Wizara ya Maliasili na Utalii, imewasimamisha kazi watumishi
wake 21 kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia ujangili wa
nyara za Serikali.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Polisi
mkoani Singida, kumkamata ofisa wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya
ya Singida, kwa tuhuma za kupatikana na silaha mbili na nyara za
Serikali, kinyume cha sheria.
Akitangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema Serikali
inasikitishwa na vitendo viovu vinavyofanywa na watumishi wake na
haitavivumilia. “Tumesikitishwa na kitendo cha ofisa wanyamapori
wilayani Singida kukamatwa na bunduki mbili na ndege aina ya Heroe 12
nyumbani kwake, hatua tuliyochukua ni kumsimamisha kazi na kufikishwa
mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Wizara baada ya kufanya uchunguzi, imegundua kuwa
kuna watumishi wanaoshirikiana na mtandao wa ujangili, hivyo
imewasimamisha kazi watumishi 21 wa Idara ya Wanyamapori na tutachukua
hatua zaidi.”
Alisema kati ya watumishi hao, 11 wanatoka katika
Kikosi cha Kuzuia Ujangili mkoani Arusha, wanne wanatoka Mkoa wa Rukwa
katika Pori la Akiba la Lwafu, mmoja Kikosi cha Bunda, watatu Pori la
Akiba la Maswa, mmoja Selous, na mwingine mapori ya Lupika, Lumesule na
Lusangu.
Akifafanua kuhusu uhaba wa watumishi katika Idara
ya Wanyamapori, Nyalandu alisema kwa zaidi ya miaka 10 wizara hiyo
haikuwa ikiajiri watumishi hali inayosababisha kukosa watumishi wenye
ujuzi.
“Tunajipanga kuajiri watumishi wengine wenye ujuzi
na kuangalia maendeleo ya teknolojia hasa kwa kujifunza kwa wenzetu
Afrika Kusini,” alisema.
Kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, alisema
Serikali imeunda tume ya kimahakama itakayowahoji askari waliohusika na
kurudisha taarifa. Hata hivyo alisema wako mbioni kuendelea nayo.
“Rais Jakaya Kikwete ameunda tume ya kimahakama na
itatoa taarifa, ila sisi hatutalala, tutahakikisha kuwa tunapambana na
ujangili ili kulinda nyara za Taifa,” alisema Nyalandu.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wizara yake kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kuwakamata wahalifu.
“Jitihada hizi siyo zetu wenyewe, tunashirikiana
na vyombo vya ulinzi na usalama. Tunawaomba wananchi washirikiane
kulinda na kutoa taariza zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu.
Tunawaomba watumishi wetu wafanye kazi kwa moyo na uaminifu,” alisema
Nyalandu.
Mamlaka ya wanyamapori
Akiwa katika pori la akiba la Selous hivi karibuni, Nyalandu alieleza mkakati wa Serikali wa kuanzisha mamlaka ya wanyamapori ili kuwapa mamlaka watendaji wa sekta hiyo katika kutunza maliasili.
Akiwa katika pori la akiba la Selous hivi karibuni, Nyalandu alieleza mkakati wa Serikali wa kuanzisha mamlaka ya wanyamapori ili kuwapa mamlaka watendaji wa sekta hiyo katika kutunza maliasili.
0 comments:
Post a Comment