Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kipo katika
harakati za kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam,
uliompa ushindi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe.
Zitto ambaye pia ni Mbuinge wa Kigoma Kaskazini,
juzi aliibuka mshindi katika maombi yake ya kuizuia Kamati Kuu (CC) ya
chama hicho kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama
wake, hadi kesi ya msingi kuhusu suala hilo itakapokuwa imesikilizwa.
Kadhalika, chama hicho kupitia kwa Mkurugenzi wake
wa Mawasiliano na Uenezi, John Mnyika kimesema kinaendelea na
utekelezaji wa uamuzi wa Kamati Kuu wa kutompa Zitto ushirikiano wa aina
yoyote.
Wakili wa Chadema, Peter Kibatala, alisema jana
kuwa japo wanauheshimu uamuzi wa Mahakama, hawajaridhika nao na kwamba
wanakusudia kwenda Mahakama ya Rufani kuupinga.
“Ingawa uamuzi huu ni Interlocutory (uamuzi
usiomaliza kesi), lakini sisi hatukuridhika nao. Hatukuridhika na uamuzi
wa kutupilia pingamizi letu la awali, hati ya kiapo na hata amri
yenyewe ya zuio la muda,” alisema Wakili Kibatala na kuongeza:
“Kuna namna nyingi za kufanya kupinga uamuzi huo,
kama vile kukata rufaa, kuomba marejeo au namna nyinginezo. Kwa hiyo kwa
sasa tunaangalia namna bora ya kwenda Mahakama ya Rufani bila kuathiri
matakwa ya kisheria.”
Wakili Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema kuna haja ya kuiomba
Mahakama ya Rufani kuuchunguza uamuzi huo kwa kuwa una athari si kwa
Chadema tu, bali hata vyama vingine dhidi ya wanachama wake.
Kauli ya Mnyika
Mnyika kwa upande wake alisema kutompa ushirikiano
Zitto ni uamuzi wa Kamati Kuu ambao ulitokana na hatua yake ya kwenda
mahakamani kwa masuala ya chama, kinyume cha matakwa ya Katiba ya
Chadema na Kanuni zake.
Mnyika alikuwa akirejea taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa, baada ya kikao hicho akiwataka viongozi wa
ngazi zote za chama hicho, wanachama, mashabiki na wapenzi wake,
kutoshiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yote ya nje, ndani
au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto na
mawakala wake.
Ushindi wa Zitto
Katika maombi hayo namba 1 ya 2014, Zitto kupitia
kwa Wakili Albert Msando, Zitto aliiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda
kwa CC ya Chadema, hadi kesi yake ya msingi namba 1 ya 2014
aliyoifungua mahakamani hapo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Awali, mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa
chama hicho, Tundu Lissu na Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa
hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake juzi, Jaji John Utamwa
alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza
matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
Maombi hayo ya Zitto yaliyotolewa uamuzi juzi
yalitokana na kesi ya msingi aliyofungua mahakamani hapo Januari 2,
2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema.
Katika kesi hiyo anaiomba mahakama ikizuie chama
hicho, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote
au kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa anayokusudia
kuikata Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa nyadhifa,
itakaposikilizwa.
Pia aliiomba Mahakama Kuu imwamuru Katibu Mkuu wa
Chadema ampatie mwenendo na taarifa za CC za kumvua nyadhifa zake zote
alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika
utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Kesi hiyo
ya msingi imepangwa kutajwa mahakamani hapo Februari 13, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment