Monday, 6 January 2014

KUMI WAFA MAJI NA WENGINE WAENDELEA KUTAFUTWA

Filled under:



Watu 10 wamekufa maji na wengine wanaendelea kutafutwa baada ya boti mbili kupigwa dhoruba na mojawapo kuzama katika maeneo tofauti ya Bahari ya Hindi.
 
Vifo vya wanne vimetokea mkoani Pwani baada ya boti waliyokuwa wanasafiria kuzama baharini, na miili ya watu sita ilipatikana ikiwa miongoni mwa waliozama majini baada ya boti ya Mv Kilimanjaro II iliyopigwa dhoruba katika mkondo wa Nungwi ikitokea Bandari ya Mkoani, Pemba kwenda Unguja jana.

Ajali ya Zanzibar,Boti ya Mv Kilimanjaro II iliyokuwa imebeba abiria 380 ilipigwa na upepo mkali na kuleta taharuki kwa wasafiri, huku watu waliokuwa wamekaa juu wakidaiwa kuteleza na kutumbukia baharini.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini, Riziki Juma alithibitisha kupatikana kwa miili hiyo sita jana jioni.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif Suleiman alisema kundi la wazamiaji lilikuwa limekwenda wamekwenda katika eneo la ajali hiyo kwa ajili ya uokoaji.
Waziri Seif alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikutana kwa dharura mchana wa jana kujadili tukio hilo, kisha kwenda eneo la tukio kushirikiana na wataalamu wengine kuwatafuta watu hao.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Ilembo alisema boti hiyo iliondoka Pemba asubuhi na baada ya kufika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa wimbi kali na  injini yake kuzima.
Ilembo alisema abiria waliokuwa wamekaa juu ya boti hiyo waliteleza na kutumbukia baharini wakiwemo watoto na tayari mpango wa kwenda katika eneo la tukio kuwatafuta kwa kushirikiana na wananchi umekamilika.
Hata hivyo, alisema uhakiki wa orodha ya abiria unaendelea ili kupata majina ya watu ambao hawajaonekana na umri wao, kwa kuwa kuna meli mbili zilisafiri kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usafiri wa Baharini (ZMA), Mhandisi Abdi Maalim alisema jana alasiri mabaharia walianza kazi ya kuwatafuta watu wanaosadikiwa kuzama.

 Ni mapema mno kusema lolote, siwezi kusema kama wamekufa au wako hai, kuna watu wameripotiwa kutoweka baada ya meli hiyo kupata dhoruba na hawafahamiki mahali walipo,” alisema Mhandisi Abdi.
 
Ofisa mmoja wa Kampuni ya Azam Marine, alisema meli hiyo ilibeba abiria 380 na chanzo cha tukio hilo ni dhoruba iliyoambatana na upepo mkali.
“Wakati chombo kimezimika watu walianza kukata maboya ya uokozi na mtafaruku wa abiria kutaka kujinusuru ulikuwa mkubwa, chombo hakikuzama na kiliendelea na safari na kimefika katika Bandari ya Malindi,” alisema.
Ajali hiyo ni ya kwanza kutokea mwaka huu ambapo hadi jana alasiri watu walionekana kukaa katika vikundi vikundi na wengine wakieleza kutokuwaona ndugu zao.
 
 

0 comments:

Post a Comment