Rais Jakaya Kikwete hataweza kukamilisha uteuzi wa wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba katika muda wa wiki mbili kama ilivyokuwa
imekadiriwa awali, kutokana na wingi wa majina yaliyopendekezwa kwa
ajili ya uteuzi huo.
Ugumu wa mchakato wa uteuzi wa wajumbe hao
unatokana na Rais Kikwete kupokea zaidi ya majina 5,000 yaliyopendekezwa
na kuwasilishwa kwake kutoka taasisi na asasi mbalimbali za kijamii,
huku yeye akitakiwa kuteua wabunge 201 tu, sawa na asilimia nne ya idadi
ya majina yaliyopendekezwa.
Wateule hao wa Rais wataungana na wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
kuunda Bunge Maalumu la Katiba, ambalo linatarajiwa kuanza mwanzoni
mwa mwezi ujao mjini Dodoma.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
ameliambia gazeti hili kuwa ofisi yake ina kazi ngumu ya kuchagua majina
ya wajumbe watakaoingia kwenye Bunge la Katiba na huenda kazi hiyo
ikakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Balozi Sefue alisema Januari 15 iliyotajwa na Rais Kikwete yalikuwa ni makadirio tu ya awali, lakini kazi bado ni ngumu.
“Makadirio yangu ni mwisho wa mwezi huu (Januari).
Ni kweli, Rais alitoa tarehe hiyo, lakini yalikuwa ni mapendekezo ya
awali tu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza:
“Hapa kuna mapendekezo ya vikundi zaidi ya 600 na
kila kikundi kimetoa majina tisa; kwa hiyo kuna majina zaidi ya 5,400,
kati yao tupate majina 200. Tunahitaji muda mrefu ili tufanye kazi kwa
ufanisi.”
Desemba 13 mwaka jana, Rais Kikwete alitoa
tangazo kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2A) cha kifungu cha 22 cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 akialika kila kundi kutoka
pande zote za Muungano kuwasilisha kwake majina kwa ajili ya kuzingatiwa
kwenye uteuzi.
Mgawanyo wa wajumbe
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe hivi
karibuni kuwa makundi ya kijamii yalitakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha
ya majina ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa mujibu wa
sheria.
Alibainisha kuwa kila kundi linatakiwa kuzingatia
umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya mtu aliyependekezwa.
Idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar haitapungua moja ya tatu ya wajumbe
wote.
Chikawe alisema wabunge hao 201 mchanganuo wao upo kwenye sheria
na kwamba 20 watatoka kwenye taasisi zisizokuwa za kiserikali, ambapo
nusu yao lazima wawe wanawake na moja ya tatu kutoka Zanzibar.
Wengine ni wajumbe 20 kutoka taasisi zote za dini, wajumbe 42 kutoka vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
“Vipo vyama 21 kwa maana hiyo, kila chama
kitaleta wajumbe wawili, mgawanyiko ni huohuo, kwa hiyo kwa vyama vya
siasa hapa lazima mmoja atoke Zanzibar na mwingine Bara na lazima mmoja
awe mwanamke na mwingine mwanaume,” alisema Chikawe.
Wajumbe wengine na idadi yao kwenye mabano ni
Taasisi za Elimu ya Juu (20), makundi ya watu wenye ulemavu (20), vyama
vya wafanyakazi (19), vyama vinavyowawakilisha wafugaji (10), vyama
vinavyowawakilisha wavuvi (10) na vyama vya wakulima 20.
Mwakilishi wa Asasi
Mwakilishi wa Asasi za kiraia, Marcosy Albanie
alisema kuwa tatizo la kufurika kwa majina linatokana na asasi nyingi
kutokubali kuungana na kupeleka majina machache.
“Kuna jumla ya asasi za kiraia zaidi ya 66,000
nchini. Sisi katika muungano wa asasi za kiraia tulikubaliana tukutane
Dodoma ili tuchague watu wachache. Lakini kuna taasisi zimejifungia
ndani zikapeleka majina yao wenyewe kwa ubinafsi wao,” alisema Albanie
na kuongeza: “Kazi hapo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, achukue majina ya
taasisi tuliokaa Dodoma na kujadili kwa siku mbili, nyingine zikakaa
zenyewe binafsi. Huo siyo utaratibu wa kidemokrasia.”
Akizungumzia utaratibu uliotumika kuwapata wajumbe
hao, Albanie alisema kuwa wamechagua watu 40 yaani wanawake 20 na
wanaume 20 kwa kujali usawa wa jinsia.
“Tumeangalia sekta 11, kanda tisa, maana tunataka
kila kanda iwakilishwe. Katika kila kanda na sekta, majina ya watu
wawili kwa aliyepata kura nyingi zaidi. Jina la mwanamke na mwanaume kwa
kujali usawa wa jinsia. Pale tulipokosa mwanamke tumeweka wanaume
wawili,” alisema Albanie.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema kuwa chama hicho kimezingatia sheria ilivyosema.
“Chadema tumepeleka majina kwa mujibu wa sheria.
Sheria ilisema majina yasiyopungua manne na yasiyozidi tisa, tumefanya
hivyo kwa kupeleka majina manne. Ikulu waeleze ni chama kipi au taasisi
ipi iliyokiuka sheria na kivipi,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa chama hicho kilishatoa ushauri wa
kurahisisha uteuzi ikiwa pamoja na Serikali kutaja makundi na majina ya
taasisi.
“Ndiyo
maana katika mapendekezo yao kwao juu ya muswada wa sheria, tulitaka
siyo tu sheria kutaja makundi kwa jumla, bali pia majina ya taasisi
zinazopaswa kufanya uteuzi na idadi ya wateule kwa kila taasisi,”
alisema.
Hivi karibuni akitoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa
chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mnyika aliwataja
waliopendekezwa kuwa ni Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando, Nasra
Juma Burhan na Method Kimomogoro.
“Marando huyu ni msomi mwenye shahada ya Sheria na
ni wakili wa Mahakama Kuu, Kimomogoro ni msomi wa sheria na ni Wakili
wa Mahakama Kuu, Profesa Safari ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu
aliyebobea kwenye mambo ya sheria, vilevile ni Wakili wa Mahakama Kuu na
mama Burhani ni mwalimu kwa taaluma,” alisema Mnyika.
Chadema kimekuwa kikikosoa mchakato huo, hali
iliyofanya mwaka 2012 kwenda Ikulu kukutana na Rais Jakaya Kikwete
kikitaka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kubadilishwa. Baada ya chama
hicho, vyama vingine navyo vilialikwa Ikulu na kuzungumza na Rais.
Naye Naibu Natibu Mkuu wa Cham cha Wananchi (CUF),
Julius Mtatiro amesema kuwa chama hicho kimefuata sheria ilivyosema
kuwa majina yasipungue manne na yasizidi manne.
“Sisi tumefuata sheria ambayo ilitutaka tupeleke
majina manne hadi tisa. Tumezingatia jinsi na ukanda kwa kuteua nafasi
za wanaume sawa na wanawake. Hata hivyo, siwezi kukwambia idadi wala
kutaja majina kwa sababu sera ya chama hairuhusu,” alisema Mtatiro.
0 comments:
Post a Comment