Mwanasiasa wa Chama cha upinzani nchini Zambia cha Alliance for a
Better Zambia (ABZ), Frank Bwalya, amekamatwa na polisi na kufunguliwa
mashtaka kwa madai ya kumkashifu rais wa nchi hiyo, Michael Satta, kwa
kumwita kiazi.
Bwalya anadaiwa kumwita Rais Satta kuwa ni ‘Chumbu Mushololwa’, akimaanisha kiazi, kupitia kituo kimoja cha redio nchini humo.
Katika lugha ya Kibemba, maneno hayo yana maanisha kiazi kitamu,
ambacho humegeka kinapopondwa, akimaanisha kuwa rais huyo hasikilizi
ushauri wa wengine.
Aidha, taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa iwapo itathibitika
kiongozi huyo wa ABZ kutoa matamshi hayo, atatiwa hatiani na kuhukumiwa
kifungo cha miaka mitano jela.
Bwalya anakuwa mwanasiasa wa pili kuingia matatani baada ya
mwanasiasa mwingine wa upinzani, Nevers Sekwila Mumba, wa Chama cha
Movement for Multiparty Democracy kuhojiwa na polisi mwaka jana kwa
kumwita Rais Satta muongo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Stephen Kampyongo,
alisema Bwalya alikamatwa kwa kutoa matamshi ya kumharibia sifa Rais
Satta.
Kutokana na kukamatwa kwa kiongozi huyo, kambi ya upinzani imetaka
Bwalya aachiwe huru huku ikisisitiza kuwa kiongozi huyo ni mwanasiasa
asiyemuogopa mtu yeyote.
Aidha, wanasiasa wa upinzani wamesema kuwa matamshi ya Bwalya si matusi kama inavyotafsiriwa.
Hali ya kisiasa si shwari kwa sasa nchini Zambia kutokana na mvutano kati ya upinzani na utawala.
0 comments:
Post a Comment