Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono ametoa ufafanuzi
juu ya uhusiano wake na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto
Kabwe.
Hatua hiyo ya Mkono imekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu kuwa aliwahi kumpa Zitto magari mawili.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mkono alisema
kuna magari mawili yanayohusishwa na Zitto na kuyataja kuwa ni Toyota
Land Cruiser na Nissan Patrol.
“Sijawahi kumpatia Zitto magari, isipokuwa kuhusu
hiyo Land Cruiser, nilitoa msaada wa kuwanusuru Zitto na Mbowe
(Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), kule Tarime kwenye msiba wa
marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Chadema), kwani
walikuwa wakitishiwa kupigwa.”
Alisema alitoa gari hilo lililokuwa na Bendera ya
Bunge liwachukue Mbowe na Zitto na kuwapeleka Mwanza... “Walipofika
Mwanza, Zitto aliwasiliana na mimi kuhusu ununuzi wa gari hilo na
kupitia wakala wangu nilimuuzia,” alisema Mkono.
Kuhusu Nissan Patrol, Mkono alisema lilikodishwa kwa Zitto na mpaka sasa bado analipa gharama za kulikodisha...
“Hata nyaraka za umiliki wa gari hili ninazo mimi
mwenyewe kama mmiliki halali. Ninamiliki magari mengi tu hata wewe
mwandishi ukitaka Vogue (aina ya gari) nitakukodisha tu,” alisema Mkono.
Alisema wanafahamiana kwa siku nyingi hata kabla
ya Zitto kuwa mbunge na kwamba aliwahi kufanya mazoezi kwa vitendo
katika ofisi yake (Mkono), alipokuwa mwanafunzi.
Kuhusu tuhuma kwamba anawahonga wapinzani wake
wajitoe katika uchaguzi ili apite bila kupingwa alisema katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 alipita bila kupingwa kutokana na
uchapakazi wake wa kiwango kikubwa.
Mkono pia alijibu tuhuma zilizotolewa na Zitto
jana kwamba Mbowe alipewa mamilioni ya fedha na Mkono kwa nyakati
tofauti na kusema hajawahi kutoa fedha zozote kusaidia Chadema.
Zitto akana Katika hatua nyingine, Zitto ameitaka Chadema kumwandikia mashtaka mapya yaliyoibuliwa na Lissu ili aweze kujitetea.
“Mashtaka yangu ni yale tu ya waraka na kugombea uenyekiti na
shtaka moja la masuala ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa kuwa hawakuniandikia mashtaka hayo kinachobakia ni majungu tu,
masuala ya kuhongwa magari ni tuhuma zinazorudiwarudiwa bila ushahidi
wowote,” alisema na kuongeza:
“Mkono ananihonga ili nimpe nini? Yeye mbunge na
mimi ni mbunge pia. Hiyo hongo tunabadilishana na nini? Katika kumaliza
Shahada yangu ya Uzamili ya Sheria na Biashara nilifanya `internship’
(mafunzo kwa vitendo) kwa Mkono na hivyo kuna uhusiano wa kikazi wa baba
na mtoto.”
Zitto alisema kuwa Mkono ni kama mzee wake na suala la kumpa chochote kile si hoja.
Kitila amruka Slaa
Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk
Kitila Mkumbo amesema kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Dk Wilbrod Slaa kuwa alikiri kwamba Zitto alikuwa akiujua waraka wa
Mkakati wa Mabadiliko 2013, ni za kutunga.
Juzi, wakati akieleza uamuzi wa kikao cha Kamati
Kuu kuwafukuza uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba na Dk Kitila, Dk Slaa alisema wakati akihojiwa
na Kamati Kuu, Dk Kitila alisema Zitto alikuwa akiujua waraka huo.
“Siyo kweli. Hata siku moja sijawahi kukiri kwamba Zitto alikuwa akiufahamu waraka, kilichosemwa na Dk Slaa ni uongo.”
Mwigamba afafanua
Mwigamba alisema hakuhojiwa na Kamati Kuu kwa
sababu yeye ni Msabato na Siku ya Sabato, hairuhusiwi kufanya jambo
lolote zaidi ya kumwomba Mungu.
“Waliniita Ijumaa (Januari 3) ili nihojiwe lakini
mpaka saa 12 jioni sikuwa nimehojiwa na niliwaeleza kuwa jua likizama
sitakubali kuhojiwa kwa sababu itakuwa imeanza Siku ya Sabato,” alisema.
Alisema kikao cha Kamati Kuu kiliendelea Januari
4, mwaka huu, pia hakuweza kwenda kuhojiwa kwa sababu ilikuwa Sabato,
pia alikuwa kanisani, “Niliwaambia kuwa nipo tayari kuhojiwa Jumapili,
hawakunijulisha kama wameridhia.”
0 comments:
Post a Comment