, ambaye anasambaza kazi zake mwenyewe, na sasa
anatarajia kuanza kuchukua na wasanii wengine.
Alisema Mtitu anaonekana kuleta mapinduzi kwenye suala la usambazaji
na ndiye atamfanya abadili nia yake ya kutaka kujiweka pembeni na
masuala ya filamu kutokana na kudhulumiwa na wajanja wachache.
“Kuna matumaini makubwa Kampuni ya 5 Effects Film inaweza kuwa ndiyo
mkombozi wetu na imenifanya nibadili nia, kwani nakusudia kwenda kuonana
na mkurugenzi wake, Mtitu ili nianze kutengeneza filamu nyingine ambayo
ataisambaza yeye na si vinginevyo,” alisema Wolper.
Kwa sasa 5 Effects Film, inasambaza filamu zinazotengenezwa na
mkurugenzi wake ambaye pia ni msanii wa ‘muvi’ za Kibongo na tayari
ameshafanikiwa kuziingiza sokoni filamu zake tatu ambazo ni ‘The Return
of Omega’, ‘Nyati’ na ‘The Omega’ huku akitarajiwa kuiachia ‘Big Deal’
hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment