Tanzania imetangaza siku tatu za
maombolezo kuanzia tarehe 6 hadi 8 Desemba, 2013, kufuatia kifo cha rais wa
zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Rais Jakaya Kikwete wa nchi hiyo pia
ameagiza kuwa katika kipindi hicho cha siku tatu bendera zote zitapepea nusu
mlingoti.
Kufuatia kifo hicho Rais Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia
kwake kwa mkewe Bi Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya
Kusini kufuatia kifo cha Mzee Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba,
2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Rais ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu sote.
"Afrika ya Kusini, Afrika na
dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na
21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza
kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu".
Ameongeza Rais Kikwete.
Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa
ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na
upendo uliomwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja
baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu
wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana Afrika Kusini,
Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata
maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake". Rais ameongeza kusema,
"Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mandela
mahali pema peponi".
Mandela amefariki huko Johannesburg
akiwa na umri wa miaka 95 na yeye ndiye aliyeiongoza Afrika Kusini kutoka
mikononi mwa watawala wa ubaguzi wa rangi baada ya kufungwa jela kwa miaka 27.
Mandela alikuwa anatibiwa homa ya
mapafu nyumbani kwake baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi mitatu.
Katika taarifa yake kwa watu wa
Afrika Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa Mandela amewaaga lakini yuko mahali
salama.
Rais Zuma amesema kuwa taifa limepoteza
mtu waliyemjua kama mtoto wa taifa hilo.
Mandela aliwahi kushinda tuzo ya
amani ya Nobel, na kutambulika kama rais aliyeheshimika sana hasa kwa
kupatanisha watu wa Afrika Kusini baada ya kutoka gerezani.
0 comments:
Post a Comment