Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wameiomba Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu iwaweke kwenye magereza tofauti ili wasije wakauana kwenye
Gereza la Segerea.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo wanatokea Dar es Salaam ambao ni
Chibago Magozi (32), Juma Kangungu (29), Msungwa Matonya (30) na Mianda Mlewa
(40) wote wakazi wa Vingunguti, Dar es Salaam na John Mayunga (56) mkazi wa
Kiwalani.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi, Longishu Losingo (29),
dereva na mkazi wa Kitunda, Masunga Makenza (40), mkazi wa Tabata Darajani,
Paulo Mdonondo (30), mkazi wa Buguruni, Zacharia Msese (33) na mkazi wa
Mwananyamala, Ahmad Kitabu (30).
Ombi hilo, lilitolewa jana na Losingo mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo
muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Yasinta Peter kuiambia mahakama kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba ipange tarehe ya kuitaja.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Fimbo aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19,
mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ndipo Losingo aliponyoosha mkono na kuieleza
mahakama kuwa wanagombana na kutishiana kuuana wenyewe kwa wenyewe kila siku
gerezani.
“Mheshimiwa, sisi wenyewe kwa wenyewe tunatishiana kuuana, tunagombana kila
siku gerezani tutauana tunaomba tusambaratishwe, magereza yapo mengi
mheshimiwa, tutauana sababu kila mtu anamtuhumu mwenzie kuwa ndiye aliyetoa
taarifa ahusishwe kwenye tukio hili kwa simu,” alisema Losingo.
Mshtakiwa mwingine, Masunga Makenza aliunga mkono hoja hiyo na kuongeza kuwa
wingu la ugomvi ndani ya Gereza la Segerea miongoni mwao linarindima kila siku,
“Tunaomba tusambaratishwe kila mmoja kwenye gereza lake.”
Wakati Losingo na Makenza wakieleza hayo, washtakiwa wenzao nao walinyoosha
mikono na wakitaka kusema jambo. Hata hivyo, Hakimu Fimbo hakuwapa nafasi na
kuwaambia: “Kwa sasa hakuna magereza ya kutosha ya kuwatawanya, mkae hukohuko
Segerea, muelewane na likapotokea lolote muutaarifu uongozi wa gereza.”
Awali, akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Serikali, Aida Kisumo alidai kuwa,
Novemba 3, mwaka huu washtakiwa hao kwa pamoja walifanya kosa hilo la mauaji ya
Dk Mvungi kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
0 comments:
Post a Comment